Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Awekaji wa Jiwe la Msingi Jengo la Skuli ya Sekondari ya Wingwi Mkao wa Kaskazini Pemba.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akihutubia Wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba wakati wa hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi jengo la Skuli ya Sekondari ya Wingwi ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar. 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa elimu bure kwa wananchi wake kama ilivyo kwa sekta ya afya na katu haitorudi nyuma.
Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la Skuli ya Sekondari Ziwakije Wingwi Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni shamrashamra za sherehe za miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika hotuba yake hiyo, Rais Dk. Shein alisema kuwa elimu itaendelea kutolewa bure na kueleza kuwa yeyote ambaye atabadilisha malengo ya Serikali ya kutoa elimu na afya bure atachukuliwa hatua zinazofaa kwani hayo ni matunda ya Mapindyzi matukufu ya Januari 12, 1964.
Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa historia ya Mapinduzi na harakati zake za kupigania huru wa wanyonge na kusema kuwa Mapinduzi yamekuja kutokana na madhila makubwa yaliokuwa wakifanyiwa Waafrika wa Zanzibar.
Aleleza kwua Watawala wa Kwanza walikuwa Wareno ambao walikuja mnamo mwaka 1503 ambao walikaa zaidi ya karne tatu ambapo baadae waliondoshwa na ndipo alipokuja Mfalme wa Oman na kufanya maskani Zanzibar na kujitangaza kuitawala Zanzibar.
Alisema kuwa zaidi ya miaka 300 Zanzibar ilitawaliwa na Wakoloni ambapo kabla ya hapo Zanzibar ilikuwa huru na kusema kwamba mpaka yanafanyika Mapinduzi mwaka 1964 wanyonge walikuwa hawapati nafasi ya kusoma.
Aleleza kuwa elimu ilianza Zanzibar mnamo mwaka 1890 ambapo ilikuwa ikitolewa kwa kwa jamii ya Kihindi, na kueleza kuwa ndani ya miaka saba Zanzibar ilikuwa ikipigania Uhuru wake.
Alisema kuwa wakati Zanzibar ikisherehekea miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar ni vyema wananchi wakajua kuwa kabla ya Mapinduzi hapakuwa na usawa na badala yake palikuwa na mafarakano, na Sheria ya Rais ilizungumzzia umoja, amani na maelewano.
Alisema kuwa mnamo Septemba 23 mwaka 964 Marehemu Mzee Karume alitangaza kuwa elimu itatolewa bure kwa watu wote wa Unguja na Pemba jambo ambalo na yeye katika Awamu yake ya Saba anayoiongoza analiendeleza.
Alisema kuwa mpaka Mapinduzi yanafanyika Zanzibar ilikuwa na skuli 2 tu za Nasari ambazo ni Saateni na Jangombe ambapo hivi sasa kuna Nasari 382 baada ya miaka 56 ya Mapinduzi, Aidha, skuli za msingi zilkuwa 62 za msingi tu na hivi sasa zipo 381.
Alisema kuwa kabla ya Mapinduzi kulikuwa na skuli za Sekondarii zilikuwa 4, ambapo Pemba kulikuwa na skuli moja tu ambapo hivi sasa zipo skuli 2, 734.
Rais Dk. Shein alisema kuwa hapana mbadala wa elimu, kwani elimu ndio aliyoitukuza Mwenyezi Mungu na yoyote anayemzuia mwenziwe asisome huyo si mtu mzuri na ndio maana uwamuzi wa Serikali ya Zanzibar ni kuwa watu wasome.
Alisisitiza kwamba tokea alipoingia madarakani juhudi za makusudi amezichukua na Serikali anayoiongoza na kupelea kujenga skuli 48 skuli za kisasa za Sekondari zikiwemo skuli za msingi za ghorofa na kueleza kuwa Serikali imebadilisha Mitaala ambapo kabla ya Mapinduzi ilikuwa mwisho ni darasa la 8 kwa watoto wa kinyonge.
Alisema kuwa miaka 20 iliyopita Zanzibar haikuwa na Chuo Kikuu hata kimoja ambapo hivi sasa Zanzibar ina Vyuo Vikuu 3 ambavyo vinasomesha kada zote zinazopatikana katika vyuo vikuu vilivyopo nje ya nchi.
Rais Dk. Shein alieleza jinsi huduma muhimu za kijamii zilivyokuwa zikitolewa kwa ubaguzi ikiwemo huduma ya afya, ambapo mnamo Machi 8mwaka 1964 Marehemu Karume alitangaza afya bure hatua ambayo alisema kuwa Awamu ya Saba imerithi.
Aliongeza kuwa katika bajeti ya mwaka 2019 Serikali imeitengea Wizara ya Elimu TZS Bilioni 178.917 katika bajeti yake, ambapo anasema kuwa wakati anaingia madarakani  katika bajenti ya mwaka 2010  Bajeti ya Wizara ya Elimu ilikuwa ni Bilioni 47.09.
Aliongeza kuwa juhudi zinaendelea kuchukua katika ujenzi wa skuli ambapo Serikali inatarajia kujenga skuli 3 za kisasa Unguja na Pemba  sambamba na uendeelezaji wa ujenzi wa vyuo vya amali huko Mtambwe Pemba na Makunduchi Unguja hatua ambayo itaifanya kila Mkoa kuwa na chuo cha amali chake hali ambayo inaweka usawa.
Alisisitiza kuwa Serikali inawapenda watu wake wote hivyo, itaendelea kuwapelekea maendeleo wananchi wote lakini hata hivyo wapo watu wanaotoa kauli ili watu waichukue Serikali yao na kueleza kuwa Serikali si mtu mmoja na wala sio kikundi bali ni ya wananchi wote.
Rais Dk. Shein aliwataka wananchi kuiunga mkono Serikali yao na kuwataka wasidanganywe na wasikubali kufanya vitendo vilivyokuwa havina faida katika maisha yao na kuwataka wakaazi wa Wingwi kujivunia huduma hiyo ya elimu ambayo itakuwa hadi darsa la 14.
Alieleza kuwa kuna baadhi ya watu wanayachukia Mapinduzi na kushangazwa na wale wanaosema kuwa Serikali imewanyanganya ardhi na kueleza kuwa anavyotambua yeye kuwa ardhi yote ya Unguja na Pemba ni ya Serikali na wakoloni hawajaja na ardhi.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alisisitiza juu ya suala zima la amani, utulivu na maelewano na kuwaleza wananchi kuwa watu wote wa Unguja na Pemba ni wamoja na haipaswi kudharauliana.
Alieleza kuwa siasa ni masuala ya dunia lakini kubwa ni kuimarisha kwa amani na utulivu na kueleza kuwa Zanzibar ni nchi yenye amani na kamwe haitokwenda kinyume yake hivyo.
Rais Dk. Shein aliwatahadharisha na kuwasisitiza wananchi kuimarisha na kuendeleza amani, mapenzi na mashirikiano sambamba na kama hakuna msaada basi pasiweko kejeli.
“Tusiipelekea Zanzibar pale ambapo haitakiwi iende, kila mtu aishi vizuri kwani kila mtu mweye asili yake”, alisisitiza Dk. Shein.
Mara baada ya kuweka jiwe la Msingi la Skuli hiyo, Rais Dk. Shein alipata maelezo juu ya ujenzi wa skuli hiyo kutoka Kampuni yaUsimamizi wa jengo hilo Peter Lazaro.
Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kuendelea kuwaletea maendeleo wananchi wote wa Unguja na Pemba bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
Alieleza kuwa skuli hiyo iliyowekewa jiwe la Msingi moja imejengwa huko Wingwi Mkoa wa Kaskazini Pemba na nyengine iko Mwanakwerekwe Mkoa wa Mjini Magharibi majengo ambayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto ya uhaba wa nafasi kwa wananfunzi skuli.
Alieleza kuwa Serikali imeshavuka asilimia ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM katika ujenzi wa skuli ambapo tayari majengo 10 ya ghorofa na imeshajenga na imeshajnga majengo mengine ya ghorofa huko Fumba, Pangawe, Kwarara. Jengo la biashara pamoja na majengo mengine ambayo yote hayamo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Aidha, Wizara hiyo ya Elimu na Mafunzo ya Amali iliahidi kuendelea kufuata miongozo ya Rais Dk. Shein pamoja na kuendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafanzo ya Amali akisoma taarifa ya kitaalamu juu ya ujenzi wa skuli hiyo alisema kuwa skuli hiyo ina pacha wake ambayo ni skuli ya Mwanakwerekwe ambayo itawekwa jiwe la msingi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli.
Alisema kuwa skuli hiyo inajengwa kupitia mradi wa “Zanzibar Improving Student Prospects” (ZISP) mradi wa miaka mitano kuanzia 2016/17-2020/21 unaogharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia mkopo wa Benki ya Dunia.
Aliongeza kuwa lengo la mradi huo ni kuimarisha ubora wa katika masomo ya Sayansi na Hisabati kwa ngazi ya elimu ya Sekondari na Kiengereza kwa ngazi ya elimu ya Msingi na Sekondari (Darasa la 5 na Kidato cha 2).
Alisema kuwa mradi huo una vipengele vinne ikiwemo Mafunzo ya walimu, Kutoa ruzuku kwa skuli kwa ajili ya kusaidia skuli gharama za kujiendesha na kuzipatia zawadi katika masomo yao, kuimarisha miundombinu ya skuli kwa kujenga skuli mbili za ghorofa pamoja na kuifanyia mapitio na kuimarisha mifumo ya tathmini ya mitihani, ukaguzi pamoja na takwimu.
Alieleza kuwa jumla ya Dola za Kimarekani USD 35 Milioni zitatumika kuutekeleza mradi huo mpaka kukamilika kwake ambapo ujenzi wa Skuli hiyo ulianza mnamo Septemba 2018 na ulitarajiwa kukamilika mwezi wa Agosti mwaka 2019.
Hata hivyo, kutokana na changamoto mbali mbali ikiwemo ya upungufu wa mchanga Unguja na Pemba haukuweza kukamilika katika kipindi hicho na hivyo kuongezwa  muda hadi mwezi Machi mwaka huu wa 2020.
Alieleza kuwa Kampuni ya ujenzi ya M/S RANS COMPANY Ltd ya Tanzania Zanzibar ndiyo inayojenga skuli hiyo ambapo kazi za usimamizi wa ujenzi zinasimamiwa na Kampuni ya Arques Africa Architects & Interio Designers kutoka Tanzania Bara ambayo ndio wanaosimamia mradi wote huko Pemba.
Alisema kuwa gharama za ujenzi wa Skuli hiyo ni TZS Bilioni 2.455 ambapo katika ujenzi huo Serikali imesamehe ushuru kwa vifaa  vyote vya ujenzi.
Kwa maelezo ya Katibu Mkuu huyo ujenzi wa Skuli ya Wingwi baada ya kukamilika kwake itakuwa na madarasa 12 maabara 3 za sayansi, maabara ya lugha, maktaba, chumba cha kompyuta, ukumbi wa kufanyia mitihani na vyoo 17.
Katibu huyo alisema kuwa skuli imezingatia elimu mjumuisho kwa kuwa na miundombinu inayojali wanafunzi wenye mahitaji maalum kama vile “ramps” na vyoo maalum ambapo wanafunzi wapatao 960 wanatarajiwa kupata nafasi za masomo katika skuli hiyo kwa mtindo wa shifti ya asubuhi na jioni.
Katika hafla hiyo, wanafunzi wa skuli ya Msingi ya Konde walionyesha umahiri wao kwa kuimba nyimbo inayomsifu Rais Dk. Shein na viongozi wengine waasisi wa Taifa hili sambamba na kuyapongeza Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.