Habari za Punde

Taarifa ya Waziri wa Elimu na mafunzo ya amali kufunguliwa kwa skuli na ulipaji wa ada za masomo kwa skuli binafsi

TAARIFA YA MHESHIMIWA RIZIKI PEMBE JUMA, WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI KUHUSU KUFUNGULIWA KWA SKULI NA SUALA LA ULIPAJI WA ADA ZA MASOMO KWA SKULI BINAFSI BAADA YA KUFUNGULIWA KWA SKULI 

Ndugu Manaibu Katibu Mkuu wa WEMA
Ndugu Wakurugenzi wa WEMA na Maafisa wa Elimu,
Ndugu, Mwenyekiti na Viongozi wa Jumuia ya Umoja wa Skuli Binafsi (ZAPS), Zanzibar
Ndugu, Viongozi wa Wizara,
Ndugu, Wamiliki na Walimu wakuu wa Skuli za Binafsi,
Ndugu, Walimu na Wazazi/Walezi 
Ndugu,Waandishi wa Habari na Jamii kwa Ujumla

Assalaam Aleykum Warrahmatullahi Wabarakatuh, 

Kutokana na nchi yetu kama mataifa mengine kukumbwa na janga la maradhi ya korona, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitangaza kuvifunga Vyuo Vikuu na skuli zote tarehe 18/03/2020. 

Baada ya maradhi ya Korona kupungua, Serikali ilitangaza kufunguliwa Vyuo Vikuu, Vyuo vya Ualimu na Mafunzo ya Amali pamoja na wanafunzi wa Kidato cha Sita siku ya Jumatano tarehe 27/5/2020.  

Hivi sasa, shughuli zote za masomo katika Taasisi za Elimu ya Juu na Vyuo vya Mafunzo ya Amali zinaendelea vizuri. Pia wanafunzi wetu wa Kidato cha Sita, jana Jumatatu tarehe 29/06/2020 wameanza rasmi kufanya mitihani yao ya Taifa. 

Tumefuatilia katika skuli mbali mbali za Serikali na Binafsi na tumeridhika na shughuli za mitihani zinavyoendelea. Ninawatakia kheri na mafanikio katika mitihani yao.

Katika hatua ya pili, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliamuru kuzifungua skuli zote za Maandalizi, Msingi na Sekondari (kidato cha 1-5) za Serikali na Binafsi kuanzia Jumatatu ya tarehe 29/06/2020. 

Tangazo rasmi la kufunguliwa Skuli hizo nililitoa siku ya Alkhamis tarehe 25/06/20202. 

Wizara inafuatilia ufunguaji wa skuli zote hatua kwa hatua na hadi sasa tumeridhika na hatua zinazochukuliwa na Serikali za Mitaa kupitia Baraza la Mji, Manispaa na Halmashauri katika kutekeleza mwongozo tulioutoa kuhusu utaratibu wa masomo katika skuli. Zipo changamoto ndogo ndogo zilizojitokeza na zitatatuliwa hatua kwa hatua.

Kwa upande wa Skuli za Binafsi, tunawapongeza wamiliki wengi wa Skuli za Binafsi kwa kuendelea kutoa huduma ya elimu wakati skuli zilipofungwa kwa njia ya mtandao na wanafunzi wote kufuatilia masomo kwa njia ya radio na Televisheni. 

Hivi sasa Skuli zimefunguliwa vizuri. Hatahivyo, Wizara imepokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wazazi wa wanafunzi kwa baadhi ya skuli binafsi kuwataka wazazi wa wanafunzi walipe ada ya masomo kwa kipindi ambacho skuli zilipofungwa mwezi Machi hadi kufunguliwa kwake. 

Kutokana na changamoto hii iliyojitokeza, Wizara ya Elimu inapenda kutoa ufafanuzi na kukumbushia mambo yafuatayo.

 Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na Marekebisho  yake ya mwaka 2010, ibara ya 10(f) imeeleza kuwa  “kwa madhumuni ya kuendeleza umoja na maendeleo ya watu na ustawi wa jamii katika nchi itakuwa ni jukumu la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha kwamba zipo huduma za kutosha za kiafya kwa watu wote, zipo fursa sawa na za kutosha za kielimu katika madaraja yote na kwamba utamaduni wa Zanzibar unalindwa, unaimarishwa na unaendelezwa”

Kwa kulisimamia hili Sheria ya Elimu ya mwaka 1982 na Marekebisho yake ya mwaka 1994  kifungu cha 20 kinamtaka kila  Mzazi/wazazi au walii wa kila mtoto aliyeandikishwa skuli atahakikisha  au watahakikisha kwamba  mtoto huyo anahudhururia skuli ipasavyo mpaka atakapomaliza elimu ya lazima kwa wote au kama hajamaliza elimu hiyo hadi atakapofikia umri wa miaka kumi na nane.

Pamoja na jitihada kubwa zinazochukuliwa na Serikali kusimamia elimu kwa wote kwa kuondoa michango kwa wanafunzi wote wa skuli za Serikali kuanzia ngazi ya maandalizi, msingi na sekondari hadi Kidato cha Nne, Serikali  ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini michango inayotolewa na wadau mbalimbali wa elimu katika  kusaidia na kuunga mkono juhudi za Serikali.

 Hivyo, skuli za binafsi zina nafasi kubwa sana katika kusaidia maendeleo ya elimu na kufikia haki ya elimu kwa wote, Zanzibar. Ni suala lisilopingika kuwa Serikali inajivunia jitihada zinazochukuliwa na skuli binafsi katika kusaidia na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutoa na kusimamia elimu kupitia taratibu zilizowekwa.

Kuhusu utozaji wa ada kwa skuli za binafsi ni kwa mujibu wa sheria ya Elimu nambari 6 ya mwaka 1982 na marekebisho yake ya mwaka1994, kifungu cha 52(1) kinaeleza kuwa skuli yoyote ya binafsi , skuli ya kidini  au skuli inayosaidiwa  itaweza kutoza  baada ya kuruhusiwa na Waziri, kutoza ada au kupokea michango kwa ajili ya uandikishaji au mahudhurio ya mwanafunzi au kama ada ya masomo. 

Mradi viwango vya ada, michango au malipo mengine ya aina hiyo lazima viwe  vimekubalika mapema na Waziri kabla ya kutumika.

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, inawaagiza wamiliki wa Skuli Binafsi na walimu wakuu wote wa skuli zisizo za Serikali kutotoza ada ya masomo kwa miezi ya Aprili, Mei na Juni 2020 kwa vile skuli zote zilifungwa  kutokana na janga la Maradhi ya Covid-19. Janga hilo ni la Kimataifa sote tumeathirika kwa njia moja au nyengine. 

Serikali ilizuwia mikusanyiko ya watu na kupelekea harakati za masomo na shughuli nyengine muhimu za kiuchumi na kijamii kusimamishwa kama ilivyo kawaida yake na badala yake kupangiwa utaratibu maalum. Jambo ambalo lilisababisha baadhi ya shughuli za kiuchumi kushuka. Hivyo sote tukubali kutoa mchango wetu katika janga hilo bila ya kuwatwika mzigo wazazi wa wanafunzi. 

Aidha kwa agizo hili,Wizara inawataka  wamiliki na walimu wakuu hao kutowafukuza wanafunzi kwa kutokulipa ada kwa kipindi kilichoainishwa hapo juu. Ada ambazo wazazi watapaswa kulipa zianzie mwezi Julai 2020.

Napenda kuwatahadharisha wamiliki wote wa Skuli za Binafsi wafuate agizo la Serikali na pindipo watakaidi utekelezaji wa agizo hili, Wizara itawachukulia hatua za kisheria na inapobidi hatutosita hata kuzifunga baadhi ya skuli. 

Kwa mara nyengine nawatakia kheri na mafanikio wanafunzi wetu wote wanaofanya Mitihani ya Kidato cha Sita. Nina imani kubwa watafanya vizuri mitihani yao na wote watafaulu katika madaraja ya juu.

 Pia, napenda kutoa wito kwa Walimu na Wanafunzi Wazazi na Wananchi wote kwa jumla kuwa tuendelee kufuata miongozo inayotolewa na Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya kujikinga na maradhi ya Korona nchini kwetu.

‘Zanzibar bila ya korona inawezekana na tutaishinda na kuitokomeza Kwa juhudi zetu sote’

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Imetolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali,
Siku ya Jumanne tarehe 30 Juni 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.