Habari za Punde

Uwajibikaji unahitajika kampeni ya kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi

Na Ramadhani Ali -  Maelezo                         
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashidi Mohamed amewataka Viongozi wa siasa, Wafanyakazi na Wananchi wote kuwajibika kwa vitendo katika kuhakikisha Kampeni ya kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi inafanikiwa.
Alisema Zanzibar inauwezo mkubwa katika kuhakikisha hakuna mwanamke anaefariki kwa matatizo ya kujifungua iwapo kila mmoja atatekeleza wajibu wake ipasavyo.
Waziri Hamad alieleza hayo katika Ukumbi wa Idrissa Abdul Wakil Kikwajuni alipokuwa akizindua Kampeni hiyo iliyoenda sambamba na uzinduzi wa Mkakati wa miaka mitano ya afya ya uzazi ya mama na mtoto pamoja na uzinduzi wa boti ya dharura kwa wajawazito watakaopata matatizo wakati wa kujifungua kwenye visiwa vidogo vidogo vya Pemba.
Alisema pamoja na kuwa idadi ya vifo vya akinamama wakati wa kujifungua na watoto wachanga vimepungua lakini bado vinaendelea kutokea na juhudi za pamoja zinahitajika.
Waziri wa Afya aliweka wazi kuwa baadhi ya vifo hivyo vinatokana na ushirikiano mdogo ndani ya familia, kutowajibika kikamilifu kwa baadhi ya watoa huduma katika vituo vya kujifungulia na kuchelewa kuwahishwa Hospitali mzazi inapopata matatizo ya kuzaa.
Aliwashauri akinababa kuwapa ushirikiano na kuwa karibu zaidi na wake zao wakati wa ujauzito hadi wakati wa kujifungua na kushiriki kikamilifu katika zoezi la kwenda kliniki ili wote kwa pamoja waweze kujua afya zao.
Aliwataka madaktari na watoa huduma za uzazi katika vituo vya kujifungulia kuhakikisha wanatumia vizuri rasilimali zilizopo na kuhakikisha zinatumika vizuri .
Akizungumzia kuwepo kwa boti itakayotoa huduma kwa wazazi watakaopata matatizo katika visiwa vidogo vya Pemba, Waziri wa Afya aliweka wazi kuwa boti hiyo itatumika kwa dharura na kitu cha msingi wanawake wanapopata ujauzito ni kuhakikisha wanajiwekea kinga kujiepusha na matatizo wakati wa kujifungua.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Asha Juma Abdalla alieleza kuwa katika kuhakikisha vifo vinavyotokana na uzazi vinapungua, Serikali imeongeza vituo vya kuzalisha kufikia 47 na baadhi ya vituo hivyo vinatoa huduma kwa saa 24 katika siku zote saba za wiki.
Alisema Hospitali na vituo vyote vya afya vinavyotoa huduma za kuzalisha zimewekwa vifaa muhimu, wafanyakazi wenye ujuzi na  dawa za kutosha ili kuhakikisha vifo vinavyotokana na uzazi na watoto wachanga vinapungua na hatimae vinaondoka kabisa.
Mwakilishi mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA) Jacqueline Mhon alisifu uwajibika bora wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa wananchi wake katika kuhakikisha usalama wa mama wajawazito wakati wa kujifungua na watoto wachanga.
Alisema kutokana na uwajibikaji huo Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo, inasaidia Serikali katika utekelezaji wa dira 2020, Mkakati wa kupunguza umaskini (MKUZA 111) kwa lengo la kufikia malengo ya Maendeleo endelevu na ajenda ya Afrika 2063 katika sekta ya afya.
Aliweka wazi kuwa huduma za afya ya mama na watoto ni moja ya njia ya kuwekeza katika kujenga taifa lenye watu wenye afya bora wenye uwezo wa kukuza ukuaji wa uchumi.
Kaulimbiu katika Kapeni ya kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi  ni  ‘ Vifo vya uzazi vinaepukika. Wajibika maneno basi, sasa vitendo’.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.