Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Uongozi na Wafanyakazi wa ZBC Redio katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo Zanzibar, kushoto Waziri wa Habari Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar.Mhe.Mahmoud Thabit Kombo,Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar. Bi. Khadija Bakari na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.Mhe Hassan Khatib Hassan.
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameutaka uongozi
wa Shirika la utangazaji Zanzibar (ZBC) kuwa na mipango madhubuti ya kuwapatia
mafunzo wafanyakazi wake ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Dk.Shein amesema hayo wakati alipokuwa akitoa ufafanuzi kwa
Viongozi na wafanyakazi wa Shirika hilo (ZBC Redio) juu ya hoja mbali mbali
zilizoibuliwa katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Utamaduni Rahaleo,
Mjini hapa.
Alisema kuna umuhimu mkubwa kwa uongozi wa shirika hilo kuwa na
mipango madhubuti ya muda mfupi na mrefu, itakayowawezesha wafanyakazi hao
kupata mafunzo ndani na nje ya nchi, na hivyo kuliwezesha shirika hilo kupata
wataalamu wanaohitajika katika kuliendeleza.
Alisema ni jambo jema kwa uongozi huo ukandaa mipango hiyo
kuambatana na vitengo vilivyopo na kuwapatia fursa hizo wafanyakazi bila ya maombi au kufanya upendeleo wowowte.
Aidha, alitaka kuwepo uwiano kati ya Uongozi wa Shirika hilo,
Wizara na Bodi ya Shirika katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali
zinazojitokeza, akibainisha kuwepo mapungufu katika kushughulia masuala hayo hivi
sasa.
Vile vile alitaka kufanyika juhudi katika upatikanaji wa
nyenzo, ikiwemo fedha za kujikimu, usafiri na vifaa ili kufanikisha kazi pale
waandishi wanapotoka nje ya vituo vyao
vya kazi kwa ajili kutafuta habari.
Rais Dk. Shein alisema Wizara kwa mashirikiano na taasisi zake
inapaswa kuwa na vipaumbele vya mahitaji kutoka katika vitengo vyake vyote na hivyo kutatuwa
changamoto zolizopo kwa mujibu wa bajeti ya fedha zitakazopatikana.
Vile vile Dk. Shein alitowa rai kwa uongozi wa Wizara na ZBC
kuwaruhusu bila vikwazo wafanyakazi wote
wanaohitaji uhamisho wa kwenda taasisi nyeingine ya Serikali, pale panapokuwa
na makubaliano kati ya Taaasisi moja na nyingine.
Katika hali hiyo, Dk. Shein alisema ni jambo jema kwa Viongozi
hao kuwajengea mazingira bora na kuvutia wafanyakazi wao ili waendelee kubaki
katika maeneo yao ya kazi, na kuainisha kuwa pale wanapotoka kuondoka, basi ni
vyema wakaruhusiwa bila vikwazo.
Katika hatua nyengine, Dk. Shein alisema ZBC ni Shirika jipya
la Serikali lililoundwa kwa lengo la kuimarisha huduma za Utangazaji nchini ili
kuchochea maendeleo.
Alisema Bodi ya ZBC ina jukumu kubwa la kusimamia na
kuliongoza Shirika hilo ili kufikia mafanikio yaliolengwa.
Alisema madhumuni makubwa ya serikali kuziunganisha taasisi za
Redio na Televisheni umezingatia wafanyakazi wote wa vyombo hivyo kuwa wamoja
na wenye maingiliano ya karibu katika utendaji wa kazi zao.
Alisema Shirika hilo lina malengo yalio sawa na mashirika
mengine ya Kimataifa kama vile DW, BBC, Aljazeera na mengineyo, yakitofautiana
na ZBC kutokana na uwezo wake wa
kiutendaji.
Alieleza kuwa Shirika hilo lina kazi kubwa ya kufanya mbele
yake ili kufanikisha malengo yaliokusudiwa pamoja na kushinda vikwazo mbali
mbali vinavyozorotesha maendeleo.
“Kazi ya kulifanya Shirika
hilo kupata mafanikio sio ya kufumba na kufumbua, bali inahitaji muda
mwingi2, alisema.
Alisema Serikali imegharamika sana katika uundaji wa Shirika
hilo kwa kutumia zaidi ya shilingi Bilioni 17 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na
mitambo, hivyo akasistiza umuhimu wa ZBC, Bodi na Wizara kushirikiana, sambamba
na kuitaka Bodi kufanyakazi ya kuwatumikia na kuwaunganisha wafanyakazi,pamoja
na kuwashajiisha kufanya kazi zao kwa bidii.
“……..hayo mashirika makubwa , nayo yamepita katika hali hii
hii kwa taabu, kujenga ni kazi kubwa na mimi ninavyoliona shirika hili litafanikiwa sana”, alisema.
Alisema hivi sasa Shirika hilo bado linategemea ruzuku kutoka serikalini katika
upatikanaji wa mahitaji mbali mbali kwa ajili ya wafanyakazi wake, ikiwa pamoja
na vifaa.
Akigusia historia ya Utangazaji Zanzibar, Dk. Shein alisema
Zanzibar ina mengi ya kujivunia, akibainisha kuwepo wafanyakazi wengi kutoka
nchi mbali mbali za Afrika Mashariki na Duniani kwa ujumla waliokuja nchini
kujifunza.
Mapema,
Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulahamid
Yahya Mzee, akitoa ufafanuzi wa masuala mbali mbali alisema, Serikali inatowa
kipaumbele kwa jamii ya watu wenye ulemavu pale zinapotokea fursa za ajira na
kuwepo watu wengine wenye sifa zinazofanana.
Aliwataka
watu wenye ulemavu kuwasilisha malalamiko yao serikalini pale wanapobaini
taratibu za ajira kuvunjwa, pamoja na kuwataka waajiri kuisaidia ajmii hiyo kutokana na hali zao.
Alisema
Serikali imekuwa ikiwashajiisha wafanyakazi kusoma na kuwataka kuondokana na
utamaduni wa kukimbilia vyuo vya nje katika
aina ya masomo ambayo vyuo vya ndani vinafundisha.
Alisema
Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma, imeamuwa kuwa an mfuko wa kuwaendeleza
kitaaluma watumishi wa serikali, sambamba na kuzitaka taasisi zote kutenga
fedha kwa ajili ya kusomesha wafanyakazi wao.
Akigusia
suala la uhamisho wa wafanyakazi kutoka taasisi moja kwenda nyingine, Dk.
Abdulahamid alisema kinachohitajika ni makubaliqno kati ya taasisi mbili na kubainisha
pale panapokosekana makubaliano, Katibu Mkuu Kiongozi ndie mwenye dhima
ya kutoa maamuzi kwa maslahi ya Taifa.
Aidha,
alitoa ufafanuzi juu ya Posho la mazingira magumu na kusema kuwa kila
mfanyakazi anapaswa kutambua aina ya kazi na changamoto zake pale anapoajiriwa.
Alisema
Serikali tayari imetowa madaraja kwa kila shirika, hivyo kila mfanyakazi wa
shirika linalohusika atapaswa kupata posho kulingana na aina ya daraja la
shirika analofanyia kazi.
Nae,
Waziri wa Habari, Utamaduni na Mambo ya kale, Mahamoud Thabit kombo, aliwataka
Viongozi wa Vitengo vilivyomo ZBC kukaa
pamoja na kuyatafutia ufumbuzi matatizo yanayojitokeza na pale inaposhindikana
kuyatuma uongozi wa juu kwa hatua.
Alisema
uongozi wa Wizara hiyo utaendelea kusimamia vikao vya ngazi za chini za uongozi
ili kutatuwa matatizo mbali mbali yaliojitokeza ikiwemo uchakavu wa majengo na mahitaji ya vifaa
mbali mbali vyenye gharama nafuu.
Akizungumzaia
suala la mafunzo kwa wafanyakazi, alisema hatua zinaendelea kuchukuliwa ,
kukiwa na matarajio makubwa ya kupatikana fursa hizo pamoja na kuongeza idadi
ya mafundi kupitia vijana wapya watakaosomeshwa kwa kuzingatia wale wachache
waliopo wako njiani kustaafu.
Vile
vile, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni na Mambo ya Kale, Khadija Bakari
alitowa wito kwa wafanyakazi kutekeleza majukumu yao kuambatana na maadili,
silka, kanuni na miongozo ya Utumishi wa Umma.
Abdi Shamna,
Ikulu Zanzibar
Postal
Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822
E-mail: abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment