Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akitowa mkono wa Pole kwa Familia ya marehemu Rais Mstaaf wa Awamu ya Tatu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin William Mkapa, alipofika nyumbani kwa marehemu Masaki Jijini Dar es Salaam (kulia kwa Rais) Mjane wa Marehemu Mama Anna Mkapa na Mtoto wa Marehemu Nico Mkapa. l
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ametoa mkono wa
pole kwa familia ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Bejamin William Mkapa na kueleza kuwa kiongozi huyo atakumbukwa kwa
mazuri mengi aliyoifanyia Tanzania.
Rais Dk. Shein alifika nyumbani kwa marehemu Rais Mstaafu
wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bejamin William majira ya
saa tano za asubuhi katika Mtaa wa Masaki Jijini Dar es Salaam ambapo alitoa
mkono wa pole kwa familia pamoja na kumpa
mkono wa pole Mjane wa Marehemu Mama Anna Mkapa.
Mapema mara tu baada ya kufika nyumbani kwa marehemu Rais Dk. Shein
alitia saini kitabu cha maombolezi na
kutoa pole kwa kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Bejamin William Mkapa huku
akimuomba Mwenyezi Mungu aipe subira familia
ya Rais Mkapa katika kipindi hichi kigumu cha msiba.
Akitoa mkono wa pole kwa familia ya Rais Mkapa, Rais Dk.
Shein alieleza jinsi alivyoguswa na kifo cha Rais Mkapa na kuitaka familia hiyo
kuwa na subira na kuendelea kumuombea Marehemu kutokana na mema mengi aliyoyafanya
kwa wananchi pamoja na nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mara baada ya matukio hayo, Rais Dk. Shein alipata fursa ya kufanya
mahojiano na waandishi wa habari ambapo katika mazungumzo yake alimuelezea Rais
Mkapa kuwa ni kiongozi mahiri aliyefanya kazi nae kwa muda wa miaka minne na
nusu na kuweza kujifunza mambo mengi.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa Rais Mkapa aliweza kuifikisha Tanzania mahala
pazuri sana kwa kusimamia misingi ya uchumi ambayo hatimae iliipelekeaTanzania
kuimarika.
Aliongeza kuwa Rais Mkapa ameitumikia nchi kwa nidhamu kubwa sana ikiwa
ni pamoja na kusimamia nchi kiuchumi na kimaendeleo sambamba na kuisimamia nchi
kwa misingi yote ya amani na utulivu mkubwa
Alisema kuwa msiba huo ni wa Watanzania wote na kwa kila anaependa maendeleo
wa ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akisisitiza kumuombea ili
apumzike kwa salama.
Katika kufuata misingi ya Rais Mkapa, Rais Dk. Shein aliwataka viongozi
waliopo madarakani wazee na vijana kujifunza uongozi kutoka kwa Rais Mkapa kwani
kiongozi huyo alikuwa ni mtu aliyeishi vizuri na watu wa maeneo yote tena bila
ya kuwabagua.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa anayakumbuka mengi aliyoyafanya Rais Mkapa
wakati anafanya kazi nae pamoja ikiwa ni pamoja na kusaidia sana kuibadilisha
nchi kwa kufanya mabadiliko ya kiuchumi sambamba na kuimarisha utawala bora kwa
kuanzisha Wizara ya Utawala Bora ambayo ilikuwa ndiyo Wizara ya mwanzo katika
Serikali za nchi za Bara la Afrika huku
akisimamia kwa vitendo uchumi wa Tanzania.
Alisema kuwa wakati Rais Mkapa anaingia madarakani makusanyo yalikuwa
madogo sana kwani yalikuwa ni wastani wa TZS Bilioni 1.7 mnamo mwaka 2005 lakini kutokana na juhudi zake makusanyo
yaliimarika zaidi hatua ambayo pia ilipelekea kufanyika kwa mabadiliko ya
sayansi na teknolojia.
“Ninayakumbuka mengi sana aliyoyafanya Rais Mkapa tukiwa pamoja
Serikalini na ni muhali kuyasema hapa yote kwa muda huu mfupi kwani amefanya
mambo mengi wakati nilishirikiana nae”, alisema Dk. Shein.
Alieleza kuwa kubwa kabisa na la muhimu alilofanya Rais Mkapa ni kusimamia
mwenendo mzuri wa uchumi wa nchi kwani hilo linatokana na uzoefu wake wa
uongozi kwani awali aliwahi kuwa Waziri katika Wizara kadhaa za Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hatua ambayo imesaidia kumpa ujuzi na uwezo
mkubwa wa kuongoza nchi.
Kutokana na Rais Mkapa kumtaja Rais Dk. Shein katika kitabu chake cha “My
Life, My Purpose” Rais Dk. Shein alisema kuwa ameweza kumtaja katika kitabu
chake hicho kwani alifanya kazi nae na kuishi nae vizuri kwani akiwa Makamo wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Dk. Shein alifanya kazi na Marehemu
Mkapa na kumuheshimu na kumuweka kuwa ni kiongozi wake, mkubwa wake na pia,
alikuwa ni kiongozi wake wa Chama.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa yeye kwake ilikuwa ni rahisi sana kufanya
kazi na Rais Mkapa kwani ni mkubwa wake na pia ni kiongozi wake wa kazi hivyo, alifanya
kazi kwa kumuheshimu na kuishi nae vizuri na kumuacha afanye kazi zake bila ya
kumuingilia hiyo ni kutokana na kumuamini wakati wote.
“Kwa vile alikuwa ananiamini, mtakumbuka hata mnamo mwaka 2003
alipokwenda nje ya nchi kwa muda kidogo lakini wakati huo yeye hayupo mimi
niliweza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa kutokana na mafunzo yake aliyonipa……..ni
mtu ambaye ukifanya kazi nae unaona raha sana”, alisema Rais Dk. Shein.
Hivyo, Rais Dk. Shein alisema kuwa hatua yake hiyo ilimpelekea kufanya
kazi kwa kujiamini na kusisitiza kuwa ni mtu ambaye ukifanya kazi nae unaona
raha sana kwani anakuachia kufanya kazi zako vizuri kwani ni mtu aliyekuwa
akishaurika na ni mtu aliyekuwa akielekeza namna ya kufanya kazi kwani alikuwa mtu wa mfano wake.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment