Habari za Punde

Waziri Mhagama Atoa Miezi Miwili Mabaraza ya Wafanyakazi Yasiyo Hai Kuhuishwa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akihutubia Wafanyakazi wa Ofisi wa Taifa ya Takwimu alipokuwa akifungua Mkutano wa Tatu wa Baraza la Tano la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo uliofanyika kwenye leo tarehe 23 Januari, 2020 Jijini Dodoma.
Sehemu ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa Mkutano huo.

Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Mabaraza ya Wafanyakazi yasiyo hai yaliyopo katika Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali yametakiwa kuhuishwa na kuanza kutekeleza majukumu yake yalioainishwa kisheria.

Agizo hilo limetolewa leo jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alipokuwa akifungua Kikao cha Tatu cha Baraza la Tano la Wafanyakazi la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Waziri Mhagama amesema kuwa Mabaraza ya Wafanyakazi ni muhimu kwani ni chachu ya kuhakikisha kunakuwepo na mfumo maridhawa wa mawasiliano na majadiliano kati ya menejimenti na watumishi ikiwa ni sehemu ya kuweka mazingira mazuri na wezeshi ya utekelezaji wa mipango ya taasisi husika.

“Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2019 jumla ya Taasisi 487 za Umma na Binafsi zilipaswa kuwa na Mabaraza ya Wafanyakazi ambapo kati ya Mabaraza 211 kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni Mabaraza 161 tu ndiyo yalikuwa hai pia kati ya Mabaraza 276 kutoka Serikali Kuu, Mabaraza 260 tu ndiyo yalikuwa hai hivyo, natoa miezi miwili kwa Mabaraza yasiyo hai kuanza kutekeleza majukumu yake”, alisema Waziri Mhagama. 

Waziri Mhagama ameongeza kuwa pamoja na kufanya vikao hivyo, lazima wafanyakazi wapewe nafasi ya kuzungumza matatizo yao kwa uwazi ili kuweza kuboresha utendaji kazi na kupata suluhu ya changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Aidha, Waziri Mhagama ameipongeza NBS kwa kuwa na Baraza la Wafanyakazi lililo hai pia amewataka watambue kuwa taasisi hiyo ni kiungo muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi na hasa wakati huu nchi inapoelekea katika kutekeleza malengo iliyojiwekea ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa amesema kuwa Menejimenti ya NBS imekuwa ikifanya mikutano ya Baraza hilo kama ilivyoainishwa kwenye Agizo la Rais Na. 1 la Mwaka 1970 na kwa kuzingatia ratiba ya mikutano hiyo kwa mujibu wa mkataba wa makubaliano kati ya menejimenti ya NBS na Chama cha Wafanyakazi (TUGHE).

“Utekelezaji wa Agizo hilo la Mhe. Rais ni sehemu ya uongozi shirikishi katika kukamilisha uongozi unaozingatia utawala bora kwa kufanya maamuzi yanayowashirikisha wafanyakazi katika utoaji wa maamuzi”, alisema Dkt. Chuwa.

Akizungumzia kuhusu masuala ya takwimu, Dkt. Chuwa amesema kuwa, kwa kushirikiana na Divisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa (UNSD) na wadau wengine kama Kamisheni ya Uchumi ya Afrika inaandaa utaratibu wa kuwezesha kutumia takwimu  zinazozalishwa  na vyanzo  vingine vikiwemo vya sekta binafsi kama asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali kujumuishwa katika kuzalisha takwimu rasmi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.