Habari za Punde

Mahenda Awashauri Wananchi Iringa Kuchangamkia Fursa za Utalii.


Mkurugenzi wa Qwihaya, Leonard Mahenda akiwaelekeza wananchi wa Iringa waliotembelea banda lake la maonyesho namna wanavyoandaa nguzo za umeme.

Na.Tumaini Godwin - IRINGA
Mkurugenzi wa Kiwanda cha Qwihaya kinachozalisha nguzo za Umeme mjini Mafinga, Leonard Mahenda amewataka wakazi wa mkoa wa Iringa na mingine iliyopo  Nyanda za Juu Kusini kuchangamkia fursa za utalii  zilizoanza kutangazwa kwenye maeneo yao ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Mahenda alisema hayo  wakati akizungumza na wananchi waliotembelea banda lake wakati wa maonyesho ya utalii wa kusini yanayoendelea kufanyika mjini Iringa.

Mahenda alisema zipo fursa nyingi zinazotokana na utalii ambazo kama watazitumia ipasavyo zinaweza kuwasaidia katika kujikwamua kiuchumi.

Aliipongeza Serikali kwa kuanzisha mkakati wa kutangaza vivuto vya utalii vilivyo kwenye mikoa hiyo kwa sababu vingi vilikuwa havijulikani licha ya kuwa vinaweza kuchangia katika kukua kwa pato la taifa.

Alisema kampuni hiyo imeweka  banda la maonyesho kwenye maadhimisho hayo kwa sababu kuna uhusiano mkubwa baina ya mazao ya misitu na utalii.

“Tumeamua kutumia vizuri hii fursa ya maonyesho kwa sababu bidhaa za misitu zinahamasisha utalii, sio tu kwamba zinaweza kutumika kwenye ujenzi wa hoteli na vitu vingine lakini zinahamasisha pia utunzaji wa mazingira,” alisema Mahenda.

Awali Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Enock Ugulumo amesema bado inahitajika nguvu kubwa zaidi kutangaza vivutio hivyo ili watalii waanze kumiminika kama wanavyojitokeza kwenye mikoa ya kaskazini.
“Tunaweza kufikia ndoto ya kuwa kitovu cha utalii kama kila mtu atashiriki kutangaza vivutio hivi, binafsi nimefarijika kuona maonyesho ya aina hii kwenye mikoa yetu niombe tu, mkakati huu usiwe zimamoto,” alisema Ugulumo.

Awali, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Ritha Kabati alisema vivutio vya utalii wa nyanda za juu kusini ni ndiyo nguvu ya uchumi na uanzishwaji wa viwanda kwenye mikoa hiyo ikiwa itatumia vizuri.

Utalii wa Nyanda za Juu kusini unaundwa na mikoa ya Iringa, Mbeya, Ruvuma, KatavI, Morogoro, Songwe na Rukwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.