Habari za Punde

Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Yakanusha Taarifa Iliosambazwa Katika Vyombo Vya Habari Kuhusu Wanafunzi 350 Waacha Kwa Utoro na Mimba.


                                   JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
                                   HALMASHAURI YA WILAYA YA TUNDURU
(Barua zote zipitie kwa Mkurugenzi Mtendaji) 
 MKOA WA RUVUMA                                                                     MKURUGENZI MTENDAJI  
SIMU NA: 2680004                                                                              S.L.P 275,                 
FAX NA: 2680208                                                                                TUNDURU
Website:    www.tundurudc.go.tz
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KUKANUSHA TAARIFA ZA VYOMBO VYA HABARI KWAMBA WANAFUNZI 350 WA WAACHA SHULE KWA UTORO, MIMBA

Tunduru 30, Oktoba 2019.
Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma inapenda kukanusha habari ya upotoshaji  iliyotolewa na Gazeti la Habari Leo la tarehe 28 Oktoba 2019 na Kituo cha Televisheni cha ITV ikisomeka kuwa “Wanafunzi 350 waacha shule kwa utoro, mimba,”  habari hii haina ukweli wowote kama ilivyoripotiwa.
Tunapenda kuuarifu umma kuwa baada ya kuwepo kwa taarifa hiyo Ofisi ya Mkurugenzi imefanya ufuatiliaji wa kina katika Shule ya Sekondari Marumba ambayo imetajwa katika habari hiyo iliyosema kuwa wanafunzi 350 wa shule hiyo wameshindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya utoro na mimba kwa kipindi cha miaka minne mfululizo  kuanzia mwaka 2016 hadi 2019.
Ni vyema umma ukafahamu kuwa katika kipindi cha miaka minne yaani 2016 hadi 2019, shule hii ilipangiwa idadi ya wanafunzi 603 ikiwa wavulana 320 na wasichana 283, waliosajiliwa kwa kipindi hicho ni wanafunzi 515 ikiwa pungufu ya wanafunzi 88 kati ya waliopangwa.
Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya wanafunzi waliopo katika shule ya Sekondari Marumba hadi kufikia tarehe 28/10/2019 ni 345 ikiwa wavulana 208 na wasichana 137 kukiwa na upungufu wa wanafunzi 170.
Akitoa ufafanuzi huo Mkurugenzi Mtendaji Halmasahuri ya Tunduru Gasper Balyomi amesema hii ni wazi kuwa idadi ya wanafunzi 350 wa sekondari ya Marumba walioripotiwa hawajulikani walipo hazina ukweli wowote kufuatia takwimu zilizotolewa na kubaini kuwa:-
1.    Kwa kipindi cha miaka minne mfululizo jumla ya wanafunzi 20 walihama kwenda katika shule nyingine.
2.    Wanafunzi 15 waliacha masomo baada ya kupata ujauzito
3.    Wanafunzi 63 waliacha masomo kutokana na sababu mbalimbali
4.    Wanafunzi 72 waliopewa nafasi ya kurudia masomo baada ya kufeli  kidato cha pili  baadhi yao wazazi waliamua kuwapeleka katika vyuo vya Ufundi stadi kama  (VETA) na shule binafsi.
Hivyo kufanya jumla ya wanafunzi 170 kwa kipindi cha miaka minne ndio hawapo shuleni tofauti na taarifa ilivyoonesha jumla ya wanafunzi 350 wa shule hiyo wameacha masomo.
Aidha kuhusu suala la utoro wa reja reja Halmshauri inaendelea kushirikiana na wazazi pamoja walezi wa wanafunzi katika kuahikisha utoro mashuleni unadhibitiwa.

Imetolewa na
Kitengo cha Habari na Mawasiliano
Halmashauri ya Tunduru


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.