WANANCHI wameipongeza hotuba ya Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyeitoa katika kilele
cha kuadhimisha miaka 56 ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 hivi
karibuni.
Wakiwa katika maeneo
mbali mbali kwa nyakati tofauti wananchi hao wameipongeza hotuba ya Rais Dk.
Shein na kumpongeza yeye mwenyewe binafsi kwa yale yote aliyoyasema katika
hotuba hiyo ambayo wamesema ni dira katika maendeleo ya Wazanzibari.
Wananchi hao walisema kuwa
mbali ya kueleza katika hotuba hiyo juhudi za Serikali anayoiongoza pamoja na
hatua kubwa zilizofikiwa katika kukuza uchumi pia, wameunga mkono kauli yake ya
kutochelea kumchukulia hatua mtu yeyote atakayejaribu kuhatarisha amani iliyopo
hapa nchini.
Walieleza kuwa juhudi
anazozichukua Rais Dk. Shein kwa kushirikiana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dk. John Pombe Magufuli za kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa
nchini ni hatua madhubuti ya kuungwa mkono na kila Mtanzania.
Wananchi hao wamepongeza
maneno ya Rais Dk. Shein katika hotuba yake hiyo jinsi ya viongozi hao
wanavyotekeleza wajibu wao wa Kikatiba na Kisheria katika kutekeleza amani,
utulivu na kulinda maisha ya wananchi pamoja na mali zao.
Wananchi hao walieleza
na kuponmgeza jinsi hotuba hiyo ilivyotilia mkazo suala la Muungano na hasa
pale Rais Dk. Shein aliposema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea
kushirikiana na Serikali ya Jamhauri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza
na kudumisha Muungano.
Aidha, wananchi hao
walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kutekeleza vyema majukumu yake katika Awamu
yake hii ya Saba katika kipindi cha miaka tisa cha uongozi wake kwa kuendelea
na juhudi za kutekeleza mipango ya mageuzi ya kiuchumi ili kuhakikisha kwamba
uchumi na ustawi wa wananchi wa Zanzibar unaimarika.
Wananchi hao walieleza
kufurahishwa na juhudi hizo ambazo ni pamoja na kuhakikisha hali ya amani na
utulivu inaimarika hatua ambayo zimepelekea kuongezeka kwa pato halisi la Taifa
kwa mara 1.6 zaidi ya kutoka thamani ya TZS Bilioni 1,768 mwaka 2010 hadi
kufikia thamani ya TZS Bilioni 2,874 mwaka 2018.
Sambamba na hayo,
wananchi hao walipongeza hatua zilizochukuliwa na uongozi wa Rais Dk. Shein
katika kuimarisha uchumi kulikopelekea ongezeko la ukusanyaji wa mapato mwaka
hadi mwaka ambapo kwa mwaka wa fedha 2018/2019 mapato ya ndani yalifikia TZS
Bilioni 748.9 ikilinganishwa na jumla ya TZS Bilioni 181.1 zilizokusanywa mwaka
2010/2011.
Katika maelezo yao
wananchi hao walimpongeza Rais Dk. Shein kwa juhudi alizozichukua katika
kuimarisha sekta za maendeleo zikiwemo elimu, afya, maji safi na salama, ajira
kwa vijana, biashara, viwanda, utalii, uvuvi na ufugaji pamoja na sekta ya
kilimo, mafuta na gesi, nishati ya umeme, miundombinu ya barabara.
Pia, Rais Dk. Shein
alipongezwa kwa mikakati yake ya ujenzi wa bandari mpya ya Mpigaduri pamoja na
Mangapwani, Mradi wa Kamera za uangalizi (CCTV), Mahakama, mazingira, Mamlaka
ya Kuzuia Rushwa na Kuhujumu Uchumi (ZAECA), kuanzisha mfumo wa Ugatuzi wa
madaraka kwa wananchi na kuimarisha sekta michezo.
Kwa upande
mwengine waliipongeza hotuba hiyo ya Dk.
Shein kutokana na juhudi zilizochukuliwa kuimarisha sekta ya habari na kuongeza
ufanisi ikiwa ni pamoja na kuliimarisha Shirika la Utanzagazi la Zanzibar (ZBC)
na Shirika la Magazeti la Zanzibar huku wakiahidi kuufanyia kazi wito wake wa
kwensda kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Walisema kuwa hotuba
hiyo imeeleza azma ya Serikali anayoingoza Rais Dk. Shein katika kuziimarisha huduma za Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume zikiwemo ujenzi wa jengo la abiria “Terminal
3” pamoja na ujenzi wa uwanja mpya wa kisasa wa Pemba kwa mashirikiano kati ya
Serikali na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB).
Walieleza kuwa
hawatokuwa wachoyo wa shukurani kwa kumshukuru Dk. Shein kwa kurekebisha
maslahi ya Wafanyakazi ya mishahara aliyoyafanya mwaka 2011, 2013, 2015 na
mwaka 2017 kwa lengo la kuwapa motisha kwa kuzingatia ukuaji wa mapato.
Aidha, walitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Shein
kwa kuwaahidi Watumishi wa Umma kuwa anamatumaini makubwa kwamba kutokana na
hali ya uchumi unavyoendelea wasishangae kuwa mwaka huu akaongeza chochote.
Walieleza kuwa kauli
hiyo imewapa faraja na kueleza kuwa Rais Dk. Shein ni kiongozi wa pekee
anaewajali wananchi wake wakiwemo wafanyakazi wa sekta za umma.
Akizungumza na
mwandishi wa habari hizi Kija Kijitu Makame
wa Majenzi Makunduchi alipongeza
Rais Dk. Shein kwa hotuba yake ambayo alisema imejaa kila kitu kuanzia masuala
ya uchumi, maji, elimu, kilimo, mishahara, majenzi, barabara pamoja na umuhimu
wakuendeleza amani na utulivu.
“Helikwacha kitu, kwa
msingi uno Mheshimiwa Rais kwake mambo yoti ni vipaumbele maana kana tazama
watu wanachaka nini, jambo lino tunamshukuru sana maana ni ishara ya kiongozi
msikivu na mwadilifu” , alisema Kija Kijitu Makame.
Aliendeleza pongezi
kwa Rais Dk. Shein kwa kuonesha kuwajali wananachi wake “Suwe wa njia ya kusini
tunamshukuru sana kutujali kwa kutuwishia shida iliyowaja Kibonde Mzungu kila
ikanya vua mtihani mpaka watu kufya, akajenga daraja zuri na katii taa vazuri
hamba Ulaya” alisisitiza Kijitu.
Aliongeza kuwa “Kigezo
chengine cha kuonesha jinsi Rais Dk. Shein anavyowajali watu ni valya Amani
wakati kana hutubia, kono jua kali sana na joto jingi basi akaamua asiisome
yoti hotuba yake ili watu wasikae too”.
“Bali yalya ya muhimu
mfano kuongeza mshahara, kuongezeka kwa uchumi na jinsi miradi ya maendeleo ilivyoimarika
kono aseme kabisa tukampigia makofi, Mungu alijaalie tuvate kiongozi mwengine
ja yeye ili tuvate maendeleo zaidi na zaidi”, alimalizia Kijitu.
Ali Hamad Ali mkaazi
wa Pembeni Wilaya ya Wete Pemba, anasema kwamba hotuba ya Dk. Shein ilisheheni
kila kitu ambacho kilichofanyika ikiwemo, ukuwaji wa Uchumi, uwajibikaji wa
Serikali, maendeleo yaliofikiwa sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya
Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka
2010-2020.
Alieleza kuwa
hotuba hiyo, ilikuwa na mchanganuo wa mambo mbali mbali, ikiwemo elimu, afya,
barabara mambo ambayo ni ya uhakika kwani kila mmoja anayaona ambayo ni tofauti
sana na miaka iliopita kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964.
Alifahamisha kuwa kubwa
ambalo halijawahi kutokea katika historia ya Zanzibar, ni pale hotuba
inavyoelezea jinsi Serikali inavyoendelea kulishughulikia suala la Mafuta na Gesi Asilia jambo ambalo
likifanikiwa litakuza uchumi wa Zanzibar maradufu.
Nae Massoud Ali
Mohammed mkaaazi wa Ndagoni Wilaya ya Chake Chake Pemba, anasema kwamba hotuba aliyoitoa
Rais Dk. Shein inaeleza ukweli mtupu kwani kila liliomo ndani ya hotuba liko wazi na linaonekana na kilichobakia kwa
wananchi wa Zanzibar ni kushirikiana na Viongozi pamoja na Serikali yao.
Alisema suala la
kuwaenzi Wazee ambalo ni moja ya hatuba alioitowa Rais katika kilele cha
sherehe za Miaka 56 ya Mapinduzi ni ukweli usiopingika ambapo wazee sasa hivi
wanafaidika na huduma ya malipo ya Pencheni Jamii “Kwa kweli nikiwa mwananchi wa Zanzibar naiopongeza sana hatuba ya
Dk. Shein”,alisema Masoud Ali.
Kwa upande wake,
Omar Mjaka Ali, Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Vitongoji ambalo hivi sasa ni Jimbo
la Wawi aliipongeza hotuba ya ya Rais Dk. Shein aliyoitowa katika kilele cha
Sherehe za miaka 56 ya Mapinduzi Zanzibar, kwa kusema ilikuwa imesheheni kila
kitu na aliyoeleza yote ni ya kweli kabisa na yamefanywa kwa vitendo.
Nae Muhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino (SAUT), kiliopo Mwanza Dk. Zakayo Bernad aliipongeza
hotuba aliyoitoa Dk. Shein ambayo ilionekana na kusikika katika vyombo vya
habari mbali mbali nchini na kusema kuwa hotuba hiyo ni kitabu rejea ambacho wanafunzi wanaweza kukitumia katika ufanyaji
wa tafiti zao.
Mkurugenzi wa Chuo cha Utawala wa Umma (IPA) Dk. Mwinyi
Talib kwa upande wake alieleza kuwa hotuba hiyo ni ushahidi wa kutosha kuwa
Rais Dk. Shein anaongoza kwa kufuata misingi ya Katiba, Sheria na Utawala Bora na
ndio maana mafanikio makaubwa yameweza kupatikana katika uongozi wake.
Bi Rahma Abasi
Madeweya mkaazi wa Fuoni Michenzani alieleza kuwa kwa upande wake amefarajika
sana na hotuba ya Rais Dk. Shein hasa pale aliposisitiza kutoa elimu bure tena
bila ubaguzi hatua ambayo itawapunguzia mzigo wazee na walezi sambamba na
kuendeleza malengo ya Bwana Abeid Karume ya kutoa matibabu bure.
Akieleza kuhusu
mafanikio makubwa katika sekta ya
utalii, Muhidini Kutengwa ambaye ni Mtembezaji watalii alikiri kuwa azma ya
Rais Dk. Shein kama alivyoeleza katika hotuba yake jinsi Serikali ilivyoweka
mikakati ya kuimarisha viwanja vya ndege na bandari itaimarisha uchumi na kukuza
pato la Taifa. “Nathubutu kusema kuwa Rais Dk. Shein ni ‘baba lao’ kwa
maendeleo Zanzibar”alisisitiza Kutengwa.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment