Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Ali Mohamed Shein, akiwa katika mazungumzo na mgeni wake Naibu Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Nje Jamhuri ya Cuba Mhe.Marcelino Medina Gonzalez, yaliofanyika Ikulu Zanzibar leo,8, Septemba 2019.
JAMHURI ya
Watu wa Cuba imepongezwa kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha
sekta ya afya na kuelezwa haja ya kutoa nafasi za masomo ya Udaktari Bingwa kwa
Madaktari wa Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo wakati
alipofanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Kwanza
wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Watu wa Cuba Marcelino Medina
Gonzalez, Ikulu mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Shein alizipongeza
juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Cuba katika kuimarisha uhusiano na
ushirikiano wa kihistoria uliopo ikiwa ni pamoja na kuiunga mkono Zanzibar
katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya afya.
Hivyo, Rais Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo
kuwa Zanzibar inathamini sana mashirikino hayo yaliopo hasa katika sekta ya
afya ambapo nchi hiyo imo katika mashirikiano na Zanzibar ya kusomesha Madaktari
ambapo tayari kuna Madaktari 15 wa Zanzibar wanasoma nchini humo hivi sasa
katika Chuo Kikuu cha Mantanzas.
Kutokana na juhudi hizo, Rais Dk. Shein alieleza
haja ya kuendelezwa mashirikiano zaidi kwa Jamhuri ya Watu wa Cuba kutoa nafasi
ya masomo ya Udaktari Bingwa kwa Madaktari wa Zanzibar hasa ikizingatiwa kuwa Chuo
Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimeshaanza kutoa wahitimu mabali mbali wa
fani hiyo.
Aidha, Rais Dk. Shein aliipongeza Cuba kwa kuendelea
kushirikiana na Zanzibar kwani pande mbili hizo zina historia kubwa hasa
ikizingatiwa kuwa nchi hiyo ni miongoni
mwa nchi za mwanzo kuyatambua Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.
Alieleza kwamba mbali ya Cuba kuiunga mkono
Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya, elimu na sekta nyenginezo pia, Rais
Dk. Shein alisisitiza haja ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano katika sekta
ya utalii hasa ikizingatiwa kuwa Cuba imepiga hatua kubwa katika sekta hiyo.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza mafanikio
makubwa yaliofikiwa na Cuba katika sekta ya utalii hasa katika eneo la Ukanda
wa Utalii unaojulikana kwa jina la Varadero, ambao unavivutio kadhaa vya
kitalii zikiwemo hoteli za kisasa za hadhi ya juu, maeneo ya kihistoria na
fukwe za kuvutia.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa
Jamhuri ya Watu wa Cuba na Tanzania ikiwemo Zanzibar ni marafiki wa damu ambapo
urafiki wao huo umekuwa ukiimarika kila uchao hivyo kuna kila sababu za
kuuimarisha zaidi kwa manufaa ya pande zote mbili.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kumueleza kiongozi huyo jinsi ya Muungano uliopo kati ya Zanzibar na
Tanganyika ambao uliasisiwa Aprili 26 mwaka 1964 kuwa ni wa kihistoria na
wapekee hadi hivi sasa kwa nchi za Bara la Afrika.
Nae Naibu Waziri wa Kwanza wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Watu
wa Cuba Marcelino Medina Gonzalez alimueleza Rais Dk. Shein jinsi ya nchi yake
inavyofarajika na uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na
Zanzibar na kuahidi kuuendeleza.
Naibu Waziri Conzalez ambaye alifuatana na Balozi
wa Cuba katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Profesa Lucas Domingo Hernades alimueleza
Rais Dk. Shein kuwa ujio wake hapa Zanzibar umezidi kutoa fursa ya kuendelezwa
kwa mashirikiano katika sekta mbali mbali za maendeleo ambapo umeweza
kuwakutanisha na viongozi kadhaa na hatimae kujadiliana juu ya sekta hizo.
Alisema kuwa miongoni mwa sekta hizo ni sekta ya
afya, elimu, utalii, kilimo na biashara ambapo alisisitiza kuwa iwapo
mashirikiano zaidi yataendelezwa kupitia sekta hizo mafanikio zaidi yataendelea
kupatikana kwa pande zote mbili.
Kiongozi huyo alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa
Jamhuri ya Watu wa Cuba itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha
sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuendeleza mashirikiano ya kuwasomesha
madaktari wazalendo nchini Cuba katika vyuo vyake mbali mbali kikiwemo Chuo
Kikuu cha Mantanzas.
Sambamba na hayo, Naibu Waziri huyo aliyapongeza
mapokezi mazuri aliyoyapata hapa nchini na kusisitiza kuwa Jamhuri ya Watu wa
Cuba inathamini uhusiano na ushirikinao na Jamahuri ya Watu wa Tanzania katika nyanja
zote zikiwemo za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Alieleza kuwa mbali ya uhusiano katika nyanja za
kiuchumi na kijamii, pia, Jamhuri ya Watu wa Cuba ina mlahaka mzuri kati ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Kikomunisti cha Cuba (CPC) na kuahidi
kuwa mahusiano yaliopo yataendelezwa kama walivyoanzwa na waasisi wa Mataifa
hayo.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment