Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akihutubia Wajumbe wa Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa katika ukumbi wa White House Jijini Dodoma leo 10/7/2020.
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ambaye pia, ni
Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar amesema kuwa mchakato wa kumpata mgombea wa
nafasi ya Rais wa Zanzibar umekwenda vizuri tokea ulipoanza hadi kukamilika
hivi leo.
Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati akitoa salamu zake
katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), kilichofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa CCM “White House” Jijini Dodoma.
Makamo Mwenyekiti huyo alieleza kuwa mchakato wa kuwapata
wagombea hao umekwenda vizuri kwa mujibu
wa Katiba ya CCM, Kanuni na taratibu zote za chama hicho chini ya uongozi wake.
Akizungumza kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo wa kumpata
mgombea wa nafasi ya Urais wa Zanzibar, Rais Dk. Shein alisema kuwa
kilichofanyika Zanzibar katika vikao vya chama hicho ni kutafuta wagombea ili
kuendeleza mchakato huo wa kumpata mgombea mmoja atakaepeperusha bendera ya
CCM.
Alisisitiza kuwa lengo la chama hicho ni kutafuta ushindi
katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka huu na kusisitiza kuwa CCM itashinda.
Katika salamu zake hizo, Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM
Zanzibar alieleza uzoefu wake ndani ya chama hicho ambapo amekitumikia kwa takriban
miaka 51 hivi sasa.
Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuepuka maneno yasiokuwa
na msingi katika kukiimarisha chama hicho na kwuataka kuwa waungwana ikiwa ni
pamoja na kukemea vikali kauli za kubeba mgombea katika mchakato huo wa kumpata Rais wa
Zanzibar.
Katika Kikao hicho cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), majina
matatu yalipigiwa kura baada ya wagombea hao mapema kutoa salamu zao na kuomba
kura kwa wajumbe wa mkutano huo.
Waliopigiwa kura katika kikaohicho ni Shamsi Vuai Nahodha
aliyepata kura 16 sawa na asilimia 9.75, Dk. Khalid Salum aliyepata kura 19
sawa na asilimia 11.58 na Dk. Hussein Mwinyi aliyepata kura 129 sawa na asilimia
78.65 kati ya wapiga kura 166 na hatimae kuibuka kidedea katika uchaguzi huo.
Aidha, katika kikao hicho kilipitisha jina la mgombea wa
nafasi ya CCM katika nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John
Pombe Joseph Magufuli ambaye atakwenda kupigiwa kura katika Mkutano Mkuu wa CCM
hapo kesho.
Pamoja na hayo, Rais Magufuli alimpongeza Rais Dk. Shein
kwa umakini wake mkubwa katika kuiongoza Zanzibar sambamba na mafanikio makubwa
yaliyopatikana katika sekta mbali mbali za maendeleo.
Rais Magufuli ambaye pia, ni Mwenyekiti wa CCM Taifa
aliwapongeza viongozi wote wa CCM pamoja na wale wote waliomdhamini huku
akiwataka Wazanzibari kuwa wamoja katika kuiimarisha CCM na hatimae kuhakikisha
inapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi Mkuu ujao.
Mapema wagombea wote watano wa nafasi ya Urais wa Zanzibar
na wakiwemo wale watatu waliopitishwa katika Kamati Kuu ya chama hicho
walitumia fursa hiyo kutoa salamu zao ikiwa ni pamoja na kutoa shukurani kwa
(CCM) kwa kuweza kupata nafasi ya kugombea nafasi hiyo muhimu.
Nae Katibu Mkuu wa CCM Taifa Dk. Bashiru Ali Kakurwa
alieleza mafanikio yaliyopatikana katika uongozi wa Rais Magufuli katika
uongozi wake wa kipindi cha Kwanza cha miaka mitano huku wajumbe wa mkutano huo
walitoa pongezi kwa Rais Magufuli pamoja na Rais Dk. Shein kwa mafanikio hayo.
Baada ya kutangazwa kuwa mshindi
wa kura hizo Dk. Hussein Mwinyi ambaye alikuwa Mbunge wa Kwahani na pia, Waziri
wa Ulinzi aliwashukuru wajumbe wote kwa kuonesha imani kwake na kuahidi kufanya
kazi na kulitumikia Taifa kwa uwezo wake wote. "Hizi ni kura nyingi
sana...nikuahidini kuwa tutakuwa pamoja tukatafute ushindi wa Chama Cha
Mapinduzi,"
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment