Wasanii wa kundi hilo la UDOM wakiwa jukwaani wakati wa onesho lao usiku wa kuamkia leo kwenye tamasha la 38 la Sanaa Bagamoyo.
Na.Andrew Chale. Bagamoyo.
Kikundi cha sanaa cha Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) kimekonga nyoyo mashabiki na wadau wa burudani usiku wa kuamkia leo katika tamasha la 38 la Sanaa na Utamaduni.
Katika tukio hilo waliweza kuonesha ngoma ya muheme ya kabila la Wagogo ambayo ni ngoma ya unyago wanayopigiwa watoto wa kike wanaokua.
Mmoja wa wanafunzi wa UDOM, Maro Materego akielezea aina ya ngoma hiyo waliocheza, ambapo alifafanua kuwa, ngoma hiyo inapigiwa wasichana katika masuala ya unyago.
“Ngoma hii inapigiwa mwisho wa mafunzo ya unyago kwa mabinti waliomaliza mafunzo yao. Kuonesha kuwa yupo tayari kwa ajili ya kuolewa ndio anapigiwa hiyo ngoma na kwa hiyo wanaume wengi wenye ng’ombe ndio wanajitokeza ili kupata bahati yake ya kuoa binti hao waliomaliza mafunzo” alieleza Maro
Aidha, akiongelea kuhusu mti unaotengenezea ngoma hiyo, alisema ni mti aina ya muheme ambao unachongwa kisha kuwambwa na ngozi ya kenge ili kuweka ladha ya mapigo.
Wanafunzi hao wa UDOM wamebainisha kuwa, ngoma hii ya Muheme ni matokeo ya mafunzo ya vitendo ambayo wameyapata wakiwa chuoni na ya wakufunzi hao Profesa Froini Nyoni, Dkt. Asha Salm na Dk. Dogratius Ndungulu.
Chuo hicho kwa mwaka huu ndio mara ya kwanza kushiriki kufanya onesho kwenye tamasha kubwa kama hilo la TaSUBa.
Tamasha hilo kwa mwaka huu limedhaminiwa na wizara ya Maliasili na Utalii kupitia tamashak lake la Urithi Wetu, Road to Freedom (Germany), Clouds Plus, PSS, Classic fm, tsn, Habari Leo, Mtanzania, Mlimani TV, Michuzi Media Group,EDP.TBC, ACTO LIGHT, Oceanic Bay, Fullshangwe na wengine wengi.
No comments:
Post a Comment