Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Goerg Simbachawene alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulia leo baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo.
RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza
haja kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuendelea kusimamia amani na usalama wa wananchi pamoja
na mali zao wakati wote.
Hayo aliyasema leo wakati alipokutana na kufanya
mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi George Boniface Simbachawene Ikulu
Jijini Zanzibar alipofika kwa ajili ya kujitambulisha kufuatia kuteuliwa
kushika wadhifa huo hivi karibuni.
Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alimueleza
Waziri huyo kuwa ipo haja kwa Wizara hiyo ya kuendeleza kasi katika
kushughulikia suala zima la kulinda amani na usalama kwa wananchi wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia
Vikosi vyake vyote vya ulinzi ili kuhakikisha amani, usalama na utulivu
unaendelea kudumu hapa nchini.
Alieleza kuwa Serikali ya Mapnduzi ya Zanzibar kwa
upande wake imekuwa ikiendelea kuhakikisha amani, usalama na utulivu unakuwepo
kwa wananchi pamoja na mali zao na ndio maana imeanzisha mradi wa Mji Salama
katika maeneo yote ya Jiji la Zanzibar ukiwemo Mji Mkongwe ambao umepata
umaarufu sana kwa utalii.
Rais Dk. Shein
alieleza kuwa Mradi huo wa Mji Salama mbali ya kuhakikisha usalama kwa
wananchi wa Zanzibar pia una lengo la kuhakikisha wageni wote wakiwemo watalii
wanaotembelea Jiji la Zanzibar wako salama.
Hivyo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa vikosi
vya ulinzi vya Jeshi la Polisi kuhakikisha linaendelea na utaratibu wake wa
kuwalinda wananchi pamoja na mali zao kwa maeneo ya mjini na mashamba hasa zile
sehemu za ukanda wa Utalii.
Aidha, Rais Dk. Shein ameeleza juhudi
zinazoendelea kuchukuliwa na Jeshi hilo la Polisi katika kusimamia ulinzi na
usalama wa wananchi na mali zao pamoja na kusifu juhudi za Jeshi la Uhamiaji
kwa kuendelea kudhibiti na kupambana na wahamiaji haramu hapa Zanzibar.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein ameendelea
kulisisitiza Jeshi la Polisi kuendelea kusimamia vyema usalama wa barabarani
kwa lengo la kuepuka ajali zisizo za lazima pamoja na kuhakikisha sheria na
kanuni elekezi za barabarani zinafuatwa.
Aliongeza kuwa kutokana na juhudi za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar za kuimarisha miundombinu
ya barabara hatua hiyo imepelekea madereva wengi kuvunja sheria kwa kwenda
mwendo wa kasi na hatimae kuhatarisha maisha kwa wananchi.
Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kumpongeza
Waziri Simbachawene kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dk. John Pombe Magufuli kushika wadhifa huo na kumuahidi kuwa yeye pamoja na
Serikali anayoiongoza wataendelea kumsaidia na kuipa mashirikiano Wizara
anayoiongoza hasa ikizingatiwa kuwa ni
Wizara ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili iendelee kufanya kazi zake
vyema.
Nae Waziri George Boniface Simbachawene, Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa atahakikisha amani
na usalama vyote kwa pamoja vinaendelea
kudumishwa hapa nchini ili Tanzania iendelee kusifika ndani na nje ya Bara la
Afrika.
Waziri Simbachawene alimueleza Rais Dk. Shein kuwa
ni jukumu la Wizara hiyo la kuhakikisha usalama na amani kwa wananchi pamoja na
mali zao unakuwepo wakati wote na kusisitiza kuwa kwa mashirikiano ya pamoja ya
vikosi vya ulinzi na usalama jambo hilo litaendelea kutekelezwa.
Waziri huyo alitoa pongezi zake kwa mashirikiano
makubwa kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoendelea kuyapata Wizara
anayoiongoza pamoja na vikosi vyote vya ulinzi na usalama vilivyomo katika
Wizara hiyo.
Aidha, Waziri Simbachawene alitumia fursa hiyo
kutoa pongezi kwa Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa kupatiwa eneo la
kujenga Ofisi za Idara ya Uhamiaji hapa Zanzibar.
Pamoja na hayo, Waziri huyo alimuhakikishia Rais
Dk. Shein kuwa juhudi za makusudi zitaendelea kuchukuliwa na Jeshi la Polisi
katika kuhakikisha sheria na kanuni zinafuatwa hasa zile za usalama barabarani.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment