Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Zanzibar Mustafa Aboud Jumbe akizungumza na Jumuiya ya Gari za Abiria kwa mikoa mitatu ya Unguja juu ya hatua zinazohitajika kuchukuliwa ili kudhibiti kuenea janga la maradhi ya Corona, katika Ukumbi wa Bodi ya Usafiri barabarani Mwanakwerekwe Zanzibar .
Mkuu wa Trafik Zanzibar ambae pia ni Kamishna Msaidizi wa Polisi Robert Hussein akitoa tahadhari kwa Jumuiya ya Gari za Abiria ya mikoa mitatu ya Unguja juu ya hatua zinazohitajika kuchukuliwa ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya Corona, Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Bodi ya Usafiri barabarani Mwanakwerekwe Zanzibar.
Wanajumuiya ya Gari za Abiria wa Mikoa mitatu ya Unguja wakisikiliza maelezo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji,zanzibar Mustafa Aboud Jumbe juu ya hatua zinazohitajika kuchukuliwa ili kudhibiti kuenea janga la maradhi ya Corona, Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Bodi ya Usafiri barabarani Mwanakwerekwe Zanzibar
Picha zote na Khadija Khamis Maelezo Zanzibar
Na Kijakazi Abdalla - Maelezo 02/04/2020
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi ,Mawasiliano na Usafirishaji Mustafa Aboud Jumbe amezitaka jumuiya za gari za abiria kufuata utaratibu uliowekwa na Wizara ya Afya kwa lengo la kuepuka maambukizo ya maradhi ya corona.
Hayo ameyasema katika Ukumbi wa Bodi ya Usafiri Barabarani Mwanakwerekwe katika kikao cha Idara ya Leseni na jumuiya za gari za abiria kwa Mikoa mitatu ya Unguja.
Amesema ni vyema kwa madereva na makonda kufuata masharti yaliyowekwa na Wizara ya afya ili kudhibiti kuenea kwa janga la maradhi ya corona.
“Ni vyema kufuata masharti yaliowekwa na wataalamu kwani maradhi hayo si ya kuyafanyia mzaha hata kidogo”.Amesema katibu.
Aidha amewataka viongozi wa jumuiya kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanachukua tahadhari kwa vyombo vya usafiri kwa abiria wanaotumia usafiri wa nchi kavu ili kudhibiti kuenea kwa maradhi ya corona.
Nae Kamishna Msaidizi wa Polisi ambae pia ni Mkuu wa Trafik Zanzibar Robert Hussein amewataka madereva na makonda wa gari za abiria kufuata maelekezo yanayotolewa na jeshi la polisi kwani kwenda kinyume ni kosa kisheria.
Amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi litamchukulia hatua dereva na Konda atakaebainika anavunja sheria na kuwahakikishia kuwa hatua zitachukuliwa hapo kwa hapo.
“Jeshi la Polisi lipo kwa kulinda mali za raia na halina nia ya kumkomoa mwananchi, hivyo ni vyema kila mtu kufuata muongozo uliowekwa na jeshi hilo”.Amesema Mkuu huyo.
Miongoni mwa maazimio ya kikao hicho ni pamoja na kuwataka wakuu wa jumuiya kuhakikisha kila gari inachukua abiria kwa idadi walioruhusiwa.
Aidha viongozi wa jumuiya ya gari za abiria wametakiwa kutoa elimu ya uelewa wa maradhi ya corona kwa madereva na makonda ili kuweza kudhibiti kuenea mambukizo ya maradhi hayo pamoja na kupulizwa dawa gari zote za abiria.
Vilevile mabaguani wametakiwa kusimamia zoezi la abiria kukaa masafa ya kutosha wanapokuwa vituoni pamoja na gari itayobainika kuchukua abiria kinyume na uwezo iliopewa ishushwe abiria na kuwekwa kituoni.
Aidha Idara ya Usafiri na Leseni kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kuangalia gari chafu na kuchukuliwa hatua pamoja na jumuiya kuhakikisha gari hazikatishi kutoa huduma mpaka usiku ili kuepusha mrundikano wa abiria vituoni.
No comments:
Post a Comment