Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mwanahamisi Munkunda akielezea
mtawanyiko wa huduma za jamii katika wilaya wakati wa maonesho ya ramani za
huduma za jamii za wilaya hiyo pamoja na maeneo ya kuhesabiwa watu kwa Sensa ya
Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Mrasimu ramani kutoka NBS Jerve Gasto akiwaonesha
viongozi wa Halmashauri ya Bahi, wageni waalikwa wakiwemo wadau Maendeleo
maeneo ya kuhesabia watu katika halmashauri hiyo.
Na.Said Ameir.
Shiriki la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya
Watu (UNFPA) na Benki ya Dunia zimeeleza kuendelea kusaidia uzalishaji wa
Takwimu nchini ikiwemo Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.
Taasisi hizo zimetoa ahadi hiyo wiki hii wakati wa
hafla ya Kutangaza Matokeo ya Zoezi la Kutenga Maeneo katika Wilaya ya Bahi na
Uzinduzi wa Kitabu cha Taarifa za Kiuchumi na Kijamii cha Halmashauri ya Bahi
kwa Mwaka 2019 huko Bahi mkoani Dodoma.
Naibu Mwakilishi wa Shirika la UNFPA nchini Dk.
Wilfred Ochan alieleza kuwa shirika lake linaisaidia Tanzania sio tu katika
maandalizi ya awali ya Sensa bali katika uchambuzi wa data, kutoa matokeo hadi
kuyasambaza matokeo hayo ya Sensa kwa wadau.
Alibanisha kuwa shirika lake lina historia ya muda
mrefu ya ushirikiano na Tanzania katika kutekeleza Sensa za Watu Makazi pamoja
na uzalishaji wa Takwimu nyingine.
“UNFPA inajivunia mchango wake katika mafaniko ya
Tanzania kutekeleza Sensa za Watu na Makazi katika miongo iliyopita, katika
kuimarika kwa uwezo wa Tanzania wa kuzalisha takwimu za msingi na zile tafiti
za kitakwimu zinazowahusu wananchi” Dk. Ochan alieleza.
Aliongeza kuwa
anaamini fika kuwa kutokana na uzoefu wa Ofisi za Takwimu nchini (NBS na OCGS),
sifa za kitaaluma walizonazo watumishi wa Ofisi hizo pamoja dhamira na utashi
wa serikali, Sensa ya mwaka 2022 itakuwa ya mafanikio makubwa.
Dk. Ochan alieleza
kuwa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 itakuwa ya kipekee kwa kuwa kwa mara
ya kwanza Tanzania itatumia tekinolojia mpya za kisasa tangu maadalizi ya
mwanzo hadi mwisho wa utekelezaji wake.
“Matumizi ya
simu janja, vishikwambi (tablets) na mifumo ya inayotumia mitandao katika
kuhesabu watu ambayo ni sehemu ya mapinduzi ya data katika mukhtadha wa Sensa
za miaka 2022 naamini kila mmoja wetu atakuwa anajivunia kuona sehemu ya
mapinduzi haya yanaongozwa na Ofisi yetu ya Taifa ya Takwimu” Mwalikishi huyo
alieleza.
Kabla ya
uzinduzi huo viongozi wa wilaya ya Bahi wakiongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo Mwanahamisi Munkunda, wageni waalikwa wakiwemo wadau
wa Maendeleo waliangalia ramani zinazoonesha mtawanyiko wa huduma mbalimbali za
jamii katika wilaya hiyo pamoja na ramani za kuhebia watu kwa ajili ya Sensa ya
Watu na Makazi ya Mwaka 2022.
Kwa upande wake, Benki ya Dunia imeahidi kuendelea kuisaidia Tanzania kuimaisha
maendeleo mfumo wa Taifa wa Takwimu nchini.
Bi Elizabeth Talbert aliyeiwakilisha benki hiyo katika
hafla hiyo alieleza kuwa benki hiyo imekuwa mstari wa mbele kuisaidia Tanzania
kuimarisha mfumo wa taifa wa Takwimu.
“Tunashirikiana na Tanzania katika miradi na programu
mbali mbali za maendeleo katika sekta nyingi ikiwemo uimarishaji wa sekta ya
Takwimu” Alisema Bi Talbert.
“Ramani tulizozishuhudia hapa zinaeleza picha halisi
ya hali ya huduma za jamii katika wilaya hivyo zinasaidia kutuongoza katika
mikakati yetu ya kusaidia wilaya hii” alisema mwakilishi huyo.
Bi Talbert aliwapongeza watumishi wa NBS na OCGS kwa
kazi nzuri wanayoifanya katika kutenga maeneo na uzalishaji wa ramani hizo na
kusisitiza kuwa kufikia Agosti, 2019 ni lazima nchi nzima iwe imegawanywa
katika maeneo ya kuhesabia watu ili Sensa ifanyike kwa muruwa.
“Tumeona hapa kazi nzuri na kubwa iliyofanywa kwa
wilaya hii. Fikirieni kuna wilaya ngapi hapa Tanzania Bara na Zanzibar.
Tunataka kila mtu ahesabiwe mwaka 2022. Hakuna kumuacha mtu nyuma” Alisisitiza
Mwakilishi huyo wa Benki ya Dunia Elizabeth Talbert.
Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina
Chuwa alieleza kuwa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ina umuhimu wa
kipekee kwa kuwa Takwimu zitakazokusanywa zitatumika kupima mafanikio ya Dira
ya Maendeleo 2025 na Utkelezaji wa Malengo Endelevu ya Dunia Mwaka
2030”Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa.
No comments:
Post a Comment