Habari za Punde

HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN, WAKATI WA KULIVUNJA BARAZA LA TISA LA WAWAKILISHI, TAREHE 20 JUNI, 2020


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akihutubia Wajumbe wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar kabla ya kulivunja rasmin, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa mkutano wa Baraza Chukwani Jijini Zanzibar. 

Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid; Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar,

Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi; Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar,

Mheshimiwa Job Ndugai; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mheshimiwa Kassim Majaaliwa Majaaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mheshimiwa Omar Othman Makungu; Jaji Mkuu wa Zanzibar,

Mheshimiwa Mgeni Hassan Juma; Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi,

Waheshimiwa Wenyeviti wa Baraza la Wawakilishi,

Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,

Waheshimiwa Mabalozi Wadogo mlioko Zanzibar,

Wawakilishi wa Mashirika mbali mbali ya Kimataifa,

Makamanda wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Idara Maalum za SMZ,

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa,

Ndugu Wageni Waalikwa,

Mabibi na Mabwana


Assalam Aleikum

Mheshimiwa Spika,
Tuna wajibu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu Subhanahu Wataala, kwa kuendelea kutupa neema ya uhai na afya njema tukaweza kukutana katika hadhara hii tukiwa salama na kutuwezesha kuishuhudia siku hii muhimu katika historia ya Baraza hili.  Namuomba Mola wetu atuwezeshe kuutekeleza wajibu wetu huu wa kikatiba kwa ufanisi na aupe kheri na baraka mkusanyiko wetu huu.

Mheshimiwa Spika,
Nnakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kulihutubia Baraza hili  la tisa kabla ya kulivunja.  Kwa hivyo, kikao hiki cha leo kimeitishwa kwa ajili ya kutekeleza matakwa ya kikatiba kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa katika kifungu cha 91(2)(a) cha Katiba ya Zanzibar ya 1984.  Kadhalika, kikao hiki, ni utekelezaji wa kifungu cha 92(1) cha Katiba ya Zanzibar kuhusiana na uhai wa Baraza la Wawakilishi kuwa ni kipindi cha miaka mitano tangu ulipoitishwa mkutano wa kwanza na leo tarehe 20 Juni, 2020 ndio nalihutubia Baraza la tisa kwa mara ya mwisho kabla ya kulivunja, ili kupisha Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba, mwaka 2020.

Mheshimiwa Spika,
Kwa hakika nimeridhishwa sana na kazi nzuri iliyofanywa na Baraza hili la Tisa la Wawakilishi, kwa utekelezaji mzuri wa jukumu lenu hili la Kikatiba katika kipindi chote tangu pale nilipolizindua rasmi tarehe 5 Aprili, 2016.  Kwa nyakati mbali mbali kwenye hotuba zangu nimekuwa nikieleza wazi wazi kuridhishwa kwangu na kazi nzuri inayofanywa na Wajumbe na wafanyakazi wa Baraza hili.  Hivyo, basi, natoa shukurani zangu za dhati kwako Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kwa umahiri na uongozi wako bora na kazi kubwa uliyoifanya ya kuliongoza Baraza hili, kwa kipindi chote kuanzia tarehe 5 Aprili, mwaka 2016 hadi sasa.  Hapana shaka kwamba umeliongoza Baraza hili na kuziendesha shughuli zake zote kwa mafanikio makubwa, ingawa nnafahamu kwamba kazi hio haikuwa rahisi, kwani ilihitaji ujasiri, uvumilivu na hekima kubwa.  Kama nitaimithilisha kazi hio uliyoifanya na unahodha wa meli, basi meli hio umeifikisha bandarini na kufunga gati; salama usalimini. Nakupongeza kwa dhati na nasema hongera sana.

Mheshimiwa Spika,
Kadhalika, natoa shukurani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Mgeni Hassan Juma, Naibu Spika, Mheshimiwa Mwanaasha Khamis Juma na Mheshimiwa Shehe Hamad Mattar, Wenyeviti wa Baraza, Wenyeviti wote wa Kamati za Baraza na kwenu nyote Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, kwa namna tulivyoshirikiana na tulivyosaidiana, kwani bila ya kufanya jitihada hizo, tusingeweza kuyapata mafanikio tunayoyaelezea hivi leo.  Mmeyatekeleza vyema majukumu yenu kwa moyo wa kizalendo na kwa ari kubwa mlioionesha na bila ya juhudi zenu mafanikio haya tusingeyapata.  Wakati wote mmeweka mbele maslahi ya wananchi kwa kutambua kuwa tunawatumikia wao na sote na tunawajibika kwao.  Hapana shaka,  wananchi wameridhishwa na kazi mliyoifanya na wamejenga imani kwenu kwa kuwawakilisha vyema kwenye Baraza hili muhimu la kutunga sheria.   Nnakupongezeni kwa dhati kutokana na kazi nzuri mlioifanya ya kuijadili; kuichangia na baadae mkayakubali na kuyapitisha mapendekezo ya bajeti za Wizara mbali mbali za Serikali na hatimae bajeti ya Serikali (Makadirio ya Mapato na Matumizi) kwa mwaka wa Fedha 2020/2021; ambazo jumla ya TZS  Trilioni 1.579.2 zimeidhinishwa.  Hongereni sana.  Hiki ni kiwango cha historia ambacho Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haijapata kuleta katika Baraza hili la kutunga sheria.

Mheshimiwa Spika,
Nilipolizindua Baraza la Nane la Wawakilishi la Zanzibar hapo tarehe 11 Novemba, 2010, nilielezea mtazamo wangu uliotokana na misingi ya Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2010 na MKUZA II na nikaelezea kazi iliyokuwa mbele yetu.  Niliyataja majukumu na vipaumbele vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba katika sekta zote za maendeleo ya nchi yetu.  Niliahidi kuwatumikia wananchi wote wa Zanzibar bila ya woga wala ubaguzi wa aina yoyote na kwa kuzingatia misingi ya haki na utawala bora inayotokana na Katiba ya Zanzibar ya 1984 na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.

Nilipolihutubia Baraza la Wawakilishi hapo tarehe 26 Juni, 2015, kwa madhumuni ya kutoa tamko la kulivunja Baraza hilo hapo tarehe 13 Agosti, 2015; nilielezea kwa urefu mafanikio tuliyoyapata na changamoto tulizokabiliana nazo, katika kipindi cha miaka 5 ya mwanzo  ya uongozi wangu.
Mheshimiwa Spika,
Vile vile, kwa wale mliokuwepo katika Baraza hili, mtakumbuka kuwa katika hotuba yangu ya uzinduzi wa Baraza la Tisa la Wawakilishi, niliyoitoa tarehe 5 Aprili, 2016, nilielezea mwelekeo wa mipango ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kipindi cha pili cha uongozi wa Awamu ya Saba.  Kwa mara nyengine, natoa shukurani kwa Chama changu, Chama cha Mapinduzi, kwa kuniamini na kunipa heshima kubwa ya kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa vipindi vyote viwili.  Kadhalika, nawashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kunichagua kwa kura nyingi mimi na wagombea wengine wa Chama cha Mapinduzi na kutuwezesha kupata ushindi mkubwa.  Ushindi huo ulitupa uwezo wakikatiba wa kuiongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, ambayo imepata mafanikio makubwa katika nyanja zote za kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Katika muda wote wa uongozi na utendaji kazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba, tumekuwa tukiwashukuru na kuwapongeza viongozi wa Awamu zilizopita.  Katika uongozi wetu huo, tulizingatia namna ya kuyafikia matumaini na matarajio ya wananchi ya kuyaendeleza mafanikio yaliyotokana na utendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu zilizotangulia. Wakati wote tulizingatia malengo na misingi madhubuti ya Mapinduzi Matukufu ya tarehe 12 Januari, 1964 na utekelezaji wa Sera na Mipango mikuu ya maendeleo yenye lengo la kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa jamii.

Katika vipindi vyote viwili vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba, niliiongoza kwa kuzingatia utekelezaji wa Mipango Mikuu ya Kitaifa ambayo ni Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya Mwaka 2010 na 2015, Dira ya Maendeleo ya 2020, MKUZA Awamu ya Pili na ya Tatu na Malengo Endelevu ya Dunia.  Pamoja na mipango hio, vile vile tumezingatia utekelezaji wa ahadi nilizozitoa katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na 2015 pamoja na vipaumbele vyengine ambavyo Serikali iliona kuna haja ya kuvizingatia na kuvitekeleza kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,
Kwa hakika sote tumefanikiwa na tumeridhika na mafanikio makubwa tuliyoyapata katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya vipindi vyote viwili (2010 na 2015). Mafanikio hayo ni makubwa ya kupigiwa mfano tuliyoyapata ambayo yametokana na jitihada mbali mbali za pamoja zinazofanywa na Serikali, Mashirika na Taasisi mbali mbali za Kitaifa na Kimataifa, zinazotuunga mkono.  Vile vile, utendaji mzuri wa viongozi wa ngazi mbali mbali, kwenye jamii yetu, watumishi wa umma pamoja na wananchi waliovinjari kushirikiana na Serikali yao, nao wameongeza nguvu na ari ya mafanikio haya.  Ni dhahiri kuwa mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM, ambayo ni mkataba baina ya Serikali yetu na wananchi, yamezidi kukijengea heshima chama chetu na kimezidi kuaminika kwa wananchi.  Hivyo basi, nna matumaini makubwa kuwa katika Uchaguzi utakaofanyika baadae mwaka huu, bila ya shaka, wananchi wataendelea kukichagua Chama cha Mapinduzi na wagombea wake wote watakaowasimamisha, ili kiweze kuongoza Serikali na kuwaletea maendeleo zaidi.
  
Mheshimiwa Spika,
Tuliianza Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tukiwa tumebeba dhima ya matumaini makubwa ya Wazanzibari ya kuwaunganisha kama Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilivyoelekezwa na Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya Mwaka 2010, kwenye kifungu cha 171 (a-c); ukurasa wa 212-213 na kuhusu Ulinzi na Usalama katika kifungu cha 191 ukurasa 230-231.  Kwa hivyo, nilifahamu kwamba dhima tuliyoibeba; mbali ya kuwatumikia wananchi wa Zanzibar, kwa kuwatatulia shida zao na kero zao zitakazowakabili haitotosha bila ya kuendeleza na kuimarisha amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa miongoni mwa Wazanzibari na Watanzania kwa jumla.

Niliahidi na nilijidhatiti katika kipindi cha uongozi wangu kufanya kila nililoweza, ili kuendeleza amani, umoja na mshikamano, ili Wazanzibari tuendelee kuwa wamoja, tunaopendana, tunaoshirikiana na tunaosaidiana; bila ya ubaguzi wa aina yoyote au tafauti ziliopo baina yetu. Niliahidi kwa kusisitiza katika uongozi wangu wote kwamba Zanzibar itaendelea kuwa nchi ya amani, usalama na utulivu.  Leo nnapolihutubia Baraza hili, ili baadae tuagane, kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa, hapana shaka sote ni mashahidi kwamba nchi yetu iko salama, yenye amani na utulivu na bado tungali wamoja.  Kwa hakika haya ni mafanikio makubwa tuliyoyapata katika uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba, ingawa yalikuwepo baadhi ya matukio yaliyotishia kuudhoofisha umoja wetu na hata kutaka kuhatarisha amani ya nchi yetu, katika kipindi cha mwanzo na mwanzoni mwa kipindi cha pili cha Awamu ya Saba ya Serikali nnayoiongoza. 

Mheshimiwa Spika,
Katika vipindi vyote hivyo viwili, walikuwepo baadhi ya wananchi wenzetu waliojaribu kupandikiza chuki za kila aina na kuleta fadhaa na vurugu miongoni mwa ndugu na watu wamoja wanaopendana.  Vile vile, walikuwepo baadhi ya watu walioonesha dharau na kejeli kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ili wananchi waichukie, waibeze na waione Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar si Serikali yao.  Zaidi ya hayo, ziliandaliwa njama, hila na mazingira ambayo hayakupaswa yawepo, ili utokee mtafaruku.  Lakini kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu na mapenzi yake kwa Zanzibar, uwezo wa viongozi wa Serikali, Vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama, ari na imani ya wananchi kwa nchi yao, Mwenyezi Mungu ametujaalia hali ya amani, umoja,  mshikamano na utulivu, hadi hii leo kwa viwango vile vile tunavyovitarajia na Ishaallah, amani, umoja na utulivu vitaendelea kudumu hapa Zanzibar.

Kutokana na jitihada za viongozi wa Serikali, uongozi wao bora na msimamo wao wa dhati na kwa kushirikiana na viongozi wengine wa jamii, viongozi wa dini na wananchi wenyewe tumefanikiwa kupambana na changamoto zilizojitokeza na tukaweza kuzishinda kwa kuzingatia Katiba yetu na Sheria zilizowekwa.  Kadhalika, navipongeza vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Idara Maalum za SMZ, kwa kazi nzuri wanazozifanya za ulinzi wa nchi yetu. Hongereni sana.

Mheshimiwa Spika,
Nawashukuru viongozi wote pamoja na wananchi kwa kuiendeleza na kuiimarisha amani, umoja na mshikamano, kwa sababu haya ni mambo muhimu na ya lazima katika kuwaletea wananchi maendeleo.  Hapana mbadala wa mambo haya muhimu, kwa hivyo ni lazima wakati wote tuwe makini na tuchukue tahadhari dhidi ya wenye nia mbaya na Serikali yetu.

Mheshimiwa Spika,
Niliahidi kuisimamia amani, umoja na mshikamano, kuidumisha na kuiendeleza katika kipindi chote cha uongozi wangu; ikiwa ni misingi madhubuti ya maendeleo yetu. Serikali imeweza kuyatekeleza majukumu yake katika sekta zote, kutokana na ahadi nilizozitoa, nilipowaomba wananchi ridhaa yao ili wanichague, mimi na Chama changu Chama cha Mapinduzi pamoja na wagombea wenzangu wa CCM.

Mheshimiwa Spika,
Leo ni siku ya mwisho kwa Baraza la Tisa la Wawakilishi la Zanzibar, ambapo linamaliza uhai wake katika kufanya kazi zake.  Kwa hivyo, natumia fursa hii kuelezea majukumu ya Serikali ya Awamu ya Saba, namna yalivyotekelezwa.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, tangu ilipoingia madarakani tarehe 3 Novemba, mwaka 2010 hadi hivi sasa, imeendelea na juhudi za kuitekeleza mipango mbali mbali ya kiuchumi, ili kuhakikisha kwamba uchumi na ustawi wa wananchi wa Zanzibar unaimarika.  Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2010 kifungu cha 123 (a,b,c, na d) ukurasa wa 157-158 na Ilani ya mwaka 2015 kifungu cha 68 (a,b,c, na d) ukurasa wa 123-124 iliielekeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ijenge mazingira yatakayouwezesha uchumi wa Zanzibar ufikie kiwango cha uchumi wa nchi zenye kipato cha kati, mfumko wa bei ubaki katika tarakimu moja na wastani wa pato la kila mwananchi liongezeke. Vile vile, mapato yaendelee kudhibitiwa pamoja na nidhamu ya matumizi ya Serikali, kupunguza utegemezi kwa Wahisani wa Maendeleo, misamaha ya kodi isiyokuwa na tija na kuongezeka kwa kiwango cha ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2019, Pato la Taifa limeweza kukua kutoka thamani ya TZS Bilioni 1,768 mwaka 2010 hadi kufikia thamani ya TZS Bilioni 3,078 mwaka 2019.  Ongezeko hilo ni sawa na mara 1.74 zaidi ya wakati Awamu ya Saba inaingia madarakani.  Kasi ya ukuaji wa uchumi imeongezeka kutoka asilimia 4.3 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 7.0 mwaka 2019.  Vile vile, Pato la Mwananchi nalo limeongezeka kutoka TZS 942,000 sawa na USD 675 mwaka 2010, hadi kufikia TZS 2,549,000 sawa na USD 1,114 mwaka 2019.  Ongezeko hilo ni kubwa sana ambalo tumefikia sawa na asilimia 170.59.

Kadhalika, mfumko wa bei nao kasi yake imeshuka kutoka asilimia 14.7 mwaka 2011 hadi asilimia 2.9 mwaka 2019.  Kwa hakika hali hii imetoa faraja sana kwa wananchi kuweza kupata bidhaa muhimu kwa bei ya kuridhisha.   Hatua  ya kukua kwa uchumi imeiwezesha Serikali kupata ongezeko la mapato mwaka hadi mwaka.  Katika mwaka 2019/2020, mapato ya ndani yalifikia TZS Bilioni 748.9 ikilinganishwa na jumla ya TZS Bilioni 181.1 zilizokusanywa mwaka 2010/2011.  Kadhalika, hali ya utegemezi wa bajeti imepungua kutoka wastani wa asilimia 30.2 mwaka 2010/2011 na kufikia wastani wa asilimia 5.7 mwaka 2018/2019.  Hatua hio, imeiwezesha Serikali kutekeleza Mipango yake ya Maendeleo kwa kutumia fedha zake yenyewe za mapato inazokusanya, kwa kiasi kikubwa. Nazipongeza Taasisi zetu za kukusanya mapato; Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuweza kuyatekeleza kwa ufanisi majukumu yao na tukaweza kuyafikia mafanikio haya ya kuridhisha katika kipindi  cha uongozi wa Awamu ya Saba.

Mheshimiwa Spika,
Hivi sasa, tumedhamiria kuwekeza zaidi katika kuwejengea uwezo wafanyakazi, ili  tuwe na wataalamu wa kutosha katika sekta mbali za uchumi na kijamii, ikiwa ni pamoja na kuendeleza Uchumi wa Buluu ambao umejumisha  uvuvi, utalii, usafiri wa bahari, mafuta na gesi asilia, ufugaji wa mazao ya baharini.  Tumejidhatiti katika kuwawezesha    wajasiriamali na kukuza  Maendeleo ya viwanda kwa kushirikiana na sekta binafsi. Tutaongeza nguvu katika kuunganisha sekta ya utalii na sekta nyengine za uzalishaji, ili utalii uweze kuwa na manufaa zaidi.

Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi kilichofikia Disemba 2010, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliidhinisha miradi 648 yenye mtaji wa makisio wa TZS bilioni 5.9 na kutarajiwa kutoa ajira zipatazo 51,822 kwa wazalendo. Katika kipindi chote cha Awamu ya Saba, Serikali imefanya jitihada kubwa za kushajiisha na kuendeleza uwekezaji nchini. Idadi ya miradi iliyoidhinishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba kupitia Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), hadi kufikia Juni mwaka 2020, imefikia jumla ya miradi 749 yenye mtaji wa makisio wa TZS bilioni 6.7 na ajira kwa wazalendo zinazotarajiwa kupatikana ni 55,888.

Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi hiki, Serikali imetayarisha sera ya ardhi, ili kusimamia na kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi.  Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita tulikamilisha Mkakati wa Matumizi ya Ardhi Zanzibar (National Spatial Development Strategy - 2015).  Katika Mkakati huu, Miji Kumi na Nne (14) ilipangwa, ikiwemo Mji wa Zanzibar, Chake-Chake, Wete, Mkokotoni, Konde na Kengeja. Kati ya Miji hiyo, Serikali imekamilisha mipango ya miji mitano ambayo ni Mji wa Zanzibar, Nungwi, Mkokotoni, Chwaka na Makunduchi. Matayarisho ya mipango ya miji ya Chake-Chake na Wete imeshaanza.

Kadhalika, katika mwaka 2014, Serikali ilikamilisha Mpango Mkuu wa Mji wa Zanzibar.  Katika Mpango huo, Serikali imeamua kuanzisha eneo jipya la Biashara na Utamaduni.   Eneo lote kutoka Darajani hadi Kariakoo na kutoka Maisara hadi Kinazini litapangwa upya, ili kuanzisha ujenzi wa nyumba za ghorofa, kuweka kituo kipya cha mabasi, kuongeza sehemu mpya za maduka na biashara na kujenga sehemu mpya za bustani. Aidha, Mji wa Zanzibar utakuwa na miji mitatu mipya; Chuini kwa upande wa Kaskazini, Tunguu kwa upande wa Mashariki na Fumba kwa upande wa Kusini. Mipango hii inafanywa kuhakikisha kuwa Zanzibar inaendelea ikiwa na uwiyano wa kiuchumi, kijamii na kimazingira, ili kufikia lengo lake la Milenia na kuelekea katika Malengo Mapya ya Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goals).

Katika Awamu hii ya Saba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, iliandaa na kutekeleza miradi mbali mbali ya kimkakati ikiwemo kuanzisha Idara ya Mipango Miji na Vijiji mwaka 2013. Mpango Mkuu Mpya uliandaliwa wa kuliendeleza Jiji la Zanzibar (Zanzibar City) pamoja na miji yetu mingine iliyopo Zanzibar.  Uamuzi huo ulianzisha Mpango Mkuu wa Matumizi ya Ardhi kwa kuweka maeneo maalum ya makaazi, biashara na shughuli nyengine zikiwemo za kilimo na ufugaji.  Katika utekelezaji wa azma hio, kwa kushirikiana na Sekta Binafsi, Serikali ikahamasisha miradi ya ujenzi wa nyumba za kisasa za makaazi, biashara na za kutoa huduma nyengine mbali mbali.  Serikali ilifunga mkataba na Bakhresa “Group of Companies”, ili kujenga miundombinu katika Maeneo Huru ya Uchumi ya Fumba.  Jumla ya kilomita 12.7 za barabara zimejengwa, umeme umefikishwa na maji yamesambazwa. 

Hadi sasa jumla ya nyumba 200 zimejengwa pamoja na kiwanda cha maziwa na maeneo ya kupumzikia watu.  Vile vile Kampuni ya SS Bakhresa “Group of Companies” imekamilisha ujenzi wa Hoteli ya Verde huko Mtoni, iliyowekwa jiwe la msingi tarehe 3 Januari, 2017 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na ilifunguliwa rasmi tarehe 11 Januari, 2020 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.  Ujenzi huo pia ulijumuisha maeneo ya michezo ya maji (water park) na “Marina”.

Mradi wa Ujenzi wa Mji wa Kisasa wa Kibiashara pamoja na hoteli kubwa ya nyota tano ulioanza kutekelezwa na Kampuni ya “Pennyroyal” ya Gibralter kwa gharama ya USD Milioni 800, ulioanza katika mwaka 2013.  Ujenzi wa hoteli uko katika hatua ya maandalizi hadi leo.
Mradi mwengine wa nyumba za makaazi unaendelea kutekelezwa huko  Nyamanzi na Kampuni ya CPS, ambapo hadi mwaka huu wa 2020, jumla ya nyumba za makaazi 465 zimejengwa. Nyumba 169, miongoni mwao  zimeshamalizika na 120 zimeshakabidhiwa kwa wenyewe waliozinunua na naamini miongoni mwa Wajumbe wa Baraza hili mtakuwemo. Nakupongezeni sana. Hatua za ujenzi wa nyumba nyengine zinaendelea. Vile vile, Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) imekamilisha ujenzi wa majengo 15 ya  nyumba za kisasa za ghorofa 7 zenye jumla ya fleti 210 huko Mbweni, ambapo fleti 146 tayari zimeuzwa na zilizobakia zimo katika utaratibu wa kuuzwa.

Hivi sasa, Mfuko huo unaendelea na ujenzi wa majengo mawili yenye fleti 28 na kuanza ujenzi wa sehemu za michezo na biashara kwenye eneo hilo. Hivi sasa, Serikali inaendelea  na ujenzi wa nyumba za  kisasa kwa ajili ya wananchi katika eneo la Kwahani,  ambapo majengo 3 ya ghorofa sita  yenye fleti 70, yanaendelea kujengwa na Kampuni inayojenga itaikabidhi Serikali katika mwezi wa Septemba, 2020.  Hatua hii ya ujenzi ni  Awamu ya Kwanza, ambapo ujenzi huu utaendelea katika awamu mbali mbali hapo baadae, hadi nyumba zote zitakapokamilika kujengwa katika eneo hilo.

Kwa upande wa majengo ya biashara na kuimarisha haiba ya Jiji la Zanzibar, Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) inakamilisha mradi wa ujenzi wa majengo mawili ya kisasa katika eneo la Michenzani na itajenga jengo jengine kwa ajili ya maegesho ya gari (car park). 

Jengo la kwanza linalojulikana kwa jina la “Michenzani Shopping Mall” na jengo la pili la biashara ambalo limepewa jina la Marehemu “Sheikh Thabit Kombo Mall”,  ujenzi wake unatarajiwa kukamilika hivi karibuni. Hapana shaka majengo haya yatabadilisha kabisa haiba ya eneo la Michenzani na vile vile yataendeleza dhamira ya Mwasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari, 1964, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ya kuupa hadhi mtaa wa Michenzani na kuliendeleza Jiji la Zanzibar kwa kujenga majengo ya kisasa.

Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi hiki cha Awamu ya Saba, ilikamilisha ujenzi wa nyumba za fleti za Mpapa, ambapo jumla ya nyumba 24 zilikamilishwa na kupewa wananchi.   Pamoja na kuzifanyia matengenezo nyumba kadhaa za maendeleo za Mtemani Wete Pemba na Madungu Chake Chake Pemba kwani  nyumba hizo zilikuwa katika hali mbaya.  Kazi hii itaendelezwa na Shirika la Nyumba kwenye Miji mingine, hatua kwa hatua.

Pamoja na hatua hio, Serikali pia imelifanyia matengenezo makubwa jengo maarufu la “Chawl”, maarufu Jumba la Treni liliopo Darajani, lililojengwa mwaka 1880, ili kulipa haiba nzuri jengo hilo muhimu la biashara.  Sasa linaonekana vyengine na biashara zimepamba moto.

Mheshimiwa Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba, inaendelea kuimarisha mazingira ya biashara kwa kushirikiana na sekta binafsi. Licha ya kwamba hatujaweza kuuweka vyema uwiano na urari wa biashara, usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya Tanzania unaendelea kuimarika. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, jumla ya tani 2,937,198.4 za bidhaa zenye thamani ya TZS Bilioni 4,120.25 ziliingizwa nchini ikilinganishwa na bidhaa zenye thamani ya TZS Bilioni 769.85 zilizosafirishwa kwenda nje ya nchi. Jumla ya bidhaa zenye thamani ya TZS Bilioni 1,997.88 zilisafirishwa kwenda Tanzania Bara na bidhaa zenye thamani ya TZS Bilioni 1,245.62 ziliingizwa Zanzibar kutoka Tanzania Bara katika kipindi hicho.

Mheshimiwa Spika,
Kuhusu biashara ya karafuu, katika kipindi hiki cha miaka kumi, Serikali imenunua jumla ya tani 37,995.60 za karafuu, zenye thamani yaTZS Bilioni 511.27 kutoka kwa wakulima na kati ya hizo jumla ya tani 37,782.2 za karafuu zenye thamani ya TZS Bilioni 614.86, sawa na USD Milioni 324.37 ziliuzwa nje ya nchi. 

Kwa kipindi cha miaka tisa mfululizo, Serikali ilimlipa mkulima  kiwango cha asilimia 80 ya bei ya karafuu katika soko la dunia, ambayo ni sawa na TZS 14,000; kwa kilo moja ya karafuu kavu za daraja la kwanza. Vile vile, TZS 12,000 kwa kilo moja yya karafuu kavu za daraja la pili na TZS 10,000 kwa kilo moja ya karafuu za daraja la tatu. Mkakati hii imelenga katika kumnufaisha mkulima na kuhakikisha kwamba zao la karafuu linazidi kuimarishwa kwa hali yoyote. Vilevile, Serikali ilianzisha bima maalum kwa wachumaji wa karafuu wanaopata ajali na kuwazawadia wakulima bora. Hatua hizo ziliongezea wakulima ari na juhudi za kukiendeleza kilimo cha karafuu.

Mheshimiwa Spika,
Mpango Mkakati wa Miaka Kumi wa Kuliendeleza Zao la Karafuu umefanikiwa sana. Jumla ya miche milioni 3,465,034 imetolewa kwa wakulima katika kipindi hiki ambapo baadhi ya mikarafuu hio hivi sasa imeanza kuzaa. Aidha, jumla ya Vituo vipya 22 vya kisasa vya kununulia karafuu vilijengwa huko Pemba. Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC), lilifanyiwa mageuzi makubwa, ili lijiendeshe kibiashara.

Kwa hakika, nawashukuru wakulima wa karafuu wa Unguja na Pemba kwa kuziuza karafuu zao katika vituo vya ZSTC. Kadhalika, nawapongeza wananchi, ZSTC, Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi na Idara Maalum za SMZ kwa kuliendeleza na kuliokoa zao la karafuu kiwa ni pamoja na kupambana na magendo ya karafuu na kuyadhibiti.

Sheria ya Viwango Namba 1 ya mwaka 2011 ililenga kuimarisha sekta ya biashara na viwanda kwa Zanzibar na Sheria ya Ushindani Halali wa Biashara na Kumlinda Mtumiaji Namba 5 ya 2018 zimeanza kutekelezwa kwa mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Spika,
Sekta ya Viwanda imeendelea kutoa mchango mkubwa katika kipindi hiki cha Awamu ya Saba. Mchango wa Sekta hio katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 8.2 mwaka 2013 hadi 17.8 mwaka 2018.  Katika kuimarisha Soko la Ajira, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, imeandaa mipango mbali mbali yenye lengo la kukuza sekta ya viwanda. Utengenezaji wa bidhaa katika baadhi ya viwanda vilivyokuwapo awali na vyengine viliyoanzishwa katika miaka ya karibuni umezidi kuimarika. Jumla ya viwanda 340 vilianzishwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Mheshimiwa Spika,
Serikali imeanzisha Wakala wa Maendeleo ya Viwanda Vidogo Vidogo na vya Kati (Small and Medium Industries Development Agency - SMIDA) kwa mujibu wa sheria Namba 2 ya mwaka 2018.  Wananchi waliojiajiri wenyewe katika sekta hii hadi mwishoni mwa 2018 wamefikia watu 180,851. Nawapongeza wawekezaji wote waliowekeza katika sekta ya viwanda, kwa kuitikia wito wa Serikali na kuimarisha maendeleo ya sekta hii. 

Serikali imeendelea kushirikiana na Sekta Binafsi katika kuimarisha sekta ya viwanda na biashara pamoja na kwa kuyafanyia kazi mapendekezo yanayotolewa na Baraza la Biashara la Zanzibar (ZNBC), katika mikutano ya kila mwaka tunayoifanya pamoja na kuendeleza Tamasha la biashara.

Mheshimiwa Spika,
Serikali ya Awamu ya Saba iliahidi kuwa itauimarisha utalii, ili uwe ni kichocheo cha maendeleo ya sekta ya biashara, usafirishaji na uchukuzi wa barabara, baharí na anga na kuujenga utalii wenye kuheshimu mila zetu, desturi na utamaduni wa Mzanzibari.

Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi hiki cha miaka kumi Serikali imetekeleza kwa mafanikio makubwa Mpango wa Utalii kwa Wote (Tourism for All) tulioutangaza rasmi tarehe 16 Oktoba, 2011 katika ukumbi wa Salama, Bwawani.  Tumefanya jitihada kubwa za kuitangaza Zanzibar katika masoko mapya ya Bara la Asia na Ulaya na jitihada zetu za kushajiisha uwekezaji na ujenzi wa hoteli kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya utalii zilifanikiwa sana. 

Hadi kufikia mwezi Novemba, 2019, Zanzibar ilikuwa na hoteli zilizosajiliwa na kutoa huduma zipatazo 509 za madaraja mbali mbali, ambapo 26 kati yao ni za nyota 5 na 20 ni za nyota 4 na nyengine ni za daraja mbali mbali.  Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watalii walioitembelea Zanzibar imeongezeka kutoka 133,000 katika mwaka 2010 hadi kufikia 538,264 mwaka 2019, ikiwa ni sawa na ongezeko la mara 4 katika miaka kumi iliyopita.  Mipango mbali mbali imeandaliwa ya kuongeza idadi ya watalii watakaoitembelea Zanzibar katika siku zijazo. Serikali imechukua hatua madhubuti kuhusu ulinzi na usalama kwa watalii kwenye maeneo mbali mbali wanayotembelea na kwenye hoteli wanazoishi.

Mheshimiwa Spika,
Serikali imeziimarisha huduma za makumbusho na mambo ya kale kwa  kuipa umuhimu unaostahiki historia ya Zanzibar na kuimarisha utalii.  Majengo ya kihistoria yakiwemo magofu na majengo ya makumbusho na mapango mbali mbali ya kihistoria yaliopo katika Mikoa yote ya Unguja na Pemba yameanza kufanyiwa matengenezo makubwa.  Majengo ya historia ya Bungi Miembe Mingi; kwa Bi. Khole, Fukuchani, Kaskazini na mingine yameanza kufanyiwa ukarabati na tayari yanatembelewa na watalii.

Katika kipindi hiki jumla ya wageni 24,863 waliyatembelea maeneo yetu ya historia kwa mwaka 2019, ikilinganishwa na wageni 13,251 waliotembelea mwaka 2010.

Mheshimiwa Spika,
Natoa wito kwa wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla waendelee  kuyahifadhi maeneo ya historia na mambo ya kale, ambayo ni  muhimu kwa utamaduni wetu na ni hazina muhimu kwa historia na nnawahimiza  wayatembelee maeneo yetu ya  historia, kwa lengo la kuuimarisha  utalii wa ndani.

Mheshimiwa Spika,
Kwa lengo la kukuza uchumi, kupata lishe bora na kuwa na usalama wa chakula nchini, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha kilimo cha mazao mbali mbali. Katika kipindi hiki Serikali imeendelea kuimarisha kilimo cha mpunga kwa kutoa ruzuku kwa wakulima ya asilimia 75 ya pembejeo za kilimo pamoja na huduma za matrekta wao wenyewe wanatoa 25% tu. Teknolojia ya kisasa ya kilimo cha mpunga shadidi ilitumika kupitia Mradi wa Kuongeza Uzalishaji na Tija (ERPP), na imechangia kuongezeka mavuno ya zao la mpunga.

Jitihada hizo zimepelekea kuongezeka kwa mavuno ya mpunga kutoka tani 21,014 mwaka 2010 hadi tani 47,507 mwaka 2019. Mazao mengine ya chakula, matunda na mboga nayo yaliongezeka kutoka tani 289,481 mwaka 2010 hadi kufikia tani 404,285 mwaka 2019, sawa na ongezeko la asilimia 30.  Mafanikio hayo, yameiwezesha Zanzibar kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 60 mwaka 2018, kutoka asilimia 51 mwaka 2011. 

Mheshimiwa Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetekeleza Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, kifungu 72(c) kwa kuanzisha ujenzi wa miundombinu ya  umwagiliaji maji katika hekta 2,200 za mabonde ya Cheju, Kibokwa, Kilombero kwa Unguja na Mlemele pamoja na Makwararani kwa Pemba, ili kuimarisha na kukiendeleza kilimo cha mpunga. Mradi huo ulizinduliwa tarehe 2 Januari, 2020 huko Kisongoni na umegharimu USD Milioni 50, ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Exim ya Jamhuri ya Korea na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechangia USD Milioni 14.  Kadhalika, hivi sasa, Serikali imeanza kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo ya Zanzibar (ASDP) wa miaka kumi, unaogharimu USD Milioni 148 kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo.

Mheshimiwa Spika,
Jambo moja la kufurahisha sana ambalo limefanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kupandisha hadhi Kituo cha Utafiti wa Kilimo Kizimbani kuwa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Zanzibar, kwa mujibu wa Sheria Namba 8 ya mwaka 2012. Kituo hiki kina historia kubwa kwani ni kituo cha kwanza kabisa Afrika Mashariki kilichoanzishwa katika miaka ya 30.  Watu walikuja kujifunza kilimo hapa Zanzibar miaka hio.  Tafiti mbali mbali za mbegu za mazao ya chakula, biashara, mboga na matunda zimefanywa katika Taasisi hio na matokeo yake yanatumika kwa kukiendeleza kilimo. 

Mheshimiwa Spika,
Vile vile, Serikali imeanzisha maonesho ya kilimo, uvuvi na ufugaji kila mwaka, tangu mwaka 2018. Maonesha hayo yanafanyika huko Chamanangwe kwa Pemba na Langoni kwa Unguja. Kadhalika, Serikali imenunua matrekta mapya 30 kutoka katika Kampuni ya Mahindra Mahindra ya India, ambapo matrekta 20 yameshawasili nchini na mengine kumi yako njiani yataletwa. Katika jitihada za kukiendeleza Kituo chetu cha  Matrekta cha asili kule Mbweni, Serikali imeanzisha Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo kwa mujibu wa Sheria Namba 2 ya mwaka 2019; kwa ajili ya kuyahudumia matrekta na zana zote za kilimo hapa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,
Katika mwaka 2017, Serikali ilianzisha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo kwa mujibu wa sheria Namba 7 ya mwaka 2020, inayoshughulikia na kuzipatia ufumbuzi changamoto za wafugaji.  Vituo vya huduma za mifugo Unguja na Pemba, vimeimarishwa, ili viweze kutoa huduma kwa ufanisi. Jumla ya ng’ombe 110 aina ya Fresian na Jersey Unguja na Pemba, wamepandishwa kwa njia ya sindano, ambayo ni sawa na asilimia 200 ya lengo. Kadhalika, jumla ya vijana 224 wamepatiwa mafunzo ya kinga na tiba na huduma za ugani, ili kuendeleza shughuli za ufugaji kwa ufanisi.   Vile vile,  vikundi mbali mbali vya  ufugaji  vimeanzishwa na vimepewa  ng’ombe wa maziwa bure 368 na  mbuzi wa maziwa 720, ili waendeleze ufugaji.

Mheshimiwa Spika,
Katika Kuendeleza Sekta ya Uvuvi, Serikali ilianzisha upya kampuni ya Uvuvi (ZAFICO).  Kampuni hio tayari imenunua boti ya kisasa ya uvuvi iitwayo Sehewa II ambayo ilizinduliwa tarehe 2 Disemba, 2019. Boti hio tayari imeanza kazi kwa ajili ya uvuvi wa Bahari Kuu na imetoa mafunzo kwa wafanyakazi wake.  Boti nyengine ya pili itawasili nchini mwezi wa Septemba, 2020.  Boti zote mbili kila moja ina uwezo wa kuchukua tani 40 za samaki kwa wakati mmoja.  Kadhalika, Serikali kupitia ZAFICO imeanza mradi wa ujenzi wa chelezo na mtambo wa kusarifu samaki kwenye bandari ya Malindi na shughuli za wavuvi wadogo zimeimarishwa. Jitihada hizi za Serikali zimewezesha kuongezeka kwa kiwango cha samaki waliovuliwa kutoka tani 25,396 mwaka 2010 hadi kufikia tani 36,728 mwaka 2019. Sambamba na hatua hizi, Serikali imeanzisha Taasisi ya Utafiti ya Uvuvi na Mazao ya Baharini, ambayo nayo imeanza kazi vizuri sana.  Jengo la Taasisi hio jipya linaendelea vizuri pale Maruhubi. 

Mheshimiwa Spika,
Kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Kilimo na Chakula (FAO), Serikali imeanzisha mradi wa ujenzi wa kituo cha kutotolea vifaranga wa samaki huko Beit  Ras, uliogharimu USD Milioni 3.23, zilizotolewa na Serikali ya Korea, kupitia Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Kimataifa la Korea (KOICA). Lengo la mradi huu ni kuzalisha vifaranga milioni moja kwa mwaka, vya samaki, kaa, majongoo na kuvigawa kwa wananchi wa Unguja na Pemba.  Tayari vifaranga 195,000  vya samaki vimegaiwa kwa wafugaji wa samaki.

Mheshimiwa Spika,
Hatua za kuliongezea tija zao la mwani zimechukuliwa. Ahadi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwapa wakulima wa mwani Unguja na Pemba, vihori 500 kwa kwa ajili ya kubebea mwani tayari imetekelezwa, kama ilivyoelekezwa katika kifungu cha 76(c) cha Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Kwa kushirikiana na wataalamu na wawekezaji wa Kampuni za “Ocean Fresh” na “Kaappa Carrageenan Nusantaran” za Indonesia, kiwango cha ubora wa mwani wa Zanzibar kimeongezeka sana kutokana na mafunzo yaliyotolewa kwa wakulima wa mwani na tunatarajia kujenga Kiwanda cha Mwani huko Chamanangwe, Wete Pemba, kuanzia mwezi wa Agosti, 2020.  Fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho, tayari tunazo, eneo la ujenzi limesafishwa na michoro iko tayari. Muda wetu ukifika mwezi wa nane tutaanza kazi.  Hawa ni watu wa kweli.  Tutaendelea kushirikiana nao.

Wakulima wa  mwani wawe na subira mambo yao yatakuwa mazuri.  Matumaini yangu bei ya mwani itapanda mara 3 au 4.  Wakulima wa mwani wasivunjike moyo.  Kampuni ya Kaappa Carageenan watanunua mwani huo.

Mheshimiwa Spika,
Serikali iliandaa Sera Mpya ya Mazingira ya mwaka 2013 yenye kutoa muongozo wa shughuli za uhifadhi wa mazingira hapa Zanzibar na Sheria mpya ya Usimamizi wa Mazingira Namba 3 ya mwaka 2015.  Kutokana na Sera na Sheria ya mazingira, Serikali imesimamia kwa ufanisi mkubwa upigaji marufuku wa uingizaji na utumiaji wa mifuko ya plastiki kuanzia mwaka 2011.  Hadi kufikia mwezi wa Mei 2020, jumla ya tani 9.30 za mifuko ya plastiki zilikamatwa na watuhumiwa waliopatikana na makosa walitozwa faini ya jumla ya TZS Milioni 86.40.  Nimethibitishiwa kwamba fedha hizo walizilipa.

Kadhalika, Serikali imeendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuyatunza na kuyaendeleza mazingira, kuzitunza raslimali  zisizorejesheka hasa mchanga, mawe, kokoto na kifusi pamoja na kuzuia ukataji ovyo wa miti na kuwahamasisha wananchi wapande miti kwa wingi sana.  Naipongeza Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Serikali inakabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutekeleza  mpango mkakati wa miaka mitano, kwa mafanikio makubwa.  Kadhalika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba imelisimamia kwa mafanikio makubwa suala la maafa, kwa kuzingatia sheria Namba moja ya 2015. 

Katika kukabiliana na maafa, jitihada mbali mbali zimechukuliwa na Serikali zikiwemo ujenzi wa misingi ya kupitisha maji ya mvua ambayo husababisha maafa ya mafuriko katika makaazi ya watu kwenye maeneo mbali mbali ya Jiji la Zanzibar.  Serikali ilibuni na ilitekeleza Mradi wa Huduma za Jamii Mijini (ZUSP) uliofanikiwa kuliondoa tatizo hilo la mafuriko ya maji ya mvua, katika maeneo mbali mbali.

Mheshimiwa Spika,
Katika vipindi vyote wiwili vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba, imeelekeza juhudi kubwa katika  kupambana na usafirishaji na  matumizi ya dawa za  kulevya. Hatua hizo ni pamoja na kuwakamata na kuwachukulia hatua wale wanaofanya kazi hii ya haramu ya kusafirisha dawa za kulevya.

Kadhalika, mafanikio yamepatikana katika kuvivunja vikundi vingi vilivyokuwa vikitumia dawa za kulevya.  Vile vile, kwa lengo la kuwarekebisha watumiaji wa dawa za kulevya, Serikali imewaweka kwenye nyumba maalum za nafuu (Sober Houses), vijana wapatao 9,030, ambapo kati ya hao vijana 3,161 sawa na asilimia 35, walifanikiwa kuachana kabisa na dawa hizo.

Vile vile, Serikali ya Awamu ya Saba, imejenga kituo cha tiba na marekebisho ya tabia kwa waathirika wa dawa za kulevya kilichopo Kidimni, Wilaya ya Kati Unguja.  Ujenzi huo umo katika hatua za mwisho kukamilika na ununuzi wa vifaa mbali mbali vya tiba na kurekebisha tabia za vijana hao umekamilika.  Kituo cha dharura cha tiba na marekebisho, kwa hivi sasa kimefunguliwa katika Hospitali ya Wagonjwa wa Akili, Kidongo Chekundu.  Vile vile, katika jitihada za kupambana na janga hili, jumla ya watuhumiwa 398 wametiwa hatiani katika kipindi hiki, wakiwemo raia wa kigeni.

Idadi ya kesi za dawa za kulevya imekuwa ikiongezeka mfululizo kutoka kesi 183 kwa mwaka 2015,  kesi 354 kwa mwaka 2016,  kesi 694  kwa mwaka 2017, kesi 654 kwa mwaka 2018 na kesi 503 kwa mwaka 2019.  Vile vile, kuna ongezeko la kiwango cha dawa zinazokamatwa, kimebainika ambapo katika mwaka 2015, zilikamatwa kilogramu 68.6, mwaka 2016 kilogramu 45.28, mwaka 2017 kilogramu 138.94, katika mwaka 2018 zilikamatwa kilogramu 722.22 na  mwaka 2019 zilikamatwa kilogramu 701.73 za dawa za kulevya.   Hali hio si nzuri sana.

Ni dhahiri kuwa ongezeko hilo la kasi na kiwango cha dawa za kulevya zilizokamatwa pamoja na wahalifu waliohusika  limetokana na jitihada za Serikali  kupitia vyombo vyake pamoja na raia wema katika kukabiliana na janga hili.  Leo tumetoa taarifa hizi rasmi, ili wananchi wajue tulikuwa hatukulala.  Tulikuwa tunangoja tu muda ufike tuwaeleze.

Natoa wito kwa viongozi na wananchi kuendelea kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kuratibu na Udhitiiti wa Dawa za Kulevya na vyombo vyengine vya ulinzi katika kufanikisha mapambano dhidi ya usafirshaji na matumizi ya  Dawa za Kulevya, ambazo huathiri zaidi vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa letu.  Sheria mpya tuliyoitunga inafanya kazi vizuri sana.

Mheshimiwa Spika,
Wananchi wamefaidika sana na juhudi zetu za kuhamasiha uanzishwaji na uendelezwaji wa vyama vya ushirika na SACCOS kwa lengo la kujipatia ajira na mikopo ya kujiendeleza.

Mheshimiwa Spika,
Kipindi cha miaka kumi si kidogo, ndio maana tumefanya mambo mengi na makubwa.  Baraza hili ndilo yaliyoyafanikisha maendeleo haya ambayo mimi leo naona raha na furaha kuyaelezea.  Naamini  na nyinyi mnaona raha hivyo hivyo; kwa hivyo, endeleeni kunivumilia.

Katika hotuba yangu ya ufunguzi wa Baraza la Tisa la Wawakilishi nilitoa ahadi kuhusu azma ya Serikali katika kipindi hiki, ya kuviendeleza vikundi vya ushirika kwa kuvipatia mafunzo, mikopo na kuvifanyia ukaguzi kwa lengo la kuviimarisha.  Leo nataka nieleze bayana kwamba, jumla ya vyama vya ushirika 39 vya Akiba na Mikopo na vyengine 1,652 vya uzalishaji mali vimesajiliwa.  Hatua hio imefanya idadi ya vyama vya ushirika vilivyosajiliwa hadi mwezi Oktoba, 2019 kufikia 3,676.  Vile vile, mwamko wa wananchi kujiunga na SACCOS umewezesha kuongezeka kwa mitaji ya Taasisi hizo kutoka TZS Bilioni 3.5 mwaka 2013 na kufikia TZS Bilioni 14.3 mwaka 2019.

Mheshimiwa Spika,
Mafanikio yameendelea kupatikana katika kuimarisha huduma za Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na kukabiliana na tatizo la ajira.   Tangu mikopo hio yenye masharti nafuu na isiyo na riba ilipoanza kutolewa mwaka 2014 hadi tarehe 31 Machi 2020 imefikia jumla ya mikopo 3,758 yenye thamani ya TZS Bilioni 5.684 imetolewa na imewanufaisha wananchi 51,973 wa Unguja na Pemba kati yao wakiwemo wanawake 27,992 ambao wapo wengi kuliko wanaume ambapo wanaume 23,981. Kinamaa oyee!

Kadhalika, kwa lengo la kuwawezesha vijana kiuchumi, katika mwezi wa Septemba, 2019 Serikali ilianzisha Mfuko wa Vijana wenye mtaji wa USD Milioni 20 sawa na TZS Bilioni 46, ikiwa TZS Bilioni 23 kutoka kwenye Khalifa Fund (Mfuko wa Mtawala wa Jumuiya ya Falme za Kiarabu UAE) na TZS Bilioni 23 kutoka SMZ.  Juhudi hizi za Serikali zitaongeza fursa za ajira na kuimarisha maendeleo ya vijana.  Matayarisho ya matumizi ya fedha hizo yanaendelea na utekelezaji wake utaanza muda wowote kuanzia sasa.

Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi hiki, Serikali iliuendeleza Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, tuliviendeleza vituo vya mafunzo ya amali, tuliyaimarisha mazingira ya uwekezaji na shughuli za utalii; ili maeneo hayo yaongeze fursa za ajira nchini hasa kwa vijana.  Katika mwaka 2014, tuliuanzisha na tuliuzindua Mpango Mkakati wa Ajira kwa Vijana, ulioweka vipaumbele katika sekta za ujasiriamali, elimu ya amali na ufundi stadi.

Serikali ya Awamu ya Saba, imeweza kutoa nafasi 21,850 za ajira kwa wazalendo na  ajira 20,394 zimetoka kwenye sekta binafsi, ambazo kati ya hizo 13,248 ni za ndani na 7,146 ni ajira za nje.  Naipongeza sana sekta binafsi kwa mchango wao muhimu katika kuongeza fursa za ajira kwani Serikali haiwezi kukabili changamoto ya ajira bila ya kushirikisha sekta binafsi. Wataalamu wanasema “private sector is the engine of growth” tafsiri sekta binafsi ndio injini ya kuufufua uchumi.

Mheshimiwa Spika,
Katika hotuba yangu ya ufunguzi wa Baraza la Tisa  niliahidi kuchukua hatua mbali mbali za kuimarisha mazingira ya kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na sera ya utumishi, maslahi ya watumishi, kuimarisha fursa za mafunzo, usalama kazini na upatikanaji wa vifaa vya kazi na nyenzo, ili kuongeza ufanisi katika sehemu za kazi.  Katika kuyafikia malengo hayo, kama tulivyoahidi, Serikali ilifanya mageuzi makubwa ya Utumishi wa Umma baada ya kutungwa kwa Sheria ya Utumishi wa Umma Namba 2 ya mwaka 2011 na Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2014. Ofisi ya Rais inayohusika na Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeanzishwa pamoja na kuandaa mpango wa maendeleo ya wafanyakazi na Miundo ya Utumishi “ Scheme of Service” ya kila Wizara, Idara, Mashirika na Taasisi zake na kuandaa Miundo na Mifumo ya Taasisi zote hizo.  Suala la mgawanyo wa mamlaka na dhamana, nidhamu na uwajibikaji wa kazi na kufanya kazi kwa mujibu wa kanuni ya utumishi yote yametekelezwa kama nilivyoahidi.

Marekebisho ya mishahara ya wafanyakazi yalifanywa mara nne kuanzia mwaka 2011, 2013, 2015 na 2017, kwa lengo la kuwapa motisha wafanyakazi kwa kuzingatia mapato yetu wenyewe.  Haya yote ni kwa mapato yetu yenyewe.  Haijapata kutokea.  Awamu ya Saba tumeweza. Viwango vya mishahara ya wafanyakazi wa ngazi mbali mbali, wataalamu na mabingwa wa fani mbali mbali; vilibadilishwa na viliimarishwa.  Hivi karibuni, Serikali imekamilisha kazi muhimu ya kuweka viwango vya mishahara na maposho ya Mashirika yote ya Serikali yenye mfumo mmoja unaolingana na Idara ya Serikali.  Kazi hii imefanyika vizuri na taarifa nilizoletewa ni kwamba uongozi wa Mashirika, Idara za Serikali na watumishi wao wameridhika na wamefurahi sana.  Ni matumaini yangu kwamba tatizo lililokuwepo la muda mrefu la kila Shirika la Serikali kufanya utaratibu wake wa mishahara na maposho, halitotokea tena.  Tatizo la mishahara na mapato leo halipo tena.

Mheshimiwa Spika,
Hatua ya kupandisha mishahara ililenga kuwapa motisha na ari watumishi, ili waongeze juhudi na ufanisi katika kazi zao, kwa lengo la kuwatumikia wananchi kwa nidhamu kubwa na uadilifu.    Haikuwa ruzuku ni wajibu wao.  “Mchezo kwao hutunzwa”.  Vile vile, hatua hio ni matokeo ya ukuaji mzuri wa uchumi wetu na kuongezeka kwa mapato.  Kwa uamuzi huo wa Serikali, matumizi ya Serikali kwa ajili ya mishahara yakaongezeka hadi kufikia TZS Bilioni 417.9 kwa mwaka 2018/2019, sawa na ongezeko la asilimia 48. Kiwango cha malipo ya mishahara katika mwaka 2010/2011 kilikuwa ni TZS Bilioni 83.1.  Hata hivyo, licha ya ongezeko hilo, Serikali imemudu kulipa mishahara kwa wakati kwa kipindi chote cha miaka kumi na inaendelea kumudu, kwa vile uchumi wetu umeendelea kukua kwa kasi na kiwango cha kuridhisha.

Sambamba na kuimarishwa kwa mishahara ya watumishi wa umma,  vile vile, Serikali katika kipindi hiki imeongeza kwa vipindi viwili malipo ya pencheni za wastaafu,  katika mwaka 2011 na mwaka 2017. Kadhalika, Serikali imewatayarishia watumishi mazingira bora ya kufanyia kazi, kwa kujenga majengo mapya yaliyo bora kwa ajili ya Ofisi mbali mbali za Serikali kwa Unguja na Pemba nyote mashahidi mnayaona.  Miongoni mwa majengo ya ofisi hizo ni pamoja na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Katiba na Sheria, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati Zanzibar (ZURA) na majengo ya wizara za Serikali yaliyopo Gombani huko Chake Chake Pemba yanayotumika kwa Wizara sita na mengineyo.  Baada ya kuyasimamia mabadiliko makubwa ya utumishi wa Umma yaliyotekelezwa, tumeshuhudia kuongezeka kwa ufanisi wa kazi na uwajibikaji kazini, ingawa bado bidii zaidi inahitajika.  Sijayataja yale ya Idara Maalum ambayo nayo yako mengi sana.  Kazi nyengine muhimu tuliyoifanya, ni ya mishahara inayoitwa “mishahara hewa”. Nyinyi Wajumbe wa Baraza mlilizungumzia hili humu Barazani, na mimi nikamtaka CAG alete ripoti yake ya mishahara hewa.  Kwa hivyo ripoti ile ni ya kwangu mimi, na nikaifanyia kazi.  Nikaunda timu nzuri ya watu waliokuwa na nidhamu na wanaojua kuwajibika wakaziangalia wizara tano zilizodhaniwa kuwa na matatizo ya mishahara hewa.  Mbili kati ya hizo hazikuwa na matatizo makubwa, kwa hivyo tukazitaka fedha wazirudishe. 

Tatu miongoni mwao zilihitaji matatizo yao kuzungumzwa na kuzingatiwa.  Taarifa hizi tukazizungumza Serikalini na tukawajibisha.  Walikuwa wakichukua mishahara kwa ghilba na hila. Nikamwambia Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi atangaze katika vyombo vya habari mambo tuliyoyaona na nyie mkayasikia. Kisha wengine tukawafuza kazi na wengine tukawabadilisha wizara kwa sababu ya heshima ya Serikali.  Haya lazima myajue Waheshimiwa Wawakilishi kwamba hali yaikuwa nzuri.  Sie tunachuma tupate sote, lakini wenzetu, tena wengine wako nchi za nje, huku fedha zinaingia katika akaunti zao.  Akhasi kuliko zote ilikuwa Wizara ya Elimu.  Mwenyewe Waziri shahidi anajua.  Yeye hakuhusika aliyakuta mengine lakini ndio uongozi.  Kwa hivyo tumechukua hatua madhubuti. Udanganyifu si mzuri, na kwa kweli huu ni wizi si udanganyifu.

Ni wazi kwamba katika mfumo wowote wa maisha, hata kwa wanyama panakuwa na uongozi; na uongozi unakuwa na heshima na thamani yake.  Lakini unapoitwa kiongozi unakuwa na kitu cha ziada ambacho watu wanakiratajia.  Hali hii inathibitika katika ile hadithi ya bwana muuza kasuku.

Kuna bwana mmoja alikwenda kwa wauza ndege kutika kununua  kasuku.  Akakuta kasuku  wa rangi tatu, mmoja mwekundu, mmoja wa kijani na mmoja manjano.  Akaulizwa unataka kununua?. Akasema ehee.  Akaambiwa chagua.  Akachagua mwekundu akauliza kiasi gani?.  Akaambiwa Dola 500.  Akauliza huyu wa kijani kiasi gani?. Akaambiwa Dola 500,000, na huyo ya mwisho Dola Milioni Moja.  Akauliza sasa wanatafauti gani?, mbona huyu ghali zaidi?.  Akaambiwa hawa wote wanamwita huyu bosi. Kila mtu anataka ubosi lakini, ili uupate ubosi ni lazima ufanye kazi.

Mheshimiwa Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba ilitambua kuwa lengo lake la kukuza uchumi wa Zanzibar halitaweza kufanikiwa bila ya  kwenda sambamba na uimarishaji wa barabara, bandari, viwanja vya ndege pamoja na kuwa na nishati ya uhakika ya umeme. Kwa hivyo, katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, jitihada kubwa zimefanywa na Serikali katika kuimarisha miundombinu hio.

Mheshimiwa Spika,
Kuhusu miundombinu ya barabara, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba,  hadi kufikia mwezi Disemba 2019, imejenga jumla ya kilomita 129 za barabara kwa kiwango cha lami kwa Unguja na Pemba.  Kiwango hiki ni kikubwa cha Zanzibar.  Miongoni mwa barabara hizo ni barabara ya Jendele-Cheju-Kaebona (km 11.7), barabara ya Njia nne hadi Umbuji (km5), Mwanakwerekwe-Fuoni (km5), Mfenesini-Bumbwini (km 13.6) Magogoni-Kinuni (km 2.15) na barabara ya Bububu-Mahonda-Mkokotoni (km 31), Matemwe-Muyuni (km 7.6), Pale-Kiongele (km 4.6) kwa Unguja.  Kwa upande wa Pemba ni barabara tano katika Mkoa wa Kaskazini Pemba zenye urefu wa km 34.85 nazo ni Wete-Konde (km 15), Wete-Kando (km 13) Bahanasa-Daya-Mtambwe (km 13.6), Mzambarautakao-Pandani-Finya (km 8) na Mzambarau Karimu-Mapofu (km 8.6). Nyengine ni barabara ya Mkanyageni-Kangani (km 6.5) na barabara ya Mgagadu-Kiwani (km 7.6).  Tumefanya mambo makubwa sana na yote haya yametokea hapa hapa katika Baraza lenu, na Baraza hili ndio chem chem ya maendeleo yetu. Anayesema vyengine hiari yake, lakini wananchi wote wanajua hivyo.

Mheshimiwa Spika,
Vile vile, Serikali imejenga daraja na barabara kwa kiwango cha lami, yenye urefu wa mita mia nne katika eneo la Kibondemzungu pamoja na kuweka taa za barabarani.  Ujenzi huo umekamilika na daraja hilo lililopewa jina la “Daraja la Dk. Ali Mohamed Shein” ambalo lilifunguliwa rasmi tarehe 9 Januari, 2020. Hivi sasa kazi za ujenzi wa barabara zinaendelea katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.  Kwa upande wa Unguja, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami unaendelea kwa barabara kutoka Kibondemzungu hadi kituo cha Polisi Fuoni (km 1.6), Koani-Jumbi (km 6.3), Fuoni-Kombeni (km8.59), na barabara ya Jozani-Charawe-Ukongoroni-Bwejuu (km 23.3).  Kwa upande wa Pemba, kazi ya ujenzi wa barabara ya Ole-Kengeja (km 35) upo hatua ya mwisho kukamilika na ianze kutumika rasmi.  Naipongeza kwa dhati Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mbali ya ujenzi wa barabara unaofanywa na Wakandarasi, Serikali iliamua kununua zana na vifaa vipya vya kisasa vya kutengenezea barabara, ili kazi hio ifanywe na Wakala wa barabara.  Vifaa hivyo viligharimu jumla ya TZS Bilioni 14. Vile vile, katika kipindi hiki cha miaka kumi, zimewekwa taa za barabarani na za kuongozea vyombo vya moto katika barabara zetu kwenye maeneo mbali mbali ya Jiji la Zanzibar na katika manispaa za mji wa Chake Chake, Wete na Mkoani.  Kazi inaendelea vizuri, lakini juzi nimepata taarifa mbaya za kunitia huzuni na kunifadhaisha.  Nimeambiwa taa mpya tulizozitia kule Pemba kuna watu wanaojidhania kuwa mashujaa wamezing’oa.  Mimi nataka niwambie waliofanya kazi hio ya kuharibu taa zetu, wende wenyewe wakajisalimishe vituo vya polisi, maana tutawakamata na tumeanza kuwajua.  Ni vyema wende wenyewe kabla ya hatujenda kuwakamata sisi.  Tukiwashika sisi yatakuwa mengi sana.  Nawanasihi ndugu zangu wa Pemba wasiwe na ghulka hii ya kuharibu mtu kitu chake.  “Chako ni chako”, lazima ukithamini.  Tabia ya kuvuruga vitu vya Serikali vyenye manufaa na wananchi wengi, ni jambo la kishetani sana.  Nawaambia ndugu zangu wa Chake na Wete kuwa hili liwe la mwisho.

Mheshimiwa Spika,
Uimarishaji wa usafiri wa anga ni miongoni mwa masuala yaliyozingatiwa na Serikali ya Awamu ya Saba, kama nilivyoahidi wakati nilipoingia madarakani mwaka 2010 ni kuikamilisha kazi ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume, iliyoanzishwa na Serikali yetu ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mstaafu Dk. Amani Abeid Karume.  Wakati wetu wa Awamu ya Saba, tumejenga njia za kupitia ndege (taxi ways) kutoka mita 1,805 hadi kufikia mita 3,427. Tumenunua vifaa vya kisasa kadhaa, kwa mfano mashine mpya tano za kisasa za ukaguzi wa abiria na mizigo.  Kadhalika, tumejenga uzio wenye urefu wa kilomita 11 unaozunguka eneo lote la uwanja kwa lengo la kuuhifadhi uwanja huo.  Katika uwanja wa ndege na sehemu nyengine za mji wetu tumeshughulikia ulinzi kwa kufunga kamera za usalama CCTV, ili kujihami na matukio ya ujambazi ndani ya uwanja wa ndege na sehemu nyengine.  Kiwanja cha ndege cha Zanzibar sasa ni miongoni mwa viwanja virefu katika Afrika ya Mashariki ni kiwanja chenye njia ndefu za kurukia ndege kuliko viwanja vyote vya Afrika Mashariki. Ndege yoyote inatua Zanzibar. Uwanja wa Abeid Amani Karume ni kiwanja cha Kimataifa.

Hivi sasa Serikali inakamilisha ujenzi wa jengo jipya la abiria la Terminal III ambalo litakapomalizika mwezi wat isa mwaka huu, tutakapokabidhiwa, litafikia gharama za USD Milioni 128.4 badala ya USD 70.4, za mkataba wa mwanzo.  Tuliongeza mkataba na mambo kadhaa, ili kuupa hadhi ya juu uwanja huu.  Jengo hili litaongeza huduma na haiba ya uwanja huo na linatarajiwa kuwahudumia kiasi cha abiria 1,600,000 kwa mwaka.  Tumepiga hatua kubwa sana.

Mheshimiwa Spika,
Kuhusu kiwanja cha ndege cha Pemba, Serikali imechukua hatua za kuimarisha huduma za kiwanja hiki kwa kuweka taa, ili kuziongoza ndege kuruka na kutua kwa usalama. Kadhalika, jengo la abiria limefanyiwa matengenezo makubwa na eneo la ziada la maegesho ya ndege limeongezwa. Serikali inaendelea na hatua za kukiimarisha kiwanja cha ndege cha Pemba kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), iliyosaidia kufanywa kwa upembuzi yakinifu pamoja na kuandaa mahitaji yote yanayohusu ujenzi wa kiwanja kipya cha kisasa cha Pemba.  Ripoti ya upembuzi yakinifu tayari imeshakabidhiwa kwenye Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kwa ajili ya kuomba mkopo wa fedha za ujenzi kwa kuzingatia taratibu ziliopo. Tunatarajia kwamba ujenzi wa Uwanja huu mpya utaanza mara tu baada ya mkopo huo kupatikana.  Mimi na Rais John Pombe Magufuli tumeiomba Benki ya Maendeleo (AfDB) kujenga uwanja wa ndege mpya wa Pemba.

Mheshimiwa Spika,
Juhudi hizo za Serikali zimeleta mafanikio katika usafiri wa anga ambapo safari za ndege kwa Unguja na Pemba zimeongezeka kutoka safari 42,733 mwaka 2010 hadi kufikia safari 66,393 mwaka 2019. Vile vile, abiria wanaotumia viwanja vya ndege vya Zanzibar wameongezeka kutoka abiria 596,252 mwaka2010 hadi kufikia abiria 1,426,866 mwaka 2019 na mizigo iliyopitia katika  Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume imeongezeka kutoka tani 584 mwaka 2010 hadi kufikia tani 2,538 mwaka 2019.
  
Mheshimiwa Spika,
Serikali imezingatia umuhimu wa bandari ikiwa ni lango kuu la biashara na uchumi. Katika hotuba yangu ya ufunguzi wa Baraza la Tisa la Wawakilishi, niliahidi kuwa Serikali itatekeleza mradi wa ujenzi wa bandari mpya ya kisasa ya kuhudumia mizigo katika eneo la Mpigaduri. Bandari ya Malindi itaendelezwa kwa kuiongezea vifaa vya kisasa vya kutolea huduma za abiria na mizigo nalo hili limeanza kutekelezwa pamoja na bandari ya Mkoani Pemba.  Vile vile, Serikali iliahidi kujenga gati ndogo ya Mkokotoni na Tumbatu, ili kurahisisha huduma za usafiri hasa kwa wananchi wa Tumbatu.  Gati ndogo ya Tumbatu tayari imejengwa na ile ya Mkokotoni ujenzi wake utaanza hivi karibuni.

Jitihada hizo za kuimarisha bandari na usafiri wa baharini zilifanikiwa katika kipindi hiki cha takriban miaka kumi, ambapo zana na vifaa vya kisasa vya kazi vilinunuliwa kwa ajili ya kuimarisha huduma katika bandari zetu za Unguja na Pemba.  Kwa upande wa bandari ya Malindi, utoaji wa huduma hivi sasa umeimarika sana, ambapo meli kubwa zinazofika katika bandari hio zenye uwezo wa kuchukua makontena 6,000, sasa zinahudumiwa kwa siku tatu tu badala ya wiki moja kama ilivyokuwa hapo kabla.

Katika kipindi hiki majengo manne ya kuwahudumia abiria yamejengwa katika bandari ya Malindi, Wete na Mkoani ambapo majengo mawili yenye uwezo wa abiria 1,085 wanaweza kuhudumiwa kwenye bandari ya Malindi, abiria wapatao 300 wanaweza kuhudumiwa kwenye bandari ya Mkoani na abiria 200 wanaweza kuhudumiwa katika bandari ya Wete.  Vile vile, bandari ndogo ya Mkokotoni imeimarishwa kwa kujengwa ofisi ya Shirika la Bandari pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa gati ndogo ya Tumbatu.

Bandari za Zanzibar zimetoa huduma kwa meli za kigeni 1,509 na kuhudumia mizigo mchanganyiko yenye uzito wa tani milioni 2.6.  Vile vile, jumla ya abiria 20,499,164 walihudumiwa katika bandari ya Unguja na abiria 9,541,686 walihudumia katika bandari za Pemba.  Haya ni mafanikio makubwa sana yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka kumi.

Mheshimiwa Spika,
Uamuzi wa Serikali wa kujenga Bandari ya Mpigaduri upo pale pale kama ilivyoelezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya 2010/2015 katika kifungu cha 90(a) ukurasa wa 151.  Hata hivyo, ujenzi huo umechelewa kuanza kutokana na sababu zifuatazo:- Kwanza, gharama za ujenzi zilizokisiwa na Kampuni iliyokubaliwa ijenge bandari hio; hapo mwanzo zilibainika kuwa kubwa na ilichukua muda Serikali kujadiliana juu ya namna ya kupata mkopo wa ujenzi huo.  Pili, michoro na ramani ya ujenzi huo haikutayarishwa katika makisio yaliyofanywa mwanzo, hivyo ilikuwa ni vigumu kuuendeleza mkopo huo na ujenzi wake.  Kwa hivyo, Serikali ililazimika ichukue hatua za kuandaa mpango kamili ikiwemo michoro, ramani za ujenzi na gharama halisi kwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri.  Kazi hio sasa inaendelea vizuri pamoja na kutafuta mkopo wa bei nafuu kwenye benki ya Exim ya Indonesia na Benki ya Exim ya Afrika.  Tunatarajia ujenzi huo utaanza baadae mwaka huu. Hata hivyo, ujenzi wa mradi huo tutauanza kuutekeleza kwa fedha zetu wenyewe za ndani, ambazo tumezitenga kwenye bajeti ya 2020/2021.
Katika ziara yangu ya mwezi wa Aprili, 2019 nilipokitembelea kisiwa cha Uzi-Ngambwa, nililiona tatizo la usafiri wa kwenda na kurudi huku na niliahidi kulifanyia kazi suala hili.  Kwa hivyo, Serikali imeanza maandalizi ya ujenzi wa daraja la Unguja Ukuu na Uzi Ng’ambwa.  Ujenzi huo utaendelea kutekelezwa kwenye bajeti ya 2020/2021.  Ninaamini kwamba Serikali ya Awamu ya Nane itamaliza ipasavyo kazi hii.

Mheshimiwa Spika,
Kwa lengo la kuimarisha usafiri wa baharini kati ya Unguja na Pemba na bandari za mwambao wa Afrika ya Mashariki, Serikali ilinunua meli mpya ya Mapinduzi II yenye uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na tani 200 za mizigo na meli mpya ya mafuta inayoitwa MT Ukombozi II yenye uwezo wa kuchukua tani 3,500 za mafuta.  Meli zote mbili zilianza kazi mara tu baada ya kuwasili katika mwaka 2015 na 2018. Kadhalika, hivi sasa Serikali inashughulikia matengenezo makubwa ya meli ya MV Maendeleo iliyopelekwa Chelezoni huko Mombasa.  Vile vile, Serikali inashughulikia ununuzi wa boti tano za kisasa za kusafirishia abiria wanaoishi katika visiwa vidogo vidogo.

Jitihada hizi za kuimarisha usafiri wa baharini zimeweza kupata mafanikio zaidi kwa kuungwa mkono na wawekezaji wazalendo ambao wamechukua hatua ya kuleta nchini meli za kisasa na boti zinazokwenda kwa kasi zinazotoa huduma kwa abiria na mizigo katika bandari ya Unguja, Pemba, Dar es Salaam, Tanga na bandari nyengine za ukanda huu wa Afrika Mashariki.  Hatua ya wawekezaji hawa zimerahisisha sana kuwepo kwa huduma za uhakika za usafiri wa bahari, na vile vile kukuza shughuli za biashara, hasa biashara ya utalii hapa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
Nishati ya umeme ni muhimu katika kuimarisha ukuaji wa uchumi wa nchi na ustawi wa maendeleo ya wananchi wetu. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, katika awamu zake mbali mbali imefanya jitihada kadhaa za kuhakikisha kwamba Zanzibar inakuwa na huduma za nishati za umeme za uhakika. Katika uongozi wa Awamu ya Saba, niliahidi kuendeleza jitihada zilizoanzishwa na Awamu za Uongozi wa Serikali zilizotangulia katika kusambaza na kuwafikishia wananchi huduma hizi popote walipo.

Nnafuraha kueleza kuwa hadi sasa Serikali imeweza kuufikisha umeme katika shehia zote za Unguja na Pemba.  Nishati hii inapatikana katika vijiji 2,882 kati ya vijiji 3,259 sawa na asilimia 88.43 vikiwemo vijiji 354 vilivyopatiwa umeme katika kipindi hiki.  Jumla ya visiwa vidogo vidogo vitano (5) navyo vimepatiwa umeme ambavyo ni Kisiwa Panza, Makoongwe, Shamiani (Mwambe), Fundo na Uvinje.  Jitihada za kuufikisha umeme katika kisiwa cha Kokota na Njau huko Pemba zilipata changamoto na kusababisha kuchelewa kidogo. Hata hivyo, fedha kwa ajili ya kazi hio zimeshatengwa na utekelezaji wa mpango huo utaendelezwa kama nilivyoahidi.  Nawanasihi wakaazi wa kisiwa cha Kokota na Njau waendelee kuwa na subira, Mwenyezi Mungu atatujaalia dhamira yetu hii njema itafanikiwa.  Naupongeza uongozi na wafanyakzi wa Shirika la ZECO pamoja na Wizara kwa kazi kubwa ya kusambaza umeme hapa Zanzibar.

Kutokana na ongezeko la mahitaji ya nishati ya umeme yaliyojitokeza pamoja na kupata msaada wa Kampuni ya MCC ya Marekani kwa kuunganishwa waya wa baharini wa Megawati 100, mwaka 2010, Serikali imeamua kuwa ipo haja ya kuwa na umeme wa uhakika na tayari ishaanza kutafuta njia mbadala za kupata vyanzo vipya vya nishati ya umeme.  Utafiti uliofanywa kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) umeonesha kuwepo kwa uwezekano mkubwa wa Zanzibar kupata nishati ya umeme kutokana na nishati ya jua.  Kwa hivyo, hivi sasa Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hilo na limefikia hatua nzuri sana, kwa kushirikiana na Benki ya Dunia pamoja na sekta binafsi, ili kuongeza upatikanaji wa uhakika wa nishati hii.  Tumeambiwa kuwa Benki ya Dunia itatuunga mkono kwa kuanzia kupata MW 35, lakini wapo wawekezaji walojiandaa kuwekeza zaidi ya MW 70 na kadhalika.

Mheshimiwa Spika,
Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia ni eneo jipya la nishati ambalo niliahidi Serikali italishughulikia katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Saba. Kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria ya Mafuta Namba 21 ya mwaka 2015 iliyoipa mamlaka Serikali zetu mbili, kila moja itunge sheria yake ya Mafuta na Gesi Asilia.  Kwa mara nyengine tena, nataka nimpongeze kwa dhati Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kushirikiana nami kwa kuifanya kazi hii kwa uzalendo mkubwa.  Kwa hivyo, sheria ya Mafuta na Gesi Asilia Namba 6 ya mwaka 2016 ya Zanzibar, ilitungwa hapa hapa Baraza la Wawakilishi na nyinyi ndio mlioitunga, kwani bila ya nyie haya yasingelifanyika.  Kutokana na sheria hio, Mamlaka ya Udhibiti na Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPRA) na Kampuni ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC) zilianzishwa rasmi. Lengo la kuanzishwa kwa Taasisi hizo ni kuleta ufanisi zaidi katika usimamizi na udhibiti wa mafuta na gesi hapa Zanzibar.

Baada ya kutiliana saini Mkataba wa Uzalishaji na Mgawano wa Mafuta na Gesi Asilia baina ya ZPDC na RAK GAS ya Ras Al Khaimah, hapo tarehe 23 Oktoba 2018, utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia katika kitalu cha Pemba-Zanzibar zinaendelea na zimefikia hatua kubwa sana.  Nampongeza na namshukuru kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa namna tulivyoshirikiana katika kulifanikisha suala hili.  Katika hatua hii tuliyoifikia, nawanasihi wananchi waendelee kuwa na subira kuhusu jambo hili kwani watalaamu wa Kampuni zetu mbili wanaendelea kushauriana juu ya namna ya kuziarifu Serikali, ili hatimae wananchi waelezwe matokeo ya utafiti huo uliofanyika.  Taarifa zilizopo nzuri.  Tungoje kampuni zilizopewa majukumu zitwambie, ili baadae tuwaeleze wananchi.

Mheshimiwa Spika,
Katika kuhakikisha kwamba, tatizo la upungufu wa mafuta linapatiwa ufumbuzi wa kudumu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba inaendelea na azma ya ujenzi wa bandari ya Mafuta na Gesi Asilia, Mangapwani, kwa ajili ya shughuli za upakuaji wa mafuta na gesi.  Serikali inakamilisha mradi ujenzi wa nyumba 31, uliofikia asilimia 72, ambazo zinatarajiwa kupewa wananchi waliohama katika eneo litakalojengwa bandari hio.

Mheshimiwa Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, ilitambua wazi kuwa kuimarisha huduma za jamii ni jukumu lake la msingi na hatua muhimu ya kuendeleza shabaha ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari, 1964.  Katika kutekeleza azma hio, Serikali imechukua jitihada mbali mbali katika kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za Elimu, Afya na Maji Safi na Salama katika maeneo yote ya Unguja na Pemba, mjini na mashamba.

Mheshimiwa Spika,
Kwa upande wa Sekta ya Elimu, Serikali imeendeleza mafanikio ya elimu yaliyopatikana katika Awamu zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizotangulia.  Kadhalika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeimarisha ubora wa elimu inayotolewa katika ngazi zote kuanzia Maandalizi, Msingi, Sekondari, Elimu ya Juu pamoja na Elimu ya Mafunzo ya Amali na Elimu Mbadala.  Vile vile, Serikali imefanikiwa kuimarisha masomo ya Sayansi hasa kwa watoto wa kike, mafunzo ya elimu maalum kwa watu wenye ulemavu, kuimarisha maslahi ya walimu pamoja na kuyaimarisha mazingira ya kusomea yakiwemo majengo na vifaa vya maabara na vitabu vya kiada na ziada.

Mheshimiwa Spika,
Ni jambo la kufurahisha, kuona mafanikio makubwa ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, imeweza kuyapata katika utekelezaji wa malengo iliyojiwekea kwa upande wa Sekta ya Elimu, ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2010-2015, Ilani ya mwaka 2015-2020, Dira ya Maendeleo ya 2020 na Mipango mingine ya Kitaifa.

Wakati tukiwa katika mwaka wa kumi wa uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, tunafarajika kwa mafanikio makubwa ya kuandikisha watoto wote waliofikia umri wa kusoma.  Serikali imeondoa michango ya wazazi katika elimu ya msingi katika mwaka 2015/2016 na kuondoa gharama za mitihani yote ya skuli za Sekondari kuanzia mwaka fedha 2016/2017, ili kuwawezesha watoto wote wapate elimu bure kwa shabaha ile ile ya tamko la Mwasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, alilolitangaza tarehe 23 Septemba, 1964. Katika kipindi hiki cha miaka kumi, tumeweza kuongeza idadi ya wanafunzi wapya wanaoandikishwa katika ngazi ya elimu ya lazima; Maandalizi, Msingi na Sekondari kutoka jumla ya wanafunzi 317,278 mwaka 2010 hadi kufikia wanafunzi 529,688 mwaka 2020.

Mheshimiwa Spika,
Ongezeko la idadi ya skuli, taasisi nyengine za elimu na wanafunzi katika ngazi zote ni miongoni mwa mafanikio yaliyofikiwa katika Sekta ya Elimu.  Idadi ya vituo vya “Tucheze Tujifunze” - (TUTU); vimeongezwa kutoka vituo 178 kwa mwaka 2010 hadi kufikia vituo 366 mwaka 2020.   Ongezeko hili ni sawa na asilimia 51.  Vituo hivi vipo kwenye Wilaya zote za Unguja na Pemba.

Hadi Disemba 2019, idadi ya skuli za Maandalizi imefikia 382 zenye wanafunzi 85,974, ikilinganishwa na skuli 238, zilizokuwa na jumla ya wanafunzi 29,732 katika mwaka 2010.  Ongezeko la skuli ni asilimia 62.3 na ongezeko la wanafunzi ni asilimia 6.

Mheshimiwa Spika,
Skuli za msingi zimeongezeka na zimefikia skuli 381 zenye wanafunzi 290,510 mwaka 2019, kutoka skuli 299, zilizokuwa na wanafunzi 226,812 katika mwaka 2010.  Ongezeko la skuli ni asilimia 27.4 na ongezeko la wanafunzi ni asilimia 28.

Kwa upande skuli za sekondari, hivi sasa zipo skuli 287 zenye wanafunzi 135,519, ikilinganishwa na skuli 105, zilizokuwa na wanafunzi 80,008, katika mwaka 2010.  Ongezeko la skuli ni asilimia 73.3 na ongezeko la wanafunzi ni asilimia 69.4.  Majengo kadhaa ya ghorofa ya skuli za Msingi na Sekondari yamejengwa na Serikali katika Wilaya zote za Unguja na Pemba.  Vile vile, katika kipindi hiki cha miaka kumi, zipo skuli za sekondari za ghorofa, zilizojengwa na wafanyabiashara wazalendo.

Mheshimiwa Spika,
Vile vile, Serikali imejenga vituo 22 vya ubunifu wa kisayansi (Hubs), (13 Unguja na 9 Pemba) ambavyo kwa jina la kitaalamu vinaitwa “Hubs”. Vituo hivi vyote vina maabara za sayansi, vyumba vya kompyuta, maabara za lugha,  maktaba na vyumba vya kujisomea wanafunzi. Kadhalika, katika mradi huu, zimejengwa skuli mbili za sekondari katika maeneo ya Mwanakwerekwe kwa Unguja na Wingwi kwa Pemba. 

Mheshimiwa Spika,
Sambamba na hatua hizo, Serikali imezipatia skuli vifaa vya kusomea vikiwemo vitabu vya masomo mbali mbali,vifaa vya maabara za masomo ya sayansi, vitabu vya maktaba, kuongezeka kwa walimu, mambo ambayo yameongeza ubora wa elimu kwa vigezo mbali mbali.  Katika kulishughulikia tatizo la upungufu wa madawati, katika skuli za Msingi na Sekondari, Serikali imenunua jumla ya seti za viti na meza 44,620 kwa ajili ya skuli za Sekondari Unguja na Pemba na kwa ajili ya wanafunzi 42,195 wa skuli za msingi ambavyo tayari vimewasili nchini na vimeanza kutumika na vyengine vinatarajiwa kuwasili wakati wowote kuanzia sasa kutoka nchini China.  Mambo yetu mazuri sana.

Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi hiki cha miaka kumi, Serikali imejenga majengo mapya kwa ajili ya Mafunzo ya Amali, huko Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja na Daya Mtambwe, katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.  Kwa kujengwa vituo hivi viwili mafunzo ya amali sasa yatatolewa katika Mikoa yote mitano ya Zanzibar. Vile vile, katika kipindi hiki Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume, iliyopo Mbweni, imeimarishwa na imeanza kutoa Mafunzo ya Shahada ya Kwanza, katika fani ya Urubani na Uhandisi wa Ndege, ambapo vijana 53 wamejiunga na masomo hayo na hapo baadae Taasisi hio, itatoa mafunzo ya Shahada ya Kwanza ya Ujenzi, Usafirishaji na Umeme.

Mheshimiwa Spika,
Mafunzo ya ualimu yanaendelea kutolewa katika Chuo cha Kiislamu Mazizini, Chuo cha Kiislamu Micheweni pamoja na vyuo vikuu vitatu vilivyopo Zanzibar;  Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) na Chuo cha Al-Sumeit. Katika mwaka 2018/19 vyuo hivi vilikuwa na jumla ya wanafunzi 7,090 wanaochukua masomo ya fani mbali mbali kuanzia ngazi ya Cheti, Stashahada, Shahada ya Kwanza, Shahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamivu.

Katika kipindi cha Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ilikiunganisha Chuo cha Afya, Chuo cha Kilimo, Chuo cha Utalii, Chuo cha Fedha na Chuo cha Uandishi wa Habari na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, SUZA.  Katika kuunganishwa huku vyuo hivi vimepewa hadhi ya kuwa skuli za SUZA (Schools) na vinatoa shahada, stashahada na vyeti mbali mbali.  Kwa mara ya kwanza wanafunzi 73 wamemaliza masomo ya Udaktari (Doctor of Medicine) katika mikupuo miwili, katika mwaka 2017 na 2018.  Kadhalika, mafunzo ya Shahada ya Uzamivu katika lugha ya Kiswahili yanaendelea kutolewa ambapo wanafunzi watano walifaulu katika mwaka 2017/2018 na mwanafunzi mmoja katika mwaka 2018/2019.  Vile vile, mafunzo ya Shahada ya Uzamili yalianzishwa katika masomo mbali mbali.  Idara za SUZA zimeongezeka kutoka 1 mwaka 2010 hadi 8 mwaka 2020.

Mheshimiwa Spika,
Kama ilivyoagizwa katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, kifungu 100(ii), ambacho nakinukuu kama ifuatavyo: “Kuongeza nafasi za masomo katika elimu ya juu na kuimarisha mfuko wa Bodi ya Mikopo, ili kuongeza idadi ya wanafunzi watakaonufaika…..”.  Serikali imeunda Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar iliyoanzishwa kwa Sheria Namba 3 ya mwaka 2011 kwa lengo la kuwasaidia vijana wetu kuendelea na masomo ya juu katika fani mbali mbali, ili tupate wataalamu wetu wenyewe imetekeleza vyema majukumu yake. Bodi hii  imetumia jumla ya TZS Bilioni 60.2, kwa ajili ya kuwadhamini wanafunzi 6,087  wa elimu ya juu katika  vyuo vikuu mbali mbali vya ndani na nje ya nchi. Sambamba na hili, Uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, umeanzisha utaratibu wa kuwalipia gharama zote za masomo wanafunzi wanaofaulu daraja la kwanza katika mitihani ya kidato cha sita. Utaratibu huu ulianza mwaka 2016 kwa wanafunzi 10 na kufikia wanafunzi 60 katika mwaka 2019.

Mheshimiwa Spika,
Wahenga wanasema, “Mti hawendi ila kwa nyenzo”, na mafanikio yote yaliyopatikana katika Sekta ya Elimu, nyenzo tafauti zimetumika zikiwemo nguvu kazi, vifaa mbali mbali vyakufundishia na kujifunzia, mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu na majengo mazuri ya kusomea. Mafanikio yote yaliyopatikana yametokana na kuongezeka bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imeongezwa mara 3.8; kutoka TZS Bilioni 47.093 mwaka 2010/2011 na kufikia TZS Bilioni 178.917 mwaka 2019/2020.  Tumefanya kazi kubwa sana.

Ndugu Wananchi,
Kadhalika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatekeleza kwa mafanikio makubwa Sera yake ya kutoa matibabu bure kama ilivyoanzishwa mara tu baada ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964.

Kutokana na kuongezeka kwa bajeti ya Wizara ya Afya kwa mara 9.6 kutoka TZS Bilioni 10.81 mwaka 2010/2011 hadi TZS Bilioni 104.24 mwaka 2019/2020, huduma za afya zimeimarika sana na zinaendelea kutolewa bure. Ongezeko la fedha za bajeti zimesaidia sana katika kuziimarisha  huduma za tiba na kinga katika hospital kumi, vituo vya afya na zahanati zote za Serikali 158 kwa Unguja na Pemba.  Serikali imetekeleza Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kifungu 102(b) kwa kuziimarisha huduma za Hospitali ya Mnazi mmoja hadi kufikia hadhi ya hospitali ya rufaa. Nanukuu kifungu hicho kama ifuatavyo: “Kuendelea kuifanya hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa ya rufaa kwa kuongeza huduma za matibabu ya saratani na kuimarisha huduma za uchunguzi na ununuzi wa vifaa kama Magnetic Resonance Imaging (MRI) ……”.  Kutokana na hatua hii, hivi sasa hospital hio inatambuliwa rasmi kuwa ni hospitali ya kufundisha madaktari, miongoni mwa hospitali za Jumuiya za Nchi za Afrika ya Mashariki. Hospitali ya Abdalla Mzee ya Mkoani, imepandishwa daraja na kuwa hospitali ya Mkoa baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa na kupatiwa vifaa, zana na nyezo mpya mbali mbali za kisasa.  Hospitali ya “Cottage” ya Kivunge na Makunduchi zimepandiswa daraja na kuwa hospitali za Wilaya Januari, 2019 baada ya huduma zake kuimarishwa.

Jitihada za Serikali za kusomesha madaktari, wakiwemo madaktari bingwa, zimewezesha kuongeza idadi ya madaktari na watumishi wengine wa afya.  Jitihada hizi zimeimarisha uwiano wa madaktari na watu wanaohudumiwa. Hivi sasa daktari mmoja anawahudumia watu 6,276 (1:6,276) kutoka daktari mmoja kuwahudumia watu 31,838 (1:31,838), mwaka 2010.  Kwa hivyo, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya madaktari na wataalamu wengine mbali mbali wa fani za afya, upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa maradhi na nyenzo mbali mbali za kufanyia kazi, pamoja na kuimarishwa kwa maeneo ya kufanyia kazi kumepelekea huduma za tiba na kinga zizidi kuimarika.

Jitihada za Serikali za kupambana na Malaria zinaendelezwa na kasi ya kuenea kwake bado ipo chini ya asilimia moja (0.4%), ingawa baadhi ya maeneo machache ya Mjini yamebainika kuongezeka wagonjwa wa Malaria. Juhudi zinaendelezwa za utoaji elimu kwa wananchi, ugawaji wa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu na upigaji wa dawa za ndani ya nyumba na maeneo yenye mazalia ya mbu.

Ndugu Wananchi,
Kadhalika, maambukizo ya UKIMWI yameendelea kushuka na  hivi sasa yamefikia kiwango cha asilimia 0.4 kutoka asilimia 0.6 mwaka 2010. Kuhusu vifo vinavyotokana na uzazi vimepungua na vimefikia 155 kwa kila vizazi hai 100,000, ikilinganishwa na vifo 288 kwa kila vizazi hai 100,000 katika mwaka 2010.  Jitihada za kuwaelimisha wajawazito wajifungulie hospitali badala ya majumbani, zimesaidia sana, ambapo mwaka 2010 wajawazito 51,912 walijifungulia majumbani ikilinganishwa na 37,803 mwaka 2019.

Pamoja na mafanikio niliyoyaelezea katika hotuba yangu hii, kwa kudhibitiwa kwa baadhi ya maradhi, lakini zipo changamoto zilizobainika katika hospitali zetu za Unguja na Pemba; ambazo ni kuongezeka kwa maradhi yasiyoambukiza kama vile maradhi ya sukari, matatizo mbali mbali ya maradhi ya moyo, maradhi ya figo, saratani ya shingo ya kizazi na saratani nyengine.  Matarajio yangu ni kwamba wataalamu wa Taasisi ya Utafiti ya Afya na wengine waliopo katika Idara mbali mbali za hospitali zetu na kwa kuendelea kushirikiana na wataalamu wengine wa Kimataifa; watafanya kazi zao za utafiti kwa bidii, ili Serikali iweze kuchukua hatua za kukabiliana na maradhi hayo.

Mheshimiwa Spika,
Sekta binafsi katika Sekta ya Afya imesaidia sana kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali za Serikali. Sekta hio inazo hospitali 3 na vituo vya afya 63 vya binafsi vilivyosajiliwa kisheria. Natoa pongezi na shukurani  kwa uongozi wa hospitali hizo kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wananchi katika kuimarisha huduma za afya nchini.

Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kuziimarisha huduma za maji safi na salama katika Mikoa yote ya Unguja na Pemba kwa kuzingatia maelekezo ya Ilani katika vipindi vyote viwili. Utekelezaji wa Mradi wa maji wa Mkoa Mjini Magharibi, kwa mkopo wa Dola za Kimarekani Milioni 21.246 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika, umekamilika na umezinduliwa tarehe 6 Januari, 2020. Wananchi wanaoishi katika Shehia 11 za Mji Mkongwe na Shehia 16 za maeneo mingine wananufaika na Mradi huu.

Kadhalika, mradi uliotekelezwa na Kampuni ya “First Highway Engineering of China” uliokamilika mwezi Aprili, 2018 umewanufaisha wananchi 11,850 katika shehia 21 za Mkoa wa Kaskazini Unguja na Kusini Unguja. Vile vile, Serikali ya Ras  Al Khaimah ilisaidia kuchimba visima 150, kati ya visima hivyo, visima 59 tayari vinafanya kazi na maji yanapatikana.  Katika visima hivyo, vinavyotoa maji, visima 32 vipo Unguja na 27 vipo Pemba.  Hivi sasa, kijiji cha Mtende na Uroa vinapata maji asilimia mia moja na kijiji cha Michamvi kinakisiwa kinapata maji asilimia 90.  Kazi ya ukamilishaji wa miundombinu inaendelea.  Wastani wa upatikanaji wa maji katika Mikoa mitano ya Zanzibar, hivi sasa imefikia wastani wa asilimia 80 katika kipindi hiki cha miaka kumi iliyopita. Hivi sasa, Serikali inaendelea na matayarisho ya kuanza mradi mwengine mkubwa kwa mkopo nafuu wa Dola za Kimarekani Milioni 92, uliotolewa na Serikali ya India.  Kadhalika, Serikali ya Japan imetoa msaada wa Dola za Kimarekani Milioni 100 kwa ajili ya kuendeleza huduma za maji.

Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati imeanzisha Chuo cha Kuwahudumia Wafanyakazi watakaoshughulikia huduma za maji.  Jumla ya wanafunzi 80 wamechaguliwa kuanza mafunzo hayo.

Mheshimiwa Spika,
Kwa lengo la kuziimarisha huduma za mawasiliano, Serikali ilianzisha mradi wa serikali mtandao (e-government), ambao ulizinduliwa rasmi mwezi Januari, mwaka 2013. Hadi hivi sasa jumla ya majengo 130 ya Serikali yameunganishwa katika serikali mtandao na yananufaika kupata huduma za mtandao bila ya malipo kipitia mradi huu. Huduma za mradi huu sasa zimeendelezwa kwenye “e-Heath” na “e-Tax” kwa lengo la kuongeza ufanisi na utendaji katika utumishi wa umma. Jumla ya hoteli 200 za madaraja mbali mbali zimeshaunganishwa katika mfumo huo.

Mheshimiwa Spika,
Serikali ilianzisha Shirika ka Utangazaji la Zanzibar (ZBC), lenye kushughulikia kwa pamoja matangazo ya redio na  televisheni ya Zanzibar. Juhudi kubwa zimefanywa katika kuubadilisha mfumo wa urushaji wa matangazo ya redio na televisheni kutoka kwenye analojia na kwenda dijitali, ambapo mitambo ya kisasa ya TV na Radio ilinunuliwa na kufungwa na tayari inatumika.  Kampuni ya Z-MUX imeanzishwa kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa ZBC TV.

Hivi sasa Shirika la  ZBC linawahudumia wananchi kwa kurusha matangazo saa 24, na linaongeza programu mpya za vipindi vinavyohusu masuala muhimu ya kiuchumi na kijamii. Hatua nyengine ya mafanikio ni kuanza kuonekana kwa ZBC TV kupitia king’amuzi cha DSTV katika chaneli ya 291, jambo ambalo limeongeza idadi ya watazamaji wa televisheni ya ZBC katika nchi mbali mbali za Afrika.  Hongereni ZBC kwa kuelimisha “Corona” nimeiona kali yenu!.

Kwa upande wa Shirika la Magazeti la Zanzibar, Shirika limefanikiwa kulichapisha Gazeti la Serikali la Zanzibar Leo, hapa hapa Zanzibar katika Wakala wa Serikali wa Uchapaji. Gazeti hilo sasa linapatikana na kusambazwa kwa urahisi, ikiwemo kupitia mitandaoni. Kuanzia mwezi Novemba 2019, Shirika limeanza kuchapisha gazeti la Kiingereza liitwalo “Zanzibar Mail”, ili kuwawezesha watumiaji wa lugha ya Kiingereza, wakiwemo watu mbali mbali pamoja na watalii, wanaokuja Zanzibar, kufuatilia taarifa muhimu za maendeleo ya Zanzibar.  Kadhalika, Wakala wa Serikali wa Uchapaji Zanzibar umeimarishwa kwa kupatiwa mitambo na vifaa vya kisasa ya kuchapisha nyaraka mbali mbali za Serikali zikiwemo vitabu vya hotuba, vitabu vya risiti na kuchapisha gazeti la Zanzibar Leo.  Taasisi hii imesaidia sana kuwezesha gazeti la Zanzibar Leo kuchapishwa hapa Zanzibar na kupatikana kwa urahisi.

Mheshimiwa Spika,
Kuhusu sekta ya utamaduni na sanaa, studio mpya ya kisasa ilimezinduliwa Rahaleo mwaka 2016, iliyotokana na studio ya zamani kwa ajili ya wasanii wa filamu na muziki ambayo inatumika vizuri. Vile vile, kuanzia mwaka 2010 hadi sasa, bado wasanii wanaendelea kulipwa mirabaha ambapo jumla ya TZS Milioni 402.80 zimekusanywa na kugawiwa kwa wasanii na wabunifu.  Kadhalika,Tamasha la Filamu la Kimataifa (ZIFF), Sauti za Busara, Tamasha la Utamaduni la Mzanzibari na mengine ya asili yamefanyika.

Kwa lengo la kuienzi na kuiendeleza Lugha ya Kiswahili, jumla ya  makongamano matatu ya kimataifa ya Kiswahili yaliyowajumuisha washiriki 419 yamefanywa. Makongamano hayo, yameleta hamasa  katika kuiendeleza lugha ya Kiswahili. Vile vile, Kikundi cha Taifa cha Taarab Asilia kimeimarishwa kwa kupatiwa ofisi na vyombo vipya.

Mheshimiwa Spika,
Tumezindua rasmi uwanja wa michezo wa Mao-Zedong tarehe 3 Januari, 2018 baada ya kufanyiwa matengenezo na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, na hivi sasa unatumika kwa michezo mbali mbali. Kadhalika, mpango wa Serikali wa kujenga viwanja vya michezo vya wilaya hivi sasa  unaendelea vizuri, katika Wilaya tano. Vile vile,  Serikali imeweka nyasi bandia na mpira wa kukimbilia katika uwanja wa  Amaan Unguja na Gombani Pemba.

Timu yetu ya mpira wa miguu ya Zanzibar Heroes  iliandaliwa vizuri na ilifanikiwa kupata ushindi wa pili katika mashindano ya Chalenji ya Mpira wa Miguu mwaka 2017.   Timu ya michezo ya watu wenye ulemavu imefanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa ya michezo mbali mbali. Nazipongeza timu zetu zote hizo.

Kadhalika, Serikali imeendelea kuwahamasisha wananchi wafanye mazoezi ya viungo hasa baada ya kuitangaza tarehe mosi ya Januari ya kila mwaka, kuwa siku ya mazoezi hayo kwa Unguja na Pemba.  Jumla ya mabonanza manane yameshafanyika. Idadi ya vikundi vya mazoezi vinavyoshiriki Bonanza la Mazoezi hapa Zanzibar vimeongezeka kutoka vilabu 12 mwaka 2010/2011 kutoka Unguja tu na kufikia vilabu 82 kutoka Unguja, Pemba na Tanzania bara katika mwaka 2019.

Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi hiki, ushirikishwaji wa wanawake katika ngazi mbali mbali za uongozi Serikalini pamoja na vyombo vya utungaji wa sheria, sera na utoaji wa maamuzi umeimarishwa. Kwa mfano, katika chombo hiki cha kutunga sheria, idadi ya wajumbe wanawake katika Baraza la Nane walifikia 26, na katika Baraza hili la Tisa, idadi yao ni 32 ikilinganishwa na wajumbe 20 waliokuwemo katika Baraza la Saba, mwaka 2005-2010.   Kama lilivyokuwa Baraz la nane na la tisa vijana wameliongezea ufanisi na haiba.

Vile vile, Serikali katika kipindi hiki imeanzisha skuli za sekondari maalumu za watato wa kike na imevihamasisha vikundi vya ujasiriamali kwa kuvipatia mafunzo pamoja na mikopo yenye masharti nafuu.  Kadhalika, imeanzisha kituo cha kuwafundisha wanawake kutengeneza vifaa vinavyotumia umeme wa nishati ya jua kwenye Chuo cha “Barefoot” Kibokwa, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mheshimiwa Spika,
Serikali inapiga vita vitendo vya udhalilishaji vya wanawake na watoto na inapambana dhidi ya vitendo hivyo kwa kushirikiana na taasisi mbali mbali na wananchi.  Kampeni ya Miaka Mitano wa Kupambana na Vitendo hivyo ulizinduliwa tarehe 6 Disemba, 2014 na ule wa kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na Mpango ulizinduliwa Agosti, 2017.  Jitihada hizo za Serikali zimesaidia sana dhidi ya vitendo hivyo kwa wanawake na watoto.

Jumla ya matukio 1,091 ya udhalilishaji yaliripotiwa katika vituo vya Polisi Unguja na Pemba kwa mwaka 2017/2018 ikilinganishwa na matukio 2,449 yaliyoripotiwa mwaka 2016/2017.  Vitendo hivyo vimepungua kwa zaidi ya nusu ya idadi ya matukio yote.  Kwa mwaka 2019, matukio ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji vilivyoripotiwa katika vituo vya polisi vya Mikoa yote yalikuwa 941, sawa na upungufu wa asilimia 61.6.  Kampeni iliyofanywa pamoja na programu hizi zimesaidia sana mapambano hayo, lakini jitihada zaidi bado zinahitajika kwani vitendo hivi vinaendelea kuripotiwa na vyombo vya habari kila baada ya muda.

Mheshimiwa Spika,
Kuhusu maendeleo na ustawi wa watoto, Sheria mpya Namba 6 ya mwaka 2011, inayozingatia utekelezaji wa haki zote za msingi za watoto, ilianzishwa ambayo imeipatia sifa Zanzibar duniani kote. Kwa dhamira ya kuwatendea haki watoto, Serikali ilianzisha mahakama ya watoto mwaka 2013. Vile vile, Serikali imevifanyia   matengenezo makubwa viwanja maalumu vya kufurahishia watoto vya Kariakoo Unguja na Tibirinzi Pemba.

Mheshimiwa Spika,
Bado lipo tatizo la ajira kwa vijana, lakini Serikali inachukua hatua.  Kwanza imeandaa mafunzo ya Amali katika vituo vya Serikali, katika vituo vya amali na katika Kituo cha Ukuzaji Wajasiriamali Mbweni.  Pili,  wamepatiwa mikopo,  ili waweze kujiajiri wenyewe kwenye shughuli zao. Tatu, wamewezeshwa kwenye kilimo kama vile pilipili hoho, ufugaji na ushoni.  Vijana 39,499 wamepatiwa mikopo wenye thamani ya TZS Bilioni 4.32 kwa jili ya kuwaendeleza katika kilimo, ufugaji na ushoni.

Mheshimiwa Spika,
Kuwatunza wazee katika maisha yao ya kila siku kwa kuwapatia mahala bora pa kuishi, huduma za msingi za kila siku katika maisha yao,  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ilikuwa inawalipa wazee wote Unguja na Pemba, waliofikia umri wa miaka 70 na kuendelea posho la TZS 20,000 kwa kila mwezi.  Uamuzi wa Serikali, sasa umetungiwa Sheria Namba 2 ya mwaka 2020, ambapo utaratibu wa kisheria umewekwa kuhusu masuala ya wazee.  Hivi sasa, jumla ya wazee 28,022 wamesajiliwa katika programu hii ya Pencheni Jamii.

Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi hiki, Serikali iliamua kuanzisha Idara ya Watu wenye Ulemavu chini ya Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar.  Sambamba na hatua hio, watu wenye ulemavu wameshirikishwa katika vyombo vya uamuzi, na kuhakikisha kuwa wanapata huduma zote muhimu zikiwemo elimu, afya, michezo, ajira na masuala mengine ya maendeleo na ustawi wao.  Vile vile, Serikali katika mwaka 2012, ilianzisha Mfuko wa Watu wenye Ulemavu, kwa kuanzia na jumla ya TZS Milioni 167 kwa lengo la kuwawezesha katika shughuli zao mbali mbali.

Mheshimiwa Spika,
Umuhimu wa utawala bora umeelezwa kwa ufasaha na kwa ufupi mno na Professor na Mwanasaikolojia,Bwana Amit Abraham pale aliposema,  There should be only one political ideology and that is good governance,”  kwa maana ya kuwa, inapaswa pawe na itikadi moja tu ya kisiasa, ambayo  ni utawala bora. Katika kuhakikisha kuwepo kwa Utawala Bora, Serikali ilianzisha Taasisi mbali mbali za kuusimamia mfumo huo.

Katika kupambana na vitendo  vya rushwa na  ubadhirifu wa mali ya umma, Serikali ya  Mapinduzi ya Awamu ya Saba, imeanzisha Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na  Uhujumu wa  Uchumi Zanzibar (ZAECA) chini ya Sheria  Nambari 1 ya mwaka 2012. Jumla ya tuhuma 950 za vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma zimefikishwa na Taasisi hii tangu ilipoanzishwa. Tuhuma 751 kati ya hizo, bado zinachunguzwa na nyengine zimeshatolewa maamuzi. Vile vile, Mamlaka imefanikiwa kuokoa na kurejesha Serikalini fedha na mali zenye thamani ya TZS milioni 411.90 tangu kuanzishwa kwake.

Kadhalika, Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilianzishwa kwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Nam 8 ya 2015. Waheshimiwa Wajumbe, suala la maadili ni muhimu kwa sisi viongozi tuzingatie maadili na kuwa wakweli, ili tujenge imani kwa wananchi tunaowaongoza na tujiamini sisi wenyewe tunapoikabili jamii kwa masuala mbali mbali.

Tunapokuwa na tabia zisizopendekeza kwenye jamii, huwa tunakosa kujiamini na mara nyingi huishi katika maisha ya wasi wasi.  Kipo kisa cha bwana mmoja hakuwa na maadili bora huku akifuga kasuku.

Bwana huyu, alikuwa na tabia zisizopendeza kwa jamii huku akifuga kasuku.  Siku moja alipofika nyumbani alimkuta kasuku wake hayupo, bila ya kujua kama katoroka au kaibiwa.  Kwa hivyo, kwa kuwa yule bwana hakuwa na tabia nzuri, alitoka mbio kwenda kuripoti tukio hilo moja katika kitengo cha usalama, ingawa alipaswa kuanza kuripoti tukio hilo katika kituo cha polisi cha kawaida.  Kufika kituoni akaanza kusema huku anatetemeka. “My talking parrot has disappeared” . Kwa maana ya kwamba, kasuku wangu ambae anazungumza ametoweka.

Askari wa kitengo cha usalama wakashangaa na baadae wakamuuliza na kumueleza: “Why have you come here? Go to the regular police”.  Kwa nini umekimbilia huku, nenda karipoti kituo cha polisi cha kawaida!.

Yule jamaa, kutokana na wasi wasi aliokuwa nao kutokana na tabia na vitendo visivyopendeza alivyokuwa akivifanya kisiri siri, akaanza kujishtaki na kujitetea kabla hajaulizwa lolote kuhusu tabia zake na mambo aliyokuwa akiyafanya kwa kusema; “I will, I’m just here to you that I disagree with whatever that parrot is going to say”.  Kwa maana kwamba, nitakwenda, lakini nimeona kwanza nije hapa, kitengo cha usalama, kukwambieni kwamba mimi sikubaliana na hata jambo moja ambalo kasuku wangu atakwambieni au kusema.

Mkasa huu unatufundisha kwamba unapokuwa na tabia zisizo za kupendeza katika jamii, unakosa kujiamini, na unakuwa unaishi maisha ya wasi wasi kwa kila jambo unalohisi linaweza kuifanya jamii kujuwa tabia na mwenendo wako.  Mtu kama huyu akiwa kiongozi ni hatari kwa jamii na watu anaowaongoza.  Viongozi wenzangu lazima tuwe na tabia njema na tuendelee kushikamana na maadili ya kazi na katika jamii tunazoishi.

Taasisi hizi ni muhimu katika kuimarisha maadili ya viongozi na kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma.  Sote tunatekeleza vizuri, matakwa ya sheria ya maadili ya Viongozi wa Umma.  Tuendelee kutimiza wajibu wetu na tujipambe na sifa za uongozi bora unaofuata maadili.

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) imeanzishwa kwa Sheria Namba 2 ya mwaka 2010. Serikali imeimarisha mfumo wa haki jinai kwa kuiwezesha ofisi hio kusimamia utaratibu wa upelelezi na utaratibu maalum wa uendeshaji wa kesi za udhalilishaji pamoja na dawa za kulevya. Hali hii imepelekea kupunguza kwa kiasi kikubwa mrundikano wa kesi mahkamani.  Ofisi hii, inasimamia kituo cha Mafunzo ya Sheria na Utafiti ambapo jumla ya washiriki 513 wamehitimu katika kituo hicho. Natoa pongezi kwa Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kupitisha Sheria zenye kuimarisha Utawala bora.

Kadhalika, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, katika kipindi hiki cha miaka kumi imeimarishwa na kujengewa mazingira ya kuiwezesha kufanya kazi zake kwa uhuru zaidi.  Ripoti za uchunguzi na ukaguzi wa hesabu za Serikali zinawasilishwa katika Baraza la Wawakilishi kwa wakati kwa mujibu wa ibara ya 112(5) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984.  Kadhalika, wafanyakazi wa Ofisi hio wameendelezwa kwa kupatiwa mafunzo ya kazi zao ikiwemo mafunzo ya ukaguzi yakinifu na ukaguzi wa kiuchunguzi (forensic audit).

Kwa kipindi kirefu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ilikuwa ikifanya kazi zake kwa kuzingatia masharti ya Katiba na yaliyomo katika sheria mbali mbali.  Mnamo mwaka 2013, Serikali ilianzisha rasmi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kisheria, kwa Sheria Namba 6 ya mwaka 2013.  Ofisi  hii imetekeleza vyema majukumu yake ikiwemo kuzisimamia kesi za Serikali, kuandaa Miswada ya Sheria na kutoa ushauri wa kisheria kwa Wizara na Taasisi mbali mbali za Serikali.

Mheshimiwa Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, ilianzisha Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa Sheria Namba 7 ya 2014 na Tawala za Mikoa kwa Sheria Namba 8 ya 2014.  Kufuatia kutungwa sheria mbili hizo, shughuli zote zinazohusiana na elimu ya msingi, afya ya msingi (huduma zote za afya katika vituo na wafanyakazi wake) na shughuli zote za kilimo za ugani zimehamishiwa katika Halmashauri za Wilaya ya Unguja na Pemba.

Baada ya kugatuliwa, Wizara hizi tatu, masuala ya  Uongozi, Utawala na Matumizi yamehamishiwa sasa katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ.  Kuhusu Idara Maalum za SMZ, katika kipindi hiki, Idara hii imeimarishwa ambapo maslahi ya Makamanda na Wapiganaji wote yameimarishwa, baadhi ya majengo ya makaazi yao yamejengwa upya na mengine yamekarabatiwa kwenye Idara Maalum zake zote (KMKM), JKU, Valantia, Zimamoto na Jeshi la Uokozi pamoja na Chuo cha Mafunzo.

Katika kipindi hiki cha miaka kumi, Serikali imeanzisha mradi wa mji salama, unaosimamiwa na Idara Maalum za SMZ ambao ulizinduliwa tarehe 3 Oktoba, 2018.  Awamu hii ilihusisha ufungaji wa camera za uangalizi (CCTV) katika maeneo mbali mbali ya mji wa Unguja.  Sehemu ya pili ya mradi huo, ulihusisha uokozi na uzamiaji wakati wa majanga ya baharini na ulizinduliwa rasmi tarehe 2 Januari, 2019.  Miradi yote miwili hivi sasa, inaendelea vizuri sana.  Na kwa upande wa Pemba, ujenzi wa mradi wa CCTV umeanza kutekelezwa hivi karibuni katika mji wa Chake Chake.

Ili kuleta ufanisi wa kuundeleza mji wa Zanzibar, jiji la Zanzibar (Zanzibar City) limeanzishwa rasmi na umeandaliwa Manispaa zake tatu; ya Mjini, ya Magharibi “A” na Magharibi “B”.  Manispaa hizi na zile za Pemba, zote zina uongozi wake kamili.

Mheshimiwa Spika,
Kwa upande wa muhimili wa Mahkama, juhudi kubwa zimefanywa katika kuimarisha utendaji wa muhimili huo. Tumeimarisha maslahi ya watumishi na kuongeza idadi ya Majaji, Mahakimu na Makadhi. Vile vile, tumeyafanyia matengenezo majengo na Ofisi za mahkama .pamoja na kuyapatia vitendea kazi. Idadi ya Majaji imeongezwa kutoka wanne mwaka 2010 hadi wanane hivi sasa, ambapo watatu kati yao ni wanawake. Idadi ya Mahakimu imefikia 65 kutoka 13 mwaka 2010 na Makadhi ni 14.  Ongezeko la Majaji na Mahakimu, limesaidia sana katika kuzidisha kasi ya  kusikiliza kesi na kurahisisha utoaji  wa haki kwa wananchi.  Serikali imeanza hatua ya ujenzi wa jengo la kisasa la Mahkama Kuu lenye thamani ya TZS Bilioni 16 huko Tunguu, ili kukidhi mahitaji ya nafasi ya  Mahkama Kuu ya Zanzibar. 

Katika kipindi hiki, Sheria Namba 13 ya  Mwaka 2019 ya kuanzishwa kwa Skuli ya Sheria imeanzishwa pamoja na Sheria mpya ya Mawakili Namba 2 ya 2020, imetungwa kwa ajili ya kuweka utaratibu mzuri wa Mawakili Zanzibar. 

Kuhusu kudumisha Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 nnafuraha kwamba wananchi wanaendelea kunufaika na matunda yake kwa kuwa huru tukiwa na mihimili mitatu yenye uwezo kamili ambayo ni Mamlaka ya Utendaji, Baraza la Wawakilishi na Mahakama.  Kadhalika, wananchi wa Zanzibar wanaendelea kufurahia uhusu wa kufanya maamuzi mbali mbali yanayohusu masuala yao ya maendeleo, kiuchumi, kisiasa na kijamii pamoja na kupata huduma za kijamii zikiwemo elimu, afya, maji safi na salama kwa misingi ya usawa.  Hayo ndiyo matunda ya Mapinduzi ambapo Waasisi wetu walijitolea kuyapigania na kuyajengea misingi imara kwa manufaa ya watu wote.  Kwa hivyo ni wajibu wetu sote tuendelee kuyadumisha.

Mheshimiwa Spika,
Suala la kulinda na kudumisha Muungano wetu wa Serikali mbili, kwangu halina mbadala. Nitaendelea na juhudi za kudumisha Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar wa Serikali mbili, ulioasisiwa mwaka 1964 na Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ambao unatimiza Miaka 56 ifikapo tarehe 26 Aprili 2020.

Waheshimiwa Wajumbe, tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba Serikali zetu mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaendelea kuimarisha mashirikiano na kufanya kazi kwa umoja na ukaribu zaidi katika kupanga na kuitekeleza mikakati ya uchumi na mipango mengine ya maendeleo.  Nitaendelea kuhakikisha kwamba tunaimarisha mashirikiano, udugu na mapenzi baina ya watu wa pande mbili hizi.  Nitaendelea kushirikiana na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kudumisha hali ya amani na utulivu, iliyodumu tangu kuundwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 26 Aprili, 1964.

Mheshimiwa Spika,
Kama mnavyofahamu kwamba Tume ya Uchaguzi ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar hivi sasa zinaendelea na matayarisho ya Uchaguzi Mkuu, utakaofanyika hapo baadae mwezi wa Oktoba.  Kwa hivyo, ni imani yangu kwamba wananchi ambao wametimiza masharti na vigezo vya Tume kwa ajili ya mpiga kura, wamejiandikisha na kuhakiki majina yao katika daftari la kudumu la mpiga kura, ili waweze kuitumia haki yao ya kidemokrasia ya kupiga kura, kwa kuwachagua viongozi wanaowataka, wakati wa kufanya hivyo utakapofika.

Mheshimiwa Spika,
Kwa mara nyengine tena natoa shukurani zangu za dhati kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Tisa kwa kuendelea kuweka misingi ya Utawala Bora na Demokrasia.  Ni dhahiri kuwa baada ya Uchaguzi Mkuu nitakamilisha kipindi changu cha Pili cha Urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.   Si haba nimeitumikia nchi yangu.  Sitaongeza hata nukta moja. Panapo uhai na majaaliwa, nitamkabidhi Rais aje kama mie nilivyokabidhiwa.  Matumaini yangu makubwa sana kwamba nitamkabidhi mwana CCM mwenzangu.  Nasema hivyo kwa ushahidi, sisemi tu. Hii ni kutokana na utekelezaji huu wa Ilani tulioufanya katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.  

Juzi tumemsikia Rais Magufuli mafanikio aliyoyaeleza kwa miaka mitano pekee na haya ni ya miaka kumi.  Chama gani kitafanya kama CCM? Atakaepinga mwambieni hayo niliyoyasema mimi. Kwanza hakuna chama kilichofanya haya.  Pili, hakitatokea.  Katika kipindi hiki tumefanya kwa ari na kasi kubwa tukijiamini katika Serikali hii ya Awamu ya Saba.  Walidhani wananiacha Awamu ya Saba sehemu ya pili ningeshindwa. Mawe! Wameniacha uporo nipo nadunda naiongoza Zanzibar. Kwa hakika mmeweza kuutekeleza wajibu wenu wa kikatiba wa kutunga sheria na kuisimamia Serikali kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 5A(1) na kufafanuliwa katika kifungu 5A(2) cha Katiba ya Zanzibar ya 1984.

Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi cha miaka kumi, mmetekeleza majukumu yenu kwa kufanya mikutano yenu katika hali ya salama na utulivu,  mmeyajadili  masuala muhimu na mmeweza kuipitisha miswada ya sheria 128 na baadae iliwasilishwa kwa Rais kwa ajili ya kutiwa saini na sasa imekuwa sheria kamili za Zanzibar.

Takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi hiki cha miaka kumi, maswali 3,468 ya msingi na maswali ya nyongeza 4,894 yameulizwa kwa Serikali na yalipata majibu sahihi.  Kadhalika, Kamati za Baraza nazo zilitekeleza majukumu yake kwa uadilifu na umakini mkubwa.  Nawapongeza wajumbe wote wa Kamati hizo kwa kufuatilia na kuibua masuali juu ya mambo mbali mbali, kuyaleta Barazani kwa kujadiliwa na baadae kuishauri Serikali juu ya mambo yaliyojitokeza.  Kadhalika, nalipongeza Baraza kwa kupokea na kujadili hoja binafsi mbali mbali zilizowasilishwa.

Leo ni siku ya furaha kwa upande mmoja na ni siku ya huzuni kwa upande mwengine.  Nnasema hivi kwa sababu tutalivunja Baraza hili kwa mbwembwe na madaha kutokana na mafanikio makubwa tuliyoyapata  katika kujenga nchi yetu.  Lakini leo ni siku ya huzuni kwa sababu tunaagana na baadae nitalivunja rasmi Baraza la Tisa na kwa hivyo, huenda ikapita kipindi bila ya baadhi yenu kuonana, ingawa tunategemeana kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Spika,
Kwa wale wenye dhamira ya kurejea majimboni, kwa ajili ya kutafuta ridhaa ya wananchi kwa mara nyengine, nawatakia kila la kheri na mafanikio, ili warudi tena kwa miaka mitano mingine.  Kwa wale ambao wamefikia uamuzi wa kutogombea tena, nawanasihi sana waendelee kutumia maarifa na uzoefu walioupata katika Baraza hili, katika kuongoza, kuhamasisha na kushiriki kikamilifu katika harakati za nchi yetu.  Naamini ndani ya nafsi yangu kuwa yote mtakuwa hazina kubwa katika kupanga na kuitekeleza mipango ya nchi hii.

Hata hivyo, kwa wale mtakaojaaliwa kuchaguliwa tena na wananchi na kurudi Barazani, nakunasihini na nakukumbusheni kuwa mnapokuwa kwenye Baraza hili muendelee kuilinda, kutii na kuitetea kwa vitendo Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, sheria ziliopo na kanuni za Baraza hili. 

Mheshimiwa Spika,
Baraza la Wawakilishi ni Muhimili uliowekwa ndani ya Katiba.  Hiki ni chombo kikubwa, hakiendeshwi kwa ukaidi wala kwa ubabe na njia yoyote inayolingana na haya mawili niliyoyaeleza.  Baraza hili ni chombo cha wananchi wa Zanzibar, kwa hivyo, suala lolote lenye maslahi na wananchi, hapa ndipo pahala pa kisheria pakulizungumza jambo hilo.
Waheshimiwa wajumbe nyinyi ndio mnaotunga sheria za nchi, kwa hivyo, nnakunasihini sana mlizingatie jambo hili, kwamba kila sheria iliyotungwa na Baraza hili, matumizi yake yapo wazi kwa kupitia Taasisi iliyowekwa.  Vile vile, nataka mzingatie maadili ya Chama cha Mapinduzi na taratibu zake kwani nyinyi ni wanachama wa CCM; kwani mmeupata uwakilishi kwa tiketi ya CCM na hamkua wagombea binafsi.  Zingatieni sana “Three Whip Sytem”  iliyopo inafanya kazi vipi.  “Whip” ni kiboko, kwa hivyo vipo viboko vitatu.  Nyinyi mkiwa wagombea mliofaulu kuchukua majimbo ya CCM ni lazima mnajua.  Mligombea kuja Barazani kwa tiketi ya CCM na nyote nilikushikeni mkono, Wabunge na Wawakilishi wa CCM.  Leo wengine mnaniachia peke yangu.  Nataka niwe mwazi kabisa.  Mengine mnayosema nyinyi mimi sisemi na mengine mnayosema hayasemwi lakini nyinyi mnayasema.  Nasema tena msijisahau  mkiwa barazani. Mna chama chenu kilichokuleteni, kwa hivyo msifikiche pahala mkakilazimisha chama kukushughulikieni.

Mheshimiwa Spika,
Siri kubwa ya mafanikio yetu katika sekta za maendeleo nilizozielezea ni kuendelea kuwepo na kuimarika kwa hali ya amani na utulivu.  Ndio maana katika hotuba yangu ya leo nilianza kwa kulizungumzia suala hili kabla ya kuzielezea sekta nyengine.  Kwa hivyo, kwa mara nyengine tena nataka nisisitize tena umuhimu wa amani, umoja, utulivu na mshikamano kwamba si suala la Idara Maalum za SMZ na Vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama vya SMT peke yao, lakini linatushirikisha wananchi sote kwa jumla wa Tanzania na Zanzibar.  Katika kipindi chote cha miaka kumi cha uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama vimetekeleza vyema majukumu yao kwa umahiri mkubwa na utulivu.  Natumia fursa hii kuwapongeza sana kwa utekelezaji mzuri wa dhamana zao hizo walizopewa na Taifa.

Mheshimiwa Spika,
Nimefarajika sana kwa mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wangu nikisaidiana na viongozi wenzangu mbali mbali.  Hata hivyo, katika kipindi hiki tulikabiliwa na changamoto mbali mbali.  Baadhi ya changamoto hizo, zipo ambazo tulianza kuzitatua,  lakini hazikumalizika, zipo nyengine tulizifikisha hatua kubwa, lakini zipo nyengine ufumbuzi wake ni mgumu.   Changamoto hizo, sote tunazifahamu lakini nitazitaja kwa ujumla wake.  Kwanza, ni tatizo la ajira kwa vijana.  Pili, ni tatizo la upungufu wa mchanga hapa Zanzibar. Tatu, ni tatizo la udhalilishaji wa wanawake na watoto.  Nne, ni tatizo la uharibifu wa mazingira na  mabadiliko ya tabianchi na Tano, ni tatizo la janga la COVID-19. 

Nataka niizungumzie kwa ufupi changamoto iliyotukumba hivi karibuni, nayo ni kuzuka kwa maradhi ya homa ya mapafu yanayosababishwa na virusi vya “Corona”.  Tatizo la COVID-19.  Maradhi haya yalipoingia Tanzania mwishoni mwa mwezi wa Machi, yametuletea madhara ya afya zetu na changamoto za kiuchumi.  Madhara ya afya ya  “Corona”  tumeyashuhudia na sasa yanajulikana vizuri na tutaendelea kuyafanyia kazi.  Kuhusu madhara ya uchumi ya COVID-19, kayaelezea vizuri Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa, aliyoyaelezea  katika hotuba yake ya Bajeti ya Serikali.  Serikali zetu mbili tulishirikiana sana na tulijidhatiti kupambana nayo kwa moyo mkubwa na kwa uwezo wetu wote.  Pamoja na upya wa COVID-19, hatukuyaogopa na wala hakutokea kiongozi hata mmoja wa Serikali aliyekimbia kutekeleza wajibu wake. Hongereni sana. 

Tuliandaa mipango yetu madhubuti na tuliwaongoza wananchi kujikinga dhidi ya COVID-19.  Mipango na maelekezo ya Serikali, mipango na maelekezo ya madaktari na wataalamu wetu wengine wa afya, imani za wananchi kwa Serikali zao yalikuwa na hamasa ya hali ya juu katika kupambana na “Corona”.  Mambo yote hayo tuliyafanya kwa uhakika, kwa kujiamini na kwa uwezo mkubwa sana.  Tuliamua wenyewe, tuliongozwa na nia thabit na uzalendo mkubwa.  Hatukuwa tayari kuiga wala kuogopa.  Hatua tulizozichukua zilikuwa sahihi ambazo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ilitangaza mambo kumi hapo tarehe 29 Machi, 2020  katika kulishughulikia tatizo la COVID-19.  Kila mmoja wetu aliendelea kutekeleza wajibu wake na kazi hazikusitishwa, ziliendelea kufanywa kila pahala, pamoja na miradi yote ya maendeleo.  Tarehe 23 Mei, 2020 nilipotoa hotuba yangu ya Sikukuu ya Idd el Fitr, nilielezea uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kuregeza masharti yaliyowekwa dhidi ya “Corona” hatua kwa hatua, kutokana na hali ya ugonjwa itakavyokuwa.

Hali ilivyo sasa ni shwari kuliko ilivyokuwa mwezi wa Aprili, Mei na mwanzo wa wiki ya Juni.  Kwa upande wetu, Unguja na Pemba hadi tarehe 10 Juni vituo vyetu vyote vilivyokuwa vikiwatibu wagonjwa wa COVID-19, havina hata mgonjwa mmoja; leo ni siku 10 zimepita tangu alipotoka mgonjwa wa mwisho.  Kwa hivyo, hali yetu imekuwa bora zaidi, nami nawatangazia wananchi kwamba tutazifungua skuli za Unguja na Pemba za Maandalizi, Msingi na Sekondari kuanzia Jumatatu, tarehe 29 Juni, 2020.  Kutokana na mazingira ya madrasa, skuli za Maandalizi na Msingi za Zanzibar yalivyo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali iandae mpango madhubuti na kabambe wa namna bora zaidi kwa wanafunzi watakapokwenda masomoni.

Boti na meli zinazofanya safari, baina Unguja na Dar es Salaam, Unguja na Pemba, Pemba na Tanga, kuanzia tarehe 29 Juni, 2020 zitaruhusiwa kuchukua abiria kwa mujibu wa idadi ya viti vya vyombo hivyo, vilivyosajiliwa.  Abiria hawatoruhusiwa kusimama au kukaa popote.  Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Mamlaka ya Usafiri wa Baharini na Shirika la Bandari watapaswa wausimamie utekelezaji wa maagizo haya. Manahodha na uongozi wa vyombo hivyo watapaswa wawajibike, endapo watayakiuka maelekezo haya ya Serikali.  Vile vile, shughuli za jamii nazo ruhusa zifanyike isipokuwa ni lazima zichukuliwe tahadhari zote za kinga kama tunavyoelekezwa na wataalamu.  Tusifanye dharau, kwani COVID-19 haijamalizika kabisa.

Siku kumi hizi hazitoshi kuamini kwamba maradhi haya yamemalizika kabisa, lazima tuendelee kuchukua tahadhari.  Wizara ya Afya, Idara ya Kinga wahakikishe tahadhari zote zinachukuliwa bila ya kuwasumbua na kuwazuia watu.  Ni wajibu waendelee kuwaelimisha wananchi.  ZBC TV na Redio pamoja na magazeti ya Zanzibar Leo endeleeni kuwaelimisha watu juu ya maradhi haya.  Hatutarajii hali hii ya “Corona” ije kurejea tena.  Hata hivyo, vilabu vya michezo yote visubiri, tukiacha michezo ya ligi kuu ya mpira wa miguu.

Mheshimiwa Spika,
Kadhalika, nawapa pole wale wote walioathirika na maafa ya kipindi cha mvua kubwa za masika zilizonyesha hivi karibuni, ambazo zinasemekana ziliungana na mvua za Vuli, pamoja na upepo mkali; ambazo zilipelekea watu watano kupoteza maisha na wengine kupoteza mali na uharibifu mkubwa wa nyumba na mazingira. Nawapa pole wananchi wenzetu walioathirika afya zao kwa kuambukizwa virusi vya “Corona”.  Maradhi yaliwasibu, hali zao zilikuwa dhaifu, lakini, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, jitihada za Serikali yetu, madaktari na wataalamu wa afya, ndugu zetu hawa wamepata nafuu na wamepona. 

Nawapa pole wananchi wenzetu ambao wamewapoteza ndugu, jamaa na marafiki kutokana na maradhi ya COVID-19 yanayosababishwa na virusi vya CORONA ambayo yameingia katika nchi yetu kama yalivyozikumba nchi nyengine duniani.  Natoa shukurani kwa wananchi wote kwa kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na mitihani yote hii.  Vile vile, natoa shukurani kwa Taasisi mbali mbali na wale wote walioungana na Serikali katika kuwafariji kwa kutoa misaada mbali mbali kwa familia zilizofikwa na maafa.  Natoa wito kwa wananchi wote tuendelee kuwa na subira, tuwe wamoja na tuzidi kushirikiana katika kuikabili mitihani mbali mbali inayotokea hapa nchini.

Nachukua nafasi hii kutoa pongezi zangu za dhati kwa madaktari, wauguzi na watendaji wote wa sekta ya afya, kwa juhudi walizoonesha katika mapambano hayo. Kwa mara nyengine, natoa pongezi zangu za dhati kwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Kupambana na Maafa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, ambaye ni Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, pamoja  na wajumbe wote, na  Mwenyekiti wa  Kamati ya Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania, ya Kupambana na Maradhi haya ya COVID 19, Mheshimiwa Kassim Majaaliwa Majaaliwa, ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; pamoja na wajumbe wote, kwa kufanya kazi nzuri, kwa ushirikiano  na uzalendo wa hali ya juu; mambo ambayo yametoa  matokeo mazuri.

Vile vile,  kwa mara nyingine  shukurani zangu ziende  kwa  viongozi wa dini, vyombo vya habari, vyombo vya ulinzi na usalama, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, masheha, viongozi wa ngazi mbali mbali, wasanii, wamiliki na madereva wa vyombo vya usafiri, wafanyabiashara, wakulima, wavuvi,  na wananchi wote, kwa kila mmoja kutekeleza jukumu lake ipasavyo kwa uzalendo na uadilfu.

Kwa pamoja, tunaendelea kuyatekeleza yale mambo kumi (10) yaliyotangazwa na Serikali tarehe tarehe 19 Machi, 2020. Serikali itaendelea kuregeza masharti na kutoa miongozo mipya kwa kutegemea hali ya maradhi hayo ilivyo.  Serikali zetu zote mbili zitaendelea kuchukua uamuzi  kwa kuzingatia uwezo na maisha halisi ya wananchi, bila ya kutaka kuiga maamuzi na mipango ya nchi, taasisi au watu wengine.

Tuongeze nguvu katika kufuata miongozo inayotolewa na Serikali huku  tukiwa na subira. Tuendelee kumuomba na tumshukuru Mwenyezi Mungu, atuvue na janga hili na majanga mengine. Kwa uwezo wake Yeye, atatunusuru  na atatuvusha kwa salama hapa tulipo, ili maisha yetu yarejee katika hali ya kawaida na iliyo bora zaidi.

Mheshimiwa Spika,
Leo tunaagana, lakini itakuwa kwa kheri ya kuonana.  Tutaendelea kuonana, kwani tuna kazi kubwa iliyotukabili sote ambayo ni kushiriki kwenye uchaguzi kwa kupiga kura.  Kwa hivyo, ni vyema tukahakikisha kwamba kila mwenye sifa na haki ya kushiriki katika uchaguzi, anafanya hivyo, akielewa kuwa kufanya hivyo ni msingi muhimu wa utawala bora na demokrasia.

Ni wajibu wetu tuiheshimu kazi, majukumu ya Tume zetu za Uchaguzi NEC na ZEC, vyombo ambavyo vimeundwa kikatiba.  Serikali imetunga Sheria ya Uchaguzi Namba 4 ya mwaka 2018.  Sheria hii imelenga kuweka utaratibu bora wa uchaguzi na kuondoa kasoro zote zilizojitokeza katika chaguzi zilizopita.  Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar itafanya kazi nzuri na kila mmoja atapata haki yake.  Kuchukua uamuzi kinyume na utaratibu uliowekwa na sheria, itakuwa kusababisha zogo na kuanzisha fujo.  Zogo na fujo ndio chanzo cha watu kugombana na hatimae kuingiyana maungoni.  Hayo si madhumuni ya uchaguzi.  Kwa hivyo, uchaguzi wa Oktoba mwaka huu utakuwa huru na haki.  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, itaendelea kuhakikisha kwamba hali ya amani na utulivu iliyopo nchini hivi sasa itaendelea kudumu.  Wale wenye nia au mawazo ya kutaka kuuharibu uchaguzi kwa njia yoyote au kufanya fujo, jambo hilo halitawezekana kwenye uchaguzi wa mwaka huu.  Nawathibitishia wananchi, sheria ya uchaguzi ipo, katiba ipo, fedha zetu wenyewe za kuendesha uchaguzi zipo, vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama vipo.  Nawatangazia leo mimi na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli tupo macho, hatutasinzia, tutatekeleza wajibu wetu.  Watakaofanya vituko dhidi ya sheria tutawashughulikia.

Nawatakia kheri wale Waheshimiwa wote ambao kwa sababu mbali mbali hawatokuwepo katika Baraza lijalo baada ya Uchaguzi wa Oktoba, 2020.  Wale wanaoomba kurejea pamoja na wengine ambao sasa si wajumbe nawanasihi wazingatie kuitunza amani na utulivu katika harakati za uchaguzi.  Huu ni wakati wetu sote tudhihirishe ustaarabu katika siasa zetu, umoja wetu, mshikamano na utiifu wa sheria.  Kuitunza amani ni dhamiri yetu sote.

Mheshimiwa Spika,
Kwa mara nyengine tena nnakushukuru kwa dhati Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, kwa kuliongoza Baraza la Wawakilishi kwa busara, haki, uadilifu na ufanisi mkubwa.  Umefanya kazi kubwa ya kuliendesha Baraza hili na umetoa mchango mkubwa katika kukuza demokrasia na utawala bora.  Nakutakia kila la kheri katika maisha yako. Lakini nakushukuru wewe na wajumbe wote kwa kupitisha azimio la kunipongeza.  Ahsanteni sana.  Lakini sifa hii tunastahiki sote.

Nampongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na namna tunavyoendelea kushirikiana; anavyokiongoza Chama chetu, Chama cha Mapinduzi na jitihada zake katika kuuendeleza na kuuimarisha Muungano wetu.  Vile vile, natoa shukurani kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Kassim Majaaliwa Majaaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana nami nikiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na kwa juhudi zao za kuuimarisha Muungano wetu.  Vile vile, namshukuru Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana nami katika shughuli mbali mbali za Chama na Serikali.

Kadhalika, nampongeza na namshukuru Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kazi kubwa anayoifanya katika kunisaidia kuiongoza Zanzibar. Tumefanya mambo mengi sana makubwa.  Wakati mwengine huwa nashangaa anafanikiwa vipi.  Namwagiza afanye mambo wakati mwengine najua namsumbua lakini ndiyo kazi yenyewe niliyompa anisaidie.  Hajanambia sifanyi hata siku moja.  Hajanung’unika kwa kazi hata siku moja.  Amekua mtiifu kwangu wakati wote. Nakupongeza wewe Balozi Seif Ali Iddi na Mama Asha Suleiman Iddi.  Hongereni sana.  Nafahamu tuna muda mfupi kabla ya kumaliza.  Tutapongezana zaidi baadae Serikalini.

Mheshimiwa Spika,
Nawapongeza viongozi wastaafu niliofanya kazi nao katika Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwemo Rais Mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi, nimefanya kazi na Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa ambae nimefanya kazi nae kwa miaka minne na nusu, nilipokuwa Makamo wake wa Rais.  Kwa furaha kubwa sana nampongeza Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, tangu yeye akiwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.  Nimefanya kazi nae kwa miaka minne na nusu na baadae akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda wa miaka mitano.  Nilifanya kazi nae nikiwa Makamo wake wa Rais. Tumezoeana na tumeshirikiana vyema katika kuwatumikia wananchi, tumekuwa na udugu na urafiki mkubwa sana.  Kadhalika, nawapongeza na viongozi wengine wa CCM na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania niliofanya nao kazi.

Vile vile, natoa shukurani kwa Mheshimiwa Dk. Salmin Amour, Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Tano ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa kuniteuwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na kisha kuwa Naibu Waziri wa Afya katika mwaka 1995.  Kadhalika, namshukuru Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Sita ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuniteua kuwa Waziri wa Katiba na Utawala Bora mwaka 2000.  Nawashukuru sana viongozi wote wawili kwa kuniamini na kuniteua kushika nyadhifa hizo.  Nawashukuru kwa kushirikiana nami  katika nafasi mbali mbali za uongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi.  Ushirikiano walionipa umetoa mchango mkubwa katika kufanikisha maendeleo ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,
Pongezi zangu za dhati nazitoa kwa Mheshimiwa Jaji Mkuu, Mawaziri  na Manaibu Mawaziri wote. Nampongeza Mheshimiwa Said Hassan Said Mwanasheria Mkuu, huyu ni Mheshimiwa makini sana namuamini kama ninavyoiamini nafsi yangu.  Hongera sana.  Nampongeza Mufti wa Zanzibar na Kadhi Mkuu.  Vile vile, nampongeza kwa dhati Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, ni mfanyakazi aliyebobea katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.  Uwezo wake wote sina shaka nao.  Anaifahamu Serikali kweli kweli.  Amekuwa Katibu Mkuu kwa miaka mingi. Anaiheshimu Serikali na viongozi wake.  Miaka kumi yote amenisaidia sana. Wakati mwengine namuweka macho hadi usiku mkubwa.  Hajawahi kunung’unika hata siku moja.  Nampongeza kwa ustahamilivu wake.  Si mpole tu ndio alivyo ni mpole kwa kufanya kazi.  Dk. Abdulhamid, hongera sana.  Namshukuru Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi kwa kushirikiana nami katika kipindi cha mwanzo cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba.

Nawapongeza Washauri na Wasaidizi wa Rais pamoja na wafanyakazi wote wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na watumishi wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.  Kadhalika, nawapongeza viongozi wote wa Serikali, Viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani, viliomo Barazani; TADEA, ADC, Chama cha Wakulima na wengine wanaoiunga mkono Serikali hii, ambao hawapo Barazani.  Nawashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kunichagua kwa kura za ushindi na kuwa Rais wa Zanzibar na kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba.  Shukrani maalum nazitoa kwa uongozi wa CCM na wana CCM wote kwa kunipa heshima kubwa ya kuniteua nikagombea Urais wa Zanzibar.  Hili ni deni kubwa kwangu na katika familia yangu.  Sina namna ya kuelezea shukrani zangu na pongezi, nasema Ahsanteni sana wana CCM na viongozi wote.

Kadhalika, nampongeza na namshukuru Mama Mwanamwema Shein, mke wangu kwa kunisaidia, kuniunga mkono, kunistahamilia na kunivumilia wakati wote katika maisha yetu na nikiwa katika utumishi wa Serikali ya Mapinduzi na Serikali ya Muungano wa Tanzania.  Vile vile naipongeza familia yangu yote, ndugu, jamaa na marafiki zangu katika siku hii muhimu kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,
Ili kutoa nafasi kwa matayarisho ya mwisho kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka 2020, kwa madaraka niliyonayo kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 91(2)(a) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, natamka kwamba tarehe ya kuvunjwa kwa Baraza la Tisa la Wawakilishi la Zanzibar itatangazwa kwenye Gazeti Rasmi la Serikali hapo baadae.


Nakutakieni kila la kheri.

MUNGU IBARIKI ZANZIBAR
MUNGU IBARIKI  TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRIKA

Ahsanteni kwa kunisikiliza.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.