Habari za Punde

Maafisa Habari kuweni vinara katika kutangaza habari za serikali


Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Juliana Shonza akizungumza alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa awamu ya pili ya mafunzo ya Mawasiliano ya Kimkakati kwa Maafisa Habari kutoka wizara, taasisi, mashirika ya  umma  na halmashauri nchini leo tarehe 02 Desemba 2019 Jijini Dodoma.          

Na Anitha Jonas & Shamimu Nyaki - WHUSM Dodoma.
Naibu Waziri Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza amewataka Maafisa Habari nchini kuwa vinara katika kutangaza shughuli mbalimbali za serikali  ikiwemo miradi inayotekelezwa.

Mhe.Shonza ametoa kauli hiyo leo Jijini Dodoma alipokuwa akifungua mafunzo ya awamu ya pili ya Maafisa Habari nchini yanayofanyika kwa siku tano yenye lengo la kuwajengea uwezo.

‘Katika kutangaza habari za serikali kwa umma kila Afisa Habari ni lazima kutumia vyanzo vyote kusambaza habari ikiwemo mitandao ya kijamii kwa sababu inasambaza habari kwa haraka zaidi na kufikia watu wengi,’alisema Mhe.Shonza.

Akiendelea kuzungumza katika ufunguzi huo Naibu Waziri Shonza alisisitiza kuwa kwasasa waandishi wa habari  wanatakiwa kuwa na elimu kulingana na Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 kwani tasnia hii inatakiwa kuondokana na makanjanja.

Kwa Upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi amesisitiza kuwa Maafisa Habari wanapaswa kuandika na kutangaza habari za kimkakati zinazotekelezwa na serikali ili wananchi wafahamu maendeleo yanayofanywa na serikali.

"Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kutangaza shughuli mbalimbali za serikali lakini wapo baadhi hawafanyi vizuri na ndiyo maana tumeona tuwape mafunzo haya ili kurekebishana  katika utendaji,"alisema Dkt.Abbasi.

Naye Katibu wa Chama cha Mawasiliano Serikalini (TAGCO) Bw. Abdul Njaidi amesihi Maafisa hao kuzingatia elimu watakayoipata katika mafunzo hayo ili waweze kutangaza vizuri utekelezaji wa Serikali katika maeneo yao.

Pamoja na hayo mmoja wa Maafisa Habari  Bibi.Nuru Mfaume kutoka  Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda alitoa shukrani zake kwa Msemaji Mkuu wa Serikali na uongozi wa TAGCO kwa mafunzo hayo ambayo yatawaongezea ujuzi.

"Kweli kabisa mafunzo haya yametusaidia kujitathimini utendaji wetu na kugundua makosa yetu na baada ya hapa hakika kutakuwa na mabadiliko katika utendaji ikiwemo uandishi wa habari zetu"alisema Bibi.Nuru.

Mafunzo hayo yanahudhuriwa na Maafisa Habari mia moja kutoka Wizara,Taasisi,Mashirika,Mikoa na Halmashauri za Tanzania Bara ambapo mada mbalimbali zitatolewa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.