Habari za Punde

Elimu Kwa Watu Wenye Ulemavu wa Kutokusikia Inahitajika Pale Wanapofikwa na Tatizo.

Na Mwashungi  Tahir      Maelezo     23-12-2019.
Mkurugenzi Mtendaji Kamisheni ya Maafa Ndg.Makame Khatib Makame amesema elimu kwa watu wenye ulemavu wa kusikia wanahitaji kupewa mafunzo ya lugha za alama ili waweze kujinusuru pale wanapofikwa na tatizo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Ulemavu Abeida Rashid  huko kwenye Ukumbi wa Tume ya Uchaguzi ulioko Maisara wakati wa kufunga mafunzo ya  Lugha ya Alama kwa walemavu wa kusikia.

Amesema elimu hiyo ni ya lazima kupatiwa watu hao kwa lengo la kukuza lugha ya alama na kuweza kutumika kwenye jamii na kuwalinda ili wanapofikwa na madhara na waweze kufahamika.

Pia amesema mafunzo hayo yanatoa mwanga kwa kuweza kuelewa ili kutoa ushahidi mahakamani pale watu hao  wanapofikwa na vitendo viovu hasa vitendo vya udhalilishaji ambavyo vimekithiri nchini.

“Mafunzo haya ya lugha ya alama nakutakeni muyatumie vizuri ili muweze kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu wa kusikia pale wanapofikwa na vitendo viovu ikiwemo vya udhalilishaji hasa panapotakiwa kutolewa ushahidi”, alisema Mkurugenzi huyo.

Aidha amesema Serikali inaangaliya fursa kutoa lugha za alama na imekuwa na sasa inatumika sehemu nyingi ikiwa sehemu za mikutano, katika  Baraza la Wawakilishi  na sehemu nyingi zinazotumiwa na jamii.

Hata hivyo aliwaomba watoaji wa mafunzo  kukamilika kwa mafunzo hayo isiwe mwisho bali iwe endelevu  yazidi kuendelezwa na kutoa mafanikio zaidi.

Nae mwanafunzi wa mafunzo  hayo Fatma Said Khamis  akisoma risala ameitaka Serikali ione umuhimu wa kutupatia mafunzo ya ulemavu wa kusikia  ili kuweza kuhudumia jamii na kuisaidia wanapofikwa na matatizo.

Amesema wanaomba mafunzo hayo  yawe endelevu kwa Serikali na binafsi ili waweze kutumia taaluma kwa watu wenye ulemavu wa kusikia kwa kuhakikisha  wanapatiwa haki zao.

Pia amesema  wameweza kufarijika kwa kupatiwa mafunzo hayo ya lugha za alama na kupata muamko wa kutoa huduma kwa jamii.

Hivyo wameishukuru Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais na Idara ya Watu wenye Ulemavu kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo watayafanyia kazi na kuwa walimu kwa wenzao.

Kwa upande wake mshiriki wa dawati la jinsia Mkoa wa Kaskazini Unguja Salum  Khamis Machano  amesema mafunzo haya ya lugha za alama kwa watu wenye ulemavu wa kusikia yataweza kuwasaidia hususan wahanga wanaokumbwa na vitendo vya udhalilishaji.

Mafunzo hayo ya siku kumi yamewashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo  Jeshi la Polisi,Mahkama,Wanasheria na Dawati la Udhalilishaji.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.