WAZEE wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Kusini Pemba wamempongeza Makamu Mwenyekiti
wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM
ya mwaka 2015-2020 kwa vitendo.
Kwa nyakati tofauti wazee hao waliyasema hayo katika
mikutano ya Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar ambaye pia, ni Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyoifanya
katika Mkoa huo.
Wazee hao wa Mkoa huo walieleza kuwa juhudi alizozichukua
Rais Dk. Shein katika kutekeleza kwa vitendo na kwa kasi kubwa Ilani ya
Uchaguzi ya mwaka 2015-2020 ni za kupigiwa mfano kwani mafanikio yaliopatikana
ni makubwa.
Walieleza kuwa Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar ameweza kuiletea maendeleo makubwa Zanzibar ikiwa ni
pamoja na kuiimarisha na kuiendeleza miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya
maji, elimu, afya, miundombinu ya barabara, usafiri na usafishaji, ujenzi wa
ofisi za Serikali.
Waliongeza kuwa maendeleo makubwa yameendelea kupatikana
chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein katika ujenzi wa barabara zenye viwango,
upandishaji wa bei za karafuu, fedha za kila mwezi kwa wazee wa umri wa miaka
70 ambao miongoni mwao wanafaidika, ongezeko la fedha kwa wastaafu na uwekaji
wa umeme na maji salama katika visiwa vya Unguja na Pemba na mengineyo.
Pamoja na hayo, wazee hao walieleza hatua anazozichukua
Rasi Dk. Shein katika kuwajengea uwezo vijana, wanawake sambamba na kuwawekea
mazingira mazuri wazee wa Unguja na Pemba abapo wazee hao walitumia fursa hiyo
kumuahidi kushirikiana nae bega kwa bega.
Wazee hao walimpongeza Rais Dk. Shein na kueleza kuwa
kitendo cha kwenda kukutana nao ni kielelezo kuwa anawajali na kuthamini juhudi
zao ama mchango wao ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha, wazee hao walimpongeza Rais Dk. Shein kwa jinsi
alivyoweza kudumisha amani na utulivu nchini jambo ambalo limemfanya aweze
kutekeleza kwa ufanisi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.
Wazee hao pia, walitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk.
Shein kwa kuendelea kuyaenzi Mapinduzi matukufu ya Zanzibar kwa vitendo kwa
kuendeleza kwa kasi matunda yake kama vile kuendeleza huduma za afya na elimu
bure kwa wananchi.
Sambamba na hayo, wazee wa Makongwe kwa upande wao walitoa
pongezi zao za pekee kwa Rais Dk. Shein kwa kuwapelekea umeme katika kisiwa
hicho ambapo wananchi wa kisiwa hicho
wamekuwa wakifaidika na huduma hiyo muhimu katika maisha ya mwananadamu ikiwa
ni pamoja na kufanya biashara kwa ufanisi mkubwa.
“Tunafahamu kuwa hichi ni kipindi chako cha kumalizia muda
wa uongozi wako kwa nafasi ya urais ahadi yetu kwako tutakuwa na wewe bega kwa
bega kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinaendelea kushika Dola na
kuwaletea maendeleo wananchi wote”, walieleza wazee hao wa CCM wa Mkoa wa
Kusini Pemba.
“Sisi Wazee tunakutakia kila la kheri katika maisha yako
Mwenyezi Mungu akuzidishie hekma uvumilivu na upendo kwa unaotuongoza
tutaendelea kuchota na kufuata nyayo zako katika yote mazuri kutoka kwako sisi
pamoja na vizavi vyetu”, waliongeza wazee hao.
Nae Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein
ameeleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kununua boti mpya ili
kuwasaidia wananchi wakiwemo wazee wanaoishi katika visiwa vidogo vidogo vya
Unguja na Pemba waweze kuvuka kwa uhakika.
Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar tayari imeshaanza mchakato huo ambao utakapokamilika utawasaidiaa kwa
kiasikikubwa wananchi wanaoishi visiwani.
Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alivitaja visiwa sita
ambavyo vimelengwa kupata boti hizo mpya na za kisasa ili ziwe msaada mkubwa
kwao katika kuwasaida kuwavusha kikiwemo Kisiwa Panza, Makongwe, Fundo, Uvinje,
Kokota na Tumbatu.
Aidha, Rais Dk. Shein amesisitiza haja ya kufanya kazi pamoja
na wazee kwani ni watu muhimu sana katika jamii ambao bado mchango wao
unahitajikakatika maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Alisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini
na inazijali juhudi za wazee walizozichukua hadi kupelekea kupatikana kwa uhuru
wa Tanganyika na uhuru wa Zanzibar kupitia vyama vya siasa vya ASP na TANU
wakati huo.
Rais Dk. Shein alisema kuwa miongoni mwa mambo ambayo wazee
waliyapakipaumbele ni kujitolea na ndio maana uhuru kwa Tanganyika na Zanzibar ukapatikana
pamoja na mambo mengine makubwa ya kujenga nchi yaliyofanyika baada ya
kupatikana uhuru huo ambayo hayo yote yalitokanana falsafa ya kujitolea.
Katika mazungumzo hayo na wazee wa Mkoa wa Kusini Pemba ambapo
Mama Mwanamwema Shein alishiriki kikamilifu, Dk. Shein alisema kuwa CCM ndio
chama kinachowatetea wanyonge hivyo, ni lazima kitegemee nguvu za wanachama
wake katika kufikia malengo yao waliyoyakusudia ikiwa ni pamoja na kuendelea
kuongoza Dola na kuwaletea maendeleo endelevu wananchi wote.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi
alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) bado kinaendelea kuwatunza, kuwaenzi na
kuwathamani wazee na ndio maana wameingizwa katika taratibu zote za chama
hicho.
Aliongoza kuwa hikma za kuwaenzi wazee zimeanza kabda ya
Mapinduzi chini ya Jemedaru Hayati Mzee Abeid Amani Karume na hadi hivi leo
hikma na busara hizo zinaendelea kutumika ikiwa ni pamoja na kuwatuza wazee
wote wa Unguja na Pemba tena bila ya ubaguzi.
Nao viongozi wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba walieleza
kufarajika kwao na juhudi za makusudi anazozichukua Rais Dk. Shein katika kuwahudumikia
wananchi wa Zanzibar wakiwemo wazee ambao amewawekea mazingira mazuri katika
maisha yao jambo ambalo bado nchini nyingi ndani nan je ya Bara la Afrika
halijafanya la kuwapatia wazee waliotimia umri wa miaka 70 pencheni jamii kwa kila mwezi.
Viongozi hao walitumia fursa hiyo kwa kumpongeza Rais Dk.
Shein kwa kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment