Habari za Punde

HOTUBA YA KAMATI YA BAJETI KUHUSU MAJUMUISHO YA MIJADALA YA BAJETI ZA WIZARA ZA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR KWA MWAKA 2020/2021



UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Kwanza kabisa naanza Hotuba hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu aliyetujaalia afya njema na uzima tukaweza kukutana tena katika Baraza lako na kuendelea kuwatumikia wananchi wetu ambao wametuamini na kutupa dhamana kubwa ya kuwasemea na kutetea hoja zao mbali mbali kupitia chombo hichi. Aidha, nachukua fursa hii kumpongeza Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein pamoja na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa uongozi wao imara uliopelekea kudumu kwa amani na utulivu katika nchi yetu. Kutokana na juhudi za viongozi wetu hawa pamoja na wasaidizi wao tumeshuhudia maendeleo makubwa katika nyaja za kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Mheshimiwa Spika, natoa shukrani zangu za dhati kwako kwa namna unavyotuongoza katika Baraza letu katika kipindi chote tulichotumikia pamoja na wasaidizi wako akiwemo Naibu Spika na Wenyeviti wa Baraza. Aidha, nawashukuru watendaji wa Baraza hili tukufu wakiongozwa na Katibu wa Baraza Ndg. Raya Issa Msellem.
Mheshimiwa Spika, nikiri kuwa, kukamilika kwa hotuba hii kumetokana na ushirikiano mkubwa ambao nimeupata kutoka kwa wajumbe wa Kamati katika kuibua hoja mbali mbali zilizojadiliwa katika kikao cha majumuisho. Kwa kweli wamefanya kazi hii kwa ufanisi mkubwa na napenda kuwatambua kwa kuwataja majina yao kama ifuatavyo:
1.    Mhe. Dkt. Mohamed Said Mohamed                                     Mwenyekiti
2.    Mhe. Bahati  Khamis Kombo                                                M/Mwenyekiti
3.    Mhe. Abdalla  Ali Kombo                                                      Mjumbe
4.    Mhe Ali Salum Haji                                                               Mjumbe
5.    Mhe. Asha  Abdalla Mussa                                                      Mjumbe
6.    Mhe. Mohammedraza Hassanali                                           Mjumbe
7.    Mhe. Salha Mohamed Mwinjuma                                          Mjumbe
Mheshimiwa Spika, Kamati katika kutekeleza na kufanikisha majukumu yake imekuwa ikisaidiwa na Sekretarieti iliyoundwa na makatibu watatu ambao ni:-
1.   Ndg. Abdalla Ali Shauri                                                        Katibu
2.  Ndg. Shaib Fadhil Shaib                                                        Katibu na
   3.  Ndg. Asha Said Mohamed                                                    Katibu

Mheshimiwa Spika, Kanuni ya 100(2) ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi (Toleo la 2016), inaitaka Kamati ya Bajeti kufanya majumuisho kuhusu mijadala ya Bajeti za Wizara zote. Kwa kuzingatia Kanuni hii na kwa ruhusa yako naomba kuwasilisha hotuba ya Kamati ya Bajeti kuhusu Majumuisho ya Mijadala ya Bajeti za Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

Mheshimiwa Spika, Kutokana na mijadala ya bajeti ilivyokwenda, Kamati ilikaa na baadhi ya Wizara ambazo hoja zao zilihitaji kujadiliwa katika kikao cha majumuisho. Kuna baadhi ya Wizara mijadala yake yote ilihitimishwa ndani ya baraza na hivyo kutokuwa na haja ya kujadiliwa tena hoja zao katika kikao cha majumuisho.
Mheshimiwa Spika, Mbali na hoja zilizoibuka katika majadiliano ya Bajeti za Wizara ambazo zimewasilishwa katika taarifa hii, kuna maeneo ambayo yalijadiliwa sana na wajumbe na ambayo kutokana na umuhimu wake Kamati yangu imeona ni busara kuyatolea ushauri. Miongoni mwa maeneo hayo ni pamoja na uimarishaji miundombinu ya barabara. Kwa vipindi tofauti, wajumbe wamekuwa wakichangia suala la ubovu wa barabara za ndani katika majimbo yao. Pamoja na jitihada kubwa inayochukuliwa na Serikali katika kuendeleza ujenzi wa barabara, bado kuna baadhi ya barabara za ndani ambazo ni mbovu na nyengine zipo katika maeneo ya utalii ambayo ni Sekta tunayoitegemea sana katika uchumi wetu. Kamati inaishauri Serikali kusimamia marekebisho ya barabara za ndani  hususan zile ambazo zipo katika maeneo ya utalii ili kuyafanya maeneo hayo yawe mazuri na kuvutia wawekezaji.
Mheshimiwa Spika, Eneo jengine ambalo Kamati yangu imeona ni busara kulisisitiza ni kuchelewa kutumika kwa baadhi ya fedha za Programu za Miradi, hali ambayo inapelekea fedha hizo kuombwa tena katika bajeti za mbele kama ambavyo imejitokeza kwa Bajeti ya Wizara ya Vijana katika Programu ya Kuendeleza Ajira kwa Vijana. Mheshimiwa Spika, Kamati inaendelea kusisistiza kuwa ni muhimu sana kujipanga vizuri katika kuendesha miradi ya maendeleo, kwani haileti taswira nzuri kwa bajeti ya mwaka wa nyuma kuitumia miaka ya mbele. Hali hii sio tu inaathiri ufanisi wa miradi lakini pia inatoa taswira ya uwezo mdogo wa Wizara katika kutumia fedha wanazoidhinishiwa.

MAENEO YALIYOCHANGIWA NA WAJUMBE WENGI

Mheshimiwa Spika, baadhi ya maeneo yaliyochangiwa na Wajumbe wengi na kwa hisia zaidi ni pamoja na haya yafuatayo:
·       Pongezi kwa Mhe. Rais wa Zanzibar kwa maendeleo makubwa yaliyofikiwa na kuridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
  • Kuzifanyia matengenezo barabara katika maeneo mbali mbali pamoja na kuzikarabati sehemu zilizoharibika kutokana na mvua.
  • Changamoto ya migogoro ya ardhi.
  • Ajira za waalimu ambapo wajumbe wengi walichangia kuhusu umuhimu wa kuajiriwa waalimu hasa wale waliokuwa hawajaajiriwa siku nyingi.
  • Umuhimu wa kuimarisha Sekta ya Uvuvi, Wajumbe wameishauri Serikali iimarishe Sekta ya Uvuvi ili isaidiane na sekta nyengine hususan wakati sekta nyengine zinapoyumba.
  • Umuhimu wa kuondolewa vikwazo vya biashara baina ya Zanzibar na Tanzania bara.
  • Changamoto za Mradi wa Pilipili.
  • Ufanisi wa Mradi wa Ujenzi wa Viwanja vya Michezo vya Wilaya.
·       Umuhimu wa kuzitafutia ufumbuzi changamoto za ubora wa majengo ya mahkama ikiwemo majengo ya Mahkama za Wilaya na Mikoa.
·       Ofisi ya Mufti kupatiwa fungu la kibajeti (vote) ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
·       Utaratibu wa kisheria unaotumika katika kuitishwa zabuni (tender).
·       Upatikanaji wa kampuni ambayo inafanya ukaguzi katika Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
·       Kusimamiwa vyema wamiliki wa vyombo vya baharini pamoja na kuepuka kupanda kwa bei za tiketi bila ya utaratibu maalum.
·       Umuhimu wa kuratibiwa vyema usafiri wa boda boda na kutatua changamoto za ajali zinazotokana na usafiri huo.
·       Kuimarishwa kwa utunzaji wa kumbukumbu za mahkama katika mfumo wa kielektroniki na mfumo wa kawaida.

UFAFANUZI WA HOJA ZILIZOTOKANA NA MAJADILIANO YA MAJUMUISHO YA MIJADALA YA BAJETI BAINA YA SERIKALI NA KAMATI YA BAJETI
Mheshimiwa Spika, Kikao cha majumuisho kilijadili jumla ya hoja nane (8) kutoka katika Wizara (5) ambazo hazikupata ufafanuzi wa kina wakati wa mijadala ya upitishaji wa Bajeti za Wizara. Hoja hizo, zimetoka katika mafungu tofauti katika bajeti za Wizara zikiwemo hoja zinazohusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hoja za kutaka ufafanuzi wa baadhi ya mafungu ya bajeti ambayo hayakufafanuliwa kwa kina na hoja za ulipaji fidia kwa wananchi ambao wameathirika na ujenzi wa barabara.

Mheshimiwa Spika, ili kutowa urahisi wa ufafanuzi wa hoja zilizofanyiwa kazi na Kamati, Kamati yangu inaomba iwasilishe hoja hizo kwa njia ya Jadweli (Table) ambalo limegawika sehemu tatu; Sehemu ya Kwanza inahusu Hoja zilizoibuliwa, Sehemu ya Pili inahusu, Majibu ya Wizara na Sehemu ya Tatu ni Ushauri wa Kamati ya Bajeti.




Nam.
HOJA
MAJIBU YA WIZARA
MAONI YA KAMATI

Wizara ya Biashara na Viwanda
1
Hoja ya kwanza ilikua inahusu  Mradi wa Pilipili, ambapo kutokana na changamoto zinazoukabili mradi huo, Serikali iliamua Mradi huo usimamiwe na Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi pamoja na Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC). Aidha, fedha zilizobakia za Mradi huo Tsh 376,462,104 ziliamuliwa kurejeshwa Wizara ya Vijana. Baadhi ya Wajumbe waliochangia walitaka  kupatiwa  ufafanuzi kama ifutavyo:-
a.   Jee  fedha hizo tayari zimesharejeshwa Wizara ya Vijana?
b.    Iwapo fedha hizo tayari zimesharejeshwa kwanini hazikuonyeshwa katika Bajeti ya Wizara ya Vijana?
c.   Iwapo fedha hizo bado hazijarejeshwa Wizara ya Vijana, lini zinatarajiwa kurejeshwa   na zitatumika kwa bajeti ya mwaka gani?
Fedha za Mradi wa Pilipili ambazo ziliamuliwa kurejeshwa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo bado hazijarejeshwa kwakuwa ni muda mfupi tokea kutolewa maamuzi ya mradi huo kurejeshwa Wizara ya Vijana. Hatua inayoendelea sasa ni kufanya uchambuzi wa mapendekezo yaliyotolewa.  Kwa hiyo, fedha hizo hazikuonekana katika Bajeti za Wizara zote mbili kwa sababu ni fedha zinazotokana na bajeti ya mwaka 2018/2019. Aidha, kwakuwa fedha hizo, zina ahadi “Commitment” ya Serikali zitaingizwa katika Bajeti ya Wizara ya Vijana mara baada ya taratibu za uchambuzi kukamilika.
Kimsingi Kamati imeridhika na majibu ya Serikali. Hasa kwa kuzingatia kuwa msingi wa pendekezo hilo ni Wajumbe wa Baraza na Kamati husika ya Kisekta. Kamati inaendelea kusisitiza kuwa mara baada ya kukamilika kwa taratibu za uchambuzi fedha hizo ziingizwe na zitumike kwa mujibu wa malengo. Aidha, Wizara ihakikishe inasimamia vyema Mradi huo ili uwe na tija na malengo ya kuwasaidia vijana yaweze kufikiwa kwa kuzingatia maoni ya wataalamu.

Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo
1
Hoja ya pili inahusu matumizi ya fedha za Programu ya kuendeleza vijana  ambapo, kwa mujibu wa Hotuba ya Mhe. Waziri wa Vijana, Utamaduni Sanaa na Michezo, Mnamo mwezi wa Julai 2019/2020, Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo  iliingiziwa jumla ya shilingi 2,000,000,000/= kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali, fedha ambazo zinatokana na bajeti ya mwaka 2018/2019,  fedha hizo zote zimetumika kwa shughuli mbali mbali za kuendeleza vijana. Aidha, kwa bajeti ya  mwaka 2019/2020 Programu hii pia ilipangiwa tena Tsh 2,000,000,000. Kamati iliomba kupatiwe ufafanuzi ufuatao?
Kwakuwa fedha za bajeti ya mwaka 2018/2019 zimetumika katika mwaka wa fedha 2019/2020. Jee fedha za bajeti ya 2019/2020 zimepatikana ngapi na zimetumika vipi. Hasa ikizingatiwa kuwa fedha hizo hazikuonyeshwa matumizi yake katika bajeti ya 2020/2021.
Ni kweli fedha za bajeti ya mwaka 2019/2020 bado hazijatumika kutokana na kuchelewa kukamilika taratibu. Hata hivyo, mikataba ya fedha hizo tayari imeshakamilika na tayari zimeshaombwa na pia zina ahadi ya Serikali “Commitment”. Hivyo, fedha hizo zitapatikana na zitatumika kama ilivyopangwa.
Kamati imeridhika na maelezo ya Wizara kwa msingi kwamba, fedha hizo zina ahadi ya Serikali “Commitment” na pia mikataba ya matumizi yake imeshakamilika. Aidha, ili kujiridhisha na ukweli huo Kamati imeiagiza Wizara kuwasilisha nakala za mikataba hiyo kabla mjadala wa Bajeti kuu kuanza. Kamati inaendelea kusisitiza wajibu wa Taasisi za Serikali kufanya matumizi ya fedha kama zinavyoidhinishwa na kwa wakati.

Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto
1
Programu ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (PQ 0101) ilikadiriwa kutumia jumla ya TZS 1,849,399,000 kwa mwaka wa fedha 2019/2020. Aidha, katika Hotuba ya Wizara, umetolewa uchanganuzi wa matumizi wa fedha hizo kama ifuatavyo:
Jumla ya TZS 789,348,000 zimetumika kwa kutoa mikopo 811 Unguja na Pemba. Jumla ya TZS 872,818,764 zilipatikana. Kwa kuangalia kiasi cha fedha kilichopatikana na kilichotumika, kunaonekana kuna tofauti ya TZS 83,470,764 milioni. Kamati ilihoji kwa nini ufafanuzi wa matumizi ya fedha uliotolewa, haulingani na makadirio ya programu ya uwezeshaji Wananchi kiuchumi (PQ0101).
Wizara ilieleza kuwa, ni kweli Programu Kuu ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (PQ0101) ilikadiriwa kutumia jumla ya TZS 1,849,399,000 kwa mwaka wa fedha 2019/2020. Fedha hizo ziliidhinishwa kwa ajili ya matumizi mengineyo na Mishahara kwa Programu ndogo 3 ambazo ni Programu Ndogo ya Mfuko wa Uwezeshaji, Programu Ndogo ya Usimamizi na Uimarishaji wa Vyama vya Ushirika na Programu Ndogo ya Uratibu na Uendelezaji wa Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. TZS 789,348,000 ni fedha ambazo zilitumika kwa utolewaji wa mikopo na hazihusiani na fedha zilizoidhinishwa katika Kitabu cha Makadirio ya Bajeti. Programu Ndogo ya Mfuko wa Uwezeshaji kwa mwaka wa fedha 2019/2020 iliidhinishiwa jumla ya TZS 269,470,080 na kufanikiwa kupata TZS 168,793,576. Uchambuzi wa matumizi ya fedha hizo unapatikana katika Kiambatanisho Nambari 1 cha Kitabu cha Hotuba ya Waziri.
Kamati imeridhika baada ya kupatiwa ufafanuzi wa kuridhisha.

Wizara ya Katiba na Sheria

Hoja ya nyengine iliyoibuka ni matumizi yaliyopangwa katika Programu ya Uendeshaji na Uratibu wa Wizara ya Katiba na Sheria kifungu SG100302 ya Jumla ya TZS 2,344,079,000 kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021. Wakati wa mjadala wa Wizara hii, matumizi hayo hayakutolewa ufafanuzi wa kina.
Idara ya Mipango Sera na Utafiti ilipanga jumla ya Tsh 2,344,079,000 kwa ajili ya shughuli kuu 3 kwa mchanganuo ufuatao:
 i.     Mradi wa Ujenzi wa Skuli ya Sheria  Tsh 1,500,000,000
ii.     Ruzuku Skuli ya Sheria Tsh 520,000,000
iii.     Matumizi ya Kawaida Tsh 324,079,320
Jumla Tsh 2,344,079,000
Kamati iliridhika na uchanganuzi uliotolewa







Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji
1
Katika mjadala wa bajeti ya 2020/2021, Mheshimiwa Mjumbe alitoa hoja katika Kifungu P010103 kuhusu Miundombinu ya Usafirishaji. Mjumbe hakuridhika na majibu ya Mhe. Waziri kuhusiana na ulipaji wa fidia kwa wananchi walioathirika na utengenezaji wa barabara ya Wete – Gando. Mheshimiwa Mjumbe alisisitiza kwamba, mbali na wale ambao waliothirika wakati ujenzi ukiendelea lakini hata wale ambao nyumba zao zimebomolewa kwa ajili ya kupisha ujenzi bado hawajalipwa. Ametoa mfano, Bwana Hamad Iddi Hamad ambaye Mheshimiwa Mjumbe alishuhudia kwa macho yake nyumba inatiwa grader, na mpaka sasa hajalipwa fidia yake. Hoja ya Mjumbe hapa ambayo bado Wizara haijaijibu ni kuelezwa lini wananchi hawa watapatiwa fidia zao ukizingatia kwamba tathmini zimeshafanyika. Aidha katika hoja hii, Mheshimiwa Spika aliitaka Serikali ilipe fidia kwa thamani ya sasa kwani ni muda mrefu umepita.
Wizara imekiri kuwepo kwa tatizo la malalamiko ya ulipaji fidia kwa wananchi waliothirika na utengenezaji wa barabara ya Wete – Gando licha ya kwamba Serikali imeshatoa fedha zote kwa ajili ya malipo ya fidia za nyumba zilizobomolewa wakati wa ujenzi wa barabara hiyo. Kinachodaiwa kwa sasa ni fidia za vipando tu.
Kamati imegundua kwamba, kuna matatizo katika ulipaji fidia, kuna uwezekano mkubwa wahusika hawakupata fidia zao licha ya Serikali kutoa fedha za fidia hizo. Hali hii imesababishwa na watendaji wasio waaminifu pamoja na kutofuata taratibu za malipo kwa usahihi. Mfano, kumejitokeza kasoro ya baadhi ya watu kusainiwa na watu wengine wakati wa kuchukua malipo. Kutokana na hivyo, Kamati inaishauri Wizara, ifanye uhakiki wa malipo ya fidia yaliyofanyika je waliolipwa ndio waliostahiki. Pia, iwapo Wizara itabaini kama kuna watendaji wameshiriki katika vitendo vya kuwadhulumu wananchi fidia zao, iwachukulie hatua za kisheria haraka iwezekavyo. Ni matumaini ya Kamati kwamba, jambo hili litamalizwa kwa haki ili kila mwenye haki apate haki yake na kuepusha malalamiko na masononeko ya mara kwa mara.
2
Katika barabara ya  Ole - Kengeja kuna wananchi ambao bado hawajalipwa fidia zao licha ya kwamba wameshafanyiwa tathmini ya kulipwa lakini mpaka leo hii hawajalipwa. Mheshimiwa Mjumbe alipokuwa anajenga hoja yake alisema kwamba, Mhe. Rais wa Zanzibar aliwahi kutamka kwamba atakapoondoka atahakikisha kwamba kwa kila alichokianzisha kisiwe na doa, anahitaji asiache madeni. Jee fedha hizi lini zitapatikana?
Wizara imeahidi kulifanyia kazi suala hili.
Kama ilivyo katika hoja ya ulipaji fidia kwa walioathirika na ujenzi wa barabara ya Wete – Gando, Kamati inaishauri Wizara kufanya uhakiki na tathmini na iwapo kama itabaini kwamba kuna wananchi bado wanadai fidia zao, basi taratibu za kuwalipa zitekelezwe haraka. Na ikibainika kwamba, malamiko haya yamejitokeza kutokana na watendaji wasio waaminifu, basi wachukuliwe hatua za kisheria haraka sana. Tusiwe na muhali katika haki za wananchi wetu.

HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Kamati kwa vipindi tofauti ambavyo ilifanya vikao vya majumuisho baina yake na Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imefarijika kwa hatua mbali mbali za utekelezaji ambazo Serikali imechukuwa. Kwa kweli hatua hizo zimesaidia sana katika kufikia malengo ya utekelezaji wa bajeti zetu pamoja na kupata ufumbuzi wa mambo. Kwa kumalizia, Kamati inazishukuru sana Wizara zote ambazo zimeshirikiana na Kamati katika kufanikisha kazi zake mbali mbali. Aidha, kwa kuwa Kamati hii itakuwa ni mara yake ya mwisho kuwasilisha taarifa ya aina hii, ni matumaini yangu kuwa, wajumbe wengine wa Kamati ya Bajeti wataokuja katika Baraza lijalo wataendelea kusimamia na kuishauri Serikali katika kusimamia utekelezaji wa hoja mbali mbali za Bajeti zilizoibuliwa.
Mheshimiwa Spika, namalizia hotuba hii kwa kukushukuru wewe kwa kunipatia nafasi hii na pia nawashukuru Wajumbe wa Baraza lako kwa utulivu na usikivu wao kwa muda wote ambao niliwasilisha hotuba hii. Nawatakia kheri na mafanikio nyote na naomba kuwasilisha.
Ahsante,

Dkt. Mohamed Said Mohamed,
Mwenyekiti,
Kamati ya Bajeti,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.