Habari za Punde

Taasisi ya Mwanaharakati Siti Bint Saad Kumtangaza Mwanaharakati Huyo Pamoja na Kazi Zake Ndani na Nje ya Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akikabidhiwa picha ya Siti Binti Saad, “ikimoonesha Bi. Siti Bint Saad na Bwa. Ali Muhsin, aliyemuibua katika fani ya  uimbaji ” akikabidhi Katibu wa Taasisi hiyo Dkt. Mohammed Omar na (kushoto kwa Rais) Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwanaharakati Bibi Siti Bint Saad.Bi.Nasra Mohammed Hilal, hafla hiyo imefanyika leo 10-3-2020,Ikulu Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameitaka Taasisi ya Mwanaharakati Bibi Siti bint Saad kumtangaza mwanaharakati huyo pamoja na kuzitangaza kazi zake ili zifahamike ndani na  nje ya Zanzibar.

Hayo ameyasema leo, Ikulu Jijini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Taasisi ya Mwanaharakati Bibi Siti bint Saad ukiongozwa na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Bi Nasra Mohamed Hilal pamoja na Mshauri wa Taasisi hiyo Bwana Abdalla Mwinyi Khamis.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa Mwanaharakati Bibi Siti bint Saad amefanya mambo mengi ambayo yanapaswa jamii iyafahamu na hilo litafanikiwa iwapo Taasisi hiyo itachukua jukumu lake hilo na kulifanyia kazi ipasavyo.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa mengi aliyoyafanya Bibi Siti Bint Saad hayaonekani hivi sasa na mengine yamebakia kwenye picha za kubuni pamoja na kuandikwa vitabuni tu, hivyo, ni jambo jema Taasisi hiyo ikafanya juhudi za makusudi katika kuhakikisha Mwanaharakati huyo anatambulikana ndani na nje ya Zanzibar.

Aliongeza kuwa Taasisi hiyo ni vyema ikachukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha kazi pamoja na shughuli za Mwanaharakati huyo alizozifanya katika uhai wake zinajulikana na jamii iliyopo pamoja na vizazi vijavyo.

Aidha, Rais Dk. Shein ambaye pia, ni Mshauri Mkuu wa Taasisi hiyo alisema kuwa katika suala zima la kumtangaza Bibi Siti binti Saad ni vyema zikatumika kazi zake alizozifanya ikiwa ni pamoja na nyimbo zake ambazo zilikuwa na sifa, mvuto, ghaiba na elimu kubwa kwa jamii wakati huo na huu uliopo.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa nyimbo za Bibi Siti Binti Saad zimeweza kuelemisha, kuburudisha, kuadabisha na kufunza jamii kwani ziligusa katika mambo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa iwapo kazi za Bibi Siti binti Saad zitasambazwa zikiwemo CD za nyimbo zake zitapata soko kubwa sana katika ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki, Kaskazini na Kusini mwa Afrika pamoja na nje ya Bara hilo.

Alisisitiza kuwa hatua hiyo ni nzuri ambayo mbali ya kumuenzi Mwanaharakati huyo pia, itasaidia kuzitangaza kazi zake sambamba na kuongeza mtaji kwa Taasisi hiyo.

Alieleza kuwa soko la nyimbo za Bibi Siti bint Saad litapatikana kutokana na historia ya msanii huyo ambaye alikuwa ni mwanamke jasiri na aliyekuwa na kipaji cha sanaa na sauti nzuri iliyowavutia watu wengi ambayo bado watu wanatamani kuisikia na kumfahamu vilivyo Mwanaharakati huyo.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein aliipongeza Taasisi hiyo kwa kuendelea na harakati za kuzitunza kazi za Mwanaharakati huyo huku akisisitiza haja ya kuongeza kasi ya kumtangaza msanii huyo ambaye alipata umaarufu mkubwa ndani na nje ya Zanzibar.

Pia, Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa Taasisi hiyo kuandaa Mpango maalum wa muda mrefu, wakati na muda mfupi katika kumtangaza Mwanaharakati huyo ili historia yake iendelee kutambulika.

Rais Dk. Shein aliutaka uongozi wa Taasisi hiyo kutovunjika moyo kwa yale yote ambayo yalibuniwa na bado hayajafikia malengo yaliokusudiwa na kueleza kuwa waendelee na subira huku wakipanga mipango na mikakati ya kuyafanikisha.

Nae Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwanaharakati Bibi Siti bint Saad, Bi Nasra Mohamed Hilal alimueleza Rais Dk. Shein mafanikio yaliopatikana katika Taasisi hiyo pamoja na malengo yaliyowekwa.

Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Taasisi hiyo imeweza kufanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti mbali mbali zinazohusiana na Mwanaharakati Bibi Siti binti Saad pamoja na makongamano ya Kiswahili, kutoa mafunzo ya uchoraji, kutoa vyeti vya uwanachama na mengineyo.

Aidha, Mwenyekiti huyo alieleza kufarajika kwake kwa kuwa na vijana waliojiunga katika Taasisi hiyo wenye fani mbali mbali ambao wamekuwa wakitoa msaada mkubwa kwa kuiendeleza na kuiimarisha Taasisi hiyo.

Pia, Mwenyekiti huyo alieleza miradi mbali mbali ambayo imeandaliwa na Taasisi hiyo yenye lengo la kuongeza kipato kwa Taasisi pamoja na kuitangaza Taasisi hiyo kwa kuanzisha tovuti yake, kuanzisha vijarida na mambo mengineyo.

Pia, uongozi huo ulieleza azma ya kuanzisha redio ya ‘Siti Redio fm” kwa ajili ya kuzitangaza kazi za Taasisi hiyo sambamba na hivi sasa kumiliki Televisheni Mtandao. 

Bibi Siti Binti Saad alizaliwa katika kijiji cha Fumba mnamo mwaka 1870 na kuishi miaka 80 ambayo iligawika kwa miaka 40 ya kwanza ya uhai wake akiwa kwa jina la Mtumwa Binti Saad wakati huo akiwa mfinyanzi wa vyungu vya kupikia na kazi nyengine za usanii wa mikono.

Miaka 40 ya mwisho wa maisha yake kuanzia mwaka 1910 hadi 1950 alipofariki alikuwa msanii na muimbaji kwa hivyo alikuwa maarufu kwa jina la Bibi Siti bint Saad ambapo nyimbo zake zilipata umaarufu mkubwa kwa kua alikuwa muimbaji wa kwanza wa kike kuimba nyimbo za taarab tena kwa lugha ya Kiswahili.

Taasisi ya Mwanaharakati bibi Siti bint Saad ilizinduliwa rasmi Januari 7 mwaka 2014 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Wakati huo huo, Taasisi hiyo ilimkabidhi Rais Dk. Shein ambaye pia, ni Mshauri Mkuu wa Taasisi hiyo kadi yake ya uwanachama, ripoti ya miaka mitano, kazi inazozifanya taasisi hiyo pamoja na picha yenye maelezo kuhusu kuibuliwa kwa muimbaji Siti bint Saad na bwana Muhsin Bin Ali.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.