Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi
Joseph Sokoine akizundua Mfumo wa
Kitaifa wa Ukusanyaji Takwimu za Gesijoto, Ufuatiliaji, Uandaaji Taarifa na
Uhakiki katika Ukumbi wa Kituo cha Kuratibu Hewa Ukaa Chuo Kikuu cha Kilinmo Sokoine (SUA) mkoani Morogoro. Wanaoshuhudia ni Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili
na Utalii Dkt. Ezekiel Mwakalukwa na Mkurugenzi
wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Profesa William Mwegoha
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi
Joseph Sokoine amezindua Mfumo wa Kitaifa wa Ukusanyaji Takwimu za Gesijoto,
Ufuatiliaji, Uandaaji Taarifa na Uhakiki katika Ukumbi wa Kituo cha Kuratibu
Hewa Ukaa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) mkoani Morogoro.
Akizindua mfumo huo kwa
niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa ais (Muungano na Mazingira) Mhe.
George Simbachawene, Balozi Sokoine alisema
kuwa utawezesha nchi kukusanya takwimu za gesijoto kutoka
sekta mbalimbali kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki na maamuzi.
Pamoja na mambo mengine alisema pia utasaidia kuandaa
taarifa mbalimbali ambazo nchi inatakiwa kuandaa kama Mwanachama wa Mkataba wa
Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi ambazo zinabainisha kiasi cha
uzalishaji wa gesijoto kutoka sekta mbalimbali husika na uondoshaji wake
kupitia misitu.
Balozi Sokoine aklibainisha kuwa hadi sasa Tanzania
imeandaa taarifa mara mbili na kuwasilisha Sekretareti ya Mkataba mwaka 2003 na
ya pili mwaka 2015 na kwa muda wote Tanzania kama ilivyokuwa kwa nchi nyingine.
Aliongeza kuwa Tanzania imetumia wataalamu elekezi
kufanya kazi hii chini ya Mradi uliokuwa unatekelezwa na Shirika la Maendeleo
la Umoja wa Mataifa (UNDP) kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais Idara ya
Mazingira hivyo kuleta ugumu katika kuthibiti ubora na kulinganisha takwimu za
nchi mbalimbali kwani hakukuwa na mfumo au njia iliyokubalika kimataifa kufanya
kazi na haikujenga uwezo wa sekta husika.
"Mfumo wa Kitaifa wa ukusanyaji na usimamizi
wa Takwimu za gesijoto, unaozinduliwa leo utawezesha nchi kutoa takwimu sahihi na za kutosheleza kuhusu
uzalishaji wa gesijoto kutoka sekta mbalimbali husika na uondoshaji kwa njia ya
misitu, kwa hatua sahihi za uamuzi na kutoa taarifa," alisema.
Aidha Balozi Sokoine alisema kuwa uzinduzi wa Mfumo
huu umekuja wakati muafaka ambapo tunajipanga kuanza utekelezaji wa Makubaliano
ya Paris ambayo yalipitishwa na Mkutano wa 21 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa
Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabinchi na Tanzania kuridhia Mei 2018.
Aliongeza kuwa kwa sasa Tanzania inakamilisha
maandalizi ya Mchango wake katika juhudi za kupambana na Mabadiliko ya
Tabianchi hivyo Mfumo huo utasadia katika upatikanaji wa takwimu na taarifa
kuhusu utekelezaji wa NDCs na
uandaaji wa Taarifa ya Tatu ya Mawasiliano.
" Utekelezaji wa Mfumo huu utahitaji kila mdau
kubaini majukumu yake na kuyatekeleza na hivyo kila mdau anatakiwa kubaini
majukumu yake kama yalivyobainishwa katika Mfumo ili kuhakikisha kuwa Mfumo huu unatekelezwa na
hivyo kutuwezesha kufikia malengo tarajiwa," alisisitiza Balozi Sokoine.
Naibu Katibu Mkuu aliagiza Kituo Cha Kitaifa cha
Kuratibu Hewa Ukaa (NCMC) kuratibu na kusimamia mfumo wa Kitaifa wa Ukusanyaji
Takwimu za Gesijoto, Ufuatiliaji, Uandaaji Taarifa na Uhakiki.
Aliagiza Wizara za
Kisekta ziteue Wataalamu watakaohusika na usimamizi na uandaaji wa takwimu za
uzalishaji wa gesijoto katika sekta zao na kuwasilisha kwenye Kituo cha Kitaifa
cha Kuratibu Hewa Ukaa.
Pia aliagiza Wizara za Kisekta kwa kushirikiana na
Kituo cha Kitaifa cha Kuratibu Hewa Ukaa ziweke Utaratibu wa kuwasilisha
taarifa katika Kituo cha Kitaifa cha Kuratibu Hewa Ukaa kila mwaka.na
kubainisha watoaji takwimu chini ya sekta zao za uzalishaji wa gesijoto na
kuweka utaratibu wa kupata takwimu hizo.
No comments:
Post a Comment