Habari za Punde

TUME YA HAKI ZA BINAADAMU NA UTAWALA BORA


Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Mhe Khamis Juma Mwalim  akiwa na ujumbe kutoka Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora  Tanzania
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora Mhe, Jaji Mathiew Mwaimu  kulia akiwa na Makamo Mwenyekiti wa Tume hio Mhe Mohamed Khamis Hamad pamoja na Kamishna Khatib Mwinyi

Na.Raya Hamad. – WKS .                                     
WAZIRI wa Katiba na Sheria Zanzibar Mhe. Khamis Juma Mwalim ameitaka Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora kuendelea kusimamia majukumu yao kwa ufanisi kama sheria na muongozo unavyoelekeza.

Akizungumza na ujumbe kutoka Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora kwenye ukumbi wa Wizara Mazizini, alisema Tume inamajukumu ya kuendeleza na kusimamia masuala ya haki na utawala bora nchini,hivyo ni vyema kusimamia kwa uadilifu.

Mhe.Khamis ameahidi kuwa Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kufanyakazi kwa mashirikiano ya pamoja na Tume hiyo.

Aidha Wizara itahakikisha taratibu na miongozo inafuatwa katika kusimamia demokrasia, utawala bora na haki za binaadamu chini ya utawala wa sheria.

“Katiba na Sheria kwa upande mmoja, na Tume ya haki za Binaadamu na Utawala Bora kwa upande mwingine ni watoto pacha hivyo ni lazima waungane pamoja kama walivyo ili tuweze kusimamia vyema majukumu ya nchi na kuendeleza amani na mshikamano wa nchi yetu” alilisisitiza Mhe. Waziri.

Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe.Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu amesema jukumu kubwa la Tume hiyo ni kulinda, kutetea na kuhifadhi haki za binaadamu nchini.

Mwenyekiti huyo amesema katika kutekeleza jukumu hilo, Tume inayo mamlaka ya kupokea malalamiko kwa njia mbali mbali na kuanzisha uchunguzi wake endapo itaona kuna uvunjifu wa haki za binaadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

Mwenyekiti Mathew amemuhakikishia Mhe. Waziri kuwa Tume itafanya kazi kwa uadilifu na kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia taratibu na kufuata Katiba na sheria za nchi.

Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe. Mohamed Khamis Hamad alisisitiza kuwa Masuala ya Haki za Binaadamu ni sehemu muhimu inayosimamiwa na Wizara ya Katiba na Sheria

Hivyo mashirikiano yanahitajika makubwa ya kiutendaji na Wizara inayoshughukia masuala ya utawala bora ili hatimae kuwe na taarifa ambayo itawasilishwa katika Wizara moja
Katika kubadilishana mawazo Kamishna wa Tume ya Haki na Utawala Bora Mhe.Nyanda Shuli amesema watahakikisha kuwa changamoto zitakazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi.

Aidha amesisitiza kuwa Tume haitaruhusu mwanya kwa baadhi ya vikundi ama taasisi kuhatarisha amani na kupelekea ukiukwaji wa haki za binaadamu na utawala bora

Kamishna Nyanda Shuli amesema utendaji wa Tume hiyo uko chini ya Wizara ya Katiba na Sheria Zanzibar na Wizara ya Katiba na Sheria Tanzania hivyo Tume inahitaji ushirikiano mkubwa wa wizara hizo ili iweze kufanikisha upatikanaji wa haki kwa wananchi na kuweza kuzitatuwa changamoto mbali mbali kwa wakati.

Katika ujumbe huo Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora amefuatana na Makamu Mwenyekiti Mhe.Mohamed Khamis Hamad, Makamishana 5 na Watendaji wa Tume hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.