Habari za Punde

Balozi Seif Azungumza na Ujumbe Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 Wanaounda Taifa la Nigeria.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kushoto akisalimiana na Mratibu wa Washirika wa Sekta za Kijamii kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wa Nchini Nigeria Bwana Gyangyang Limave wakati akijiandaa kuzungumza na Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 ya Taifa la  Nigeria waliofika Zanzibar kujifunza Mpango Maalum wa uendeleshaji wa Miradi ya Tasaf.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ufuatiliaji pamoja na usimamizi makini wa Watendaji wa Ofisi yake katika kuratibu matumizi sahihi ya fedha zinazotekeleza Miradi ya Kijamii ndio uliopelekea kufanikisha vyema kwa Miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF}.
Alisema Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambayo ndio inayoratibu shughuli zote za Tasaf kwa upande wa Zanzibar imelazimika kuchukuwa hatua hiyo ili kulinda Heshima itakayotoa ushawishi kwa Wafadhili wa Mpango huo kuendelea kuunga mkono katika utoaji wa Mikopo zaidi.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati wa Mazungumzo yake ya Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 yanayounda Taifa la Nigeria waliowasili Zanzibar kwa ziara ya Siku mbili kuja kujifunza kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika mpango wa kuhudumia Kaya Maskini Nchini Tanzania.
Alieleza kwa vile Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} unatoa huduma  katika pande zote mbili za Tanzania, Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  zinalazimika kufuatilia mwenendo mzima wa fedha zinavyotumika katika Miradi ya Tasaf  ili kufikia lengo.
“ Serikali ililazimika kufanya uchambuzi yakinifu na kujiridhisha katika mwenendo wa wa matumizi ya Miradi ya Tasaf  ili kuepuka upotevu ambao ungegharimu machungu kwa wasimamizi wa Miradi hiyo”. Alisisitiza Balozi Seif.
Alisema ipo Miradi mingi ya Kijamii katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba Mjini na Vijijini iliyoleta ukombozi kwa Wananchi walio wengi baada ya kupata msukumo uliotokana na uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania katika Awamu tofauti uliojikita kuhudumia  moja kwa moja miradi hiyo.
Balozi Seif alisema ipo haja kwa Wafadhili wa Miradi ya Kijamii akatolea Mfano Benki ya Dunia pamoja na Taasisi nyengine za Kimataifa  za misaada ya Maendeleo kuendelea kuongeza ufadhili wao kwa vile lengo la uanzishwaji wa Miradi ya Kijamii limefanikiwa vyema.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  alisema hatua hiyo ya Wafadhili ni muhimu kwa vile inaweza kusaidia kuondoa mkwamo kwa baadhi ya Changamoto zinazotokana na Miradi inayoanzishwa hasa katika Sekta za uzalishaji kupitia Vikundi vya ujasiri amali.
Balozi Seif  aliishauri Timu hiyo ya Waratibu Wakuu wa Majimbo ya Nigeria kwamba katika kuimarisha Miradi na huduma za Kijamii ipo haja ya Mataifa ya Afrika kuzidi kushirikiana katika kubuni mbinu na njia za pamoja katika kuendeleza Miradi hiyo itakayoleta ustawi na Maisha bora kwa Waafrika walio wengi.
Alisema mfano ulioonyeshwa na Timu hiyo ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 ya Taifa la Nigeria wa kufika Tanzania kujifunza mwenendo wa uendeshaji wa Miradi ya Kijamii ni mwanzo wa kuigwa kwa Mataifa mengine yanayotekeleza Miradi kama hiyo Barani Afrika.
Mapema Mratibu wa Washirika wa Sekta za Kijamii kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wa Nchini Nigeria Bwana Gyangyang Limave ameishukuru na kuipongeza Tanzania kwa umakini wake iliyonao wa kuhakikisha Bara la Afrika linaendelea kuimarika Kiuchumi na Ustawi.
Bwana Byangyang alisema msimamo wa Tanzania katika kustawisha maisha ya Wananchi wake ni mfano wa kuigwa na Mataifa mengine Duniani yaliyoanza mpango wa kuimarisha Taasisi za Kijamii.
Alisema Serikali ya Nigeria katika muelekeo wake wa kustawisha Maisha ya Wananchi wake tayari imeshaanzisha Taasisi inayoratibu na kusimamia kasuala ya Kijamii mnamo Mwaka 2016.
Bwana Gyangyang Limave alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 1.3 zimetolewa na Serikali Kuu katika kuimarishaji wa Kaya Maskini Nchini humo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif  Ali Iddi akizungumza na Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 ya Taifa la  Nigeria waliofika Zanzibar kujifunza Mpango Maalum wa uendeleshaji wa Miradi ya Tasaf.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif.Ali Iddi kati kati waliokaa vitini akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 ya Taifa la  Nigeria pamoja na Watendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} Bara na Zanzibar.
Balozi Seif  akibadilishana mawazo na Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 ya Taifa la  Nigeria mara baada ya kupiga picha za ukumbusho wa uwepo wao Visiwani Zanzibar.
Balozi Seif  akiagana na Kiongozi wa Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 yanayounda Taifa la Nigeria Naibu Mkurugenzi wa Taasisi inayosimamia masuala ya Ustawi wa Jamii Bwana Ortutu baada ya mazungumzo yao.

Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.