Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein akitoa nasaha zake mara baada ya kulizindua Rasmi Jengo Jipya la Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amezidua nyumba ya
makaazi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na kupongeza juhudi kubwa zilizochukuliwa
katika ujenzi wa nyumba hiyo.
Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hafla fupi ya
uzinduzi wa nyumba ya makaazi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza iliopo, Isamilo Jijini
Mwanza.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alisema kuwa ujenzi huo
wa nyumba ya makaazi ya Mkuu wa Mkoa huo yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika
kuhakikisha makaazi ya kiongozi huyo yanakuwa bora zaidi.
Alieleza kuwa juhudi hizo zilizochukuliwa katika ujenzi wa nyumba
hiyo ya kisasa pia, itasaida kwa wageni watakaomtembelea Mkuu huyo wa Mkoa wa
Mwanza pamoja na yeye mwenyewe kuishi na familia yake.
Rais Dk. Shein alipongeza juhudi zilizochukuliwa katika
kuhakikisha nyumba ya Mkuu wa Mkoa iliyokuwa hapo kabla kwenye mtaa wa Machemba,
Isamilo hivi sasa imegeuzwa Ikulu Ndogo.
Hivyo, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza
wananchi wa Mwanza kwa kupata Ikulu Ndogo kwenye nyumba hiyo ambayo kwa maelezo
ya Rais Dk. Shein ina historia kubwa.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi
wa Mkoa huo pamoja na Mkandarasi wa nyumba hiyo.
Mapema Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Christopher Kadio akitoa
taarifa ya ujenzi wa nyumba hiyo alimueleza Rais Dk. Shein kuwa mradi wa ujenzi
huo ulianza kutekelezwa katika bajeti ya mwaka 2017/2018 baada ya nyumba
aliyokuwa akiishi Mkuu wa Mkoa huo kubadilishwa matimizi na kuwa sehemu ya
Ikulu Ndogo.
Aidha, alisema kuwa Mkataba wa ujenzi ulisainiwa tarehe 13
Juni, 2017 kati ya Mkandarasi Wakala wa Majengo (TBA) na Katibu Tawala wa Mkoa
wa Mwanza kwa gharama ya TZS Milioni 660.
Aliongeza kuwa Mkataba wa ujenzi huo ulihusisha ujenzi wa
nyumba kuu, nyumba ya wasaidizi, ujenzi wa uzio pamoja na kibanda cha walinzi.
Katibu Tawala huyo alieleza kuwa Mkandarasi alianza ujenzi mwezi
Septemba 2017 baada ya malipo ya awali ya kiasi cha fedha TZS milioni 150
zilizokuwa zimepangwa kwa ajili ya
ukarabati wa iliyokuwa nyumba ya Mkuu wa Mkoa na kubadilishwa kuwa Ikulu Ndogo.
Hata hivyo, kwa maelezo ya Katibu Tawala huyo baada ya
ongezeko la gharama za vifaa vya ujenzi Mkandarasi aliongezewa kiasi cha fedha
TZS milioni 50 kukamilisha shughuli za ujenzi wa uzio na ununuzi wa baadhi ya
vifaa.
Sambamba na hayo Katibu Kadio alieleza eleza kuwa kwa sasa
ujenzi wa mradi huo umekamilika kwa zaidi ya asilimia 99 ambapo kazi ya ujenzi
wa kibanda cha walinzi bado haujakamilika na unatarajiwa kukamilika hivi
karibuni.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Dk. Severine Mathias Lalika
kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuwazinduliwa
jingo lao hilo na kusema kuwa ujio wake umewasaidia kwa kiasi kikubwa katika
kuhakikisha ujenzi huo unakwenda kwa kasi na kufikia malengo yaliokusudiwa.
Hafla hiyo pia, ni miongoni mwa shamrashamra za sherehe za
kuadhimisha miaka 58 ya Uhuru wa Tanzania Bara na miaka 57 ya Jamhuri Tanzania
Bara.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment