Habari za Punde

SERIKALI YAPOKEA ZAIDI YA BILIONI 25 ZA GAWIO NDANI YA SIKU 60 ZA UTEKELEZAJI WA AGIZO LA MHESHIWA RAIS

Wawakilishi wa Taasisi waliofika kwa ajili ya kutoa gawio la Serikali wakiwa wameshikilia hundi zao katika picha ya pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Marry Maganga, na Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbuttuka wakati wa hafla ya kupokea gawio jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akipokea hundi ya kiasi cha Sh. Milioni 300, kutoka kwa Mkuu wa Masoko Kiwanda cha Simenti Mbeya Bw. Mark Chilambe. Wa pili kushoto ni  Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wa kwanza kushoto ni Msajili wa Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka, wa kwanza kulia ni Naibu Katibu wa Wizara hiyo Bi. Marry Maganga wakati wa halfa ya kupokea gawio jijini Dodoma.

Wenyeviti, Wakurugenzi wa Taasisi, Mashirika na Kampuni wamesalimika na panga la Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango baada ya kutoa gawio na michango kiasi cha shilingi bilioni 25.12, katika kipindi cha siku 60 za utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli la kuzitaka Taasisi, Mashirika na Kampuni ambazo hazijatoa gawio kwa Serikali, kuwasilisha gawio na michango ya huduma za Jamii.

Hayo yamedhihirishwa Jijini Dodoma katika hafla ya kukamilisha agizo hilo la kupokea gawio kutoka katika Mashirika, Taasisi, Wakala na Kampuni zinazomilikiwa na Serikali ambazo hazikuwa zimefanya hivyo hapo awali.

Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango alisema kuwa ameridhishwa na utekelezaji wa agizo hilo ambalo Mheshimiwa Rais alilitoa tarehe 24 Novemba, 2019 na kupokea Gawio, Michango ya asilimia 15 na Michango ya Huduma za Jamii kutoka Taasisi, Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali inamiliki hisa chache.

“Naomba tuungane kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa uongozi wake uliopelekea Mashirika, Taasisi, Wakala na Kampuni zote ambazo Serikali ina hisa kutoa gawio, michango ya asilimia 15 na michango ya huduma za jamii. Kama kawaida yake, Mhe. Rais amevunja rekodi, maana haijawahi kutokea katika historia ya nchi yetu, alisema Dkt.Mpango.

Alisema agizo limetekelezwa kwa asilimia 100 katika kipindi kifupi na kuahidi kuwa fedha zote zilizokusanywa Serikali itazitumia vizuri kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.

Aidha, Dkt. Mpango aliwaagiza Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wote wa Taasisi na Mashirika ya Umma, wasisubiri maelekezo ya Mhe. Rais ndio waanze kulipa gawio na michango kwa Serikali, kila mmoja kwa wakati wake akawajibike ipasavyo kuinua utendaji kwa kulipa gawio na michango kwa hiyari.

“Ninawakumbusha kwa niaba ya Serikali hakikisheni mnapunguza matumizi yasiyo ya lazima katika Mashirika/Taasisi mlizodhaminiwa kuziongoza. Sitarajii mwaka ujao kuona Taasisi ama Mashirika ya Umma kutoa michango yao kwa kusukumwa. Ni aibu”, alisisitiza Waziri Mpango.

Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka alisema kuwa Mashirika nne (4) pekee ndio yameshindwa kulipa gawio na michango kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutokuwa na uzalishaji, upya wa taasisi na kampuni nyingine kurejeshwa Serikalini kutokana na Mwekezaji kutokidhi vigezo vya mkataba wa Ubinafsishaji.

Alimpongeza Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuwezesha kukusanywa kwa kiasi cha Shilingi bilioni 25.12 katika kipindi kifupi na kubainisha kuwa fedha hizo zikitafsiriwa kwa harakahara ziweza kujenga wastani wa vituo vya Afya 65.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (wa pili kulia), Naibu Waziri Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (wa pili kushoto), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Marry Maganga (wa kwanza kulia) na Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbuttuka (wa kwanza kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari wakati wa hafla ya kupokea gawio kutoka kwa Taasisi sita jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.