Habari za Punde

Mbio za Uchaguzi wa Rais Zanzibar: Zogo hili lote ni la nini?

Na  Hokeringe M. Lottu

UTANGULIZI

Hivi karibuni kumetokea malalamiko, zogo na kejeli nyingi kuhusu watu wanaochukua fomu kugombea Urais wa Zanzibar. Kuna watu wengi wanalalama na kuhoji kwanini huyu, kwanini yule kachukua fomu. Huyu ni nani? Huyu hafai, huyu ana historia mbaya; basi ilimradi kila mtu anasema lake.

Uhuru wa kuongea ni mmojawapo wa misingi ya demokrasia lakini wanaolalama inaelekea hawaelewi demokrasia yenyewe. Nataka kuelezea hapa dhana ya demokrasia.

1. USULTAN

Ili dhana ya demokrasia ieleweke yafaa kuanza na Ufalme au Usultan. Nitatumia neno "Usultan" kwa  sababu ndilo maarufu sana hapa kwetu. Usultan ni mfumo wa utawala ambao kuna familia moja inahodhi haki ya kutawala. Sultan akiondoka madarakani mwanaye au nduguye anachukua madaraka. Wananchi wengine hawana haki hiyo, haki yao ni kuongozwa tu. 

Mbaya zaidi, hawana namna ya kumwondoa Sultan. Katika sehemu nyingi duniani mfumo wa Usultan ulihalalishwa kwa falsafa danganyifu kuwa Sultan amezaliwa na damu ya kipekee ya kutawala (royal blood). 

Aidha, ilisemwa pia Sultan anapewa madaraka na Mungu; siyo na wananchi. Kama Sultan ni kiongozi mbaya basi wananchi wanaambiwa kuwa wametenda dhambi ndiyo maana Mungu anawaadhibu na itabidi wamvumilie hadi mola wao atakapowaondolea madhila hayo, ama kwa kuchukua uhai wa Sultan au vinginevyo. 

Falsafa ya Usultan hujenga imani kwa umma kuwa wananchi ni watu dhaifu, kazi yao ni kumtii mtawala wao tu; hawana mchango mwingine. Wanaaminishwa kuwa Sultan wao siyo tu ametokea kwenye familia bora bali pia ni mteule wa Mungu. 

Baadaye falsafa hii ikawa haikubaliki. Ni mfumo wa ubaguzi, kuna familia bora zaidi na wengine ni watu dhaifu au raia wa daraja la pili. Changamoto kubwa ya mfumo huu ni kuwa kumbadili kiongozi inabidi mapinduzi yafanyike; damu imwagike. Hakuna namna nyingine kwa sababu hakuna uchaguzi.  

Sehemu nyingi za duniani Usultani uliondolewa kwa upanga. Tukio maarufu ni Mapinduzi ya Ufaransa ambayo yalihitimishwa kwa kwa Sultan (Mfalme) Louis XVI kukatwa kichwa katika Uwanja wa Mapinduzi, Paris,  tarehe 21 Januari 1793.

Mapinduzi ya Ufaransa yalifuatiwa na wimbi la kuondosha Usultani sehemu nyingi Ulaya na kuweka mfumo wa Jamhuri (republicanism). 

Jamhuri kama ilivyo demokrasia ni utawala unaotoa nafasi kwa wananchi wote kuongoza na kuwabadili viongozi wao. 

Mara baada ya mapinduzi ya mwaka 1964, John Okello aliitangaza kuwa Zanzibar imekuwa Jamhuri. Hata hivyo kwa zaidi ya miaka 15 uchaguzi haukufanyika. Huu ulikuwa Usultan wa namna nyingine.

2. UMWINYI

Mfumo wa pili ni utawala wa kitabaka (Aristocracy).  Nitauita mfumo huu "Umwinyi". 

Wakati Usultan ni utawala wa mtu mmoja na familia moja, Umwinyi ni utawala wa tabaka la watu wachache. Umwinyi unajengwa katika msingi kuwa nchi yafaa kuongozwa na watu bora wenye uwezo na uzoefu wa kutawala; siyo kila mtu ana uwezo huo. 

Ili upewe nafasi ya uongozi ni sharti uwe na mali, elimu kiwango fulani, imani fulani, itikadi fulani, uwe umezaliwa kwenye ukoo fulani, nk. Umwinyi unahimiza sana uzoefu wa kutawala. 

Kwenye Umwinyi kuna kuulizana, "baba yako alikuwa nani ati?"  Endapo baba yako alikuwa kiongozi basi una nafasi nzuri. Kama umetokea huko kijijini, huko madongo au makuti kuinama basi wewe sahau. 

Uingereza huwezi kuwa Mbunge katika Bunge la Mamwinyi (House of Lords) isipokuwa tu kama umetoka kwenye ukoo wa wenye mali na ardhi, wachache huteuliwa kuingia humo. Mtoto wa mlalahoi kaa mbali, siyo mahala pako.

 Pia, mtu hawezi kuwa Sultan wa Uingereza (Mfalme au Malkia) isipokuwa tu kama ni Mkiristo wa Dhehebu la Kianglikana. Wengine, hapana. Kama wewe ni Mkatoliki, pisha. 

Aidha, mtu hawezi kuwa kiongozi Uchina isipokuwa tu kama ni mwanachama wa Chama cha Kikomunisti cha Uchina, ni Umwinyi. 

Katiba yetu inasema kuwa mwananchi hawezi kugombea Urais, Ubunge na Udiwani isipokuwa tu kama ni mwanachama wa chama cha siasa. Kama siyo mwanachama na wafanya siasa  hawakujui basi haki ya kiraia inapotea; kaa mbali. Katiba yetu inaendekeza Umwinyi. 

Umwinyi ni mfumo wa ubaguzi ambao huwapa tabaka la watawala haki ya kuwabagua wananchi wengine eti kwa sababu wao wana mali, elimu, wametoka ukoo wa watawala, wana haki kuliko wananchi. 

Mfumo huu huwajengea kiburi wahusika wa tabaka hili na kujiona wao ni bora na wenye haki ya kuhodhi nafasi za uongozi.

3. DEMOKRASIA

Mfumo wa tatu ni demokrasia. 

Ni mfumo ambao mamlaka ya dola yapo mikononi mwa wananchi. 

Mwanafalsafa wa Kiyunani, Aristotle, alisema demokrasia ni utawala wa walalahoi. Walalahoi ndiyo wameshika hatamu, siyo Masultan wala Mamwinyi. Aristotle alifikiri demokrasia peke yake yaweza kuleta dhahma kwa sababu walalahoi (wananchi) wanahitaji mwongozo kiasi fulani. 

Je, wananchi wanatawala kwa namna gani? Mbona wengine  wapo Markiti, wengine wanauza nguo Mlandege; na wengine wapo forodhani wanafanya kazi ya ukuli? Jibu ni kuwa wananchi wanatawala kwa njia kuu tatu:

1. Kushiriki katika kuandika Katiba yao. 

Kupitia mchakato wa kuandika katiba ndiyo wanaamua waongozwe namna gani na Serikali yao iwe namna gani. Ni wao wenyewe ndiyo wanatakiwa kuandika katiba.

2. Kuwaweka wananchi wenzao madarakani na pia kuwaondoa. 

Uchaguzi ndiyo njia mwafaka ya kuwaweka na kuwaondoa viongozi madarakani. Uchaguzi ni kitu muhimu sana. Ni kwa sababu ya uchaguzi ndiyo tunasema Tanzania ni Jamhuri ya Muungano. Maana yake ni kuwa ni nchi ambayo viongozi wanachaguliwa wa wananchi. Nchi ambayo mfumo wake wa Utawala siyo Usultan wala Umwinyi. Ni nchi inayofuata demokrasia. 

Mfumo mzuri wa uchaguzi ni ule unaowawezesha wananchi kuwaweka madarakani watu wanaowataka na kuwaondoa wale wasiowataka. 

Ni mfumo wa kuwatunuku wale wanaojitoa kuwahudumu wananchi wenzao na wa kuwaadhibu waliofanya makosa wakiwa madarakani. 

Hivyo, uchaguzi ukivurugwa au ikiwa mfumo wa uchaguzi siyo wa haki basi hakuna utawala wa kidemokrasia, kuna Umwinyi.

3. Haki ya wananchi kutawala haiishii kwenye sanduku la kura. Baada ya uchaguzi Wananchi wataendelea kushiriki kikamilifu katika utawala. Popote walipo, ama markiti, maskani, Forodhani, na kwingineko, wana haki ya kutoa maoni kuhusu namna serikali na nchi yao inavyoendeshwa. 

Pia, wana haki ya kutoa maoni yao na kuikosoa serikali kupitia vyombo vya habari kama magazeti, radio, TV  na mitandao ya kijamii. 

Aidha, kama Katiba inakiukwa basi wana haki ya kwenda mahakamani na kusitisha huo ukiukwaji. Kama kuna mfumo unaowalinda viongozi wasishtakiwe na wananchi basi mfumo wa utawala siyo demokrasia; ni Usultani na Umwinyi.

Katika mfumo wa demokrasia wananchi ndiyo ma-boss, viongozi ni watumishi (watumwa?) wa wananchi.  Wananchi ndiyo watawala. Viongozi huongoza ilihali wananchi ndiyo hutawala. 

Serikali inaundwa na wananchi; viongozi hupata madaraka toka kwa wananchi. Kiongozi wa kidemokrasia anayedai kuwa yeye amepewa madaraka na Mungu basi anapenda Usultan. 

Masultan ndiyo waliodai kuwa walipewa madaraka na Mungu na siyo na wananchi na kwamba walikuwa na haki ya kufanya wanachotaka hata kuwatia watu ndani ili kuwanyamazisha. Kiongozi kusema mimi nimepewa madaraka na Mungu ni kufuru ya kikatiba (Constitutional blasphemy).

4. USAWA WA KISIASA WA WANANCHI

Msingi mkubwa wa demokrasia ni usawa. Wananchi wote ni sawa. Ni usawa wa aina gani haswa? Je, wote tuna haki ya kwenda hospitali na kuhudumu kama matabibu? Je, kila mtu anaweza kuwa mwalimu? La hasha, siyo usawa wa namna hiyo. 

Usawa wa kidemokrasia ni "usawa wa kisiasa". Kila mwananchi aliyefikisha umri uliokubalika ana haki ya kupiga kura. Katiba kuwazuia wananchi wenzetu waliopo magerezani kupiga kura ni Umwinyi. Vifungu hivyo  vya Katiba vinastahili kuondoshwa kwa sababu vinakinzana na msingi muhimu wa Katiba, demokrasia. 

Aidha, kila mwananchi ana haki ya kugombea uongozi wa kisiasa. Awe maskini, ana haki. Awe mkulima, muwindaji, muuza mitumba, nk, kwenye siasa ngoma  ni droo; tupo sawa. Wote tuna haki. 

Uwe umesoma saana, una rundo la vyeti na mimi nauza madafu, sawa. Tukutane ulingoni, jukwaani. Tuone wenye nchi watasema nani anafaa. 

Awe hajasoma sawa. Awe mkwea minazi huko Nungwi ni sawa. Afue tu kanzu lake aje achukue fomu. 

Mwananchi hapotezi haki yake kushiriki katika siasa kwa sababu elimu yake ni ndogo. Ndiyo maana sheria zetu ni sharti ziweke kiwango cha chini kabisa cha elimu kama sifa ya kugombea kwa sababu mfumo wa demokrasia unahitaji ushiriki wa wananchi wengi. 

Elimu siyo kigezo cha kuwabagua wengine. Miaka ya karibuni kuna watu wanadai katiba izuie wenye elimu ya darasa la saba kuwa Wabunge. Hawaelewi maana ya demokrasia; wanataka Umwinyi!

Ieleweke kuwa usawa wa kisiasa hauzingatii mwananchi ana elimu ya aina gani. Kama umesomea siasa huwezi kuwa mwanasheria lakini kugombea Urais sawa. Kama kasomea kilimo hawezi kuwa daktari lakini Urais ruksa. Kama ni Mkemia hawezi kuwa Mhasibu lakini Urais twende.

Kama ni darasa la saba ajira ya udereva serikalini hupati lakini Ubunge na Urais ni ruksa. Ni usawa wa kisiasa ambao ni msingi muhimu katika utawala wa kidemokrasia. Tutofautiane kwenye masuala mengine lakini kwenye siasa tupo sambamba, tupo sawia.  

Yawezekana demokrasia ina changamoto zake. Hakuna mtu anayesema demokrasia haina matatizo. 

Matumizi ya fedha na rushwa kwenye uchaguzi yaweza kuigeuza demokrasia kuwa Umwinyi. Wenye fedha tu ndiyo watakuwa viongozi. 

Faida kuu ya mfumo wa demokrasia ni amani. Kuwatoa viongozi wabovu kwa kura kunaondoa ulazima wa kuchukua silaha na kumwaga damu kama ilivyokuwa wakati wa mfumo wa Usultan.

5. UCHAGUZI WA ZANZIBAR

Sasa nirejee mwenye Urais wa Zanzibar. Watu wengi kuchukua fomu katika Urais wa Zanzibar ni ishara ya kukua kwa demokrasia yetu. Kila mwananchi ambaye ni mwanachama wa CCM ana haki ya kugombea.  

Haifai kabisa kumshutumu mwananchi mwenzetu kwa kitendo chake cha kuonesha nia ya kugombea. Yafaa tumpongeze kwa ujasiri wake. 

Kuna matamko mengi ya viongozi yanayosuta wananchi wenzetu waliojitokeza kugombea. Kulikoni? Iweje kutimiza haki ya kiraia iwe ni suala la kulaumiwa badala ya kupongezwa? Huu Umwinyi wa kuona kuona kuna watu wana haki ya kuchukua fomu za kugombea na wengine hawana umeanza lini? Katiba zetu mbili si zinasema utawala wetu ni kidemokrasia.

Kuna watu wameonesha wasiwasi kwa watoto wa viongozi kuchukua fomu. Inaashiria kurejea kwa Usultan unaorithisha uongozi au Umwinyi unaotoa haki ya kuongoza kwa tabaka la watu wachache. 

Hata hivyo, watoto wa viongozi nao ni wananchi wenzetu. Wana haki ya kugombea. Wanachotakiwa ni kutuondolea wasiwasi. 

Mfano, mmojawapo anatakiwa aseme bayana: "Mimi naitwa Mwinyi lakini sipendi Umwinyi; nagombea kwa sifa zangu binafsi jamani." Na mwingine aseme: "Jina litakalopigiwa kura ni Ali, siyo Abeid wala Karume." Na kwenye karatasi ya kura yafaa jina la "Ali" lisomeke bayana, lisifupishwe. Ieleweke dhahiri kuwa Ali ndiye mgombea, siye mwingine.

Vyama vya siasa ni taasisi muhimu za kidemokrasia. Vinatakiwa kukuza demokrasia badala kuifinya. Demokrasia inahitaji wanaochukua fomu wajipambanue; waseme watawafanyia nini Wazanzibari. Kila mmoja aseme bayana tofauti yake na wengine ni ipi. 

Sasa inaonekana chama tawala ambacho kinatakiwa kuwa mwalimu wa demokrasia kutokana na ukongwe wake kinafinya demokrasia. 

Wagombea hawaruhusiwi kuongea. Wanapigwa picha na mabegi tu. Wananchi wanaoneshwa mabegi. Demokrasia ya mabegi (handbag democracy!). 

Wagombea waachwe, waongee, walumbane. Demokrasia ni mjadala, ni malumbano. Wananchi hatuwezi kuamua bila kujua wagombea wetu watatuongoza kwa namna gani. Yafaa mijadala iruhusiwe.

Mwishowe nawapongeza wote waliochukua fomu na kuwatakia mapambano mema. Kila la kheri

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.