Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Azungumza na Waziri Zungu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi akimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Azzan Zungu alipofika kwa mazungumzo na kujitambulisha akisisitiza Mikakati yake ya kusimamia suala la Mazingira linaloonekana kukumbwa na Mabadiliko ya Tabia Nchi kwa upande wa Zanzibar.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais {Muungano na Mazingira} Mh. Mussa Hassan Zungu Kushoto akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Wa kwanza kulia ni Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar inayosimamia na kuratibu Muungano na Mazingira kwa upande wa Zanzibar.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais {Muungano na Mazingira} Mh. Mussa Azan Zungu ameahidi kuteua Wataalamu Maalum wa masuala ya Kimazingira watakaopewa jukumu la kuangalia athari za Mazingira zinazoendelea kujitokeza katika maeneo tofauti ya Visiwa vya Unguja na Pemba.
Alisema hatua hiyo ikiwa ni jukumu la Ofisi yake imekuja kuafuatia maeneo mengi hasa zile sehemu zilizo pembezoni mwa Barahi ya Hindi kukumbwa na changamoto mbali mbali za Kimazingira ikiwemo mmong’onyoko wa Ardhi.
Mh. Mussa Azan Zungu alitoa ahadi hiyo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar alipofika kujitambulisha Rasmi baada ya Kuteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kushika wadhifa huo.
Alisema Visiwa vikubwa na hata vile Vidogo ni sehemu muhimu zinazopaswa wakati wote kushughulikiwa na kuangaliwa kwa umakini mkubwa kulingana na maumbile yake ya kuzunguukwa na Maji sehemu zote ili kulinda Mazingira yake licha ya mabadiliko ya Tabia Nchi yanayoikumba Dunia hivi sasa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais {Muungano na Mazingira} alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba atapanga ziara Maalum ya kuangalia hali ya Mazingira katika maeneo ya Zanzibar kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar inayoratibu na kusimamia mambo yote ya Muungano na Mazingira kwa upande wa Zanzibar.
Mh. Zungu aliupongeza Uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dr. Ali Mohamed Shein akisaidiwa na Makamu wake Balozi Seif Ali Iddi kwa usimamizi wao makini wa kuwaletea Maendeleo Wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba.
Alisema Zanzibar imepiga hatua kubwa ya Maendeleo yanayooneka wazi ambayo tayari yanaendelea kustawisha Maisha ya Jamii sambamba na kuongezeka kwa Pato la Taifa lililoshamiri zaidi ndani ya kipindi cha Miaka Mitano inayomalizika hivi sasa.
Naye kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed alimpongeza Mwenza wake kwa upande wa Muungano kwa uteuzi aliopewa na kumuahidi milango iko wazi wakati wote katika kuona jukumu alilokabidhiwa analisimamia vyema kwa upande wa Zanzibar.
Waziri Aboud alisema yapo mambo mengi yanayoendelea kushirikisha Viongozi wa pande zote mbili za Muungano ambayo Waziri Zungu atapaswa kupewa ushirikiano wa kina ili kutekeleza jukumu lake hasa vile vikao vya Wataalamu, Watendaji Waandamizi, Mawaziri na Viongozi wa juu wa pande hizo Mbili wanaounda Kamati ya pamoja na Muungano.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar kwa kiasi kikubwa imefaidika sana na uwepo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar licha ya Wananchi wa pande hizo mbili kuwa na udugu wa Damu kwa Karne nyingi zilizopita kabla ya Muungano huo.
Balozi Seif alimueleza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais {Muungano na Mazingira} kwamba zipo fursa nyingi zinazoendelea kuwafaidisha Wananchi wa Zanzibar ndani ya Ardhi ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande wa Bara.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni pamona na Sekta ya Biashara na Ardhi inayowapa nafasi pana Wananchi wa Zanzibar walioamua kuishi Bara kuendeleza shughuli zao za Uwekezji katika masuala ya Kilimo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais {Muungano na Mazingira} Mh. Mussa Azan Zungu alikuwepo Zanzibar kujitambulisha Rasmi baada ya kuteuliwa kushika Nafasi hiyo iliyoachwa na Mh. George Simba Chawene aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.