Habari za Punde

KAMPUNI YA SIMU YA TTCL YAZINDUA KAMPENI YA UZINDUZI WA MINARA IJULIKANAYO KWA JINA LA SWITCH ON

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye (wapili kushoto), Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki ambae pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Omar Mgumba (wakwanza kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),Waziri Kindamba wakikata utepe kuashiria Uzinduzi wa Minara wenye lengo la kufikisha mawasiliano karibu na wananchi,tukio hilo limefanyika katika kijiji cha Sangasanga, mkoani Morogoro.Picha na TTCL
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye, amezindua Kampeni ya Uzinduzi wa Minara ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), ambayo itasogeza mawasiliano karibu na wananchi wa pembezoni mwa miji mikuu, vijijini na maeneo ambayo hayakuwahi kuwa na mawasiliano huko nyuma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, uliofanyika katika kijiji cha Sabgasanga, mkoani Morogoro ,Naibu Waziri alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt.John Pombe Magufuli imedhamiria kufikisha mawasiliano kwa ukaribu zaidi ili wananchi waweze kuwasiliana kwa lengo la kukuza shughuli mbalimbali za kiuchumi.
“Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita,serikali imekua katika jitihada za kuendeleza utekelezaji wa mipango na mikakati mbalimbali kwa lengo la kuinua sekta ya mawasiliano ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda” amesema Nditiye
Pia alizungumzia kukamilika kwa ujenzi wa awamu ya kwanza na pili ya Mkonga wa Taifa Mawasiliano wenye urefu wa kilomita zaidi ya 7,560 ambao umewezesha utoaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi kwa haraka na ubora nafuu sambamba na kuiwezesha serikali kushusha gharama za mtumiaji wa mwisho.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),Waziri Kindamba amesema mnara huo uliozinduliwa umegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 261 huku akiwakikishia wananchi juu ya utekelezaji wa miradi mingine vijijini na maeneo yasiyo na mvuto kibiashara ili yaweze kuwa na mvuto huo utakaoletwa na athari za mawasiliano huku akikemea tabia ya uharibifu wa miundo mbinu ya mawasiliano.
“Nitoe rai kwa wananchi kulinda minara hii ambayo tutaizindua sehemu mbalimbali nchini,shirika limewekeza kiasi kikubwa cha fedha katika mradi huu hivyo si vyema miundo mbinu hii kuhujumiwa kwani nchi itakua imepoteza kiasi kikubwa cha fedha” amesema Kindamba.
Shirika la Mawasiliano (TTCL),limekua likishirikiana pia na Mfuko wa Mawasiliano kwa wote(UCSAF) katika kuhakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana kwa Watanzania na pia kuviwezesha vikosi vya majeshi yetu kuwa na mawasiliano ya uhakikaya simu za mkononi na intaneti.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.