Habari za Punde

Shehia 388 Kunufaika na Utekelezaji wa wa Mpango wa Kuhudumia Kaya Masikini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} Kisiwa cha Unguja kwa niaba ya Kamati Mbili za Visiwa vyote vya Zanzibar Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud wa kwanza Kulia akizungumza na Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 yanayounda Taifa la Nigeria waliowasili Nchini Tanzania kwa Ziara maalum.Kushoto kwa Mh. Ayoub Mohamed ni Mkurugenzi wa Uratibu wa Shughuli za SMT na SMZ anayesimamia Mfuko wa Tasaf upande wa Zanzibar Nd. Khalid Bakar  Amran.
Na.Othman Khamis. OMPR.
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Nchini Tanzania {TASAF} upande wa Zanzibar unatarajia kuzigusa Shehia zote 388 katika muelekeo wake wa utekelezaji wa Mpango wa kuhudumia Kaya Maskini  kwa Mwaka 2019/2020 Tasaf Awamu ya Nne.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} Kisiwa cha Unguja kwa niaba ya Kamati Mbili za Visiwa vyote vya Zanzibar Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud alisema hayo wakati akizungumza na Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 yanayounda Taifa la Nigeria waliowasili Nchini Tanzania kwa Ziara maalum.
Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud ambae pia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi aliwaeleza Waratibu hao waliofika Zanzibar kujifunza Mpango Maalum wa kuhudumia Kaya Maskini  kwamba Shehia zinazohudumiwa kwa sasa zimeshafikia 233 kati ya 388.
Alisema katika muelekeo huo hakutakuwa na Shehia hata Moja isiyoguswa katika masuala ya Kaya Maskini kazi itakayokwenda sambamba na mapitio ya Shehia ambazo kwa sasa zinaendelea kuhudumiwa kutokana na kuwa na sifa za kuingia katika Kaya Maskini lakini zilishindakana kutokana na ufinyu wa Bajeti katika Awamu iliyopita.
Mheshimiwa Ayoub alitanabahisha kwamba Mapitio hayo yatachambua katika kuzifanyia tathmini Shehia ambayo zilikuwa na Kaya Maskini lakini kwa sasa tayari zimeshakuwa Kiuchumi na kukosa sifa ya kuwa Kaya Maskini.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} Kisiwa cha Unguja aliwafahamisha Waratibu Wakuu hao wa Majimbo 36 ya Nigeria kwamba yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana katika uimarishaji wa Ustawi wa Jamii kupitia Mfuko wa Tasaf.
Alisema uundwaji wa Vikundi vya Kijamii katika Shehia mbali mbali za Visiwa vya Unguja na Pemba umesaidia kuibua Miradi tofauti iliyowezesha Wananchi Kiuchumi na hatimae kupiga hatua kubwa ya mapambano dhidi ya kuondokana na ukali wa Maisha.
Hata hivyo Mh. Ayoub alisema Sekta ya Kilimo imeleta faida kubwa ndani ya Mfuko wa Tasaf  ingawa bado zipo baadhi ya changamoto zinazowakazwa Wananchi katika maeneo yao hasa kwenye Sekta ya Afya na Elimu ambazo ndio kichocheo cha kuimarika kwa Ustawi na Maisha ya Jamii kwa ujumla.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} Unguja ameipongeza Timu ya Waratibu hao Wakuu wa Majimo 36 ya Nigeria kwa uamuzi wao wa kufika Zanzibar kujifunza muenendo mzima wa harakati ya maendeleo yanayotokana na Mfuko wa Tasaf.
Akitoa Shukrani zake Kiongozi wa Timu hiyo ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 yanayounda Taifa la Nigeria Naibu Mkurugenzi wa Taasisi inayosimamia masuala ya Ustawi wa Jamii Bwana Ortutu alisema ziara yao Nchini Tanzania imekuja kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika mpango wa kuhudumia Kaya Maskini.
Bw. Ortutu alisema Tanzania ni miongoni mwa Nchi chache Duniani zilizofanya  vizuri na kuchukuwa anafasi ya juu katika kuendeleza Mpango huo, huku Visiwa vya Zanzibar vikifanya vizuri zaidi ikilinganishwa na upande wa Tanzania Bara.
Alisema ujio wao wa kuja kujifunza Nchini Tanzania utawapa nafasi ya kuibua njia zitakazowasaidia kupata mbinu za muelekeo wa kupambana na changamoto zinazowakabili katika kutoa huduma kutokana na idadi kubwa ya Wakaazi wake zaidi ya Milioni 200 wanaoishi ndani ya Majimbo 36 ya Nchi hiyo iliyo Magharibi ya Bara la Afrika.
Mapema akitoa Taarifa Mwakilishi wa Mfuko wa Tasaf wa Kanda Bibi Saida Saleh Adam alisema zaidi ya Shilingi Bilioni 27 zimeshatolewa katika Mpango Maalum wa kuhudumia Kaya Maskini Unguja na Pemba.
Bibi Saida alisema fedha hizo zililengwa katika uimarishaji wa huduma za Afya na na Sekta ya Elimu katika kuwapatia mahitaji ya Vifaa Wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu ndani ya mpango wa stawisha Maisha Vijiji 20.
Ujumbe huo wa Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 ya Taifa la Nigeria walipata fursa ya kukagua Kituo cha Afya Kiyanga kilichojengwa kupitia mradi wa Kijamii ndani ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tasaf pamoja na kuona maeneo ya uzalishaji wa mazao ya viungo.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} Unguja ambae pia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed akisisitiza jambo wakati akizungumza na Waratibu hao.
Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 ya Nigeria na Waratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} wakijadiliana mambo mbali mbali yanayohusu mafanikio makubwa yaliyopatikana katika maendeleo ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf }.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} Unguja ambae pia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed kati kati waliokaa vitini akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 ya Nigeria waliowasili Nchini kwa ziara Maalum.

Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.