Habari za Punde

Wadau Wasema Kilimo Ndicho Kitakacholeta Maendeleo Jumuishi Tanzania.

 Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia nchini Bi Bella Bird akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Hali ya Umasikini Tanzania Bara uliofanyika jijini Dodoma ambapo amesema Benki ya Dunia itaendelea kushirikiana na Tanzania katika jitihada zake za kujiletea maendeleo ikiwemo kupambana na umasikini 
 Waziri wa Biashara na Viwanda Innocent Bashungwa akihutubia wakati wa kuzindua Ripoti ya Hali ya Umasikini Tanzania Bara uliofanyika jijini Dodoma. Bashungwa ameeleza kuwa ripoti hii imechambua kwa kina hali ya umasikini nchini na kutoa dira ya kukabiliana na umasikini na hatimaye kufikia Malengo Endelevu ya Dunia ya “Hakuna Umaskini duniani ifikapo mwaka 2030”

Baadhi ya wadau wa Takwimu waliohudhuria uzinduzi wa Ripoti ya Hali ya Umasikini Tanzania Bara uliofanyika jijini Dodoma wakifuatilia uwasilishwaji wa matokeo ya ripoti hiyo.

 (Picha na Ofisi ya Taifa ya Takwimu)


Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia nchini Bibi Bella Bird amesema anakubaliana na hoja kuwa mustakabala wa ajira na ukuaji wa uchumi jumuishi kwa Tanzania uko kwenye maendeleo ya sekta ya kilimo.
Bi Bella Bird alisema hayo wakati akifunga mjadala kuhusu Ripoti ya Tathmini ya Umasikini Tanzania Bara ambao uzinduzi wake uliofanywa na Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa katika hoteli ya Morena jijini Dodoma.
Mkurugenzi huyo wa Benki ya Dunia alieleza kuwa mabadiliko yanayoendelea hivi sasa katika sekta hiyo ni muhimu kuhakikisha kuwa yanapewa kila aina ya uwezeshaji ili kilimo kiweze kuchukua nafasi yake katika uchumi wa nchi na kupunguza umasikini.
“Vijana wengi hivi sasa wameamua kujiunga na kuwekeza katika sekta ya kilimo na huko wakileta ubinifu mkubwa ikiwemo kutumia njia za kisasa za kilimo pamoja uchakataji wa mazao ya kilimo kuongeza thamani” alieleza Bi Bella Bird.
Aliongeza kuwa kinachotakiwa ni kuongeza jitihada za kuweka mazingira mazuri kuvutia uwekezaji katika sekya hiyo huku akitambua jitihada za serikali za kuimarisha miundombiu maeneo ya vijijini na kusambaza umeme vijijini ambayo amesema ni miongoni mwa vivutio vya uwekezaji katika sekta hiyo.
Hata hivyo, alieleza kuwa suala la huduma za kifedha kwa wakulima bado ni kitendawili pamoja na kuwa jitihada zimekuwa zikifanyika lakini bado hapajawa na namna bora ambayo inaweza kuwasaidia vyema wakulima kujiendeleza kiuchumi.
Geoffrey Kirenga mmoja wa wachanbuzi wa Ripoti hiyo alieleza kuwa kuingia kwa makampuni ya ngazi ya kati katika sekta ya kilimo kumechochea mabadiliko makubwa yanayoendelea kutokea katika sekta hiyo hivi.
“kuingia kwa makampuni hayo mbali ya mitaji inayoingizwa lakini kunaifanya sekta ya kilimo kufaidika na utaalamu, ujuzi na uzoefu wa sekta binafsi hivyo kuleta mabadiliko tunayoyaona hivi sasa katika sekta hii” alibainsha Kirenga.
Kirenga ambaye ni Mkuu wa Taasisi ya Southern Agriculture Growth Corridor alitoa wito kwa watunga sera nchini kuhakikisha kunakuwepo mazingira mazuri zaidi ya kuvutia watu wengi zaidi kuingia katika kilimo.
Mbali ya makampuni ya ngazi ya kati, Kirenga alieleza pia kuwa wako pia watu wengi wa mijini ambao hivi sasa wanajishughulisha kilimo na  wote hao wanasaidia wakulima vijijini kujifunza toka kwao na wao kujiendeleza.
Katika hotuba yake ya ufunguzi waziri Bashungwa alieleza kuwa ripoti hiyo imechambua kwa kina hali ya umasikini nchini na kutoa dira ya kukabiliana na umasikini na hatimaye kufikia Malengo Endelevu ya Dunia ya “Hakuna Umaskini duniani ifikapo mwaka 2030”

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.