JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
Simu: +255-26-232-2484/232-4560 Mlimwa Kusini,
11 Barabara ya Edward Sokoine,
Nukushi: +255-26-232-1955, S. L. P. 980,
1, APRILI, 2020
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MAJALIWA: ATAKAYETHIBITIKA NA CORONA
APELEKWE ENEO MAALUMU BILA KUJALI CHEO
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesisitiza kuwa mtu yeyote akithibitika kuwa na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) apelekwe eneo maalum bila kujali cheo chake na atalala palipoandaliwa.
Amewataka Watanzania
wazingatie masharti ya afya kwa kufuata ushauri unaotolewa na Serikali kwa
sababu hivi sasa nchi yetu na dunia kwa ujumla inapitia katika kipindi kigumu pia,
waendelee kupuuza taarifa za uzushi zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo
leo (Jumatano, Aprili 1, 2020) akiwasilisha Bungeni hotuba kuhusu Mapitio na
Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za
Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2020/2021, Bungeni jijini
Dodoma.
Amesema
Machi 11, 2020, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza mlipuko wa Homa Kali
ya Mapafu ijulikanayo kama COVID-19
inayosababishwa na virusi vya CORONA kuwa ni janga la Kimataifa. Aidha, tarehe
16 Machi, 2020 Serikali ilitangaza kuwepo kwa mgonjwa wa kwanza nchini, ni
muhimu wananchi kuchukua tahadhari.
Waziri Mkuu amesema tangu kugundulika
kwa ugonjwa huo, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika
kukabiliana na ugonjwa huu ikiwa ni pamoja
na kuimarisha ukaguzi, upimaji na ufuatiliaji wa wasafiri wanaoingia nchini.
Amesema la hatua hizo ni kuwabaini
wasafiri wanaoonesha dalili za ugonjwa wa COVID-19 au wenye viashiria hatari,
hata hivyo mashirika mengi yamesitisha ndege zao kwa kukosa abiria. “Abiria wote
waingiao nchini hupelekwa Isolation
house.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema
katika kukabiliana na virusi vya corona, Serikali ilitoa maelekezo mbalimbali
ikiwa ni pamoja na yafuatayo kusitisha Mbio za Mwenge wa Uhuru na fedha
zilizotengwa kwa ajili ya jukumu hilo zitumike kusaidia hatua za kukabiliana na
janga hilo.
“Mbali na kusitidsha mbio za mwenge
Serikali imesitisha michezo yote inayokusanya makundi ya watu ikiwemo ligi kuu
ya Tanzania Bara, ligi daraja la kwanza, ligi daraja la pili na aina nyingine
za michezo.”
Amesema Serikali pia imesitisha shughuli zote za
elimu kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari, vyuo vya kati hadi vyuo vikuu
pamoja na semina, warsha, makongamano na mikutano yote ya ndani na ya hadhara
yenye kuhusisha mjumuiko wa watu wengi.
Amesema suala lingine ni kuwatenga abiria waingiao
nchini kwenye maeneo maalum kwa siku 14 ili kufuatilia hali zao mpaka
tutakapojiridhisha kuwa hana ugonjwa ili kuhakikisha maambukizi ya virusi hivyo
hayasambai kwa jamii.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali
inawasisitiza Watanzania kufuata kanuni za kudhibiti maambukizi ikiwemo kunawa mikono
kwa maji yanayotiririka na sabuni, kukinga unapokohoa na kupiga chafya,
kutopeana mikono, kukaa au kusimama kwa umbali na jirani yako.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kuwaasa
Watanzania wenye safari zisizo za lazima kwenye nchi zenye maambukizi ya virusi
vya Corona, kusitisha safari hizo, na hatua zingine zitafuata.
Amesema Serikali inaendelea
na usimamizi wa karibu sambamba na kufanya tathmini na kuchukua hatua kadhaa. “Tumeunda
Kamati za kitaifa tatu zinazosimamia ugonjwa huu, niendelee kusisitiza kuwa
sote tuzingatie maelekezo yaliyotolewa na Serikali toka tulipoanza kampeni ya
kupambana na ugonjwa huu.”
Wakati huo huo, Wazirti Mkuu amesema Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake inaliomba liidhinishe
jumla ya sh. 312,802,520,000; kati ya fedha hizo, sh. 88,429,156,000 ni kwa
ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 224,373,364,000 ni kwa ajili ya matumizi ya
maendeleo.
Vilevile
Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya sh. 121,786,257,000 kwa ajili
ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, sh. 113,567,647,000 ni kwa ajili ya matumizi
ya kawaida na sh. 8,218,610,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
(MWISHO)
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA
JUMATANO,
APRILI 1, 2020.
No comments:
Post a Comment