Habari za Punde

TANZANIA YAPATA MSAADA WA BILIONI 241 KWA AJILI YA KUENDELEZA ELIMU

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Balozi wa Sweden nchini, Bw. Anders Sjoberg wakisaini mikataba ya msaada wa dola za Marekani milioni 90 sawa na shilingi bilioni 240.95 kutoka Mfuko wa Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE) kwa ajili ya kugharamia Sekta Elimu, jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Balozi wa Sweden nchini, Bw. Anders Sjoberg, wakibadilishana mikataba ya msaada wa dola za Marekani milioni 90 (shilingi bilioni 240.95) uliotolewa na Mfuko wa Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE) kwa ajili ya kugharamia Sekta Elimu, jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Balozi wa Sweden nchini, Bw. Anders Sjoberg, (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na wadau wa maendeleo waliochangia fedha za msaada wa dola za Marekani milioni 90 (shilingi bilioni 240.95) kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE), baada ya kumalizika kwa halfa ya utiaji saini wa mikataba hiyo, jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)

Na Farida Ramadhani, WFM, Dar es Salaam
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea msaada wa Dola za Marekani milioni 90 sawa na shilingi bilioni 240.95 kutoka Mfuko wa Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE), kwa ajili ya kugharamia miradi miwili ya Sekta ya Elimu.
Mikataba ya msaada huo imesainiwa katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es Salaam, na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Doto James kwa upande wa Serikali na Balozi wa Sweden nchini, Bw. Anders Sjoberg, ambaye nchi yake ni Wakala wa Msaada huo kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la nchi hiyo (SIDA).
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mikataba ya msaada huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James alisema msaada huo ni kwa ajili ya kugharamia miradi ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu (ESDP) 2016/17 – 2021/22  na nyongeza ya Mpango wa Elimu kwa Matokeo (EP4R).
“Kati ya fedha hizo za msaada, dola za Marekani milioni 38.89 (Sh. bil. 88.55) zitatumika kughagharamia Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu (ESDP) 2016/17 – 2021/22 na dola za Marekani milioni 51.11 (Sh. bil. 116.40) ni kwa ajili ya nyongeza katika mchango wa Sweden katika Mpango wa Elimu kwa Matokeo (EP4R) ulioanza tangu mwaka 2015”, alifafanua.
Alisema fedha za kugharamia Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu zitatumika kutimiza malengo mahsusi ya programu za Sekta ndogo za elimu ya msingi, elimu jumuishi na watu wazima pamoja na elimu nje ya mfumo rasmi.
Alibainisha kuwa utekelezaji wa miradi hiyo utachangia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo ya Mapango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano ambao pamoja na mambo mengine unalenga kuboresha Sekta ya Elimu kupitia Mafunzo ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (LANES), kuongeza udahili wa wanafunzi pamoja na kuboresha mazingira ya kusomea kwa kujenga madarasa.
Aliishukuru Serikali ya Sweden kwa kuratibu upatikanaji wa fedha hizi ambazo zinafanya uwekezaji wa nchi hiyo hapa nchini kufikia zaidi ya shilingi trilioni 1.25 zilizowekezwa kwenye miradi mbalimbali ikiwemo mapitio ya matumizi ya fedha za Umma, maliasili na hifadhi ya jamii, elimu, nishati, utafiti, na kusisitiza kuwa uhusiano wan chi hizo mbili utaendelea kuimarika.
Aidha, Bw. James amempongeza Mhe. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa jitihada zake kubwa za kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo maboresho makubwa katika Sekta ya Elimu, ikiwemo utoaji elimu bila malipo kuanzia shule za msingi hadi sekondari.
Naye Balozi wa Sweden Tanzania, Bw. Anders Sjoberg,  aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada mbalimbali iliyochukua katika kuboresha elimu hususani katika awamu ya kwanza ya programu ya Mafunzo ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (LANES) pamoja na Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu (ESDP) 2017 – 2021.
Aliishauri Serikali ya Tanzania kuangalia kwa karibu suala la maendeleo ya elimu ya mtoto wa kike hasa kipindi cha kutoka elimu ya msingi kwenda Sekondari pamoja na kuboresha matokeo yao.
Alibainisha kuwa Sweden na washirika wengine wa maendeleo wapo tayari kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo elimu.
Kwa upande wake Mkuu wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Uingereza (DFID), Bi. Beth Arthy akizungumza kwa niaba ya washirika wengine wa maendeleo, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kupiga hatua katika Sekta ya elimu ambayo matokeo yake yanaongezeka kila mwaka.
Alisema matokeo hayo yanatokana na mikakati mbalimbali iliyowekwa katika Sekta hiyo ikiwemo mpango wa elimu bila malipo ambao umeongeza idadi ya wanafunzi na kuiwezesha Tanzania kujizolea umaarufu duniani.
Pamoja na maendelo hayo, Bi. Arthy aliishauri Serikali kuongeza idadi ya walimu mashuleni ili waweze kuhudumia wanafunzi kwa ufanisi na kuongeza ufaulu zaidi.
“Tangu kuanzishwa kwa programu ya elimu bila malipo idadi ya wanafunzi mashuleni imeongezeka kwa kasi tofauti na idadi ya walimu waliopo hali inayowafanya walimu kufanyakazi kubwa zaidi ya uwezo wao” aliongeza Bi. Arthy.
Akipokea msaada huo kwa shukrani, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo, alisema kuwa Wizara hiyo itahakikisha fedha hizo  zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuhakikisha Elimu bora kwa wote inapatikana Tanzania.
Msaada huoumechangiwa na washirika mbalimbali wa maendeleo wakiwemo UNICEF, UNESCO, Benki ya Dunia, Umoja wa Ulaya, Australia, Canada, Denmark, Ufaransa, Korea, Uholanzi, Norway, Hispania, Uswiss, Marekani na Uingereza kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.