RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali zao zote mbili
ile ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kuidumisha amani na utulivu kwa kipindi chote cha mwaka 2019.
Rais Dk. Shein
aliyasema hayo leo katika risala yake aliyoitoa kwa wananchi kupitia vyombo vya
habari katika kuukaribisha mwaka mpya wa 2020, risala aliyoitoa huko ofisini
kwake Ikulu mjini Zanzibar.
Katika risala yake
hiyo, Rais Dk. Shein alisema kuwa wananachi wameonesha mapenzi makubwa, umoja
na mshikamano baina yao na miongoni mwa wageni wanaokuja kuitembea nchini.
Aliongeza kuwa amani,
utulivu na umoja vilivyoendelezwa vimewezesha kuitekeleza mipango ya maendeleo
kwa mafanikio makubwa ambapo umepelekea uchumi wa Zanzibar kuendelea kukua kwa
asilimia 7.1 kwa mwaka 2018 ikilinganishwa ma asilimia 6.8 kwa mwaka 2016.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa hali ya amani na utulivu iliyopo nchini imeongeza mshikamano na mapenzi
baina ya wananchi na kusisitiza kuwa nchi iko salama na kila mwananchi anafanya
shughuli zake bila ya bughudha.
Aliongeza kuwa hali ya
amani na utulivu imechangia katika kuimarika kwa sekta ya utalii ambapo watalii
na wageni mbali mbali walitembelea Zanzibar katika mwaka 2019 ambapo jumla ya
watalii 477,579 walitembelea Zanzibar katika kipindi cha Januari hadi Novemba
2019.
Alieleza kuwa
kuimarika kwa amani na utulivu nchini pia, kulipelekea Taasisi na Mashirika
mbali mbali ya Kikanda na Kimataifa yalivutiwa sana kuja kufanya mikutano yao
hapa Zanzibar katika mwaka 2019 ukiwemo Mkutano wa Jumuiya ya Majaji na
Mahakimu wa Afrika Mashariki, (EAMJA) Mahakama ya Afrika ya Haki za Binaadamu
na Watu na Mkutano wa Wabunge wa Jumuiya ya Madola.
Alisema kuwa
utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2020 ya Zanzibar ambayo sambamba na Ilani
ya Uchguzi Mkuu ya CCM ya 2015/2020 umefanyika kwa ufanisi na kupelekea
kukaribia kukifikia kiwango cha chini cha nchi za kipato cha kati cha USD 1,040
kwa mujibu wa vigezo vya Kimataifa.
“Tumemaliza mwaka bila
ya shida yoyote ya upatikanaji wa bidhaa za chakula na bidhaa nyengine muhimu
kwa maisha ya kila siku ya wananchi wa Zanzibar”,alisema.
Aidha, alisema kuwa
miongoni mwa mafanaikio makubwa yaliopatikana katika mwaka uliopita ni
kuimarika kwa sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji ambapo jitihada za Serikali na
wakulima zimewezesha kupata mafanikio makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuongeza
mavuno ya mazao ya chakula hasa mpunga, mboga, na matunda.
Alisema kuwa kwa mwaka
2018/2019 wakulima walivuna tani 47,507.1 za mpunga kutoka tani 39,682.7 mwaka
2017/2018 ambapo mafanikio hayo kwa jumla yamewezesha kujitosheleza kwa chakula
kwa asilimia 60 kutoka asilimia 51 mwaka 2011.
Kwa upande wa sekta ya
uvuvi, Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali imeanza hatua za awali za kuanzisha
Kampuni ya Uvuvi ya Zanzibar (ZAFICO), kushika nafasi ya Shirika la Uvuvi
lililokuwepo kabla.
Alisema kuwa mwaka
2019 boti ya kisasa ya uvuvi inayoitwa SEHEWA II imenunuliwa kwa TZS Bilioni
1.33 na tayari Kampuni ya (ZAFICO) imepanga kununua boti nyengine moja ya
uvuvi.
Pia, kwa maelezo ya
Rais Dk. Shein Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo imo katika
mipango ya kuongeza boti nyengine nne zenye thamani ya USD milioni 2.2 kwa
ajili ya uvuvi wa bahari kuu huku Serikali ikinunua meli mpya ya mafuta.
Katika risala hiyo,
Rais Dk. Shein alisema kuwa mwaka 2019 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilieNdeleza
juhudi za utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia juhudi ambazo zilijumuisha tafsiri
za taarifa za mitetemo ambayo ndio itakayoonesha miamba au maeneo
yanayosadikiwa kuwa na mafuta na gesi asilia.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa katika mwaka 2019 mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta za jamii
ikiwemo utekelezaji wa sera ya kutoa huduma za afya na elimu bure ambapo bajeti
ya Wizara ya Afya imeongezeka mara 9.6 kutoka bilioni 10.81 mwaka 2010/2011 hadi
TZS bilioni 104.24 mwaka 2019/2020.
Aliongeza kuwa kwa
lengo la kuendeleza sekta ya elimu, katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imeongeza bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
mara 3.8 kutoka TZS bilioni 47.093 mwaka 2010/2011 ilipoanza Awamu ya Saba hadi
TZS bilioni 178.917 mwka 2019/2020.
Alisema kuwa katika
kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji safi na salama katika mwaka
unaomalzika Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya maji safi na salama kwa
mafanuikiio katika mkikoa yote ya Unguja na Pemba na wastani wa upatikanaji wa
amaji umefikia asilimia 79.
Sambamba na hayo,
alisema kuwa miradi ya ujenzi wa mji katika eneo la Fumba na Nyamanzi
imeendelea vizuri katika mwaka 2019 ambapo pia katika mwaka huo umeanzwa mradi
wa ujenzi wa maduka ya kisasa (shopping mall) katika eneo la Michenzani na mradi wa ujenzi wa majengo ya kisiasa ya
makaazi huko Kwahani.
Alieleza kuwa miradi
ya ujenzi wa miundombinu ya barabara imeendelezwa katika maendeeo mbali mbali
Unguja na Pemba sambamba na Serikali kununua vifaa vya kutengenezea barabara
vyenye thamani ya TZS bilioni 14 ili kujeijengea uwezo Idara ya Utunzani
Barabara (UUB).
Alieleza jinsi
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ulivyofanikiwa huku akitumia fursa hiyo
kuwahimiza viongozi wenziwe hasa Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi na viongozi wote wa Serikali wa ngazi mbali mbali na watumishi wote
wa umma kuongeza jitihada kwa kufanya kazi kwa bidii katika kuwatumikia
wananchi na kuyatatua matatizo yao katika mwaka 2020.
Na kwa wale waliotoa
ahadi ya kuyatekeleza mambo kadhaa ya maendeleo walipokuwa wakiomba kura za
kutaka uongozi mnamo mwaka 2015, Dk. Shein alisisitiza kuwa wanapaswa kuzingatia kwamba mwaka 2020 tayari
ushawadia.
Rais Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kutoa pole kwa wananchi wote waliopata maafa yaliyotokana
na mvua iliyoambatana na upepo mkali iliyotokea usiku wa kuamkia Jumaamosi ya
terhe 21 Disemba, 2019. Kadhalika alitoa pongezi kwa viongozi wa ngazi mbali
mbali waliowatembelea wananchi walioathirika kwa ajili ya kuwafariji.
Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment