Habari za Punde

TANZANIA YAKABIDHIWA URAIS WA AALCO


Waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi, Dkt.Augustine Mahiga, akifurahia jambo na Katibu Mkuu wa Shirika la Mashauriano ya Kisheria kwa nchi za Asia na Afrika(AALCO), Prof. Kennedy Gastorn na   Mkurugenzi Mkuu wa Sheria za Kimataifa kutoka Nigeria, Mhe.Wilfred Ikatari

Na. Paschal Dotto-Maelezo Dar es Salaam.                                                                           
Shirika la Mashauriano ya Kisheria kwa Nchi za Asia na Afrika (AALCO) ambalo kikao chake cha 58 kimemalizika hapa Jijini Dar es Salaam safari hii kimeteua Tanzania kuwa Rais wa Shirika hilo na kwa maana hiyo Waziri wa Katiba na Sheria Tanzania, Balozi Augustine Mahiga anashika nafasi hiyo.

Kikao hicho kilichoanza jumatatu, wiki hii kimemalizika leo naajenda mbalimbali zilijadiliwa huku msukumo ukilenga kuimarisha sheria za ukanda wao na Kimataifa kwa Ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari Waziri wa Katiba na Sheria kutoka Tanzania ambaye ameanza wadhifa wake Rais Mpya wa AALCO amesema kuwa katika mfululizo wa vikao vyao kitu  kikubwa kilichojadiliwa ni suala la vikwazo dhidi ya mataifa ambalo limekuwa tatizo kwa nchi mbalimbali.

“Mkutano huu ulikuwa unaangazia masuala mbalimbali na muhimu kwa nchi za Afrika na Asia na kwingineko duniani na suala ambalo lililpewa kipaumbele ni kuhusu vikwazo ambavyo nchi mbalimbali kubwa duniani zimekuwa zikiziwekea nchi ndogo, kitu ambacho kinaumiza wananchi katika nchi hizo”, amesema, Balozio Mahiga.

Balozi Mahiga, amesema kuwa Mkutano huo ambao washiriki wake ni kutoka Asia na Afrika unazingatia masuala mengi ya kisheria, likiwemo lile la  vikwazo kwa nchi kama za Zimbabwe, Palestine, Iran na nyinginezo duniani.

Alieza kuwa suala la kuweka vikwazo halijadiliwi na nchi moja , wala mbili au tatu ambazo ni kubwa na kuwa zinajiweza kiuchumi, bali suala hilo ni la Chombo cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na hufikiwa ikiwa kuna wasiwasi wa kiusalama kwa nchi moja hiyo inayowekewa vikwazo, kwa hiyo suala la vikwazo lilikuwa kipaumbele kwenye mkutano wa AALCO.

Aidha Mkutano huo wa 58 wa AALCO ulijadilii mambo mengine sita, likiwemo lile la matumizi na utajiri ulioko baharini, rasilimali kama vile  mafuta, madini na samaki ambavyo vinahitajika sana duniani, “kwa hiyo lilikuwa ni jambo jema kujadili vitu hivyo muhimu kwa nchi za Afrika na Asia.” Amesema Rais wa AALCO.

“katika Mkutano huu wa AALCO tumezungumza na kubadilishana mawazo kuhusu utajiri ulioko kwenye bahari, ambapo kila mmoja anautaka, hivyo tunatakiwa tuweke sheria nzuri na vyombo vya kisheria ambavyo vitatufanya kutumia vitu hivyo bila kugongana sehemu” Balozi Mahiga.

Aliongeza kuwa katika masuala saba yaliyojadiliwa, suala la vikwazo na matumizi ya bahari ni busara kuyajadili hayo katika majukwaa mbalimbali ikiwemo AALCO; ili kuiambia dunia kuhusu kukua kwa maendeleo ya Sheria za Kimataifa.

Tanzania itakuwa Rais wa AALCO kwa muda wa mwaka mmoja, ambapo Mkutano wa 59 unaotarajiwa kufanyika Bara la Asia, Nchini China, ambapo  Tanzania itakabidhi kiti hicho kwa China.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.