Habari za Punde

Wapongezwa Wasanifu Wahandisi na Wakadiriaji wa Majengo Kwa Nia Njema ya Kujadili na Kutafakari Changamoto za Upatikanaji wa Mchanga.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi   akilifungua Kongamano la Pili la Siku ya Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji Majengo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein katika Ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein alisema mabadiliko ya sera za Kiuchumi yaliyotokezea katika miaka ya Tisini yamepelekea ongezeko la kasi ya mabadiliko ya Ujenzi wa Majengo ya Nyumba za aina tofauti ambayo haikwenda na uwezo wa kifedha , kitaaluma na kiufundi wa Idara iliyohusika na Ujenzi.
Alisema mabadiliko hayo pamoja na mambo mengine  yalipunguza ukali wa ushuru wa Forodha na kuondoa vipingamizi vigumu katika uingizaji wa bidhaa na huduma zilizokubalika kisheria.
Dr. Ali Mohamed Shein alisema katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akilifungua Kongamano la Pili la Siku ya Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji Majengo lililofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Verde iliyopo Mtoni pembezoni mwa Mji wa Zanzibar.
Alisema hali hiyo imechangia kuwepo kwa udhibiti na usimamizi usioridhisha wa Ujenzi wa Majengo ya Serikali na hata ya Watu Binafsi hasa katika maeneo ya Miji ya Unguja na Pemba.
Dr. Ali Mohamed Shein alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imelazimika kukabiliana na tatizo hilo kwa kuunda Taasisi kadhaa za Ujenzi ikiwemo Bodi ya Usajili wa Wakandarasi, Wasanifu na Wakadiriaji Majengo iliyokwenda sambamba na kufuta Idara ya Ujenzi na badala yake kuanzisha Wakala wa Majengo katika Mwaka 2017 kwa lengo la kusimamia majengo.
Alifahamisha kwamba Maendeleo katika ujenzi ni jambo jema, kuwa na majengo mazuri na imara ya kisasa ni jambo la kujivunia kwa vile linaihakikishia Jamii usalama wa Wananchi na Mali zao na kunawirisha Miji ikiwa katika hali ya kuvutia.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha Miji Mipya ya Fumba na Nyamazi kwa kushirikiana na Mwekezaji Mzalendo, ukiwepo mwengine wa eneo la Kwahani.
Hata hivyo Dr. Shein alisema ipo changamoto ya namna gani Miji hiyo itaendelezwa kujengwa kutokana na upungufu mkubwa wa Rasilmali ya Mchanga hasa ikizingatiwa kwamba asilimia kubwa ya Ujenzi huo inatumia mchanga mwingi mno.
“ Wataalamu lazima mjitahidi kutafuta namna bora ya kupunguza matumizi makubwa ya mchanga katika majengo na kutafuta utaratibu wa mbadala wa mchanga”. Asisitiza Dr. Shein.
Waliwapongeza Wanakongamano hao Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji Majengo kwa nia yao njema ya kujadili na kutafakari changamoto kubwa ya Upatikanaji wa Mchanga Zanzibar hasa katika Kisiwa cha Unguja utaratibu ambao ni wa kiungana wa kusaidia kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.
“ Huu ndio utaratibu wa kiungwana wa kusaidia kutatua matatizo wanaloliona badala ya kukebehi au kulaumu  wanapendekeza njia ya kulitatua. Ahsanteni sana kwa moyo wenu huu wa Kizalendo na hongereni sana”. Alisisitiza Dr. Shein.
Rais wa Zanzibar alisisitiza kwamba hali ya mazingira ya uchimbwaji Mchanga katika Visiwa vya Zanzibar hasa Kisiwa cha Unguja haihimili tena ikiashiria kupuliza firimbi ya tahadhari kutokana na mifano kadhaa inayoonekana katika maeneo mbali mbali Nchini.
Alisema firimbi hiyo inaashiria madhara makubwa ya baadae iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa za kuvidhibiti vitendo vya uchimbaji mchanga usiozingatia utararibu yakiwa tishio kwa maisha ya Watu na mali zao.
Dr. Shein alieleza kwamba hivi sasa tatizo la uchimaji mchanga linatisha likiviathiri zaidi visiwa vidogo vidogo vikiwa hatarini kutokana na udogo wake unaopelekea kufurika kwa maji ya bahari hadi kupenya kwenye makaazi ya Watu na ndani ya mashamba.
Alisema takwimu zinaonyesha kwamba takriban maeneo 145 ya kilimo, yaliyomo katika Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na makaazi ya Watu, kama vile Msuka na Kisiwa Panza kwa Pemba yamevamiwa na Maji ya Bahari.
Alifahamisha kwamba hali hiyo sio kwamba inasababishwa na matukio ya kimaumbile pekee yake lakini kwa kiasi kikubwa inasababishwa na vitendo vya binaadamu wenyewe.
Dr. Ali Mohamed Shein alitahadharisha wazi kwamba Serikali Kuu kwa kuzingatia madhara ya maafa ya uchimbaji mchanga bila ya mpango ndipo ilipochukuwa hatua ya kuzuia uchimbaji holela kwa lengo la kuhakikisha matumizi mazuri ya ardhi kwa maslahi ya Wananchi wote.
Alisema Serikali inaelewa umuhimu wa mchanga katika matumizi tofauti ya ujenzi na ndio maana haikufunga moja kwa moja uchimaji na kuondoa dhana ya baadhi ya Watu kufikiria kwamba kulikuwa na dhamira ya kuwakomoa Watu bali ni kuweka utaratibu mpya wa upatikanaji wake kupitia Wizara ya Kilimo.
Dr. Shein alisisitiza kwamba utaratibu huo unatoa fursa kwa Makampuni na Wananchi kupata Rasilmali hiyo bila ya vikwazo na kwa bei iliyoelekezwa na Serikali ili kuondoa malalamiko ya wahitaji kuchelewa kupata bidhaa hiyo kwa bei kubwa.
Alisema Serikali kupitia Wiuzara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi itaendelea kufuatilia suala hilo ili kuwabaini wale wanaozikiuka taratibu zilizowekwa za bei halali ya Mchanga.
Dr. Shein ameuagiza Uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi  kuhakikisha kwamba Wananchi wanaifahamu bei halisi ya Mchanga iliyowekwa na Serikali ili kudhibiti kudhibiti uchimbaji ovyo wa mchanga.
Aliwaonya wale wenye tabia ya kupandisha bei ya mchanga hasa Madereva wa Magari ya Mchanga kwa visingizio mbali mbali waache mtindo huo kwani si vyema kutumia ujanja kwa kujiongezea kipato bila ya kujali hali za Wananchi wenzao.
Akizungumzia Bodi ya, Usajili wa Wasanifu,Wahandisi nas Wakadiriaji Majengo Zanzibar, Dr. Shein aliwataka Watendaji wa Taasisi hiyo kuwa mstari wa mbele katika kuzisimamia vyema Sheria zilizowekwa zinazohusiana na masuala ya  Ujenzi.
Dr. Shein alisemaBodi hiyo imepewa nguvu nyingi za Kisheria katika kusimamia na kuziendeleza shughuli zake na pale inapolazimika kuzitumia ili kuvikataa vitendo vinavyokwenda kinyume na taratibu zilizowekwa basi watekeleze matakwa ya kisheria bila ya kutetereka.
Alisema ni vyema wakaendelea kushirikiana na Taasisi mbali mbali zinazoshughulikia masuala ya Ujenzi na Mipango Miji,  Halmashauri pamoja na Serikali za Mitaa ambazo ni Taasisi muhimu katika ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
“ Andaeni utaratibu mzuri wa kufanya kazi kwa pamoja na mshirikiane na Taasisi hizo kwa kuzingatia kwamba Taasisi nyingi ni changa”. Alisitiza Dr. Shein.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitoa wito kwa Taasisi zinazojihusisha na shughuli za Ujenzi Nchini zihakikishe zinashirikiana na Bodi ya Usajili Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji Majengo kuwapa fursa Wanafunzi wa fani hiyo kufanya mazoezi ya vitendo katika kila miradi yao.
Mapema Mrajisi Bodi ya Usajili, Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji Majengo Zanzibar Bibi Hawa Khamis Mzee alisema Dira ya Bodi hiyo iliyoanzishwa kwa Sheria Nambari 5 ya Mwaka 2008 na kuanza kazi zake Mwezi Januari 2009 ni kuwawezesha Waalamu wa Sekta ya Ujenzi na Washauri wa Fani hiyo kuzingatia Ujenzi bora na salama kwa maendeleo ya Jamii.
Bibi Hawa alisema Bodi katika utekelezaji wa majukumu yake imepata mafanikio makubwa katika utendaji wake kwani muamko na mabadiliko makubwa katika ujenzi yamejitokeza chini ya usimamizi wa Uongozi wa Bodi hiyo kwa kuishirikiana na Taasisi nyengine za Ujenzi hapa Nchini.
Alifahamisha kwamba Bodi Bodi hiyo tayari imeshasajili Wataalamu 121 Zanzibar, 92 kutoka Tanzania Bara, 60 Wataalamu wa Kigeni, Wahitimu 181, Mafundi Sadifu 55.
Alisema kazi hiyo ilikwenda sambamba na usajili wa Kampuni zinazotowa Ushauri wa Ujenzi zipatazo 27 Zanzibar, 62 Tanzania Bara, zile za Kigeni 2 na kuifanya jumla ya Taasisi zote zilizosajiliwa hadi muda huu kufikia 600.
Bibi Hawa alifafanua kwamba Bodi hiyo tokea kuundwa kwake imepata fursa ya kukagua Miradi 1,696 na kugundua makosa mbali mbali  ikiwemo kukosekana kwa Michoro ya Ujenzi, kutosajiliwa pamoja na kukosekana kwa Wataalamu waliosajiliwa wa Ujenzi.
Mrajisi huyo wa Bodi ya Usajili, Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji Majengo Zanzibar aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati kwa kuanza kuipatia Ruzuku ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi mzuri.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi kwenye Kongamano hilo la Pili la Siku ya Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji Majengo, Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Zanzibar Mh. Salama Aboud Talib alisema hii ni mara ya kwanza kuwakusanya Wataalamu wa Ujenzi kutoka Taasisi za Umma na Binafsi kujadili suala linaloihusu Jamii.
Waziri Salama alisema Kanuni za Majengo ni muhimu kwa wakati huu kutokana na mabadiliko makubwa ya ujenzi yanayoendelea Nchini kwa kuhusisha Majengo marefu ambayo yanahitaji muongozo wa Kitaalamu.
Mheshimiwa Salama Aboud Talib alieleza kwamba muonekano wa Kimazingira kutokana na Majengo mengi yaliyojengwa Visiwani Zanzibar haukuzingatia Mipango Miji iliyokuwepo.
Katika Kongamano hilo lililojadili upungufu wa wa Mchanga , Changamoto na Fursa mbadala za Ujenzi zitakazotumika hapa Zanzibar Balozi Seif kwa Niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitoa vyeti kwa Wahitimu Bora wa Taasisi ya Ufundi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia.
Mapema Balozi Seif alitembelea na kuona Maonyesho ya Vitu na Bidhaa mbali mbali ya zilizotengenezwa na washirika wa Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji Majengo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.