Habari za Punde

Sera ya Uendelezaji wa Miji Kuwa Suluhisho la Makazi Holela.

Washiriki wa Mjadala kuhusu Ukuaji wa Miji na Changamoto zake uliofanyika jijini Dodoma Leo Tarehe 30 Januari 2020 wakiwa katika picha ya pamoja. Aliyekaa katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Mipango Miji Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Amulike Mahenge. Mjadala huo umeandaliwa kwa pamoja na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Makazi (UN Habitat)
Baadhi ya Washiriki wa Mjadala kuhusu Ukuaji wa Miji na Changamoto zake  wakifuatilia hotuba ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Nicolaus Benjamin (Hayupo pichani) wakati akifungua Mjadala huo jijini Dodoma Leo Tarehe 30 Januari 2020. Mjadala huo umeandaliwa kwa pamoja na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Makazi (UN Habitat).
Mkurugenzi wa Mipango Miji na Vijiji Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Emaculata Senje akichangia katika Mjadala Kuhusu Ukuaji Miji na Changamoto zake uliofanyika leo tarehe 30 Januari 2020 jijini Dodoma. Mjadala huo umeandaliwa kwa pamoja na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Makazi (UN Habitat).
Washiriki wakifuatilia uwasilishwaji Mada kwenye Mjadala kuhusu Ukuaji wa Miji na Changamoto zake uliofanyika jijini Dodoma Leo Tarehe 30 Januari 2020. Mjadala huo umeandaliwa kwa pamoja na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Makazi (UN Habitat).
(Picha na Hassan Mabuye Wizara ya Ardhi)
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Imeelezwa kukosekana kwa sera maalum ya uendelezaji Miji nchini kunachangia kuendelea kuwepo makazi holela kwenye maeneo mablimbali nchini Tanzania.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Undelezaji Miji na Vijiji Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt Mukuka Hante leo tarehe 30 Januari 2020 wakati wa Kusanyiko la Mjadala kuhusu Masuala ya Ukuaji Miji na Changamoto zake lililofanyika jijini Dodoma.
Alisema, kwa sasa nchi nyingi duniani zina sera maalum ya uendelezaji miji aliyoieleza kuwa inawezesha kuwepo chombo cha kuleta maendeleo ya miji unaoenda sambamba na huduma za afya, makazi, barabara na huduma nyingine za kijamii.
Hata hivyo, Hante alisema Serikali iko mbioni kuja na sera ya Uendelezaji Miji aliyoieleza kuwa itakuwa suluhisho la makazi holela hasa kipindi hiki ambacho miji mingi imeendelea kukuwa kwa kasi.
Kwa mujibu wa Hante, Uendelezaji Miji maeneo mbalimbali unatakiwa usiwe kwenye uboreshaji makazi pekee bali uendane na mjumuiko wa uendelezaji miji na vijiji kwa kuwa maeneo ya vijiji yanatakiwa pia kuwa na makazi bora yatakayochangia uwekezaji. Aidha, alisema Miji na Vijiji vinategemeana na iwapo vijiji vitaachwe kujumishwa kwenye mpango wa uendelezaji miji basi vitaachwa  mbali na wananchi wake kuwa nyuma kimaendeleo.
Mkurugenzi huyo wa Uendelezaji Miji na Vijiji TAMISEMI alibainisha kuwa, ukuaji miji unatoa fursa ya uwekezeji kwa wananchi vijijni na kubainisha kuwa pamoja na mkazo kuwekwa katika uendelezaji miji lakini huduma nyingine kama vile Afya na barabara lazima ziendelezwe hasa kipindi hiki ambacho Seriali inapoelekea katika uchumi wa kati.
Kwa upande wake Meya wa Jiji la Dodoma Profesa Davis Mwanfupe alisema ukuaji Miji kwenye maeneo mbalimbali lazima uendane na upatikanaji huduma muhimu kwa lengo la kukabiliana na changamoto na fursa zitakazopatikana. Alibainisha kuwa, mjadala unaoendelea kuhusiana na ukuaji miji unakuja wakati muafaka ambapo dunia iko hatua ya kujadili maendeleo endelevu kwenye maeneo mbalimbali.
Akifungua Mjadala huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi Nicolaus Benjamin aliwaambia washiriki wa Mjdala huo kuwa serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha inapunguza ama kuondoa makazi holela.
Hata hivyo, aliwataka washiriki hao kuutumia mjadala huo wa siku moja kutafuta ufumbuzi wa changamoto za makazi holela sambamba na kuibuka mpango utakaotoa fursa za uwekezaji hasa uendelezaji miji, uratibu na ushirikiano kati ya wadau katika kufikia lengo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mipango Miji Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Amulike Mahenge alisema, kusanyiko la Mjadala kuhusu ukuaji Miji na changamoto zake linafanyika kwa ushirikiano baina ya Wizara yake na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Makazi (UN Habitat) na kuhusisha wadau kutoka mamlaka za upangaji nchini. Kwa mujibu wa Mahenge, Mjadala huo unaangalia fursa na changamoto zinazopatikana kutokana na ukuaji Miji na jinsi ya kutumia fursa kuwa na miji endelevu.
Hata hivyo, Mahenge alisema kwa sasa idadi ya makazi holela imeanza kupungua nchini kutokana na jitihada za serikali kuruhusu kampuni binafsi za upangaji na upimaji kushiriki katika kupanga na kupima maeneo mbalimbali ya nchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.