Na.Salum Vuai, WHUMK
WAZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo, amesema miongoni mwa mambo yanayoupandisha hadhi utalii wa Zanzibar ni kuwepo kwa mikahawa ya kisasa yenye viwango vya kimataifa.
Akizungumza juzi usiku katika mahojiano maalum kando ya sherehe ya kuadhimisha miaka sita tangu kuanzishwa kwa mkahawa mashuhuri hapa Zanzibar uitwao ‘Six Degrees South’ uliopo Shangani mjini Unguja, alisema Zanzibar inahitaji mikahawa mingi zaidi yenye hadhi kama hiyo.
Waziri Kombo alisema, watalii na wageni wengine wanaofika nchini, hawafuati vitanda vizuri kwa ajili ya kulala tu, bali pia wanahitaji sehemu zenye mvuto ambazo wanaweza kupata vyakula na vinywaji vya kuchagua na hivyo kuwafanya watumie zaidi na kuongeza pato la taifa.
“Uzuri wa mkahawa huu unaoongezwa haiba na upepo mwanana wa Bahari ya Hindi iliyopo mkabala nao, ni kivutio tosha kinachoweza kumshawishi mtalii atumie na kuona thamani ya fedha anazolipia. Nawapongeza wamiliki pamoja na wafanyakazi wote kwa namna wanavyotoa huduma za uhakika ambazo tayari sifa zake zimevuka bahari na anga hadi nchi za nje,” alieleza Waziri Kombo.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na zaidi ya waalikwa 100 wakiwemo viongozi kadhaa wa serikali na watendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Waziri Kombo alisema kwa mtu anayetembelea kisiwa hicho, hapo si pahala pa kukosa na hatajuta kufanya hivyo.
Aidha, aliahidi kuwa serikali katika azma yake ya kukuza utalii na kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea Zanzibar, itaendelea kushirikiana na kushauriana na wawekezaji juu ya mambo mazuri ya kufanya, akiamini kuwa inawezekana kufikia watalii milioni moja kwa mwaka kwani Zanzibar ni jina linalojiuza kwa mengi.
Mapema, Mkurugenzi Mtendaji wa ‘ZMMI and 6 Degrees South’ Stephi Hill, alisema ni furaha kwao kuona katika kipindi kifupi cha miaka sita tangu ulipoanzishwa, mkahawa huo umeweza kuvutia wateja wengi hasa watalii kutokana na huduma nzuri na za kipekee zinazotolewa.
“Kipaumbele chetu hasa ni kuhakikisha wateja wetu wanapata vyakula vya ndani nan je ya nchi vinavyoandaliwa na mpishi aliyebobea katika fani ya upishi na mweledi wa kuvisarifu kwa umakini ili kuleta ladha inayofanya mlo kuwa mtamu kupindukia,” alisema Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake, mmiliki wa mkahawa huo Saleh Mohammed Said, alisema ni jukumu lao kutoa huduma bora zaidi kwa wateja ili waridhike na pia kuwafanya waongeze siku za kukaa Zanzibar sambamba na kuwa mabalozi kwa watalii wengine katika nchi zao.
Saleh alizi kampuni za ‘ZMMI Wine and Spirits’ pamoja na Vodacom Tanzania kwa kukubali kuidhamini hafla hiyo na kuifanya ifane.
Ili kunogesha hafla hiyo, uongozi wa mkahawa huo ulimualika msanii nguli wa muziki wa kizazi kipya Tanzania Ali Kiba ambaye ujio wake kwa waalikwa ulikuwa wa kushtukiza (Surprise), kwani haikuwa imetangazwa kabla.
Kufika kwake mnamo saa 4:00 usiku, kulipokelewa kwa shangwe na vifijo na mara akaanza kutumbuiza kwa nyimbo zake kadhaa mashuhuri ukiwemo ‘Kadogo’ na ‘Seduce me’.
Vibao hivyo na vyengine, vilitikisha ukumbi huku wageni wengi wao wakiwa watalii na wanachama wa Jumuiya ya Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (ZATI), wakishindwa kujizuia na kujimwaga uwanjani.
No comments:
Post a Comment