Habari za Punde

HOTUBA YA WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2020/2021

HOTUBA YA WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2020/2021

UTANGULIZI
1.             Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Baraza lako Tukufu liingie katika Kamati ili niweze kutoa maelezo ya makadirio ya mapato na matumizi ya Fedha ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

2.             Mheshimiwa Spika, Kwanza kabisa, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma kwa kutujaalia uhai, uzima na afya njema. Vile vile akatuwezesha tukakutana katika kikao hiki cha bajeti katika kipindi cha uongozi wa Awamu ya Saba ya Kiongozi wetu mahiri Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Namuomba Mwenyezi Mungu atuzidishie kheri naneema zake na anipe uwezo na uwasilishaji fasaha wa hotuba hii ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yangu. Pia namuomba Mwenyezi Mungu atujaalie wasaa wajumbe wote wa kuichangia vizuri na hatimae Baraza lako tukufu liweze kuipitisha kwa kauli moja.

3.             Mheshimiwa Spika, pili, nachukua nafasi hii kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa uongozi wake imara, wenye busara na moyo thabiti katika kusimamia uimarishaji wa huduma za jamii kwa wananchi wake ikiwemo huduma ya elimu. Pongezi za pekee kwa kutimiza miaka kumi ya uongozi wake ulioleta maendeleo makubwa katika nchi yetu. Maendeleo yaliyotokana na uongozi wake imara ambao umehakikisha kuwa changamoto zote zinazowakabili watoto na vijana wote katika kupata elimu zinapatiwa ufumbuzi kikamilifu ikiwemo kufuta michango ya wazazi na Serikali kutoa fedha za ruzuku kwa skuli kufidia fedha zilizokuwa zikitolewa na wazazi kwa skuli. Mwenyezi Mungu amzidishie umri mrefu wenye kheri, afya njema na maarifa zaidi ili aendelee kuiongoza na kuiendeleza nchi yetu. Vile vile, napenda kutoa pongezi zetu na shukurani za dhati kwa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, kwa utendaji wake mzuri, uliokuwa karibu na Wizara yetu na wadau mbalimbali wa elimu wa ndani na nje ya nchi pamoja na michango yake binafsi katika kuiendeleza sekta ya elimu.

4.             Mheshimiwa Spika, Vilevile,nachukua fursa hii kukupongeza wewe, Naibu Spika pamoja na Mwenyekiti wa Baraza kwa mashirikiano yenu na miongozo mizuri mnayotupatia inayopelekea kupata ufanisi katika utendaji wa majukumu yetu unaochangia katika kuleta maendeleo ya Taifa letu. Namuomba Mwenyezi Mungu akuzidishieni busara, hekima, umahiri na uadilifu katika kuliongoza Baraza hili tukufu.

5.             Mheshimiwa Spika, Naomba pia shukurani za dhati nizifikishe kwa wajumbe wote wa Baraza hili Tukufu na hasa Wajumbe wa Kamati ya Ustawi wa Jamii chini ya uongozi mahiri wa Mwenyekiti wake Mheshimiwa Mwanaasha Khamis Juma kwa ushauri na maelekezo ya kimaendeleo wanayotupatia katika utekelezaji wa shughuli zetu mbalimbali wanapopata muda wa kuwa nasi katika taasisi za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.

6.             Mheshimiwa Spika, Kwa dhati kabisa, napenda kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Simai Mohammed Said, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kunipa mashirikiano ya karibu yaliyowezesha kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa mpango wa elimu. Aidha, nawapongeza watendaji wote wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali wakiwemo Katibu Mkuu, Manaibu Katibu Wakuu, Wakurugenzi, Wajumbe wa Bodi mbali mbali za Elimu, Maafisa wa ngazi mbalimbali wa Wizara, Viongozi na watendaji mbalimbali wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bila kuzisahau Kamati zetu za skuli kwa mashirikiano yao makubwa katika kuleta maendeleo ya elimu. Aidha, shukurani ziwafikie walimu, wazazi, wanafunzi na washirika wote wa elimu wa ndani na nje ya nchi kushiriki kikamilifu katika kusaidia harakati za utoaji na upatikanaji wa huduma ya elimu iliyo bora kwa watoto, vijana na wazee wetu waliokosa fursa hiyo. Mola awazidishie moyo wa imani na upendo ili michango yao iendelee kuwapatia elimu wahitaji wote kwa kiwango chenye ubora.

7.             Mheshimiwa Spika, Mwisho nawashukuru sana watendaji wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa ushirikiano wao ambao umechangia katika kuimarisha huduma za elimu katika mwaka 2019/20. Nimatumaini yetu kuwa ushirikiano huo utaimarika zaidi katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za elimu katika Taifa letu kwa kupitia kauli mbiu ya Wizara yetu ya “Elimu Bora Kwanza”. 

8.             Mheshimiwa Spika, kabla ya kuelezea utekelezaji wa mipango ya elimu ya Mwaka 2019/2020 na matarajio ya mwaka 2020/2021, napenda kuelezea walau kwa ufupi maendeleo tuliyoyapata katika kipindi cha miaka 10 (2011-2020) chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

HALI YA MAENDELEO YA ELIMU KWA KIPINDI CHA MIAKA 10, 2011-2020.
9.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2011 hadi 2020, miundombinu ya elimu imeimarika kwa kiwango kikubwa katika ngazi zote za elimu. Idadi ya skuli za maandalizi imeongezeka kutoka 242 (29 za Serikali na 213 za binafsi) mwaka 2011 hadi kufikia skuli 368 (35 za serikali na 328 za binafsi) mwaka 2020. Aidha, uandikishaji wa wanafunzi katika ngazi yaelimu ya maandalizi umeongezeka kutoka wanafunzi 33,229 mwaka 2011 ikiwa sawa na asilimia 37.1 na kufikia wanafunzi 92,098 mwaka 2020 sawa na asilimia 86.0.

10.         Mheshimiwa Spika, katika kuongeza ushiriki wa watoto katika ngazi ya elimu ya maandalizi, Wizara ilianzisha utoaji wa elimu ya maandalizi kupitia vituo vya Tucheze Tujifunze (TuTu) hasa katika maeneo ambayo hayakuwa naskuli. Idadi ya Vituo vya TuTu imeongezeka kutoka 179vyenye jumla ya wanafunzi 7,022 mwaka 2011na kufikia vituo 366 vyenye jumla ya wanafunzi 17,769 mwaka 2020.

11.         Mheshimiwa Spika, kwa upande wa elimu ya msingi, idadi ya skuli zimeongezeka kutoka skuli 200 mwaka 2011 zikiwa na wanafunzi 237,690 sawa na asilimia 118.5 ya uandikishaji mwaka 2011 na kufikia skuli 431 mwaka 2020 zenye wanafunzi 313,097 sawa na asilimia 120.7mwaka 2020. 

12.         Mheshimiwa Spika, idadi ya skuli za sekondari imeongezeka kutoka skuli 201 mwaka 2011 na kufikia 213 mwaka 2020. Hii imepelekea ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza hadi cha Nne kutoka wanafunzi 77,671 sawa na asilimia 67.2 mwaka 2011 na kufikia wanafunzi 124,493 sawa na asilimia 79.5 mwaka 2020. Skuli za msingi na sekondari za kisasa zenye majengo ya ghorofa zimeanzishwa chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein.

13.         Mheshimiwa Spika, kwa upande wa elimu ya Sekondari ya juu (kidato cha 5 hadi kidato cha 6) uandikishaji wa wanafunzi umeongezeka kutoka wanafunzi 4,073 mwaka 2011 na kufikia wanafunzi 5,679 mwaka 2020.

14.         Mheshimiwa Spika, Ubora wa elimu umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka kama inavyodhihirika katika matokeo ya mitihani ya Taifa. Katika mitihani ya kidato cha pili, idadi ya wanafunzi waliofaulu na kuteuliwa kuendelea na masomo ya kidato cha tatu imeongezeka kutoka watahiniwa 11,562 ikiwa ni sawa na asilimia 58.2 ya watahiniwa wote wa mwaka 2010/2011 na kufikia watahiniwa24,946 sawa na asilimia 76.8 ya watahiniwa wote mwaka 2019/2020.

15.         Mheshimiwa Spika, katika mtihani wa kidato cha nne, idadi ya watahiniwa waliofaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza na pili imeongezeka kwa zaidi ya mara Sita (6) kutoka watahiniwa 260 mwaka 2010/11 na kufikia wanafunzi 1,808 mwaka 2019/2020. Aidha, matokeo ya mtihani ya Kidato cha sita nayo yameimarika ambapo idadi ya watahiniwa imeongezeka kutoka 1,959 mwaka 2010/2011 hadi kufikia watahiniwa 2,065mwaka 2019/2020. Idadi ya wanafunzi waliofaulu imeongezeka kutoka wanafunzi 1,517mwaka 2010/2011 ikiwa ni sawa na asilimia 77.4 ya watahiniwa hadi kufikia wanafunzi 2,000 sawa na asilimia 96.9 mwaka 2019/2020. Aidha, idadi ya wanafunzi waliopata daraja la kwanza (Division 1) imeongezeka kutoka wanafunzi 24 mwaka 2010/2011 na kufikia wanafunzi 188 mwaka 2019/2020.

16.         Mheshimiwa Spika, chini ya Uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein akiwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar Chuo kimepiga hatua kubwa kwa kuimarika kwa miundombinu na kuongezeka kwa idadi ya skuli, Taasisi, programu mbali mbali za masomo, miongoni mwa skuli mpya ni skuli ya kilimo, skuli ya utibabu wa Meno na Taasisi ya Masomo ya Ubaharia. Aidha programu mbalimbali zimezinduliwa zikiwemo za Shahada ya kwanza ya Uuguzi, Shahada ya kwanza ya Sayansi na Kilimo, Shahada ya Utabibu wa Meno na Shahada ya Uzamili ya Lugha na Elimu. Vilevile katika kipindi cha miaka 10 iliyopita Chuo cha SUZA kimetanuliwa kwa kuunganishwa na vyuo vitano vikiwemo Chuo cha Afya, Chuo cha Utalii, Chuo cha Kilimo, Chuo cha Usimamizi wa Fedha na kufungua kampas ya Chuo cha ualimu cha Benjamin Wiliam Mkapa Pemba.

17.         Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka tisa bajeti ya sekta ya elimu imeongezeka kwa asilimia 91.4 kutoka TSh. 93,468,089,000/= mwaka 2010/2011 hadi kufikia TSh. 178,917,149,000/= mwaka 2019/2020. Kuongezeka kwa matumizi ya Serikali kwa sekta ya elimu kunadhihirisha namna Serikali ilivyotoa kipaumbele katika kufanikisha utekelezaji wa kauli mbiu ya “Elimu Bora Kwanza”.

18.         Mheshimiwa Spika, baada ya muhutasari huo, naombasasa nitoe maelezo ya utekelezaji wa kazi kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

MIRADI YA SEKTA YA ELIMU
19.         Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Wizara ilitekeleza kazi zake kupitia miradi mikuu mitano, ifuatayo: -
1.      Uimarishaji wa Elimu ya Maandalizi
2.      Uimarishaji wa Elimu ya Msingi
3.      Uimarishaji wa Elimu ya Lazima
4.      Uimarishaji wa Elimu Mbadala na Amali
5.      Miundombinu katika elimu

UTEKELEZAJI WA KAZI ZA WIZARA KWA MWAKA 2019/20
20.         MheshimiwaSpika, sasa naomba kuwasilisha utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya elimu kwa mwaka wa fedha wa 2019/20 kwa kupitia programu sita za Wizara yangu.

MUUNDO WA PROGRAMU
21.         Mheshimiwa Spika, programu kuu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ni hizi zifuatazo: -

Programu ya 1: Elimu ya Maandalizi na Msingi
Programu ya 2: Elimu ya Sekondari.
Programu ya 3: Elimu ya Juu
Programu ya 4: Elimu Mbadala na Mafunzo ya Amali
Programu ya 5: Ubora wa Elimu
Programu ya 6: Uongozi na Utawala

MAELEZO YA UTEKELEZAJI KWA PROGRAMU
22.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20 Wizara ilitekeleza kazi zakekupitia Programu nilizoziainisha kwa kuzingatia maendeleo ya elimu ya Kitaifa na Kimataifa ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2020, lengo la MKUZA III, vipaumbele vya sekta pamoja na lengo la nne la Maendeleo Endelevu Duniani.

23.         Mheshimiwa Spika, Programu hizo zilitekelezwa kwa mashirikiano kati ya Serikali, Jamii na Washirika wa Maendeleo wa ndani na nje ya Zanzibar. Programu zilitengewa jumla ya TSh. 178,917,149,000/-. Kati ya fedha hizo, TSh. 39,725,500,000/- kwa ajili ya matumizi ya kazi za kawaida, TSh. 65,817,601,000/- matumizi ya mshahara na TSh. 73,374,048,000/- kwa kazi za maendeleo. Kati ya fedha za maendeleo, TSh. 5,800,000,000/- ni mchango wa SMZ na TSh. 67,574,048,000/- ni mchango wa wahisani wakiwemo Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Afrika (Badea), Mfuko wa OPEC, Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na Benki ya Dunia.

24.         Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili, 2020, jumla ya TSh. 115,519,162,374/= sawa na asilimia 65 ya makadirio zilipatikana. Kati ya fedha hizo, TSh. 58,077,204,998/= sawa na asilimia 88 zilitumika kulipia mishahara ya wafanyakazi na TSh. 25,319,542,615/= sawa na asilimia 64 zimetumika kwa ajili ya kazi za kawaida. Kwa upande wa fedha za maendeleo, jumla ya TSh. 32,122,414,761/=zilipatikana. Kati ya fedha hizo TSh. 1,453,046,000/= sawa na asilimia 25 ni mchango wa Serikali na TSh. 30,669,368,761/= sawa na asilimia 45 ni kutoka kwa wahisani. Jadweli Nam. 10(b) inatoa ufafanuzi zaidi.

25.         Mheshimiwa Spika, Utekelezaji halisi wa Programu za Wizara yangu ni kama ifuatavyo: -

PROGRAMU YA KWANZA:
ELIMU YA MAANDALIZI NA MSINGI
26.         Mheshimiwa Spika, Programu hii inahusika na uimarishaji na utoaji wa elimu ya maandalizi na msingi kwa wanafunzi wenye umri kati ya miaka minne na kumi na mbili. Programu hii inatekelezwa kwa sehemu kubwa katika kazi za kawaida kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mashirikiano ya karibu sana na Wizara yangu.

27.         Mheshimiwa Spika, Programu hii ilitengewa jumla ya TSh. 9,010,580,000/-. Kati ya fedha hizo TZS. 157,169,000/- kwa ajili ya kazi za kawaida, Tsh. 383,709,000/- kwa ajili ya malipo ya mishahara ya wafanyakazi na TZS. 8,469,702,000/- kwa kazi za maendeleo kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Hadi kufikia Aprili, 2020, jumla ya TSh. 2,980,270,068/= sawa na asilimia 33 zilipatikana.
28.         Mheshimiwa Spika, Utekelezaji halisi wa programu hii ni kama hivi ifuatavyo: -
                           i).          Wanafunzi katika skuli 27 za msingi Unguja na Pemba wanafaidika na huduma ya chakula.
                         ii).          Kuongezeka kwa uandikishaji wa wanafunzi katika ngazi za maandalizi na msingi. Jumla ya wanafunzi 92,098 sawa na asilimia 86.0 wameandikishwa katika madarasa ya maandalizi kwa mwaka 2020 ikiwa ni ongezeko la asilimia 6.6 ikilinganishwa na wanafunzi 85,974 sawa na asilimia 81.4 walioandikishwa mwaka 2019.
                       iii).          Jumla ya seti 11,560 za madawati ya wanafunzi watatu watatu wa skuli za msingi zimenunuliwa kutoka China.  Jumla ya seti 7065 zimeshapokelewa na kusambazwa katika skuli za msingi Unguja na Pemba. Seti 4,495 za madawati zinatarajiwa kupokelewa katika mwezi Julai 2020
                       iv).          Skuli za maandalizi za Serikali vimepatiwa vifaa kufundishia na kujifunzia, vikiwemo mikasi 1,260, rangi za maji pc 630, brashi pc 1,080, gundi pc 617, vifutio pc 492, peni za ubao pc 630, manila bunda 87, gundi za karatasi pc 214, rangi za nta 360, vibao vya kusomea pc 1700 na penseli pakiti 35.
                         v).          Jumla ya vituo 20 vipya vya Tucheze Tujifunze (TuTu) vimefunguliwa katika Wilaya ya Kaskazini “A” (5), Wilaya ya Magharibi “A” (5) kwa Unguja na Wilaya ya Wete (5), Wilaya ya Chakechake (5) kwa Pemba. Idadi ya vituo vya TuTu imefikia 364 mwaka 2020 ikilinganishwa na vituo 342 mwaka 2019. Kati ya vituo hivyo 172 vipo Unguja na vituo 192 vipo Pemba. Aidha, walimu 728 wa vituo vya TuTu wamelipwa posho lao la kila mwezi pamoja na kuwapatia chakula wanafunzi wote wa ngazi ya elimu ya maandalizi wa skuli za maandalizi za Serikali Unguja na Pemba.
                       vi).          Vifaa vya kufundishia na kujifunzia vimenunuliwa na kusambazwa katika vituo 20 vya TuTu Unguja na Pemba. Aidha, vituo hivyo vimesaidiwa vifaa vya ujenzi yakiwemo mabati, saruji na matofali.
                     vii).          Jumla ya skuli 27 za jamii zikiwemo 11 Unguja na 16 Pemba zimeanzishwa pamoja na kupatiwa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.Aidha, jumla ya walimu 54 wa skuli za jamii na wasaidizi 26 wa vituo vya TuTu wamepatiwa mafunzo ya maandalizi kupitia Programu ya “Madrasa Early childhood”. 
                   viii).          Jumla ya walimu 412 wa skuli za maandalizi pamoja na wavituo vya TuTu Unguja na Pemba wamepatiwa mafunzo ya miezi sita ya kuwajengea uwezo wa kufundisha elimu ya maandalizi kwa ufanisi zaidi. 
                       ix).          Jumla ya walimu 350 wakiwemo 200 wa Unguja na 150 kutoka Pemba wa Madrasa na Vyuo vya Kur’ani wamepatiwa mafunzo ya umuhimu wa kutumia vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Aidha, vifaa vya kukalia na kusomea viligawiwa katika Madrasa na Vyuo vya Kur’ani 100 Unguja na 60 Pemba.

Matokeo ya Muda Mfupi;
                           i.            Jumla ya watoto 92,098 ambao sawa na asilimia 86.0 wameandikishwa katika ngazi ya elimu ya maandalizi, wakiwemo wanaume 45,524 na wanawake 46,574. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 4.6 ikilinganishwa na asilimia 81.4 ya uandikishaji ya mwaka 2019.  Jadweli namba 13(a), (b) na (c) yanatoa ufafanuzi zaidi.
                       iii.            Jumla ya wanafunzi 313,097 wameandikishwa katika ngazi ya elimu ya msingi kwa mwaka 2020 ambao ni sawa na asilimia 120.7. Kati yao, wanaume ni 158,383 sawa na asilimia 121.5 na wanawake ni 154,714 sawa na asilimia 119.8. Jadweli namba 14 linatoa ufafanuzi zaidi.

PROGRAMU YA PILI: ELIMU YA SEKONDARI.
29.         Mheshimiwa Spika, Programu hii inalenga kutoa na kuimarisha elimu ya sekondari. Kwa mwaka 2019/20 programu hii imetekelezwa kwa pamoja kati ya SMZ na Washirika wa Maendeleo wa ndani na nje ya nchi. Jumla ya TSh. 104,591,382,000/- zilipangwa kutumika. Kati ya fedha hizo, TSh. 6,824,440,000/- ni kwa kazi za kawaida, TSh. 42,362,596,000/- zilitengwa kwa ajili ya kulipa mishahara na TSh. 55,404,346,000/- kwa miradi ya maendeleo zikiwemo Tsh. 3,300,000,000/- za SMZ na TSh. 52,104,346,000/- za wahisani. Hadi kufikia Aprili, 2020, jumla ya TSh.63,477,435,535/- zilipatikana sawa na asilimia 61. Kati ya fedha hizo, TSh. 21,660,245,933/- sawa na asilimia 39 ni kwa ajili ya kazi za maendeleo. Aidha, TSh.20,828,245,933/- zimetolewa na Washirika wa Maendeleowakiwemo BADEA, Mfuko wa OPEC, Benki ya Dunia na Shirika lisilo la kiserikali la Korea (Good Neighbours) sawa na asilimia 40 na TSh. 832,000,000/- sawa na asilimia 25 kutoka SMZ.

30.         Mheshimiwa Spika, Utekelezaji kwa programu hii ni kama hivi ifuatavyo: -

                           i).          Watahiniwa 23,380 wa skuli za sekondari za Serikali waliofanya mitihani ya Kidato cha Nne mwezi Novemba, 2019 wamelipiwa TSh. 1,200,000,000/- ikiwa niada ya mitihani
                         ii).          Jumla ya TSh. 3,175,685,943/= za ruzuku zimetolewa kwa skuli 204 za sekondari za Serikali kwa ajili ya uendeshaji baada ya kufutwa michango ya wazee.
                       iii).          Jumla ya wanafunzi 59 wanaotoka maeneo ya vijijini wanaosoma Skuli ya Sekondari ya SUZA wamelipiwa kiasi cha shillingi 23,010,000/- kwa ajili ya gharama za huduma ya chakula.
                       iv).          Jumla ya wanafunzi 89,240 wamepatiwa vikalio kufuatia kununuliwa kwa seti 44,620 za viti na meza kwa ajili ya wanafunzi wa skuli za Sekondari.
                         v).          Vifaa vya maabara na kemikali kwa ajili ya Mitihani ya Taifa vimenunuliwa na kusambazwa katika skuli za sekondari 175 zenye madarasa ya kidato cha nne.Aidha, tathmini ya manunuzi ya vifaa vya maabara kwa skuli 15 zenye madarasa ya kidato cha sita kwa Unguja na Pemba ipo katika hatua ya mwisho.
                       vi).          Skuli za Sekondari za Ufundi ya Mikunguni Unguja na Kengeja kwa Pemba zimepatiwa vifaa vya kufundishia na kujifunzia masomo ya ufundi katika fani za Umeme, Ujenzi, Makenika na Kompyuta.
                     vii).          Taratibu za manunuzi ya madaftari 6,740,036 ya wanafunzi wa Sekondari zinaendelea. Ripoti ya tathmini iliwasilishwa Mamlaka ya Manunuzi kwa ajili ya kupitiwa na kupata ushauri. Ushauri huo tayari umeshawasilishwa na kwa sasa Wizara inaufanyia kazi. 
                   viii).          Wanafunzi 1,571 wa Unguja na Pemba wanaoishi dakhalia wamelipiwa jumla ya TSh. 453,240,000/= kwa ajili ya gharama za huduma ya chakula.
                       ix).          Jumla ya walimu wapya 572 wameajiriwa wakiwemo 204 wa Sayansi na 368 wa Sanaa na wamepatiwa mafunzo elekezi na tayari wamepangiwa kazi katika skuli za sekondari Unguja na Pemba.
                         x).          Jumla ya wanafunzi 18,601 wamefaulu mtihani wa Kidato cha Nneuliofanyika Novemba, 2019 nawanafunzi 4,714 wataendelea na na masomo ya Kidato cha Tano katika skuli mbalimbali za Serikali za Unguja na Pemba.
                       xi).          Jumla ya wanafunzi 2,687 wa Kidato cha Sita wakiwemo 2,218 kutoka skuli za Serikali na 469 kutoka skuli binafsi ambao walitarajiwa kufanya mitihani ya kumalizia Kidato cha Sita katika mwezi Meihawakuweza kufanya mitihani yao kutokana na janga la maradhi ya Korona ambapo skuli zote zimefungwa na mitihani imeakhirishwa mpaka litakapotolewa tamko rasmi Serikalini.
                     xii).          Jumla ya washiriki 375 walipatiwa mafunzo ya athari za utoro wa wanafunzi, lengo la mafunzo haya ni kuweza kuihamasisha jamii ili kupunguza au kuondosha kabisa tatizo la utoro katika skuli zetu.
                   xiii).          Jumla ya wanafunzi 10 wakiwemo sita kutoka Unguja na wanne kutoka Pemba wamechanguliwa kujiunga na masomo ya Kidato cha Kwanza katika Skuli za Mama Salma Kikwete za Mkoa wa Pwani Wilaya ya Rufiji na Mkoa wa Lindi katika Wilaya ya Lindi.
                   xiv).          Skuli 10 za Unguja na Pemba zimejengewa visima na matangi ya kuhifadhi maji kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Time to Help na Skuli ya Sekondari ya Feza. Skuli hizo ni Sebleni, Paje, Mgambo, Mtende, Dimani, Fuoni na Chunga kwa Unguja na skuli ya Wete, Kijumbani, Mizingani na Pujini kwa Pemba. Aidha ujenzi wa visima katika skuli za Kandwi na Uzi Ng’ambwa kwa Unguja na Mgogoni kwa Pemba unaendelea. 
                     xv).          Ujenzi wa kukamilisha Skuli ya Sekondari ya Donge uliofanywa na mhisani kutoka Falme za Kiarabu kupitia shirika lisilo la Kiserikali la Kinderhut umekamilika. Wizara imeipatia skuli hiyo seti 765 za viti na meza kwa ajili ya madarasa yote. Aidha, skuli hiyo pia imepatiwa samani kwa ajili ya walimu, maktaba, ofisi na maabara.
                   xvi).          Ujenzi wa Jengo jipya katika Skuli ya Sekondari ya Biashara Mombasa lenye madarasa tisa uliofanywa kwa msaada wa Mheshimiwa Ahmada Abdulwakil kupitia kampuni ya SHA umekamilika. Wizara imeipatia skuli jumla ya seti 360 ya viti na meza.
                 xvii).          Ujenzi wa skuli 9 za sekondari za ghorofa umekamilika licha ya kazi ndogo ndogo zilizobakia kwa skuli ya Muambe na Kizimbani Pemba. Skuli hizi zilifunguliwa rasmi na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein tarehe 05/01/2020 katika maadhimisho ya sherehe za miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha, ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Kibuteni unaendelea.
               xviii).          Ujenzi wa skuli tatu mpya za sekondari za kisasa kwa ushirikiano na Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika (BADEA) umeanza rasmi mwezi Machi 2020. Utekelezaji umeanza kwa hatua ya kutangaza zabuni na ununuzi wa gari mbili, ambazozitatumika kwa shughuli za ufuatiliaji wa kazi za ujenzi. Aidha mialiko imetangazwa kwa ajili ya kupata kampuni za Ushauri Elekezi za kusanifu michoro na kusimamia ujenzi kutoka Afrika na nchi za Kiarabu.

Matokeo ya muda mfupi;
                           i.            Jumla ya wanafunzi 112,983 wameandikishwa katika ngazi ya Elimu ya Sekondari ya awali (kidato 1 – 4).  Kati yao, wanafunzi 65,282 wa kidato cha kwanza na pili wakiwemo wanaume 30,764na wanawake 34,518.Wanafunzi wa kidato cha tatu  na nne kina jumla ya wanafunzi 47,912 wakiwemo wanaume 22,641 na wanawake 25,271
                         ii.            Jumla ya wanafunzi 4,737 wameandikishwa katika ngazi ya sekondari ya juu (kidato 5-6). Kati yao wanafunzi 2,519 ni wa kidato cha tano wakiwemo wanaume 1,140 na wanawake 1,379 na wanafunzi 2,218 wa kidato cha sita kati yao  wanaume ni 1,090 na wanawake 1,128.


PROGRAMU YA TATU: ELIMU YA JUU
31.         Mheshimiwa Spika, Madhumuni ya programu hii ni kutoa elimu itakayomuwezesha muhitimu kujiajiri au kuajiriwa. Programu hii ina programu ndogo moja ambayo ni mafunzo ya ualimu na maeneo manne ya huduma, ikiwemo Huduma ya Ushauri na Utafiti, Huduma ya Sayansi na Teknolojia, Huduma ya Mikopo ya Elimu ya Juu na Huduma ya Uratibu wa Elimu ya Juu. Utekelezaji wa programu hii ni kama ifuatavyo: -



Programu ndogo ya Mafunzo ya Ualimu
32.         Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo ilitengewa jumla ya TSh. 1,719,367,000/- za SMZ kwa kuendelea kutoa mafunzo ya ualimu katika ngazi ya Stashahada na kutoa mafunzo ya Ualimu kazini. Kati ya fedha hizo TSh. 534,531,000/- zilitengwa kwa matumizi ya kawaida na TSh. 1,184,836,000/- kwa matumizi ya mshahara.  Hadi kufikia Aprili, 2020, jumla ya TSh. 1,456,457,780/= sawa na asilimia 84.7 zilipatikana.

33.         Mheshimiwa Spika, utekelezaji halisi wa programu hii ndogo ni kama hivi ifuatavyo: -
                           i).          Moduli mbili za mwongozo wa mafunzo kazini kwa walimu wa Maandalizi na Msingi zimetayarishwa kwa lengo la kuratibu mafunzo ili kuimarisha ufundishaji wa masomo kwa wanafunzi wao.
                         ii).          Jumla ya walimu 392 wakiwemo wanawake 132 na wanaume 260 wa skuli za sekondari wamepatiwa mafunzo ya ufundishaji wa mada zinazowapa ugumu katika kuzifundisha kwa masomo ya Jiografia, Historia Kiingereza na Hisabati. Vile vile walimu hawa wamepatiwa taaluma na mbinu za namna ya kuwafundisha wanafunzi njia bora za kujibu maswali ambayo hayajibiwi vizuri katika mitihani ya Taifa.
                       iii).          Jumla ya walimu 639 wa Sanaa wanaofundisha masomo ya Sayansi na Hisabati Kidato cha Kwanza na cha Pili wanaendelea na mafunzo kazini ya kuwawezesha kufundisha masomo hayo kwa umahiri katika vituo vya walimu vya Unguja na Pemba. Lengo la mafunzo hayo ni kupunguza tatizo la uhaba wa walimu wa Sayansi na Hisabati katika skuli zetu za sekondari. Pia, walimu hawa wanapatiwa mafunzo ya lugha ya Kiingereza ili waweze kuitumia vizuri lugha hiyo katika kufundisha masomo husika. Hata hivyo, mafunzo hayo yamesimamishwa kutokana na maradhi yanayosababishwa na virusi vya Korona (COVID 19).
                       iv).          Jumla ya walimu 200 wa madarasa ya Tatu na Nne wa lugha ya Kiingereza wamehudhuria mafunzo juu ya mbinu za kufundishia, utamkaji wa maneno, matumizi ya wakati pamoja na imla kwa wanafunzi wa madarasa hayo.
                         v).          Jumla ya walimu 1,341 wamehudhuria mafunzo ya ufundishaji wa somo la Hisabati. Kati ya walimu hao 284 ni Walimu Wakuu na 1,057 ni Walimu wa somo hilo kwa madarasa ya Kwanza na Pili.
                       vi).          Jumla ya vitabu 7,500 kwa ajili ya mafunzo ya Elimu Masafa vimechapwa na kusambazwa katika vituo vya Walimu Unguja na Pemba.
                     vii).          Jumla ya walimu wanafunzi 529 wamefanya mitihani ya Elimu Masafa daraja la 3A. Wanafunzi tisa wamefanya mitihani maalum kutokana na kutofanya mitihani ya awali kwa sababu ya ugonjwa na 98 wamerudia baadhi ya masomo. Matokeo ya mitihani hiyo yameonesha kwamba wanafunzi wamefanya vizuri katika masomo yote isipokua somo la Hesabati.
                   viii).          Jumla ya ziara 80 za ufuatiliaji utekelezaji wa mafunzo ya Elimu Masafa zimefanyika katika vituo tisa vya walimu Unguja na Pemba. Matokeo yanaonesha kwamba hali ya ufundishaji ipo vizuri.
                       ix).          Jumla ya ziara 1,470 zimefanywa katika skuli za Serikali na Binafsi Unguja na Pemba. Aidha, jumla ya walimu 2,651 wa ngazi zote wamepatiwa mafunzo na ushauri juu ya matumizi ya zana za kufundishia pamoja na kuwapatia taaluma ya utungaji wa   maswali ya mitihani. 
                         x).          Jumla ya Wakufunzi 56 wa Chuo cha Kiislamu wa masomo yote wamepatiwa mafunzo ya uandaaji wa zana za tathmini ili waweze kutunga mitihani inayokidhi viwango vya ubora. Katika mafunzo hayo aina za maswali, sheria za utungaji, sifa za maswali pamoja na mambo ya kuzingatia katika kuandaa mtihani yalijadiliwa.
                       xi).          Tathmini ya awali juu ya ufundishaji wa somo la Kiingereza Unguja na Pemba imefanyika. Jumla ya walimu 120 wa Darasa la Kwanza na Sita walishiriki katika tathmini hiyo. Matokeo yameonesha kuwa walimu wanahitaji taaluma zaidi juu ya utamkaji sahihi wa maneno ya Kiingereza na kutofautisha wakati. Kati yao Walimu 108 wamepatiwa mafunzo ya somo hilo kwa awamu ya kwanza.
                     xii).          Mapitio na marekebisho yamefanywa katika Mwongozo wa kazi Namba.11 kuhusu Vituo vya Walimu. Muongozo huu uliandaliwa kwa walimu wa Msingi tu kwa wakati ule. Kwa hivyo ulihitaji marekebisho ili uweze kutumika pia katika ngazi za Maandalizi na Sekondari.
                   xiii).          Jumla ya wanafunzi 800 (600 Unguja na 200 Pemba) kautoka skuli 80 (60 Unguja na 20 Pemba) za Maandalizi wameshiriki katika mashindano ya kusoma na kuandika herufi na silabi. Lengo ni kuwatathmini walimu wa maandalizi katika ufundishaji wao. Matokeo ya mashindano hayo yanathibitisha kazi nzuri inayofanywa na walimu. Mashindano haya yameweza kuongeza ari ya ufundishaji kwa walimu wa Maandalizi.

Matokeo ya muda mfupi
i)        Jumla ya wanafunzi 976 wanasomea mafunzo ya Ualimu kwa ngazi ya Cheti cha Maandalizi, Stashahada ya Dini na Kiarabu, Stashahada ya Sayansi Jamii, Stashahada ya Elimu ya Msingi kwa Unguja na Pemba na Cheti cha Elimu Mjumuisho kwa Unguja. Kati yao, wanafunzi 702 wakiwemo wanaume 120 na wanawake 582 wanasomea Ualimu katika Chuo cha Kiislamu Mazizini Unguja na wanafunzi 274 wakiwemo wanaume 67 na wanawake 207 katika Chuo cha Kiislamu Kiuyu Pemba.

Huduma ya Elimu ya Juu, Ushauri na Utafiti
34.         Mheshimiwa Spika, Huduma ya Elimu ya Juu, Ushauri na Utafiti ina lengo la kuwaandaa wanafunzi kuingia katika fani za kitaalamu na ajira. Huduma hii inatolewa katika Vyuo vikuu vitatu vilivyopo Zanzibar ambavyo ni Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Chuo cha Kumbukumbu ya Abdulrahman Al-Sumait cha Chukwani na Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu.

35.         Mheshimiwa Spika, ngazi hii ya elimu ina jumla ya wanafunzi 7,303 wanaosoma katika vyuo vikuu vitatu. Kati ya wanafunzi hao, 3,112 ni wanaume na 4,191ni wanawake. Kwa mwaka wa fedha wa 2019/20, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kilitengewa ruzuku ya TSh. 11,239,100,000/-. Kati ya fedha hizo TSh. 500,000,000/- zilitengwa kwa matumizi ya kawaida na TSh. 10,739,100,000/- kwa matumizi ya mishahara. Hadi kufikia Aprili, 2020, jumla ya TSh. 10,666,409,562/= sawa na asilimia 95zimepatikana.

36.           Mheshimiwa Spika, utekelezaji halisi wa huduma hii ni kama hivi ifuatavyo: -
                     i).         Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kimezindua skuli skuli ya Kilimo, Skuli ya Utibabu wa Meno na Taasisi ya Masomo ya Ubaharia. Aidha, Chuo kimeanzisha programu mpya nne ambazo ni Shahada ya kwanza ya Uuguzi, Shahada ya Kwanza ya Sayansi na Kilimo, Shahada ya Utabibu wa Meno na Shahada ya Uzamili ya Lugha na Elimu.
                ii).            Jumla ya wanafunzi wapya 2,200 wa masomo ya   ngazi mbalimbali wa SUZA wamedahiliwa.
              iii).            Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kilifanya mahafali ya kumi na tano (15) tarehe 31/12/2019. Katika mahafali hayo, Mkuu wa Chuo ambaye ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein aliwatunuku shahada, stashahada na vyeti wahitimu 1,716 (wanaume 790 wanawake 926) waliohitimu katika programu mbalimbali.
              iv).            Mhadhiri Msaidizi mmoja ameajiriwa katika taaluma ya Afya. Aidha, Chuo kimeendelea kuwalipia ada za masomo wafanyakazi wake 50 ambao wapo masomoni kwenye ngazi za Shahada ya Uzamivu (27), Shahada ya Uzamili (19), Shahada ya Kwanza (4). 

Matokeo ya muda mfupi;
                             i.            Jumla ya wanafunzi 4,808 wameandikishwa katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA). Kati ya wanafunzi hao, wanaume ni 2,070 na wanawake ni 2,738. Jadweli Nambari 26(g) linatoa ufafanuzi zaidi.
                           ii.            Jumla ya wanafunzi 1,716 (790 wanaume na 926 wanawake) wamehitimu SUZA na kutunukiwa Stashahada, shahada, shahada ya uzamili na shahada ya uzamivu katika mahafali ya 15 yaliyofanyika katika Kampasi ya Tunguu, tarehe 31 Disemba 2019.
                         iii.            Jumla ya wanafunzi 875 wakiwemo wanaume 363 na wanawake 512 wameandikishwa katika Chuo cha Kumbukumbu ya Abdulrahman Al-Sumait cha Chukwani. Jadweli namba 27 linatoa ufafanuzi zaidi.
                         iv.            Jumla ya wanafunzi 1,620 wameandikishwa katika Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu, kati yao wanaume ni 679 na wanawake 941 Jadweli namba 28 linatoa ufafanuzi zaidi. 
                   
Huduma ya Sayansi na Teknolojia
37.           Mheshimiwa Spika, Huduma ya Sayansi na Teknolojiaina madhumuni ya kuimarisha elimu ya sayansi na teknolojia nchini Shughuli za huduma hii zinatekelezwa na Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia. Kwa mwaka 2019/20, Taasisi ilitengewa ruzuku ya TSh. 1,626,000,000/-. Kati ya fedha hizo, TSh. 420,100,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kazi za kawaida na TSh. 1,205,900,000/- ni kwa matumizi ya mishahara.  Hadi kufikia Aprili, 2020, jumla ya TSh. 1,393,132,060/= sawa na asilimia 86zilipatikana.

38.           Mheshimiwa Spika, Utekelezaji halisi wa huduma hii kwa mwaka 2019/20 ni kama ifuatavyo: -
                      ii).      Jumla ya wanafunzi wapya 343, wanaume 236 na wanawake 107 kwa fani zote za Taasisi wameandikishwa.
                    iii).      Wafanyakazi wapya 19, kati yao 15 wa kada ya wakufunzi na wanne wa kada za uendeshaji wameajiriwa.
                    iv).      Mafunzo mapya ya kuiendeleza Taasisi na yale ya kuisaidia jamii kwa kutumia Sayansi na Teknolojia yameanzishwa.

Matokeo ya muda Mfupi
Jumla ya wanafunzi 1,529 wakiwemo wanaume 1,297na wanawake 232 wanaendelea na masomo katika fani mbalimbali zikiwemo Shahada ya Urubani na Uhandisi wa ndege, Stashahada za Uhandisi, Stashahada ya Teknolojia ya Habari Mawasiliano na Biashara, Stashahada ya Mafunzo ya Hisabati na Sayansi kwa Skuli za Msingi, Stashahada mafunzo ya Ualimu (VTA), Stashahada ya Usimamizi wa Maabara na Cheti kwa Mafunzo ya Amali (VETA). Jadweli nambari 29 linatoa ufafanuzi Zaidi.

Huduma ya Mikopo ya Elimu ya Juu
39.           Mheshimiwa Spika, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar inatoa mikopo kwa wanafunzi wanaojiunga na wanaoendelea na masomo ya elimu ya juu katika fani mbalimbali ndani na nje ya nchi. Kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020, Bodi ilitengewa jumla ya TSh. 10,298,600,000/-. Hadi kufikia Aprili 2020, jumla ya TSh. 6,706,532,312/= sawa na asilimia 65 ya makadirio zilipatikana.

40.           Mheshimiwa Spika,Utekelezaji halisi wa programu hii ni kama ifuatavyo: -
i)           Jumla ya wanafunzi 4,081 wamepatiwa mikopo ya elimu ya juu wakiwemo wanafunzi wapya 1,860 na 2,221 wanaoendelea na masomo. Idadi hii imeongezeka kwa 562 sawa na asilimia 16 ukilinganisha na mwaka 2018/2019.
ii)         Wanafunzi 72 wamepatiwa nafasi za ufadhili wa masomo nje ya nchi zilizotolewa na washirika wa maendeleo mbalimbali wakiwemo Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China (30), Serikali ya Falme ya Oman (5), Falme ya Ras Al-Khaimah (4), Sudan (10), Algeria (8) na Malaysia (15).
iii)       Wanafunzi 108 wakiwemo wapya 60 na wanaoendelea na masomo 48 wamepatiwa ufadhili wa masomo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zasnzibar kutokana na ufaulu wao wa ngazi ya juu katika mtihani wa Kidato cha Sita.
iv)       Jumla ya wanafunzi wapya 38 wamepatiwa ufadhili wa masomo kwa vyuo vya ndani ya nchi wakiwemo 27 kupitia taasisi za Darul Imaan katika Chuo Kikuu cha Zanzibar kilichopo Tunguu  na 11 kupitia Shirika la “Direct Aid” lililotoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al-Sumait cha Chukwani.
v)         Jumla ya wanafunzi 987 wakiwemo wanafunzi 666 wanaosoma vyuo vya Zanzibar, 231 katika vyuo vya Tanzania Bara na 90 wa vyuo vya nje ya Tanzania wanatarajiwa kuhitimu masomo yao katika fani na  ngazi mbalimbali.

41.           Mheshimiwa Spika,Bodi ilitarajia kukusanya TSh. 2,300,000,000/= ikiwa ni marejesho ya mkopo hadiifikapo mwezi wa Juni, 2020. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2020, jumla ya TSh. 1,970,000,000/= sawa na asilimia 85.6 ya lengo lililowekwa zimekusanywa.

Huduma ya Uratibu wa Elimu ya Juu
42.           Mheshimiwa Spika, Huduma ya Uratibu wa Elimu ya Juuina jukumu la kusimamia na kutathmini maendeleo ya elimu ya juu. Huduma hii inatekelezwa na Kitengo cha Uratibu wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia. Kwa mwaka 2019/20 Kitengo kilitengewa jumla ya TSh. 50,000,000/= kutoka Serikalini. Hadi kufikia Aprili 2020, jumla ya TSh. 28,000,000/= sawa na asilimia 56 zimepatikana. Utekelezaji halisi ni kama ifuatavyo: -
i)        Nafasi za masomo kwa ufadhili kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi za China, Algeria, Morocco, , Malaysia, Poland, Nelson Mandela, Queen Elizabeth, Hungary, na Jumuiya ya Madola zimetangazwa. Nafasi hizo zilijumuisha fani mbalimbali zikiwemo; Udaktari, Uchumi, Uhandisi, Uuguzi na Sayansi ya Mazingira, Kilimo, Chakula na Lishe, Usimamizi wa Biashara na Utawala kwa viwango vya Shahada ya Kwanza, ya Pili na ya Tatu. Jumla ya waombaji 112 wakiwemo wanaume 78 na wanawake 34 waliwasilisha maombi yao. Kati yao, wanafunzi 38 (wanaume 27 na wanawake 11) wamenufaika na nafasi hizo.

Matokeo ya muda mfupi;
                       i.      Jumla ya wahitimu 1,120 wa fani mbalimbali zikiwemo Kilimo, Mazingira, Uongozi wa Fedha, Udaktari wa Meno kwa kiwango cha Stashanada, Shahada ya Kwanza na , Shahada ya Uzamili waliripoti kwa kujitambulisha na orodha wa wahitimu hao na fani zao za masomo zimewasilishwa Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

PROGRAMU YA NNE: ELIMU MBADALA NA MAFUNZO YA AMALI
43.           Mheshimiwa Spika, Programu hii ina madhumuni ya kutoa Elimu ya Mafunzo ya Amali na Elimu Mbadala kwa wanafunzi kulingana na mahitaji ya soko la ajira. Programu hii ina programu ndogo mbili; Mafunzo ya Amali na Elimu Mbadala na Watu Wazima.

Programu ndogo ya Mafunzo ya Amali
44.           Mheshimiwa Spika, programu hii ndogo ilikuwa na madhumuni ya kutoa elimu itakayowawezesha vijana kujiajiri ili kujikwamua na umasikini na ilitengewa jumla ya ruzuku ya TSh.7, 761,200,000/-. Hadi kufikia Aprili, 2020, jumla ya TSh. 4,916,633,665/= kutoka SMZ zilipatikana sawa na asilimia 63.

45.           Mheshimiwa Spika, Utekelezaji halisi kwa programu hii ni kama hivi ifuatavyo: -

i)        Jumla ya vikundi vitano (viwili Unguja na vitatu Pemba) vimepatiwa mkopo wenye thamani ya TSh. 33,850,550/-. Mkopo huu unalenga kuwawezesha vijana kujiajiri.
ii)      Mamlaka imesimamia ufanyaji wa Mtihani wa Taifa wa MMA kwa wanafunzi wa vituo 15 vikiwemo vitatu vya Serikali na 12 vya binafsi ambapo jumla ya wanafunzi 1,875 (1,255 wanaume na wanawake 620) walishiriki katika mitihani hiyo.
iii)    Ujenzi wa Vituo vya Mafunzo ya Amali vya Makunduchi na Daya unaendelea na umefikia asilimia 79 kwa Makunduchi na asilimia 87 kwa Daya.
iv)    Jumla ya vituo 24 vya binafsi vinavyotowa mafunzo ya amali vimefanyiwa ukaguzi wa kawaida kwa lengo la kuangalia kiwango pamoja na kutoa maelekezo ya njia nzuri za utoaji wa mafunzo ya fani husika. Aidha, vituo 16 vimefanyiwa ukaguzi wa usajili ambapo vituo viwili vimepatiwa usajili wa kudumu na vituo 14 vimepatiwa usajili wa muda. Vituo vilivyopatiwa usajili wa kudumu ni Muna Beauty Academy na Melisha Computer Training Center. Aidha, vituo vilivyopatiwa usajili wa muda ni Experience Vocational Training Center, Wingwi Alternative Learning Center, Zanzibar Technical Center, ICPS Vocational Training Center, Zanzibar Commercial Technical Training Center, Ikigai Center for Career Training, Zanzibar Aviation Training Center, Dodeani Vocational Training Center, Center for Professional and Vocational Training, Rahaleo Alternative Learning Center, ZAWA Training Center, Babel Center for Proffesional Studies, Hamasika Tailoring and Designing Vocational Training and Noah Training Center.
v)      Mamlaka imewalipia wafanyakazi wake tisa masomo ya muda mrefu wakiwemo watano wanaoendelea na masomo na wanne wapya. Pia imewapatia wafanyakazi 22 udhamini wa masomo ya muda mfupi ya Domain name and security extention (mfanyakazi mmoja),mafunzo ya matengenezo ya simu za mkononi (13), mafunzo ya Sheria ya Manunuzi (2) na wafanyakazi sita walipatiwa mafunzo ya Quick Book.
vi)    Jumla ya wanafunzi 472 wanaoishi dakhalia ya Mkokotoni (320) na Vitongoji (152) wanapatiwa huduma ya chakula ya milo mitatu kwa siku.
vii)  Jumla ya vijana wa kike 147 wamepatiwa mafunzo ya ukulima na usarifu wa mwani katika maeneo ya Paje, Unguja Ukuu, Matemwe na Kidoti kwa Unguja na  maeneo ya Kuukuu Kangani, Chokocho, Kisiwa Panza, Chwale, Kiungoni, Msuka, Gando, Shumba mjini, Tumbe na Maziwang’ombe kwa Pemba.
Matokeo ya muda mfupi;
                             i.            Jumla ya vijana wapya 250 (wanaume 138 na wanawake 112) wamejiunga na vituo vya Mamlaka ya Mafunzo ya Amali mwanzoni mwa mwaka 2020.
                           ii.            Jumla ya TSh. 21,773,050/= zimerejeshwa na vikundi vya vijana vilivyopatiwa mkopo wa kuweza kujiajiri.
                         iii.            Jumla ya vijana 1,875 wa Vituo vya Mwanakwerekwe, Mkokotoni na Vitongoji wamehitimu mafunzo yao. (Wanaume 1,255 na wanawake 620).Wanafunzi 1,113 kati ya hao sawa na asilimia 59 wamefaulu mitihani yao.

Programu ndogo ya Elimu Mbadala na Watu Wazima
46.           Mheshimiwa Spika, Programu hii inatekelezwa na Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima na ina lengo la kupunguza kiwango cha wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu miongoni mwa wanajamii. Kwa mwaka wa fedha 2019/20, programu hii ilitengewa jumla ya TSh. 8,974,245,000/-. Kati ya hizo, TSh. 535,304,000/- zilitengwa kwa kazi za kawaida, TSh. 438,941,000/- kwa matumizi ya mshahara na TSh. 8,000,000,000/- ni kwa kazi za maendeleo. Kati ya fedha za maendeleo TSh. 1,000,000,000/- ni mchango wa SMZ na TSh.7, 000,000,000/- ni kutoka ADB. Hadi kufikia Aprili, 2020, jumla ya TSh. 7,837,587,279/= sawa na asilimia 87 zilipatikana. Kati ya fedha hizo, TSh. 7,205,441,846/- ni kwa kazi za maendeleo ambazo ni sawa na asilimia 90 zikiwemo TSh. 171,046,000/= za SMZ sawa na asilimia 17.1. Aidha, jumla ya TSh. 632,145,433 kwa matumizi ya kawaida sawa na asilimia 65 zimepatikana.

47.           Mheshimiwa Spika, Utekelezaji halisi wa shughuli za programu hii ni kama ifuatavyo: -
i)          Madarasa 47 mapya ya kisomo kwa Unguja na Pemba yamefunguliwa. Idadi ya madarasa ya kisomo imefikia 528 mwaka 2020 kutoka 521 mwaka 2019. Aidha, jumla ya wanakisomo 7,874 wa kisomo cha Watu Wazima wamefanyiwa upimaji katika hatua zote nne za kisomo. Wanafunzi 474 wa hatua ya nne wamekombolewa kupitia upimaji huo.
ii)        Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima yamefanyika. Uzinduzi wa Juma hilo ulifanyika katika Wilaya ya Chake Chake Pemba katika Skuli ya Madungu Sekondari na kilele kilifanyika Wilaya ya Kati Unguja.
iii)      Jumla ya vikundi 117 (71 Unguja na 46 Pemba) vyenye jumla ya wanachama 2,583 vimeendelezwa kwa lengo la kuwapunguzia utegemezi wanawake na umasikini wa kipato.
iv)      Jumla ya wanafunzi 863 (wanaume 365 na wanawake 498) wamesajiliwa katika vituo vya kujiendeleza Unguja na Pemba. Aidha, wanafunzi 71 (wanaume 6 na wanawake 65) walioshindwa kuendelea na masomo yao baada ya mtihani wa Kidato cha Pili na cha Nne wameandikishwa katika Kituo cha Sayansi Kimu Forodhani kusomea fani ya Upishi, Ushoni, Kudarizi na Kufuma.
v)        Walimu 26 wa Vituo vya Elimu Mbadala wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo.Pia, viongozi mbali mbali wakiwemo Makatibu Tawala, Wenyeviti na Makatibu wa Mabaraza ya Madiwani, Maafisa Ustawi, Masheha, Umoja wa Vijana, Jumuia ya Wazazi, Maafisa Elimu Sekondari na Walimu wakuu walihudhuria semina ya uhamasishaji wa kutambua programu ya Elimu Mbadala.
vi)      Vipindi 20 vya Elimu Mbadala na Watu Wazima viliandaliwa na kurushwa hewani kupitia Shirika la Utangazaji la Zanzibar kwa ajili ya kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa programu zinazotolewa na Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima zenye lengo la kuhamasisha uandikishaji wa wanafunzi katika vituo ili wapate elimu itakayowakomboa na changamoto za kijamii na kiuchumi.

Matokeo ya muda mfupi;
                         i.          Jumla ya wanakisomo 690 wameandikishwa wakiwemo wanaume 48 na wanawake 642.
                       ii.          Jumla ya wanafunzi 1,254 wenye umri wa miaka 9 hadi 14 waliokuwa nje ya mfumo rasmi wa elimu wameandikishwa katika madarasa ya Elimu Mbadala. Kati ya hao, wanafunzi 677 wameandikishwa Unguja na 577 kwa Pemba wakiwemo wanaume 827 na wanawake 427.
                     iii.          Jumla ya wanafunzi 401 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 22 wameandikishwa katika Kituo cha Elimu Mbadala Rahaleo Unguja na Kituo cha Wingwi Mtemani Pemba. Kati yao, wanaume 267 na wanawake 134. Vijana hawa wanasomea fani za Umeme, Ushoni, Upishi, Udobi, Uchoraji, Kilimo, Ufugaji, Useremala, Mafunzo ya Kompyuta na Utunzaji Nyumba pamoja na masomo ya kawaida.
                     iv.          Jumla ya watahiniwa 4,155 wamefanya mtihani wa faragha wa Kidato cha Nne, kati yao wanafunzi 1,599 sawa na asilimia 38.5 ya watahiniwa wote wamefaulu. Aidha, wanafunzi 141 kati ya 219 waliofanya mtihani wa faragha wa Kidato cha Sita mwezi Mei, 2019 kwa Unguja na Pemba ambao ni sawa na asilimia 63.3 wamefaulu.

PROGRAMU YA TANO: UBORA WA ELIMU
48.           Mheshimiwa Spika, Programu hii ina lengo la kutoa elimu bora kwa ngazi zote za elimu. Progamu hii ina jumla ya programu ndogo tatu na maeneo matano ya kutoa huduma kama yafuatayo: -

Huduma ya Mitaala na Vifaa vya Kufundishia
49.           Mheshimiwa Spika, Huduma hii ina madhumuni ya kutayarisha mitaala ya elimu na kuratibu upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa ngazi za elimu ya maandalizi, msingi, sekondari na mafunzo ya Ualimu. Shughuli za utoaji wa huduma hii zinatekelezwa na Taasisi ya Elimu Zanzibar. Kwa mwaka wa fedha 2019/20, Taasisi ilitengewa ruzuku yenye jumla ya TSh. 573,100,000/-. Kati ya fedha hizo TSh. 301,600,000/- ni kwa kazi za kawaida na TSh. 271,500,000/- kwa matumizi ya mshahara. Hadi kufikia Aprili, 2020, jumla ya TSh. 503,978,320/= sawa na asilimia 88 zilipatikana. Utekelezaji halisi wa huduma hii ni kama ifuatavyo:-

i)          Muundo wa Paneli za mitaala za Kitaifa kwa ngazi ya Elimu ya Maandalizi, Msingi na kwa vituo 10 vya walimu (vituo sita Unguja na vinne Pemba) umeandaliwa. Aidha, Muundo wa utumishi wa taasisi, mpango mkakati na muongozo wa vigezo vya kuandika na kutathmini vitabu vya kiada na ziada vipo katika hatua ya mwisho kukamilika.
ii)        Rasimu za Kanuni za Sheria ya Taasisi ya Elimu ya Zanzibar zimeandaliwa.
iii)      Jumla ya Skuli 34 za maandalizi na msingi zikiwemo 23 za Serikali na 11 binafsi zilifuatiliwa Unguja na Pemba katika kuendelea na kuimarisha utekelezaji wa mitaala.
iv)      Mapitio ya Mtaala wa Elimu ya Maandalizi na Msingi yanaendelea. Jumla ya mikutano 16 iliyowashirikisha wadau 1,074 wa elimu Unguja na Pemba imefanyika kwa lengo la kupata maoni zaidi. Rasimu ya awali ya Mtaala imewasilishwa Serikalini na kutolewa mapendekezo na ushauri mbali mbali..
v)        Jumla ya wafanyakazi 23 wamepatiwa mafunzo ya muda mfupi ya ukuzaji mitaala. Wafanyakazi watatu wanaendelea na mafunzo ya muda mrefu ambapo wawili katika shahada ya uzamili fani ya uongozi katika elimu na uongozi wa fedha na mmoja shahada ya uzamivu (Kiswahili).

Huduma ya Upimaji na Tathmini ya Elimu
50.           Mheshimiwa Spika, Programu hii ina madhumuni ya kupima na kutathmini utekelezaji wa utoaji wa elimu. Shughuli za huduma hii zinatekelezwa na Baraza la Mitihani la Zanzibar. Kwa mwaka wa 2019/20 ya huduma ya Upimaji na Tathmini ilitengewa ruzuku ya TSh. 4,941,800,000/-. Kati ya fedha hizo TSh. 4,517,000,000/- zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida TSh. 424,800,000/- kwa matumizi ya mishahara.  Hadi kufikia Aprili, 2020, jumla ya TSh. 4,319,112,010/= ambazo ni sawa na asilimia 87 zilipatikana. Utekelezaji halisi wa shughuli za huduma ya Upimaji na Tathmini ni kama ifuatavyo: -

i)          Jumla ya wanafunzi 55,631  (wanaume 28,252 na wanawake 27,379) wa darasa la Nne walisajiliwa kufanya mtihani  wa kuwapima maendeleo yao kitaaluma katika ngazi ya elimu ya msingi chini (Darasa la Kwanza hadi la Nne) na uwezo wa kuendelea na darasa la elimu ya msingi juu (darasa la tano). Wanafunzi halisi waliofanya mtihani huu ni 52,307 sawa na asilimia 94 ya walioandikishwa wakiwemo wanaume 26,429 na wanawake 25,878.
ii)        Jumla ya wanafunzi 31,185 (wanaume ni 14,552 na wanawake ni 16,633) wa Darasa la Sita ambao ni sawa na asilimia 96.5 ya waliosajiliwa walifanya mtihani wa kumalizia elimu ya msingi.  Kati ya watahiniwa hao, 1,508 walifaulu kuendelea na masomo katika madarasa ya mchepuo, wanafunzi 194 walifaulu kuendelea na masomo katika madarasa ya vipawa maalumu, wanafunzi 1508 walifaulu madarasa ya mchepuo na wanafunzi 28,717 wamefaulu kuendelea na masomo ya Kidato cha Kwanza katika madarasa ya kawaida.
iii)      Jumla ya wanafunzi 32,476 sawa na asilimia 94.2 kati ya wanafunzi 34,473 waliosajiliwa walifanya mtihani wa kumaliza Kidato cha Pili, wakiwemo wanaume 14,725 na wanawake 17,751. Jumla ya wanafunzi 24,946 sawa na asilimia 76.8wamefaulu na kuendelea na masomo ya Kidato cha Tatu.
iv)      Jumla ya walimu wanafunzi 316 (Unguja na Pemba) watakaofanya mitihani ya kumalizia masomo yao ya Stashahada ya Ualimu wa ngazi ya Msingi na ngazi ya Sekondari katika Vyuo vya Kiislamu vya Mazizini Unguja na Kiuyu Pemba wamesajiliwa. Kati ya hao, 263 ni wanawake na 53 ni wanaume.
v)        Kazi ya kuupitia na kuufanyia marekebisho Mfumo wa Upimaji na Tathmini wa Baraza la Mitihani la Zanzibar inaendelea.

Matokeo ya Muda mfupi;
                         i.          Jumla ya wanafunzi waliofaulu mtihani wa Darasa la Nne ni 42,110 sawa na asilimia 80.5, Kati ya hao,  wanaume 19,337 sawa na asilimia 37.0 na wanawake ni 22,773sawa na asilimia 43.5 ya watahiniwa wote.
                       ii.          Wanafunzi waliofaulu mtihani wa kumaliza Darasa la Sita ni 30,419 sawa na asilimia 97.5 ya watahiniwa wote (wanaume ni 13,902 sawa na asilimia 44.6 na wanawake ni 16,517 sawa na asilimia  53)  .
                     iii.          Wanafunzi  24,946 kati ya waliofanya  mtihani wa kumaliza Kidato cha Pili ambao ni sawa na asilimia 76.8 wamefaulu kuendelea na masomo yao ya Kidato cha  tatu (wanaume ni 10,017 na wanawake ni 14,929).

Huduma ya Ukaguzi wa Elimu
51.           Mheshimiwa Spika, utoaji wa huduma hii una madhumuni ya kusimamia ubora wa elimu itolewayo kwa kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa inafuata sera, sheria, miongozo na taratibu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.  Shughuli za huduma hii zinatekelezwa na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Elimu.  Kwa mwaka wa fedha 2019/20, huduma hii imepangiwa jumla ya ruzuku ya TSh. 1,090,500,000/-, kati ya fedha hizo TSh. 333,600,000/- ni kwa kazi za kawaida na TSh. 756,900,000/- ni kwa ajili ya mshahara.  Hadi kufikia Aprili, 2020, jumla ya TSh. 809,277,751/= zilipatikana ambazo ni sawa na asilimia 74. Utekelezaji halisi ni kama ifuatavyo: -

i)        Jumla ya skuli 595 (470 za Serikali na 125 za binafsi) Unguja na Pemba sawa na asilimia 80.5 ya makadirio ya skuli zilizopangwa kukaguliwa zimekaguliwa. Kati ya skuli hizo 399 ni za Maandalizi na msingi, 196 za sekondari.  Aidha, skuli 28 zimekaguliwa kwa ajili ya kupatiwa usajili.
ii)      Jumla ya walimu 1,857 wamekaguliwa na kupewa ushauri kulingana na masomo wanayofundisha, Unguja na Pemba.
Huduma za Maktaba
52.           Mheshimiwa Spika, Programu hii ina madhumuni ya kutoa fursa ya kutumia vitabu na nyenzo nyengine za taaluma kwa watoto, wanafunzi wa ngazi zote na watu wote. Shughuli za huduma hii zinatekelezwa na Shirika la Huduma za Maktaba Zanzibar. Kwa mwaka wa fedha 2019/20, huduma hii ilipangiwa kutumia ruzuku yenye jumla ya TSh. 886,200,000/-.Kati ya fedha hizo TSh. 493,100,000/- kwa kazi za kawaida na TSh. 393,100,000/- zilitengwa kwa matumizi ya mshahara. Hadi kufikia Aprili, 2020 jumla ya TSh. 586,049,457/= sawa na asilimia 66 zilipatikana.

Utekelezaji halisi wa shughuli za huduma hii ni kama ifuatavyo: -
i)             Jumla ya vitabu vya msaada 25,341 kutoka Shirika la ‘Book Aid International” la Uingereza vimepokelewa na kusambazwa katika taasisi mbali mbali za elimu Unguja na Pemba. Aidha, vitabu 5,649 vimegaiwa katika taasisi 32 za elimu Unguja na Pemba. Taasisi husika ni Skuli 17 za msingi zimepatiwa vitabu 2,452, Skuli 11 za sekondari zimepatiwa vitabu 2,048 na vituo cha vya Mafunzo ya   Amali (Vitongoji na Mwanakwerekwe) vimepatiwa vitabu 380 na vitabu 769 vimepatiwa Chuo cha Mwenge Community na Chuo cha Pemba School of Health Science.
ii)           Programu 101 za watoto zilizowashirikisha watoto 5,644 zimefanyika. Miongoni mwa programu hizo, programu 82 zilifanyika ndani ya Maktaba Kuu na programu 19 zilifanyika nje ya Maktaba.
iii)         Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya kujua kusoma na kuandika (International Literacy Day) yalishirikisha watu 893 (450 Unguja na 443 Pemba) wakiwemo wanafunzi, walimu, wazazi, waandishi wa vitabu na viongozi mbalimbali yalifanyika katika viwanja vya Maktaba Kuu Maisara kwa Unguja na Maktaba ya Chakechake kwa Pemba. 
iv)         Mdahalo wenye mada ya “Nini kifanyike ili idadi ya watumiaji wa huduma za maktaba iongezeke”ulifanyika. Jumla ya washiriki 170 walitoa maoni yao juu ya kuimarisha huduma za maktaba nchini. Mdahalo huo ulifanyika katika Maktaba Kuu za Unguja na Pemba. Aidha katika midahalo hiyo, tovuti ya Shirika la Huduma za Maktaba (www.zls.go.tz) ilizinduliwa rasmi.
v)           Jumla ya programu 18za Kiingereza za “Youth English Corner” (9 za nje na 9 za ndani) kwa vijana zimefanyika nakuwashirikisha vijana 516. Programu hizi zinaendeshwa kwa mashirikiano na jumuiya isiyo ya Kiserikali ya “Youth Empowerment and Change”.
vi)         Programu mbalimbali za kijamii kupitia Kitengo cha “American Corner zinaendeshwa kwa mashirikiano na Shirika la Huduma za Maktaba na Ubalozi wa Marekani. Jumla ya wanajamii 8,513 walipatiwa huduma kupitia kitengo hicho. Watu 4,997 (3,526 wanaume na wanawake 1,471) walipatiwa huduma za kompyuta na 2,419 (1,385 wanaume na 1,034 wanawake) walipatiwa huduma ya kusoma vitabu. 
vii)       Huduma za maktaba kwa njia ya shamiana ilitolewa katika viwanja vya Skuli ya Fuoni Unguja na Skuli ya Madungu kwa Pemba. Jumla ya wanafunzi 714 walishiriki na kupata fursa ya kusoma vitabu na kupatiwa maelezo yanayohusu shughuli zinazofanywa na maktaba zetu.
viii)     Mafunzo yaliyolenga kuwaongezea uwezo wafanyakazi na kuwawezesha kukabiliana na ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano kwa wakutubi wa maktaba za umma na maktaba za skuli yalitolewa. Mafunzo hayo yalijadili mada za masuala ya ubunifu na mabadiliko (innovation and transformation), namna nzuri ya kutoa huduma kwa mteja (customer care) na huduma kwa kutumia mtandao (search 4 life). Jumla ya wakutubi 70 walishiriki katika mafunzo hayo.
Matokeo ya Muda Mfupi
                             i.            Jumla ya wanachama wapya 257 walisajiliwa katika Maktaba za Shirika Unguja na Pemba. Kati ya hao, wanachama 116 wamesajiliwa Unguja wakiwemo wanaume 72 na wanawake 44. Pia wanachama 141 kwa Pemba walisajiliwa wakiwemo 52 wanaume na 89 wanawake.
                           ii.            Idadi ya watumiaji wa maktaba imefikia 23,326 Unguja na Pemba. Kati yao, 12,864 wakiwemo wanaume 5,172, wanawake 4,338  na watoto ni 3,354 kwa Unguja na watu 10,462 wakiwemo wanaume 4,153, wanawake 4,240 na 2,529 ni watoto kwa Pemba.

Huduma ya Urajisi wa Elimu
53.           Mheshimiwa Spika, Huduma hii ina madhumuni ya kuhakikisha sheria, sera na taratibu za Wizara zinafuatwa katika skuli za Serikali na za binafsi. Huduma hii pia inatoa leseni kwa walimu na kuzisajili skuli za Serikali na za binafsi. Shughuli za huduma hii zinatekelezwa na Ofisi ya Mrajisi wa Elimu. Kwa mwaka wa fedha 2019/20, huduma hii ilipangiwa kutumia jumla ya ruzuku ya TSh. 249,600,000/-. Kati ya fedha hizo TSh. 100,200,000/- ni kwa kazi za kawaida na TSh. 149,400,000/- zilitengwa kwa matumizi ya mshahara. Hadi kufikia Aprili, 2020, jumla ya TSh. 192,966,950 sawa na asilimia 77 zimepatikana.

54.           Mheshimiwa Spika, Utekelezaji halisi wa huduma hii ni kama hivi ifuatavyo: -
i)        Mapitio ya rasimu ya Sheria ya Elimu yanaendelea kufanyiwa kazi. Rasimu hiyo imewasilishwa kwa wadau kwa kupata maoni yao kabla ya kuwasilishwa katika Kamati ya Uongozi ya Wizara.
ii)      Uhakiki wa wanafunzi ambao walipata ujauzito kuanzia mwaka 2005 hadi 2015 ulifanyika. Lengo la uhakiki huo ni kutaka kujua maendelelo ya elimu ya wanafunzi hao. Jumla ya kesi 69 za ujauzito 31 Unguja na 38 Pemba zimefuatiliwa kujua maendeleo ya wanafunzi waliokutwa na kadhia hiyo baada ya kurejeshwa skuli.
iii)    Jumla ya kesi 43 za ujauzito zilizopokelewa zikiwemo Unguja 32 na 11Pemba. Kesi hizo zimeripotiwa kwa Kamanda wa Polisi wa Mikoa husika. Kati ya hizo, kesi 30 zimejadiliwa kwa mujibu wa Sheria namba 4 (2005) ya Kuwalinda Wari na Mtoto wa Mzazi Mmoja ambayo imewapa fursa wanafunzi hawa kuendelea na masomo yao. Wanafunzi 30 wamekubali kuendelea na masomo yao na wanafunzi 8 wamekataa.
iv)    Jumla ya kesi 13 za ndoa (2 Unguja na 11 Pemba) zimeripotiwa. Kwa mujibu wa Sheria ya Elimu Namba 6 ya mwaka 1982 kifungu cha 20(3) wanafunzi hao hawaruhusiwi kuendelea na masomo yao kwa vile bado wapo katika ngazi ya Elimu ya Lazima.
v)      Jumla ya migogoro 14 ya skuli za binafsi imeripotiwa. Migogoro hiyo ni pamoja na mishahara ya walimu, kamati za skuli na uongozi, kufukuzwa kwa wanafunzi katika skuli za binafsi, migogoro ya majengo pamoja na umiliki wa skuli. Migogoro 10 kati ya hiyo imesikilizwa na kupatiwa ufumbuzi.

Matokeo ya muda mfupi;
                             i.          Jumla ya walimu 1,465 wakiwemo wa Cheti cha Ualimu, Stashahada, Shahada ya Kwanza na ya Pili walipatiwa leseni za kufundishia za muda wa miaka mitano. Kati ya hao, walimu 736 wamesomea kazi ya ualimu (LTT), walimu 211 hawajasomea ualimu wamepatiwa leseni za kufundishia za muda wa mwaka mmoja (LUT) na wametakiwa kujiunga katika vyuo vya Ualimu vilivyosajiliwa na kutambuliwa na Serikali ili kusomea kazi ya Ualimu na walimu 518 wameongezewa muda wa leseni zao.
                           ii.          Jumla ya kesi 27 za udhalilishaji zimesikilizwa, kujadiliwa na kuripotiwa kwa Kamanda wa Polisi wa Mikoa husika. Kati ya kesi hizo 5 Unguja na kesi 22 Pemba.Wanafunzi wanaohusika na kesi hizo wamepatiwa ushauri nasaha na wanaendelea na masomo yao.
                         iii.          Jumla ya skuli 30 za Serikali zimepatiwa usajili zikiwemo skuli moja ya maandalizi pekee, 14 za maandalizi na msingi, moja ya msingi na 14 za sekondari kwa Unguja na Pemba.
                         iv.          Jumla ya skuli 38 za za binafsi zimewasilisha maombi ya usajili wa muda na zimepewa usajili wao baada ya kukaguliwa. Kati ya hizo, maandalizi 27, moja ya msingi, tisa za maandalizi na msingi, skuli mbili za maandalizi msingi na sekondari.
                           v.          Chuo cha ‘Wete Institute’ huko Pemba kimesajiliwa kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ualimu ngazi ya cheti na stashahada ya elimu ya maandalizi.

Programu ndogo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Elimu
55.           Mheshimiwa Spika, Programu hii ina madhumuni ya kuifanya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano itumike katika ngazi ya utawala, kujifunza na kufundishia, kuimarishahuduma ya mawasiliano, kutunza usalama wa taarifa na katika maisha ya kila siku. Shughuli za programu hii zinatekelezwa na Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Elimu. Kwa mwaka fedha 2019/20, programu hii ilipangiwa kutumia jumla ya TSh. 526,393,000/-. Kati ya fedha hizo, TSh. 278,059,000/- ni kwa kazi za kawaida na TSh. 248,334,000/- zilitengwa kwa matumizi ya mshahara. Hadi kufikia Aprili 2020, jumla ya TSh. 390,560,250/= zilipatikana ambazo ni sawa na asilimia 74.

56.           Mheshimiwa Spika, maelezo yautekelezaji halisi wa programu hii ni kama hivi ifuatavyo: -
                        i).            Sera ya TEHAMA katika Elimu imekamilika na kuthibitishwa na Mamlaka husika. Hivi sasa, mpango mkakati wa utekelezaji wa Sera unaaandaliwa.
                      ii).            Wizara kwa kushirikiana na shirika la lisilio la Kiserikali la “Good neighbors” Tanzania imetayarisha jumla ya vipindi 74 vya televisheni vya kujifunza kwa wepesi masomo ya Kiingereza, Sayansi na Jiografia na Kiswahili. Vipindi hivi vinaendelea kurushwa hewani na Shirika la ZBC. Aidha Wizara inaendelea kutayarisha na kurusha hewani vipindi vya masomo ya Sayansi kwa ngazi ya Msingi kwa Darasa la Tano na Sita. Lengo la programu hizi ni kuwasaidia walimu na wanafunzi katika kurahisisha ufundishaji na kupunguza changamoto za mada ngumu katika kuwafundisha wanafunzi wa ngazi ya msingi.
                    iii).            Jumla ya taasisi 127 za WEMA zimefanyiwa upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuziunganisha na mkonga wa Taifa. Miongoni mwa taasisi hizo ni Skuli 83, Vituo vya Walimu 10, Vituo 20 vya Ubunifu wa Kisayansi na Taasisi 14 za WEMA. Hadi sasa taasisi 13 za WEMA tayari zimeunganishwa katika mkonga wa Taifa.
                    iv).            Jumla ya watendaji 20 wamepatiwa mafunzo. Kati yao 18 walipatiwa mafunzo ya muda mfupi na wawili walipatiwa mafunzo ya muda mrefu katika fani ya Usimamizi wa TEHAMA na Mifumo pamoja na TEHAMA na Biashara. Aidha, Wizara  iliendesha mafunzo ya TEHAMA kwa walimu wa TEHAMA ngazi ya msingi ambapo jumla ya walimu 270 walifaidika na mafunzo hayo.
                      v).            Jumla ya washiriki 150 kutoka mataifa mbalimbali ndani na nje ya nchi ya Zanzibar walishiriki katika kongamano la kimataifa juu ya matumizi ya vyombo vya habari katika uendeshaji wa programu za elimu.Washiriki hao ni kutoka Zanzibar,  Tanzania Bara, Kenya, Uganda, Korea ya Kusini na Rwanda.
                    vi).            Baada ya kufungwa kwa skuli zote kutokana na maradhi ya Korona, Wizara  imeandaa vipindi vya kufundishia kwa kutumia vyombo vya habari vya Televisheni, Redio na mitandao ya kijamii.

Matokeo ya muda mfupi;
i)        Jumla ya walimu 100 kutoka katika skuli 23 za Sekondari Unguja na Pemba wamepatiwa mafunzo ya TEHAMA na matumizi ya mfumo wa Infoskuli kwa hatua ya majaribio. Mfumo huu unalenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa za maendeleo ya wanafunzi kitaaluma (continuous assessment) zikiwemo mahudhurio, tathmini na utendaji wa kazi za walimu. Aidha, mfumo huu unamuwezesha mzazi kupata taarifa hizo za maendeleo ya mtoto wake wakati wowote na pahali popote alipo nchini kupitia simu yake ya mkononi.
ii)      Jumla ya vipindi 74 vya masomo vikiwemo vipindi tisa vya elimu ya maandalizi na 65 vya masomo ya elimu ya msingi. Vipindi hivyo vinaendelea kurushwa kupitia Shirika la ZBC, Zanzibar Cable na mitandao ya kijamii.

Programu ndogo ya Elimu Mjumuisho na Stadi za Maisha
57.           Mheshimiwa Spika, Programu hii ina jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa elimu kwa watoto wote wakiwemo wenye mahitaji maalum. Programu hii inatekelezwa na Kitengo cha Elimu Mjumuisho na Stadi za Maisha. Kwa mwaka 2019/20 programu hii ilitengewa jumla ya TSh. 77,610,000/- kwa kazi za kawaida. Hadi kufikia Aprili, 2020 jumla ya TSh. 44,111,359/= sawa na asilimia 57 zilipatikana. Utekelezaji halisi wa shughuli za programu hii ndogo ni kama ifuatavyo: -

i)           Matengenezo ya vyumba viwili vya kufanyia upimaji wa kitaalamu wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu “resource rooms” katika skuli ya Kisiwandui Unguja na skuli ya Michakaini Pemba umekamilika.
ii)         Rasimu ya Sera ya Elimu Mjumuisho imeshafanyiwa mapitio na inatarajiwa kuwasilishwa katika vyombo vya ngazi za juu vya Serikali.
iii)       Wanafunzi 21 wamelipiwa ada ya masomo ya Stashahada ya Elimu Mjumuisho katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).Aidha, wanafunzi wawili wasioona (1 mwanamme na 1 mwanamke) wamelipiwa ada ya masomo katika ngazi ya Stashahada ya Ustawi wa Jamii (Social work) katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
iv)       Mwongozo wa walimu juu uchunguzi wa awali wa changamoto zinazowakwaza wanafunzi katika kujifunza umeandaliwa.Jumla ya watendaji 15 (8 Wanaume na 7 wanawake) kutoka taasisi tafauti walishiriki.
v)         Mafunzo ya siku tatu kwa walimu 3,697 (2,512 kutoka Unguja na 1,185 Pemba) kutoka skuli 145 juu ya muongozo wa uchunguzi wa awali na changamoto zinazowakwaza wanafunzi wakati wa kujifunza yametolewa.
vi)       Skuli 50 zimejengewa miteremko (ramps), kati yake 30 Unguja na 20 Pemba. Lengo la ujenzi huu ni kuyafanya mazingira ya skuli kuwa rafiki na yanayofikika kwa wote.
vii)     Jumla ya walimu 137 kutoka katika skuli 8 za majaribio ya elimu mjumuisho Unguja na Pemba wamepatiwa mafunzo kuhusu kuimarisha wa ujifunzaji makini darasani (active learning).
viii)   Watendaji watatu (wawili Unguja na mmoja Pemba) wamepatiwa mafunzo ya matumizi ya mashine ya upimaji wa kiwango cha usikivu (audiometer) pamoja na urekebishaji wa shime sikio (hearing aids fixing) kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi viziwi waweze kujifunza kwa ufanisi.
ix)       Jumla ya walimu 1,777 kutoka skuli 145 wamepatiwa mafunzo ya kuwatambua mapema wanafunzi wenye changamoto mbalimbali zinazowakwaza katika kujifunza na hivyo kuzipatia ufumbuzi wa mapema.

Programu ndogo ya Michezo na Utamaduni katika Skuli
58.           Mheshimiwa Spika, Programu hii ina madhumuni ya kumuandaa mwanafunzi kimwili, kiafya na kiakili katika kujifunza kwa kupitia michezo. Shughuli za programu hii zinatekelezwa na Idara ya Michezo na Utamaduni katika elimu. Kwa mwaka wa fedha 2019/20, programu hii imepangiwa kutumia jumla ya TSh. 752,271,000/-. Kati ya fedha hizo, TSh. 579,611,000/- ni kwa kazi za kawaida na TSh. 172,660,000/- ni kwa matumizi ya mishahara. Hadi kufikia Aprili, 2020, jumla ya TSh. 515,472,291/= sawa na asilimia 69 zilipatikana.

59.           Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa programu hii ni kama ifuatavyo: -

                        i).            Jumla ya matamasha matano ya utekelezaji wa mpango mkakati unaolenga ushajihishaji wa uzalendo, nidhamu na kuwajenga wanafunzi katika maadili mema pamoja na kuwafahamisha historia ya nchi ‘Nchi yetu ni Urithi wetu’ yamefanyika katika kila mkoa.
                      ii).            Shughuli za ufuatiliaji wa utekelezaji wa mpango wa “Sports 55” zimefanyika katika kila Wilaya na kwa kila skuli husika. Ufuatiliaji huu wa kina umelenga kuhakikisha kwamba vifaa vilivyotolewa vinatunzwa na kutumika vizuri na walimu waliopatiwa mafunzo wanawajibika ipasavyo kutimiza lengo la mpango huu.
                    iii).            Wanafunzi 410 wa skuli za maandalizi, msingi na sekondari Unguja na Pemba wameshiriki katika Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibari lililoratibiwa na Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
                    iv).            Jumla ya wanafunzi 187 kutoka skuli 33 za msingi Unguja na Pemba wameshiriki katika mashindano maalumu ya Sanaa ya uigizaji na uchoraji yaliyoandaliwa na Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar (BASFU) yenye lengo la kuibua na kuendeleza vipaji vya Sanaa hizo.
                      v).            Jumla ya walimu 210 wamepatiwa mafunzo ya uendeshaji na usimamizi wa michezo ya riadha kwa watoto (Kids Atheletics). Mafunzo haya yametolewa kwa mashirikiano na Chama cha Riadha Tanzania na yamelenga kuwashajihisha walimu kutumia mazingira na vifaa vya kienyeji kufundishia riadha.
                    vi).            Mashindano ya michezo na sanaa ya Tamasha la Elimu bila Malipo kuanzia ngazi ya skuli, Wilaya, Mkoa hadi Taifa yamefanyika kwa ufanisi na kuongeza hamasa na ushiriki wa wanafunzi katika michezo pamoja na kuibua vipaji vipya vya michezo na sanaa.
                  vii).            Jumla ya timu tano za michezo za mpira wa miguu, wavu, meza, mikono na riadha zimeshiriki mashindano ya michezo ya skuli za sekondari za Afrika Mashariki yaliofanyika mjini Arusha. Mashindano haya ni sehemu muhimu ya mpango wa kuendeleza vipaji vilivyotokana na mashindano ya ndani.

PROGRAMU YA SITA: UTAWALA NA UONGOZI
60.           Mheshimiwa Spika, Programu hii ina lengo la kuhakikisha nyenzo zilizo bora zinapatikana na zinatumika ipasavyo kwa kuimarisha utoaji na upatikanaji wa elimu nchini. Programu hii ina programu ndogo tatu; Programu ya Uongozi kiujumla, Programu ya Uratibu wa Shughuli za Mipango, Sera na Utafiti na Programu ya Uratibu wa Shughuli za Elimu Pemba. Kwa mwaka wa fedha 2019/20 Programu hii ilipangiwa jumla ya TSh. 14,599,201,000/-. Kati ya fedha hizo TSh. 7,573,176,000/- ni kwa kazi za kawaida, TSh. 5,526,025,000/- kwa matumizi ya mshahara na TSh. 1,500,000,000/- kwa matumizi ya kazi za maendeleo kutoka Serikalini. Utekelezaji halisi wa programu ya Utawala na Uongozi ni kama ifuatavyo: -

61.           Mheshimiwa Spika, programu hii ina madhumuni ya kutoa ufanisi wa Uongozi na utawala wa rasilimali za Wizara. Shughuli za programu hii ndogo zinatekelezwa na Idara ya Utumishi na Uendeshaji. Kwa mwaka wa fedha 2019/20, programu hii ilipangiwa jumla ya TSh. 6,091,971,000/-, kati ya fedha hizo TSh. 3,631,832,000/- kwa matumizi ya kawaida na TSh. 2,460,139,000/- ni kwa matumizi ya mshahara. Hadi kufikia Aprili, 2020, jumla ya TSh. 3,556,110,296/= zilipatikana sawa na asilimia 58. Utekelezaji wa kazi za programu hii ni kama ifuatavyo: -

i)           Jumla ya walimu 967 (638 Unguja na 329 Pemba) na 65 nje ya kada ya ualimu waliajiriwa baada ya kupata kibali cha uajiri kutoka Tume ya Utumishi Serikalini. Kati yao, kwa upande wa Unguja walimu 83 ni wa Shahada ya Kwanza Sayansi, 450 Shahada ya kwanza Sanaa, 104 Stashahada ya Sayansi, 1 Stashahada ya Sanaa. Kwa upande wa Pemba, waliajiriwa walimu 48 wa Shahada ya Kwanza Sayansi, 193 Shahada ya Kwanza Sanaa, 84 Stashahada Sayansi na 4 ni walimu wa Cheti.
ii)      Jumla ya wafanyakazi 463 Unguja na 118 Pemba waliopewa likizo walilipwa posho la likizo la jumla ya TSh. 58,100,000.
iii)    Jumla ya wafanyakazi 474 (141 Unguja na 333 Pemba) walipatiwa fursa ya kujiunga na masomo katika vyuo mbali mbali vya ndani na nje ya nchi katika ngazi tofauti baada ya kukamilisha masharti ya kiutumishi na ya vyuo. Kati yao, wafanyakazi 23 wamepatiwa mafunzo ya muda mfupi na 118 ni wa mafunzo ya muda mrefu.
iv)    Jumla ya walimu 1,231 walipatiwa huduma ya likizo, walimu 84 walistaafu,  6 waliacha kazi na walimu 10 walifariki dunia. Mwenyezi Mungu awalaze mahali pema peponi Amin.
v)      Jumla ya wafanyakazi 21 walistaafu kazi kwa mujibu wa sheria. Wafanyakazi watano walifariki dunia, Mwenyezi Mungu awalaze mahali pema peponi (Amin). Aidha mfanyakazi mmoja alipewa uhamisho kwenda kuendelea na kazi katika Wizara ya Fedha na Mipango na mfanyakazi mmoja amechukua likizo bila ya malipo.
vi)    Jumla ya wafanyakazi 350 Unguja na 259 Pemba wamedhaminiwa kupata mikopo ya Benki na Saccos mbalimbali nchini. Wafanyakazi hao wamepata mikopo ya fedha taslim, vifaa vya ujenzi, vipando na vifaa vya matumizi ya nyumbani. Mikopo iliyotolewa ina thamani ya TSh.1,227,284,338/- kwa Unguja na TSh 1,363,264,310/- kwa Pemba.

Matokeo ya muda mfupi;
Hadi kufikia Aprili 2020, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ilikuwa na jumla ya wafanyakazi 7,758. Kati yao, 3,877 ni wanawake na 3,881 wanaume. Wafanyakazi 5,967 wapo Unguja (3,193wanawake na 2,774 wanaume) na kwa upande wa Pemba wapo wafanyakazi 1,791 (wanawake 684 na wanaume ni 1,107). Kati ya wafanyakazi wote hawa 5,704 ni wa kada ya ualimu na 1,664 ni wafanyakazi wasiokuwa wa kada ya ualimu.

Programu ndogo ya Uratibu wa Shughuli za Mipango, Sera na Utafiti
62.           Mheshimiwa Spika, programu hii ina madhumuni ya kufanikisha na kuratibu Mipango, Sera na Utafiti katika Wizara. Programu hii ndogo inatekelezwa na Idara ya Mipango, Sera na Utafiti. Kwa mwaka 2019/20 programu hii ilipangiwa kutumia jumla ya TSh. 5,233,552,000/-. Kati ya fedha hizo, TSh. 3,238,099,000/- ni kwa kazi za kawaida, TSh. 495,453,000/- kwa matumizi ya mshahara na TSh. 1,500,000,000/- ni kwa kazi za maendeleo. Hadi kufikia Aprili, 2020, jumla ya TSh. 2,367,449,619/= za kazi za kawaida zilipatikana ambazo ni sawa na asilimia 45.2.

63.           Mheshimiwa Spika, utekelezaji halisi wa programu hii ni kama hivi ifuatavyo: -
                       i.            Rasimu ya mapitio ya Sera ya Elimu ya mwaka 2006 imewasilishwa kwa wadau 1,200 kwa ajili ya kutoa michango yao ya kuiimarisha. Washiriki katika mijadala ilijumuisha walimu, wazee, maafisa kutoka taasisi za serikali na binafsi pamoja na viongozi mbalimbali wa Wilaya na Mikoa yote ya Unguja na Pemba. Rasimu hiyo itawasilishwa kwenye vikao vya juu vya Serikali kwa ushauri zaidi.
                     ii.            Ufuatiliaji wa utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Elimu umeendelea kwa kila robo mwaka na ripoti za utekelezaji zimetayarishwa. Aidha, Wizara imeendelea kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa miradi ya elimu iliyokamilika na inayoendelea. Miongoni mwa Miradi hiyo ni ujenzi wa Skuli Tisa za Sekondari (ZATEP), Mradi wa Uimarishaji wa Elimu ya Sekondari (ZISP), Mradi wa  Uimarishaji wa Elimu ya Maandalizi na Utekelezaji wa Mradi wa Elimu Mbadala na Amali (ALSD II). Miradi hiyo inatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo wa ndani na nje ya nchi.
                   iii.            Mkutano mkuu wa tatu wa mwaka wa tathmini ya elimu (3rd AJESR) uliowashirikisha wadau 150 wa elimu wa ndani na nje ya Zanzibar wakiwemo wahisani, wazee, wanafunzi, kamati za skuli, taasisi za serikali na za watu binafsi umefanyika. Mkutano huo ulifanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 9 - 11/03/2020 katika ukumbi wa Madinat Albahr.
                   iv.            Matokeo ya utafiti wa kutathmini upatikanaji, utumiaji na usimamizi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa skuli za sekondari Zanzibar yamewasilishwa kwa wadau wa elimu katika Mkoa wa Mjini Magharibi. Uwasilishaji pia utaendelea katika mikoa mingine.
                     v.            Zoezi la utafiti wa SEACMEQ V limeanza kwa hatua ya kutayarisha na kuhariri dodoso za kukusanyia taarifa. Hatua inayofuata ni kamati ya utafiti ya SEACMEQ kupitisha maswali ya utafiti mkuu na kuanza zoezi la utafiti. Kikao cha pamoja cha nchi wanachama kilichopangwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi wa Aprili 2020 nchini Afrika ya Kusini kiliahirishwa kutokana na ugonjwa wa virusi vya Korona (COVID 19).
                   vi.            Mfumo wa kielektroniki wa kukusanya taarifa za skuli unaendelea kutumika kwa majaribio. Mfumo huu umesaidia kuinua usimamizi wa skuli zetu katika utoaji na upatikanaji wa elimu. Aidha, Wizara imewajengea uwezo wataalamu wa ndani ili waweze kuusimamia mfumo huo. Kwa sasa kazi inayoendelea ni kuhamisha mfumo kutoka katika SERVER za kampuni ya FHI 360 kwenda katika SERVER za WEMA.
                 vii.            Wizara imeandaa mpango wa kukabiliana na athari za ugonjwa wa virusi vya Korona (COVID 19) katika elimu. Mpango huo una lengo la kuhakikisha mawasiliano ya karibu kati ya uongozi, walimu na wanafunzi katika kuhakikisha watoto wanaendelea kusoma hasa kipindi hiki ambacho watoto wapo majumbani. Aidha, mpango umezingatia pia kuendeleza ubunifu na mikakati mbalimbali iliyoibuliwa katika kujifunza na kufundisha hata baada ya COVID 19, hasa katika matumizi ya Teknolojia katika elimu, uimarishaji wa miundombinu na uhamasishaji wa jamii katika kusaidia elimu ya mtoto. 



Programu ndogo ya Uratibu shughuli za elimu Pemba
64.           Mheshimiwa Spika, Programu hii ndogo ina madhumuni ya kuratibu na kusimamia shughuli zote za elimu kwa upande wa Pemba. Msimamizi Mkuu wa shughuli za programu hii ni Afisa Mdhamini wa Wizara yangu kupitia katika Divisheni ya Idara ya Uendeshaji na Utumishi Pemba. Programu hii ndogo ilipangiwa jumla ya TSh. 3,273,678,000/-, kati ya fedha hizo TSh. 703,245,000/-kwa kazi za kawaida na TSh. 2,570,433,000/- ni kwa matumizi ya mshahara. Hadi kufikia Aprili, 2020, jumla ya TSh. 2,799,615,809/= zilipatikana sawa na asilimia 86.

65.           Mheshimiwa Spika, Fedha za programu hii zilitumika katika kusimamia na kufuatilia shughuli na programu za elimu Pemba. 

MAPATO
66.           Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kukusanya mapato kupitia usajili wa Skuli za binafsi na malipo ya leseni za walimu. Hadi kufikia Aprili 2020, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imekusanya jumla ya TSh. 104,063,190/= kati ya TSh. 195,655,000/= zilizopangwa kukusanywa. Hii ni sawa ya asilimia 53 ya makadirio. Kati ya Mapato yaliyokusanywa TSh. 58,596,850/= zinatokana na malipo ya leseni za walimu na TSh. 34,569,560/= ni za usajili wa skuli za binafsi. 

MPANGO WA UTEKELEZAJI KWA MWAKA 2020/2021 KWA MFUMO WA PROGRAMU

67.           Mheshimiwa Spika, baada ya taarifa hiyo ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa mwaka wa fedha 2019/20 naomba sasa niwasilishe vipaumbele vya Wizara yangu na kisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2020/2021.



Vipaumbele vya Wizara
68.           Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2020/2021,vipaumbele vya Sekta ya Elimu vitakuwa kama ifuatavyo: -

                    i.         Kuendelea kuzipatia skuli za sekondari fedha za ruzuku kufidia michango ya wazee kwa kuwapatia wanafunzi mabuku ya kuandikia na vifaa vyengine vya kusomeshea na kujifunzia vikiwemo chaki, vitabu vya kiada na ziada na vifaa vya maabara.
                  ii.         Kuimarisha miundombinu na mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa kukamilisha ujenzi wa madarasa 50 yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi, kuanza ujenzi wa skuli tatu mpya katika maeneo ya Mfenesini, Gamba kwa Unguja na Kifundi kwa Pemba, kujenga maabara katika skuli 11 za Sekondari pamoja na kukamilisha ujenzi wa skuli ya sekondari ya Kibuteni.
                iii.         Kukamilisha ukarabati wa Skuli ya Sekondari ya Lumumba na kuanza ukarabati mkubwa wa Skuli za sekondari za Benbella, Hailesselasie na Pajemtule kwa Unguja na Skuli ya Sekondari ya Chwaka Tumbe Pemba
                iv.         Kufanya ukarabati mdogo katika Skuli 20 za Sekondari Unguja na Pemba.
                  v.         Kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Korona (COVID 19) na kuwawezesha wanafunzi wa ngazi zote kuendelea kupata elimu kupitia Teknolojia.
                vi.         Kuendelea na matumizi ya TEHAMA katika kuinua ubora wa elimu.
              vii.         Kuzipatia fedha za zawadi skuli za sekondari na msingi zitakazoongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika katika masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza.
            viii.         Kufanya utafiti wa tathmini ya ubora wa elimu ya msingi (SEACMEQ V).
                ix.         Kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kukusanya marejesho ya mikopo kutoka kwa wahitimu wa ngazi hiyo.
                  x.         Kuwajengea uwezo walimu wanaofundisha masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza.
                xi.         Kuandaa Mitaala ya Elimu ya Maandalizi na Msingi, kuandika mihitasari ya masomo, kuandika na kuchapisha vitabu pamoja na miongozo ya walimu kwa ngazi ya elimu ya maandalizi.
              xii.         Kuwawezesha watoto wenye mahitaji maalumu kupata elimu kwa kuimarisha mazingira ya skuli kujali mahitaji ya watoto kuendana na hali zao.
            xiii.         Kutoa elimu ya ushauri nasaha juu ya udhalilishaji (ndoa za mapema na mimba za utotoni). Kuratibu mapambano dhidi ya liwati, dawa ya kulevya, UKIMWI na COVID 19 kwa kushirikiana na taasisi husika.
            xiv.         Kuimarisha huduma za dahalia kwa kuzipatia usafiri (basi moja) na chakula kwa wanafunzi 2,000.
              xv.         Kuandaa mkutano mkuu wa nne wa pamoja na wadau wa elimu kutathmini mafanikio ya Sekta ya Elimu Zanzibar (4th AJESR).
            xvi.         Kuimarisha programu za masomo katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia na Mamlaka ya Mafunzo ya Amali.

69.           MheshimiwaSpika, Naomba sasa, kuwasilisha mpango wa maendeleo ya elimu kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021 kwa mfumo wa programu kama hivi ifuatavyo: -

70.           Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021 Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali itaendelea kutekeleza malengo yake yaliyozingatia Dira 2020, MKUZA III, Sera ya Elimu, Mpango Mkuu wa Elimu (2017 – 2021), vipaumbele vya Wizara kwa mwaka 2020/21 pamoja na mikakati mengine ya Kitaifa na Kimataifa yenye lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma ya elimu nchini. Wizara pia, itaendelea kushirikiana na sekta nyengine zinazotoa huduma za jamii na kuimarisha uchumi ikiwemo Wizara ya Afya, Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Maendeleo ya Wazee, Wanawake na Watoto, Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu, Washirika wa Maendeleo na Mashirika yasiyo ya kiserikali na wananchi.

71.           Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha wa 2020/2021, Wizara yangu itatekeleza miradi mitano ya maendeleo kupitia programu zake sita kama ilivyokuwa mwaka 2019/2020. Programu ya Maandalizi na Msingi itatekelezwa kwa pamoja na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kupitia mfumo wa Ugatuzi.

72.           Mheshimiwa Spika, Jumla ya TSh. 138,145,584,000/= zimetengwa. Kati ya hizo TSh. 123,183,500,000/= ni za SMZ, TShs. 14,962,084,000/= ni kutoka kwa Washirika wa Maendeleo na TSh. 4,500,000,000/= ni mchango wa SMZ kwa miradi ya maendeleo. Fedha za Washirika wa Maendeleo zinajumuisha TSh. 6,327,084,000/= ni ruzuku kutoka GPE, Table for Two (TfT), Shirika la “Good Neighbors” la Korea na “Milele Zanzibar Foundation” na TSh. 8,635,000,000/= ni mkopo kutoka Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika (BADEA). Jadweli Nam. 49 linatoa ufafanuzi zaidi.

Mheshimiwa Spika, Miradi mitano itakayotekelezwa na Wizara ni hii ifuatavyo: -

                              i).      Mradi wa Uimarishaji wa Elimu ya Maandalizi
                            ii).      Mradi wa Uimarishaji wa Elimu ya Msingi
                          iii).      Mradi wa Uimarishaji wa Elimu ya Lazima
                          iv).      Mradi wa Uimarishaji wa Elimu Mbadala na Amali.
                            v).      Mradi wa Uimarishaji wa Miundombinu katika elimu

MAELEZO YA PROGRAMU ZA ELIMU
73.           Mheshimiwa Spika, yafuatayo ni maelezo ya programu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali yanayohusisha Madhumuni, Matokeo ya muda mfupi, Viashiria na Shabaha za utekelezaji kwa kila programu.

PROGRAMU YA KWANZA: 
ELIMU YA MAANDALIZI NA MSINGI
74.           Mheshimiwa Spika, Programu hii ina madhumuni ya kumuandaa mtoto kimwili na kiakili kwa ajili ya kupata elimu ya maandalizi na msingi na kumuwezesha mwanafunzi kujua kusoma, kuandika na kuhesabu na kumtayarisha kwa elimu ya sekondari.

Matokeo ya muda mfupi;
·         Kumtayarisha mtoto kwa ajili ya elimu ya msingi.
·         Kutoa elimu ya msingi

Viashiria vya matokeo;
·         Uwiano wa uandikishaji wa wanafunzi katika ngazi ya maandalizi na msingi.
·         Uwiano wa idadi ya walimu kwa wanafunzi.
·         Uwiano wa wanafunzi kwa darasa.
·         Uwiano wa ufaulu wa wanafunzi.

Shabaha za utekelezaji;
·         Kuongeza kiwango cha uandikishaji wanafunzi wa maandalizi kutoka asilimia 86.0 kwa mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 88 ifikapo mwaka 2021.
·         Kuongeza kiwango halisi cha uandikishaji wanafunzi wa msingi kutoka asilimia 86 kwa mwaka 2019 hadi kufikia asilimia 90 ifikapo mwaka 2021.

PROGRAMU YA PILI:  ELIMU YA SEKONDARI
75.           Mheshimiwa Spika, Programu ya Elimu ya Sekondari madhumuni yake makubwa ni kumtayarisha mwanafunzi aweze kuendelea na masomo katika ngazi za juu zaidi.

Matokeo ya muda mfupi;
·         Kutoa Elimu ya Sekondari.

Viashiria vya matokeo;
·         Uwiano wa wanafunzi wanaomaliza elimu ya lazima,
·         Uwiano halisi wa uandikishaji wa wanafunzi katika ngazi ya kidato cha nne na cha sita,
·         Uwiano wa idadi ya walimu kwa nyumba za wafanyakazi katika maeneo yasiyofikika kirahisi
·         Uwiano wa wanafunzi kwa madarasa.

Shabaha za utekelezaji;
·         Kuongeza kiwango halisi cha uandikishaji wanafunzi wa sekondari ya awali (Kidato cha 1 – 4) kutoka asilimia 79.5 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 83 ifikapo mwaka 2021.
·         Kiwango cha ufaulu cha mpito kutoka kidato cha pili kwenda cha tatu kuongezeka kutoka asilimia 76.8 mwaka 2019 hadi kufikia asilimia 78.8 ifikapo mwaka 2020.

PROGRAMU YA TATU:  ELIMU YA JUU
76.           Mheshimiwa Spika, programu hii madhumuni yake ni kutoa elimu itakayomuwezesha muhitimu kujiajiri au kuajiriwa. Programu hii ina programu ndogo moja na maeneo madogo manne ambayo ni: -

Programu ndogo ya Mafunzo ya Ualimu
77.           Mheshimiwa Spika, programu hii ina madhumuni ya kuwawezesha walimu kuwa wabunifu, wataalamu na wenye uwezo wa kuongoza ili kukuza ubora wa elimu.

Matokeo ya muda mfupi;
·         Elimu ya Diploma ya Ualimu kutolewa

Viashiria vya matokeo;
·         Idadi ya wanafunzi wote walioandikishwa vyuo vya ualimu.

Shabaha za Utekelezaji;
·         Kuongeza kiwango cha asilimia ya walimu wenye sifa kutoka 99.2 mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 99.6 mwaka 2020.

Huduma ya Elimu ya Juu, Ushauri na Utafiti 
78.           Mheshimiwa Spika, Huduma hii ina madhumuni ya kumtayarisha mwanafunzi kuingia katika fani za kitaalamu na ajira.

Matokeo ya muda mfupi;
·         Kiwango cha elimu ya Stashahada, Shahada ya kwanza, Shahada ya pili na Shahada ya tatu kutolewa.

Viashiria vya matokeo;
·         Idadi ya wanafunzi wanaomaliza ngazi ya Astashahada na Stashahada.
·         Idadi ya wanafunzi wanaomaliza ngazi ya Shahada ya kwanza ya Uzamili na Uzamivu.
·         Idadi ya tafiti zinazofanywa.



Shabaha za Utekelezaji;
·         Kuongeza idadi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu kutoka 7,303 mwaka 2019 hadi kufikia 8,000 mwaka 2021.

Huduma ya Elimu ya Sayansi na Teknolojia
79.           Mheshimiwa Spika, Huduma hii ina madhumuni ya kuimarisha elimu ya sayansi na teknolojia.

Matokeo ya muda mfupi;
·         Kuimarisha ufundishaji na kujifunza Sayansi, Hisabati na Teknolojia
·         Elimu ya Ufundi kuimarishwa.

Viashiria vya matokeo;
·         Idadi ya wanafunzi wahitimu katika Taasisi,
·         Uwiyano wa wanafunzi kwa madarasa.

Huduma ya Mikopo ya Elimu ya Juu
80.           Mheshimiwa Spika, Huduma hii ina madhumuni ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya Juu.

Matokeo ya muda mfupi;
·         Mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutolewa.
·         Fedha zilizokopeshwa kwa wanafunzi kurejeshwa.

Viashiria vya matokeo;
·         Idadi ya wanafunzi wanaopokea mikopo
·         Idadi ya wanafunzi wanaorudisha mikopo.

Shabaha za Utekelezaji;
·         Kuongeza utoaji wa mikopo kwa wanafunzi kutoka asilimia 36 ya waombaji mwaka 2018/19 hadi kufikia asilimia 45 ifikapo mwaka 2020/21.
·         Kuongeza makusanyo ya marejesho ya mikopo kutoka TSh. 1,970,000,000/= ya mwaka 2019/20 na kufikia TSh. 3,000,000,000/= mwaka 2020/21.

Huduma ya Uratibu wa Elimu ya Juu
81.           Mheshimiwa Spika, Huduma hii ina madhumuni ya usimamizi na tathmini ya elimu ya juu.

Matokeo ya muda mfupi;
·         Tathmini katika vyuo vinavyotoa elimu ya juu kufanyika.
·         Wahitimu waliomaliza masomo ya elimu ya juu kuratibiwa.

Viashiria vya matokeo;
·         Idadi ya wanafunzi wanaoendelea na masomo ya elimu ya juu kijinsia.
·         Idadi ya wahitimu wa elimu ya juu kijinsia.

PROGRAMU YA NNE: ELIMU MBADALA NA MAFUNZO YA AMALI
82.           Mheshimiwa Spika, Programu hii madhumuni yake ni kutoa elimu ya mafunzo ya amali kwa mwanafuzi kulingana na mahitaji ya soko la ajira. Programu hii ina programu ndogo ndogo mbili kama ifuatavyo;

Programu ndogo ya Mafunzo ya Amali
83.           Mheshimiwa Spika, Programu hii ina madhumuni ya kutoa elimu itakayowawezesha vijana kujiajiri ili kujikwamua na umasikini.

Matokeo ya muda mfupi;
·         Mafunzo ya Amali na ufundi kutolewa.

Viashiria vya matokeo;
·         Ukosefu wa ajira kwa vijana kupungua
·         Idadi ya wanafunzi wanaomaliza mafunzo ya amali kuongezeka.

Programu ndogo ya Elimu Mbadala na Watu Wazima
84.           Mheshimiwa Spika, Programu hii ina madhumuni ya kupunguza kiwango cha kutojua kusoma, kuandika na kuhesabu miongoni mwa wanajamii.

Matokeo ya muda mfupi;
·         Elimu mbadala na ya watu wazima kutolewa.

Viashiria vya matokeo;
·         Kiwango cha kujua kusoma, kuandika na kuhesabu kwa watu wazima,
·         Idadi ya watu wazima wanaoshiriki katika madarasa ya wanakisomo,
·         Idadi ya vijana waliojiunga na madarasa na vituo vya elimu mbadala,
·         Idadi ya wanakisomo walioanzisha vikundi vya ushirika

Shabaha za Utekelezaji;
·         Kuongeza kiwango cha kujua kusoma na kuandika kutoka asilimia 84.2 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 90 ifikapo mwaka 2022.

PROGRAMU YA TANO: UBORA WA ELIMU
85.           Mheshimiwa Spika, Programu hii ina madhumuni ya kutoa elimu bora kwa ngazi zote za elimu. Ina programu ndogo tatu na maeneo matano ya kutoa huduma kama yafuatayo;




Huduma ya Mitaala na Vifaa vya Kufundishia
86.           Mheshimiwa Spika, Huduma hii ina madhumuni ya kutayarisha mitaala ya elimu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa ngazi za elimu ya maandalizi, msingi, sekondari na mafunzo ya Ualimu. 

Matokeo ya muda mfupi;
·         Mitaala ya Elimu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa ngazi zote kutayarishwa.

Viashiria vya matokeo;
·         Idadi ya Mitaala na vifaa vya kufundishia na kujifunzia vilivyotayarishwa na kusambazwa katika skuli.

Huduma ya Upimaji na Tathmini ya Elimu
87.           Mheshimiwa Spika, Programu hii ina madhumuni ya kupima na kutathmini utekelezaji wa utoaji wa elimu.

Matokeo ya muda mfupi;
·         Malengo ya elimu kupimwa.

Viashiria vya matokeo;
·         Asilimia ya wanafunzi na kiwango cha mpito katika ngazi za darasa la nne, darasa la sita, kidato cha pili, kidato cha nne na cha sita.
·         Asilimia ya ufaulu wa walimu na wanafunzi

Huduma ya Ukaguzi wa Elimu
88.           Mheshimiwa Spika, utoaji wa huduma hii una madhumuni ya kusimamia utoaji wa elimu unaofuata mtaala na kuhakikisha ufanisi na ubora wa elimu inayotolewa.

Viashiria vya matokeo;
·         Idadi ya skuli zilizokaguliwa
·         Idadi ya ripoti za ukaguzi zilizowasilishwa

Huduma za Maktaba
89.           Mheshimiwa Spika, Programu hii ina madhumuni ya kutoa fursa ya kutumia vitabu na vyanzo vyengine vya taaluma kwa wananchi.

Matokeo ya muda mfupi;
·         Kutoa nafasi kwa wanafunzi na watu wengine ya kupata taarifa mbalimbali kupitia maktaba.

Viashiria vya matokeo;
·         Idadi ya watu wanaotumia maktaba
·         Idadi ya vitabu, CDs, magazeti na majarida yaliyopo katika maktaba.
·         Idadi ya skuli zenye maktaba kamili.

90.           Mheshimiwa Spika, Programu hii ina madhumuni ya kuhakikisha Sheria, Sera na taratibu za Wizara zinafuatwa. Pia kutoa leseni kwa walimu na kusajili skuli za Serikali na za binafsi.

Matokeo ya muda mfupi;
·         Skuli za Serikali na binafsi zenye viwango bora kusajiliwa
·         Leseni za walimu kutolewa.

Viashiria vya matokeo;
·         Idadi ya leseni za walimu zilizotolewa.
·         Idadi ya skuli zilizosajiliwa.
·         Sheria ya Elimu iliyopitiwa na kurekebishwa.
·         Idadi ya wanafunzi waliopata ujauzito na kurejea masomoni baada ya kujifungua kuratibiwa.
·         Idadi ya kesi za ndoa kwa wanafunzi zilizofuatiliwa na kutolewa uamuzi.

Programu ndogo ya Elimu Mjumuisho na Stadi za Maisha
91.           Mheshimiwa Spika, Programu hii ina madhumuni ya kutoa elimu kwa wote wakiwemo watoto wenye mahitaji maalum.

Matokeo ya muda mfupi;
·         Vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa watoto wenye mahitaji maalum kutolewa

Viashiria vya matokeo;
·         Idadi ya wanafunzi na walimu katika Elimu Mjumuisho.

Programu ndogo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
92.           Mheshimiwa Spika, Programu hii ina madhumuni ya kuifanya teknolojia ya habari na mawasiliano itumike katika kujifunza, kufundisha, ngazi ya utawala na katika maisha ya kila siku.

Matokeo ya muda mfupi;
·         Walimu na wanafunzi wanapatiwa mafunzo juu ya matumizi ya Teknolojia ya kisasa. 

Viashiria vya utekelezaji;
·         Idadi ya walimu wenye ujuzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,
·         Idadi ya vifaa vya Teknolojia ya Habari na mawasiliano katika skuli na Wizara
·         Idadi ya Taasisi za elimu zilizounganishwa na mkonga wa Taifa.
·         Mafunzo ya matumizi ya kompyuta kutolewa kuanzia katika skuli za msingi.


Programu ndogo ya Michezo na Utamaduni katika Skuli
93.           Mheshimiwa Spika, Programu hii ina madhumuni ya kumuandaa mwanafunzi kimwili, kiafya na kiakili katika kujifunza kwa kupitia michezo.

Matokeo ya muda mfupi;
·         Kuinua taaluma ya michezo katika skuli.

Viashiria vya matokeo;
·         Idadi ya walimu wenye taaluma ya michezo
·         Idadi ya skuli zenye viwanja vya michezo
·         Idadi ya skuli zenye vifaa vya michezo
·         Idadi ya wanafunzi wenye vipaji vya michezo

PROGRAMU YA SITA: UTAWALA NA UONGOZI
94.           Mheshimiwa Spika, Programu hii madhumuni yake makubwa ni kuhakikisha nyenzo zilizo bora zinapatikana na zinatumika kwa kuimarisha utoaji wa elimu. Programu hii ina programu ndogo tatu kama zifuatavyo: -

Programu ndogo ya Uongozi kiujumla
95.           Mheshimiwa Spika, programu hii ina madhumuni ya kuratibu usimamizi na ufanisi wa Uongozi na Utawala wa rasilimali za Wizara.

Matokeo ya muda mfupi;
·         Kupatikana kwa ufanisi katika utoaji wa huduma, uongozi na utawala wa rasilimali za Wizara.

Viashiria vya matokeo;
·         Idadi ya wafanyakazi wanaoajiriwa na kustaafu,
·         Mafunzo yanayotolewa kwa wafanyakazi.

Shabaha za Utekelezaji;
·         Kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa wafanyakazi na upatikanaji wa nyenzo za kufanyia kazi.

Programu ndogo ya Uratibu wa Shughuli za Mipango, Sera na Utafiti
96.           Mheshimiwa Spika, programu hii ina madhumuni ya kufanikisha na kuratibu Mipango, Sera na Utafiti katika Wizara.

Matokeo ya muda mfupi;
Kupatikana kwa sera na mipango ya Wizara, kufanya utafiti na kufanya ufuatiliaji na tathmini.

Viashiria vya matokeo;
·         Idadi za tafiti zilizofanywa
·         Ripoti za utekelezaji na ripoti za tathmini.

Programu ndogo ya kuratibu shughuli za Elimu Pemba
97.           Mheshimiwa Spika, programu hii ina madhumuni ya kuratibu na kusimamia shughuli zote za elimu kwa upande wa Pemba. Matokeo ya muda mfupi na shabaha za utekelezaji zinazotumika ni kama zile zilizoelezwa katika programu za Uongozi kiujumla na Uratibu wa shughuli za Mipango, Sera na Utafiti.

98.           Mheshimiwa Spika, msimamizi wa shughuli za programu hii ni Afisa Mdhamini wa Wizara yangu kupitia katika Divisheni ya Idara ya Uendeshaji na Utumishi Pemba.

MGAWANYO WA FEDHA KWA PROGRAMU
99.           Mheshimiwa Spika, Sehemu hii inaonesha mgawanyo wa fedha kwa Programu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali yenye kuzingatia gharama za Idara/ Vitengo/Taasisi zilizomo katika programu husika.

PROGRAMU YA KWANZA:
ELIMU YA MAANDALIZI NA MSINGI
Idara Husika:  Idara ya Elimu ya Maandalizi na Msingi
Gharama za Programu: Jumla ya TSh. 5,135,232,000/= zimepangwa kwa ajili ya kufanikisha programu hii. Kati ya fedha hizo, TSh. 1,479,669,000/= ni kwa kazi za kawaida na TSh. 3,655,563,000/= kwa kazi za maendeleo.

PROGRAMU YA PILI:    ELIMU YA SEKONDARI
Idara Husika:  Idara ya Elimu ya Sekondari
Gharama za Programu: Jumla ya TSh. 66,478,525,000/= zimepangwa kwa ajili ya kufanikisha programu hii. Kati ya hizo TSh. 53,062,304,000/= kwa kazi za kawaida na TSh. 13,416,221,000/= kwa kazi za maendeleo.

PROGRAMU YA TATU:    ELIMU YA JUU
Taasisi Husika: Idara ya Mafunzo ya Ualimu, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na Kitengo cha Uratibu wa Elimu wa Juu.

Gharama za Programu: Jumla ya TSh. 30,480,366,000/= zimepangwa kwa kufanikisha programu hii kwa kazi za kawaida.

PROGRAMU YA NNE: ELIMU MBADALA NA MAFUNZO YA AMALI
Idara Husika: Mamlaka ya Mafunzo ya Amali pamoja na Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima.

Gharama za Programu: Jumla ya TSh. 9,403,674,000/= zimepangwa kwa ajili ya kufanikisha programu hii kwa kazi za kawaida.


PROGRAMU YA TANO:    UBORA WA ELIMU
Idara Husika: Taasisi ya Elimu ya Zanzibar, Baraza la Mitihani la Zanzibar, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Elimu, Kitengo cha Elimu Mjumuisho na Stadi za Maisha, Shirika la Huduma za Maktaba Zanzibar, Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Katika Elimu, Ofisi ya Mrajisi wa Elimu, Idara ya Michezo na Utamaduni Katika Skuli.

Gharama za Programu: Jumla ya TSh. 10,201,204,000/= zimepangwa kwa ajili ya kufanikisha programu hii kwa kazi za kawaida.

PROGRAMU YA SITA:      UONGOZI NA UTAWALA
Idara Husika: Idara ya Utumishi na Uendeshaji, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti na Ofisi ya Elimu Pemba.

Gharama za Programu: Jumla ya TSh. 16,446,583,000/= zimepangwa kwa ajili ya kufanikisha programu hii. Kati ya hizo, TSh. 14,056,283,000ni kwa kazi za kawaida na TSh. 2,390,300,000/= kwa kazi za maendeleo.

100.       Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2020/21 Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imekadiriwa kukusanya mapato ya jumla ya TSh. 215,700,000/=. Mapato hayo yatatokana na usajili wa skuli na leseni za kufundishia walimu.

JUMLA YA GHARAMA ZA WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI
101.       Mheshimiwa Spika, gharama kwa programu zote sita za Wizara ni TSh. 138,145,584,000/= sawa na bajeti yote ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali inayotumia programu iliyoainishwa Barazani. Kati ya fedha hizo, TSh. 118,683,500,000/= zimetengwa kwa kazi za kawaida na TSh. 19,462,084,000/= kwa kazi za maendeleo. Kati ya fedha za maendeleo, TSh. 4,500,000,000/= ni mchango wa SMZ na TSh. 14,962,084,000/= ni mchango wa Washirika wa Maendeleo.

102.       Mheshimiwa Spika, Utekelezaji wabajeti hii utategemea kupungua au kuondoka kabisa kwa janga la ugonjwa wa virusi vya Korona (COVID 19). Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaalie ugonjwa huo umalizike. Ikiwa hivyo, wanafunzi wataendelea na masomo yao kama kawaida wakiwa skuli. Kama dhana yetu itakuwa sahihi bajeti yetu haitaathirika sana kwa yale tuliyopanga kuyatekeleza. Aidha, Ugonjwa huu ukiendelea (tunamuomba Mwenyezi Mungu asijaalie hivyo) na wanafunzi wakaendelea kuwa nyumbani, bajeti yetu itaathirika na fedha nyingi zitatumika katika utekelezaji wa mpango wa kukabiliana na COVID 19 katika kutoa elimu.


SHUKURANI
103.       Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kutoa shukurani za dhati kwa washirika wote wa sekta ya elimu wakiwemo wananchi, washirika wa maendeleo na mashirika ya misaada ya kimataifa kwa kutuunga mkono katika jitihada zetu za kuendeleza elimu.  Tunatoa shukurani zetu za pekee kwa Serikali ya Sweden, Marekani, Oman na Serikali ya Watu wa China, Serikali ya India na Iran. Pia, napenda kuyashukuru mashirika mbalimbali ya kimataifa yakiwemo, Sida, USAID, KOICA, UNESCO, UNICEF, ILO, VSO, GPE, Good Neighbours, Table for Two na Patnership for Child Development. Shukurani zetu za dhati ziende kwa Benki ya Dunia, Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika, Benki ya Maendeleo ya Afrika na Mfuko wa OPEC. Napenda pia, kuyashukuru mashirika yasio ya kiserikali yakiwemo Milele Zanzibar Foundation, Jumuiya ya Madrasa Early Childhood Education, NFU, FAWE, Save the Children Fund, Book Aid International na ZAPDD. Vile Vile napenda kuyashukuru makampuni na mashirika mbalimbali ya kifedha ya kiwemo ZTE, Benki ya watu wa Zanzibar, CRDB, Barclays, NBC, NMB, Postal Bank Tanzania, ZANTEL, kampuni ya SHA na ndugu Bakhresa. Aidha, napenda pia kuzishukuru Kampuni ya Bopar Interprise, SACCOSS mbalimbali na kampuni Tigo kwa misaada yao katika sekta yetu ya elimu na kwa wafanyakazi kwa ujumla. Shukurani za pekee ziendekwa Kamati zetu za Skuli na Halmashauri zetu za Wilaya kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kusimamia maendeleo ya elimu Zanzibar.

104.       Mheshimiwa Spika, Shukurani za pekee Chama change cha Mapinduzi kuanzia taifa hadi shina. Niushukuru uongozi mzima wa Mkoa wa Kaskazini Unguja na wananchi wenzangu wote hasa kina mama kwa kuendelea kuniamini na kushirikiana nami katika kuendelea kusimamia maendeleo kwa taifa letu.

105.       Mheshimiwa Spika, shukurani kwa familia yangu kwa ushirikiano wanaonipatia.

106.       Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa viongozi wenzangu kuanzia wewe Mheshimiwa Spika na Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kwa ushirikiano mkubwa walionipa na kwa namna watakavyoichangia hotuba yangu hii. Nasema ahsanteni sana.

107.       Mheshimiwa Spika, sasa naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe makadirio ya matumizi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya jumla ya TSh. 138,145,584,000/= kwa mwaka wa fedha 2020/21, ili kuiwezesha Wizara yangu kutekeleza majukumu yake.

  
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

KIAMBATISHO

(Takwimu za Maendeleo ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
       Kwa Kipindi cha 2015/16- 2019/20 na Hali Halisi ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa Mwaka 2019/20)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.