Habari za Punde

Wananchi Watakiwa Kuchukuwa Ushauri wa Wataalam Wakati Wanapoazisha Miradi ya Maendeleo -Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Fujoni Meli 14 alipofika kuangalia Matangi ya Maji.
Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Fujoni Meli 14 walifika kumlaki Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seiof Ali Iddi hayupo pichani alipofika kukagua maendeleo ya Mradi wao wa Maji safi na salama.
Muonekano wa Mnara wa kuhifadhia Matangi ya Maji yatakayokuwa na ujazo wa Lita 15,000 ikiwa ni Mradi unaoendeshwa kwa nguyvu za Wananchi wenyewe wa Kijiji cha Fujoni Meli 14.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif amewakumbusha Wananchi kuzingatia ushauri wa Wataalamu wakati wanapoanzisha miradi yao ya Maendeleo ili pale inapokamilika iweze kutoa huduma kwa ufanisi na kudumu kwa muda mrefu Zaidi.
Alisema ipo baadhi ya miradi ya Wananchi inayofifia na mengine kufa kabisa baada ya kukosa usimamizi wa Kitaalamu jambo linaloleta usumbufu kwao na hatimae hukosa matumaini ya kuiendeleza.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kumbusho hilo alipofanya ziara fupi ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Maji safi na salama katika Kijiji cha Fujoni Meli 14 unaendeshwa kwa nguvu za Wananchi wenyewe ambao tayari umeshafikia hatua ya ujenzi wa Mnara wa kuhifadhia Matangi ya Maji baada ya kumalizika kwa uchimbaji wa Kisima.
Aliwapongeza Wananchi wa Kijiji cha Fujoniu Meli Nne kwa uamuzi wao wa kujitafutia maendeleo kwa jitihada zao wenyewe sambamba na kuondosha changamoto inayowakabili ya upatikanaji hafifu wa huduma za Maji safi na salama katika Kijiji chao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda aliwahakikishia Wananchi hao kwamba yeye kama Kiongozi hatochoka kuunga mkono juhudi zao kwa kutia nguvu zitakazoamsha ari ya kukamilika kwa wakati Miradi ya Kijamii hasa ile ya  Huduma za Maji safi na salama.
Mapema Msimamizi wa Mradi huo Ndugu Ali Omar Maulidi alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba awamu ya kwanza ya uchimbaji wa Kisima zimeshafikia hatua nzuri na kwa wakati huu nguvu zao wamezielekeza kwenye ujenzi wa Mnara wa kuhifadhia Matagi Mawili ya Maji yenye ujazo wa Lita elfu 15,000.
Nd. Ali alisema kinachosubiriwa kwa sasa ni hatua ya kumwaga zege ili kukamilisha kazi hizo zitakazokwenda sambamba na miundombinu ya usambazaji wa Mipira ya Maji katika Mitaa ya Kijiji hicho.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Wananchi wa Kijiji cha Fujoni Meli 14 Mmoja wa Wazee wa Kijiji hicho alimshukuru Mwakilishi wao kwa moyo wake wa kuendelea kuunga mkono nguvu za Wananchi  licha ya kutangaza kutogombea tena Uwakilishi kwenye Uchaguzi wa Mwaka huu wa 2020.
Katika ziara hiyo Balozi Seif  akirejea katika majukumu yake ya kawaida alipata wasaa wa kusalimiana na Wananchi waliopo katika Kituo cha Usafiri wa Abiria Meli Nane kwa Nyanya ambacho kimekuwa na harakati za Kibiashara zilizolenga kuwahudumia Wasafiri hao.
Serikali kupitia Mkandarasi wa Ujenzi wa Bara bara ya Bububu- Mahonda, Kinyasini hadi Mkokotoni imeamuwa kujenga Kituo maalum cha Abiria ili kudhibiti Magari yanayofika eneo hilo kwa kushusha na kupakia abiria ambapo kwa wakati huu harakati hizo za usafiri huifanyika bara barani jambo ambalo ni hatari kwa maisha ya Wananchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.