Habari za Punde

KIKAO CHA KUSIKILIZA CHANGAMOTO MBALIMBALI ZA WAKUNGA NA WAUGUZI.

Waziri wa Afya wa  Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akitoa nasaha kwa wauguzi na wakunga wa ngazi ya  Uzamili katika kikao cha kusikiliza changamoto mbali mbali za wauguzi na wakunga  kilichofanyika Ukumbi wa Bohari  ya dawa  Mnazi Mmoja Zanzibar.
Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Zanzibar Dk.  Amina Abdulkadir akiwasisitiza Wauguzi na Wakunga kutimiza wajibu wao wa kazi ili waweze kuikuza Taaluma hiyo katika  Ukumbi wa Bohari  ya dawa  Mnazi Mmoja Zanzibar.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wauguzi Zanzibar Valeria Rashid Haroub akichangia mada katika kikao cha kusikiliza changamoto mbalimbali za Wakunga na Wauguzi kilichofanyika Ukumbi wa Bohari  ya dawa  Mnazi Mmoja Zanzibar.
Picha na Fauzia  Mussa - MAELEZO

Na Miza Kona Maelezo Zanzibar        22/06/2020
Waziri wa Afya Zanzibar Mhe Hamad Rashid Mohamed amewataka Wauguzi na Wakunga kutekeleza vyema majukumu yao kwa jamii ili kutoa huduma bora nchini.
Waziri Hamad ameyasema hayo Hospitali ya Mnazi Mmoja wakati akizungumza na Wauguzi na Wakunga wa ngazi ya Uzamili, amesema wauguzi wa ngazi hiyo wanajukumu kubwa la kusimamia na kutoa huduma ipasavyo kwa jamii kwa lengo la kuimarisha huduma afya nchini.
Amesema wauguzi na wakunga wana malipo mazuri kwa Mwenyezi Mungu iwapo watatekeleza vyema majukumu yao katika kutoa huduma kwa uadilifu na upendo kutokana na ugumu na uzito wa kazi hiyo.
“Kazi mnayoifanya nyinyi hapa mnamwabudu Mungu kwani mna kazi kubwa, ngumu na nzito sana ni kazi ya ibada na malipo yake mtayapata kwa Mwenyezi Mungu lakini nawasisitiza kutekeleza vyema majukumu yenu”, alieleza Waziri Hamad.
Waziri Hamadi amefahamisha kuwa serikali tayari imeshaanda maslahi mazuri (schem of service) kwa wafanyakazi wote wa Wizara ya Afya kwa lengo la kuwainua wafanyakazi wake ili kufanyakazi kwa ufanisi na kuimarisha sekta hiyo.   
Hata hivyo Waziri huyo ameliomba Baraza la Wakungaa na Wauguzi kusimamia vyuo vyote vinavyotoa mafunzo ya Afya vya serikali na binafsi kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaojiunga na elimu inayotolewa katika vyuo hivyo inakidhi kiwango kinachotakiwa.
Nae Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Dk Amina Abdukadir amewataka wauguzi haokufanyakazi kwa pamoja na kutumia vyema dhamana zao ili kuweza kukuza na kuinyanyua kada hiyo na kufanyakazi kwa ufanisi.
Aidha Dk Amina ameeleza kuwa Baraza lake litaendelea kuwasomesha wauguzi na wakunga ili kuhakikisha kwamba nafasi zote zinanyanyuka kielimu na kufanyakazi kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa jamii.
Mwenyekiti huyo amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa juhudi kubwa anayoifanya katika kuimarisha sekta ya Afya na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mapema Mkurugenzi wa Wauguzi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja Haji Nyonje Pandu amesema mashirikiano na mikakati  ya pamoja baina ya Baraza la Wauguzi na Wakunga, Watendaji pamoja na wafanyakazi yatasaidia kufanyakazi kwa uadilifu na ufanisi katika kada hiyo ya ukunga na uuguzi nchini.
Nao Waguzi na wakunga hao wamesema changamoto zinawakabili ni pamoja na uhaba wa vitendea kazi, kupatiwa miongozo ya kazi zao pamoja na kuongozewa maslahi kutokana na ugumu wa kazi hiyo.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.