Habari za Punde

UDHIBITI WA MCHANGA WALETA FARAJA - SMZ


Na.Himid Choko.                                                                                                                             
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema, kumekuwa na mafanikio makubwa  kutokana na kuweka mfumo mzuri wa udhibiti  wa matumizi ya maliasili zisizoresheka ikiwemo mchanga.
Akiwasilisha Ripoti ya utekelezaji wa Maagizo ya Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi ya Mwaka 2019/2020 kwa wizara yake, Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mmanga Mjengo Mjawiri amesema miongoni mwa mafanikio hayo ni kupungua uchimbaji holela wa mchanga, kifusi, mawe na kokoto.
Amesema hatua hiyo pia imepelekea ongezeko la matumizi bora ya mali asili   na hivyo kupunguza athari za kimazingira katika maeneo ya uvunaji wa rasilimali hizo.
Mheshimiwa Mjawiri ameongoza kusema kuwa, udhibiti wa mali asili  hizo kumepelekea kupungua kwa bei  na  upatikaji  mzuri wa mchanga kwa mahitaji ya wananchi na Miradi ya Maendeleo.
Aidha, Waziri Mjawiri amesema  wizara yake imeweza kuongeza mapato yanayotokana na mali asili  zisizorejesheka.
Mafanikio mengine yaliyopatikana ni  kuongezeka kwa mapato yanayotokana na rasilimali zisizorejesheka kutoka shilingi 558,000,000 mwaka 2015  mpaka  shilingi 16,549,056  hadi kufikia mwezi Februari 2020.” Alisisitiza Mheshimiwa Mjawiri.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Mjawiri amesema Wizara yake inaendelea na utaratibu wa upandaji wa miti katika maeneo ya uchimbanji wa mali asili hizo ambapo jumla ya Hekta 10.7 katika maeneo ya Pangatupu, na Donge Chechele kwa mwaka 2019/2020.
Nae, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha,  Biashara na kilimo ya Baraza la Wawakilishi  Mheshimiwa Dkt. Mwinyihaji Makame akitoa maoni ya Kamati yeke kuhusiana na Ripoti hiyo ameishauri Serikali kuyaruhusu Makampuni makubwa  pamoja na taasisi zenye matumizi makubwa ya mchanga  kuagizishia mali asili hiyo kutoka nnje ya zanzibar kwa utaratibu maalum ili mchanga uliopo  uendelee  kutumiwa na wananchi wa kawaida.
 Imetolewa na Divisheni ya Itifaki na Uhusiano,
Baraza la Wawakilishi, Zanzibar.
Jumatatu, Aprili 14, 2020

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.