Habari za Punde

Mtazamo wa Wananchi katika nafasi ya Mwanamke Kuwa Kiongozi.


Na Mwajuma Juma

WANAWAKE  wametakiwa kujipanga kimkakati kwa kujiandaa vizuri katika kujengeana kiuwezo ktk kupeana fursa za elimu ili waweze kukabili fursa za uongozi.

Hayo yameelezwa na wananchi mbali mbali ambao walikuwa wakizungumzia muono wao juu ya mwanamke kuwa kiongozi hasa katika Kipindi hichi Cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu 2020.

Ishaka Mohammed mkaazi wa Amaan anasema kuwa wanawake wote duniani wamezaliwa kuwa viongozi na uongozi kwao ni asili ambao unaanzia katika familia.

"Kwa mfano mdogo tuangalie kuanzia ktk familia zetu bila kuwepo mwanamke nyumba inakuwa haina hadhi wala heshima inayostahiki", anasema Mohammed.

Hata hivyo anasema kuwa taasisi mbali mbali ziwe za umma ama binafsi zenye viongozi wanawake zimekuwa zikipaa kwa maendeleo kutokana na uongozi,uaminifu,uzalendo na ustadi wa uendeshaji bora na uliotuka  wa mamlaka hizo.

Hivyo anasisitiza kuwa wanawake pindi wanapokabidhiwa dhamana za Uongozi,wapimwe kwa vigezo stahiki vya majukumu yao na sio kupimwa kwa jinsia yao kwani kufanya hivyo watakuwa wanadharauliwa na kubezwa bila kupewa haki yao.

Ali Othman anasema kuwa demokrasia ya kweli lazima izingatie mgawanyo wa madaraka katika makundi mbali mbali yaliyopo katika jamii.

Hivyo wanawake kupewa nafasi za uongozi ni haki yao kwani wengi wao waliokabidhiwa dhamana hiyo wamekuwa viongozi bora na wachapakazi.

"Ili kwenda sambamba na matakwa ya demokrasia inayozingatia haki na usawa, ni lazima jamii zibadilike kimtazamo kwa kuondokana na mifumo kandamizi ya kuwakosesha haki ya uongozi wanawake", anasema.

Kwa upande wake Hassan Vuai mkaazi wa Magomeni anasema kuwa wanawake wanatakiwa kuondokana na dhana ya kusubiri nafasi za uteuzi kutoka katika vyama wanavyovitumikia bali wasimame wenyewe katika majukwaa ya kisiasa kujenga hoja zenye nguvu ya ushawishi wa kubadili fikra jamii ili waaminiwe na kuchaguliwa na sio kuteuliwa pekee.

Nae Mharami Himid mkaazi wa Myende anasema kuwa wanawake wanapaswa kuwa viongozi ili kuweza kisaidiana na wanaume katika mambo mabli mbali mbali za kimaendeleo.

"Mie kwa uono wangu nahisi mwanamke anafaa kuwa kiongozi kwani wao ndio walezi wakuu wa familia zetu, tumeona mengi na kuyashuhudia majumbani mwetu namna wanavyoiweza kazi hiyo", anasema.

Hata hivyo chama Cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana na UN women wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanawasimamia wanawake kuwa viongozi.

Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar dkt. Mzuri Issa anasema kuwa mwanamke ana haki sawa na mwanamme katika kishika nafasi mbali mbali za uongozi.

"Katika kuwa kiongozi hakuna maana kuwa awe mwanamme tu bali sote tuna haki sawa ya kuwa viongozi", anasema.

Afisa miradi wa TAMWA Asha Abdi anasema wanawake wengi wamekuwa wakipata nafasi ya kuwania uongozi katika majimbo ambayo ni vigumu kushinda.

Aidha anasema kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu, anaviomba vyama vya siasa kuwaachia wanawake kuingia kugombea katika majimbo ambayo yana mwelekeo ya kushinda na.sio kuwapa majimbo magumu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.