Na. Eleuteri Mangi,
WHUSM, Dodoma
Serikali imesema kuwa
Idhaa ya External Service iliyokuwa inarushwa na Radio Tanzania Dar es Salaam
ilianzishwa mahususi wakati wa harakati za kupigania uhuru.
Kauli hiyo imetolewa
leo Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
michezo Juliana Shonza alipokuwa akijibu swali Na. 38 na Mbunge Taska Restituta
Mbogo (Viti Maalum) alilotaka kujua ni kwa nini TBC ilifuta kipindi cha External
Service kilichokuwa kikitangaza taarifa ya habari kwa Lugha ya Kiingereza na
kwa kutangaza taarifa ya habari kwa Kiswahili tu tunawanyima wageni fursa ya
kujua kinachoendelea nchini.
Miongoni mwa mataifa
yaliyonufaika na Idhaa ya External Service ya Radio Tanzania Dar es Salaam ni
nchi za Kusini mwa Afrika ikiwemo, Msumbiji, Zimbabwe, Namibia, Angola, Afrika
ya Kusini.
Naibu Waziri Shonza
amesema kuwa viongozi wa wapigania uhuru katika nchi hizo waliishi na kuratibu
harakati za ukombozi katika nchi zao kutokea Tanzania ambapo walirusha
matangazo ya Radio ya kuhamasisha wananchi wao kushiriki katika mapambano hayo
kupitia idhaa hiyo ya External Service na haikuendelea kurusha matangazo yake
baada ya nchi hizo kupata uhuru.
“Ni kweli kwamba kwa
kutangaza taarifa ya habari kwa lugha moja ya Kiswahili kunawanyima wageni
fursa ya kujua masuala mbalimbali yanayoendelea hapa nchini. Lakini yapo
magazeti mbalimbali yanayochapisha habari hizo hizo zinazotokea nchini kwa
lugha ya Kiingereza ambapo inawarahisishia kupata habari hizo kupitia magazeti
ya Daily News, The Guardian pamoja na The Citizen.”
Aidha, Naibu Waziri
Shonza aliongeza kuwa kwa sasa TBC kupitia stesheni ya TBC International
inayopatikana katika masafa ya 95.3, hutangaza kwa lugha ya Kiingereza hatua
inayowafanya wageni kuendelea kupata habari na taarifa za mambo mbalimbali
yanayoendelea nchini.
Zaidi ya hayo, Naibu
Waziri Shonza alisisitiza kuwa TBC1 na
TBC Taifa zinarusha baadhi ya vipindi kwa Kiingereza ikiwemo vipindi vya “This
Week in Perspective” na “International Sphere” na TBC Taifa ina vipindi
“Breakfast Express”, “Daily Edition”, “Day Time” na Overdrive kwa Kiingereza
ambapo vipindi hivi huzungumzia masuala mbalimbali yakiwemo ya kisiasa,
kiuchumi pamoja na kijamii.
Akijibu swali la nyongeza
lililoulizwa na Wabunge Kakoso Selemani (Mpanda Vijijini), Deogratias Ngalawa
(Ludewa) na Sikudhani Chikambo (Viti
Maalum) kuhusu usikivu wa TBC, Naibu Waziri Shonza amesema kuwa Serikali inaendelea
na mpango wa kupanua usikivu maeneo yote nchini ambapo usikivu umeongezeka kutoka
wilaya 87 mwaka 2017 sawa na asilimia 54 ambapo hadi Machi 2019 wilaya 102 zimefikiwa
na matangazo ya radio ambayo ni sawa na asilimia 63.
Maeneo ambayo
Serikali imefanyia marekebisho ni pamoja na ujenzi wa vituo vitano katika
wilaya za mpakani za Rombo, Tarime, Kibondo, Kakonko, Namanga, Nyasa hadi
Mbambabay umekamilika ambapo wilaya za Ruangwa, Lushoto na Mtwara ambazo
usikivu wake ulikua hafifu umeimarika na mkakati wa Serikali ni kujenga mitambo
ya Redio katika mikoa ya Katavi, Simiyu, Unguja, Pemba, Njombe, Songwe na
Lindi.
Kuhusu makakati wa
kukuza Kiswahili kama moja ya lugha nne rasmi za nchi za Jumuiya ya Maendeleo
ya Kusini mwa Afrika (SADC), Naibu Waziri Shonza amesema kuwa Baraza la
Kiswahili la Taifa kupitia mkakati wake wa miaka mitano 2015/2016 hadi
2019/2020 limejizatiti kutumia fursa hiyo likilenga kuimarisha fani ya tafsiri
na ukalimani kutoka na kwenda Kiswahili pamoja na kuendelea kuwa mdau muhimu wa
maendeleo na matumizi ya Kiswahili Afrika ya Mashariki, Afrika na duniani kote.
No comments:
Post a Comment