Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Joseph Sokoine akizungumza
katika kikao na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi kuhusu mifuko mbadala aina
ya 'non-woven' isiyokidhi viwango ambayo imebuka na kutumika kinyume cha
sheria.
Na.Robert Hokororo
Serikali imeanza msako wa kuwabaini waingizaji na
wazalishaji wa mifuko mbadala aina ya 'non woven' isiyokidhi viwango
vilivyowekwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) vya chini ya GSM 70.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Joseph Sokoine amesema hayo wakati akizungumza na waandishi
wa habari jijini Dodoma ambapo alisisitiza kuwa mifuko inayotakiwa lazima iwe
na jina la mzalishaji, uzito na mawasiliano ya mzalishaji.
Sokoine alisema kuwa kumezuka wimbi la mifuko
isiyokidhi viwango vilivyowekwa hivyo matokeo
yake wale ambao wameitikia wito wa kufungua viwanda vya mifuko mbadala wanakosa
soko.
"Elimu kwa umma itaendelea kutolewa ili watu
wajue mifuko ipi hairuhusiwi kutumika na hii itasaidia wazalishaji wa mifuko
inayokidhi viwango kupata masoko na kuweza kuisambaza hadi kule kwenye changomoto
na bei itakuwa ya kawaida ili kila mtu aweze kununua," alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa
la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka alisema kuwa
zoezi la katazo la mifuko ya plastiki kupitia Kikosi kazi cha Taifa limefanikiwa
kwa kiwango kikubwa.
Dkt. Gwamaka alisema kuwa kuanza sasa vifungashio
vya plastiki vya katoni za maji havitaruhusiwa na kuwa badala yake yatumike
maboksi kwani yanaweza kurejelezwa hivyo ni rafiki wa mazingir huku akiongeza
kuwa magazeti hayaruhusiwi kufungashia bidhaa zikiwemo vyakula kama nyama kwani
ni hatari kwa afya zikiwemo magonjwa ya kansa
Alisema kwa sasa mifuko hiyo imeondolewa lakini bado
kuna changamoto ya vifungashio kugeuzwa vibebeo huku akionya viwanda vya
vinavyojihusisha na uzalishaji wake.
"TBS imeshatoa kanuni za namna gani mifuko
mbadala inayozalishwa lakini bado tunaona mifuko hii inazalishwa kwa wingi na tunajua
bayana lazima mifuko hii iwe na GSM 70 ili kuwalinda lakini wale tunaowalinda
wanazalisha usiku wanapeleleka sokoni sasa Serikali haijalala tumeanza msako wa
kuwabaini na tutawachukulia hatua," alionya.
Aidha Mkurugenzi huyo alisema kuwa tayari kikosi
kazi hicho kimekamata kiwanda kinachozalisha mifuko hiyo kilichopo jijini Dar
es Salaam na kupiga faini huku akitoa rai kwa wananchi kutoa taarifa pindi
wanapoona viwanda kama hivyo na kuwa itatolewa zawadi kwao.
No comments:
Post a Comment