Mwashungi Tahir Maelezo 5/6/2020
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imewakumbusha wananchi wajibu wao katika kutunza na kuhifadhi Mazingira kwani ustawi wa viumbe hai ikiwemo binadamu unategemea mazingira mazuri.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Mathew Pauwa Mhina Mwaimu katika maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani, imeeleza kuwa siku hiyo inatoa fursa kwa wananchi kutafakari juu ya mazingira na kuweka mikakati mizuri ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.
Imesema mazingira safi ni haki muhimu kwa maendeleo ya binaadamu kwa vile inaunganisha uhifadhi wa haki nyengine ikiwemo haki ya kuishi, kumiliki mali , chakula, makaazi , maji safi na salama.
Taarifa ya Mwenyekiti wa THBUB imeeleza kuwa uchafuzi wa mazingira unaathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa haki hizo muhimu kwa maisha ya binadamu.
Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora imeeleza kuthamini juhudi mbali mbali za kisera , kiutawala na kisheria ambazo Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimekuwa zikichukuwa katika kuhifadhi na kutunza Mazingira.
Taarifa hiyo imesema pamoja na jitihada hizo kumekuwa na changamoto mbali mbali ambazo zimekuwa zikiathiri uhifadhi wa mazingira ikiwemo uelewa mdogo wa wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira kwa kukata miti ovyo na ujenzi holela usiofuata mipango miji.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imeiomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Makamo wa Rais Muungano na Mazingira na Wizara inayosimamia Mazingira Zanzibar kushirikisha wadau mbali mbali katika harakati za kuelimisha na kuhamasisha jamii kutunza mazingira.
Aidha Tume imewashauri Watanzania kujiweka mbali na shughuli zinazosababisha uharibifu wa mazingira nchini na kutoa taarifa pale wanapoona jamii ama taasisi inafanya uharibifu wa mazingira.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani mwaka huu ni Tuhifadhi Mazingira Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.
No comments:
Post a Comment