Habari za Punde

KATIBU MKUU UTUMISHI AGIZA UANZISHWAJI MADAWATI YA JINSIA ELIMU YA JUU.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora Dkt. Francis Michael akizungumza na Wakuu wa vyuo vya elimu ya juu waliokutana kujadili namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia katika vyuo vya elimu ya juu wakati akifunga kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma.
Picha na Mpiga Picha Wetu

Na Mwandishi Wetu Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora Dkt. Francis Michael ameziagaiza Menejimenti za Vyuo vya Elimu ya juu kuhakikisha wanatekeleza agizo la Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alilolitoa wakati akifungua Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa  kijinsia la kuanzisha madawati ya jinsia katika Vyuo vya hivyo.

Dkt. Francis ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifunga kikao kilichowakutanisha Wakuu wa Vyuo vya elimu ya juu kilichojadili namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia katika maeneo ya Vyuo vya elimu ya juu nchini.

Dkt. Francis  ameongeza kuwa tatizo la ukatili wa kijinsia limekuwa likishamiri katika Vyuo vya elimu ya juu hivyo amezitaka Menejimenti za Vyuo vya Elimu ya juu na Vyuo Vikuu Vishiriki kuhakikisha wanaweka Mikakati ya kupambana na vitendo ya ukatili wa kijinsia kwa upana wake.

Amesema kuwa Menejimenti ya vyuo ina wajibu wa kuhakikisha vyuo husika vinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Kanuni au Sheria na taratibu kwa kuhakikisha wanazalisha wataalam bora na wenye weledi wa kutosha ili waweze kulisaidia taifa katika kuleta maendeleo.

"Mkatekeleze maagizo haya na nitafuatilia kuona utekelezaji wake na mmefikia wapi, hatuwezi kuvumilia masuala haya hata kidogo yanaharibu picha ya Vyuo vyetu na taifa" alisema Dkt Francis.

Aidha Dkt. Francis amewataka wakuu wa Vyuo hao kuhakikisha watumishi wa vyuo hivyo wanafanya kazi kwa kuzingatia kanuni na Sheria zilizopo kwa kuwa waadilifu na kuhakikisha wanaepukana na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wanaume ikiwa ni ukatili wa kihisia, kimwili au ukatili wa kitandao.

Pia Dkt. Francis amewataka Wakuu wa vyuo hao kuhakikisha wanafunzi wa watumishi wanatii Sheria na kanuni zilizopo ili kuwezesha Taasisi za Elimu ya juu nchini kutimiza malengo yake iliyowekewa na iliyojiwekea kwa ufanisi mkubwa na kuwezesha kuondokana na vitendo vya kikatili na kujenga mazingira yaliyosalama katika vyuo hivyo.

Kwa upande wake Afisa Mwandamizi Mkuu kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania TCRA Bw. Semu Mwakyanjala amesema kuwa Taasisi hiyo imejipanga kupambana na tatizo la vitendo ya ukatili wa kijinsia hasa wa mitandaoni na tayari baadhi wa watuhumiwa wameshafikishwa mahakamani kutoka na kufanya vitendo vya kikatili mitandaoni kwa kuweke picha na maudhui yasiyofaaa na yanayoumiza watu kihisia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.