Habari za Punde

Wahandisi ujenzi wa barabara kuzingatia vyema kazi zao

  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwasisitiza Wahandisi wa ujenzi wa Bara bara kuzingatia umakini kwenye sehemu za Madaraja ili kuepuka mafuriko
 Msimamizi wa Ujenzi wa Bara bara ya Bububu hadi Mkokotoni Mhandisi Ismail Ibrahim Kulengwa akimuonyesha Balozi Seif Ramani ya Kituo cha Magari kitakachojengwa Mkokotoni
 Msimamizi wa Ujenzi wa nyumba za Maafa Nungwi Mhandisi Ernest Mambangula akimkaguza Balozi Srif sehemu mbali mbali ya Nyumba zitakazokabidhiwa Wananchi waliopatwa na Maafa katika Kisiwa cha Unguja
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Watoto wa Kijiji cha Matemwe alipofanya ziara ndani ya Wilaya ya Kaskazini “A”.
Picha na – OMPR – ZNZ.

NA Othman Khamis OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Wahandisi wa Miradi ya Ujenzi wa Bara bara Nchini wanapaswa kuzingatia vyema kazi zao hasa kwenye maeneo yenye mteremko unaoishia kwenye Madaraja ili kuzuia athari zinazoweza kuwapata Wananchi wanaoishi jirani na sehemu hizo.
Alisema  upo uzoefu mkubwa unaojitokeza kwenye maeneo yenye Madaraja makubwa wakati wa msimu wa mvua za masika kukumbwa na maji mengi yanayoishia katika makaazi  ya Wananchi wanaoishi karibu na Madaraja baada ya mafuriko ya madaraja hayo.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo hapo Mkokotoni wakati alipofanya ziara ya kukagua  maendeleo ya ujenzi wa Bara bara ya Bububu hadi Mkokotoni ambapo kuridhika na kazi kubwa iliyofikiwa ya uimarishaji wa Miundombinu ya Ujenzi huo.
Alisema Wahandisi wa Miundombinu ya Ujenzi wana jukumu la kukahikisha Maisha ya Wananchi yanakuwa salama katika makaazi yao  ili kuipa nafasi  Serikali Kuu pamoja na Taasisi zake kushughulikia masuala mengine badala ya nguvu kubwa kuitumia katika kuihudumia Jamii kwenye majanga yanayoweza kuepukwa mapema.
Mapema msimamizi wa Ujenzi wa Bara bara hizo Mhandisi Ismail Ibrahim Kulengwa alisema Mradi wa Ujenzi huo wa Bara bara Nne katika Kisiwa cha Unguja unaohusisha Kilomita 52 unatarajiwa kukamilika Mwezi Febuari Mwaka 2020 ukiwa tayari umeshafikia asilimia 63%.
Mhandisi Kulengwa alisema Bara bara ya Bububu hadi Mkokotoni pekee hivi sasa ujenzi wake umeshafikia asilimia 80% unaotazamiwa kukamilika Mwezi Januari Mwakani ukihusisha Madaraja 14, kati ya hayo Mamane Makubwa na sita yaliyobakia ni ya kati.
Alisema Kilomita 26 kati ya 31 za Bara bara hiyo ya Mkokotoni hadi Bububu tayari imeshawekewa Lami huku kazi ikiendelea hivi sasa itakayokwenda sambamba na uwekaji wa vyuma katika maeneo ya Daraja pamoja nay ale yenye mteremko mkubwa.
Baadae Balozi Seif aliangalia maendeleo ya ujenzi wa Nyumba watakazopewa Wananchi waliokumbwa na Mafuriko zinazojengwa na kusimamiwa na Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar.
Msimamizi wa Ujenzi wa nyumba hizo Mhandisi Ernest Mambangula alimueleza Balozi Seif kwamba ujenzi huo uko katika hatua nzuri licha ya kipindi hichi kusubiri Mabati kwa ajili ya uwezekaji ili kukamilisha kazi hiyo.
Mhandisi Ernest alisema kila Jengo litakuwa na uwezo wa kuhudumia Familia Mbili zitakazobahatika kupata vyumba Vitatu, jiko, Sebule, Jiko, pamoja na huduma muhimu za Kibinaadamu ikiwemo vyoo.
Naye Naibu Mkurugenzi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Muhidini Ali Muhidini alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Mradi huo unatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa Serikali ifikapo Mwezi Januari Mwaka 2020.
Nd. Muhidini alisema licha ya harakati hizo na maendeleo makubwa ya ujenzi wa Mradi huo lakini zipo changamoto zinazoweza kuleta athari hapo baadae iwapo hazitachukuliwa hatua mapema.
Alisema changamoto hizo alizitaja kuwa ni pamoja na kutokuwepo kwa Bara bara  ya kudumu inayoingia katika eneo hilo pamoja na umuhimu wa kuwepo kwa uzio wa kulizunguuka eneo hilo linaloonekana kwa sasa dalili za baadhi ya Watu kujenga majengo ya kudumu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.