VIONGOZI wa ndani na nje ya nchi wakishuhudiwa na maelfu
ya Watanzania wakiongozwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli waliungana
pamoja kuuaga kitaifa mwili wa Marehemu Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin William Mkapa.
Viongozi wa Kitaifa
waliuaga mwili wa Hayati Mkapa wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dk. John Pombe Magufuli, wanafamilia, Makamo wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na viongozi wa dini.
Tukio hilo limefanyika
leo uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali
wa ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wananchi.
Aidha Rais John Pombe
Magufuli alitumia fursa hiyo kwa niaba ya Serikali pamoja na wananchi kutoa
mkono wa Pole kwa familia ya Hayati Mkapa akiwemo Mama Mkapa, Watoto pamoja na
wajukuu na ndugu na jamaa wote.
Alieleza kuwa msiba
huo ni wa Watanzania wote na sio wao pekee yao na kutoa pole kwa Watanzania
wote kwa kuondokewa na kiongozi huyo na kuwataka wananchi kuendelea kua
watulivu na huku wakiendelea kumuomba Mwenyezi kuipumzisha roho ya Marehemu
Mkapa.
Akimuelezea Rais
Mstaafu Hayati Mkapa kwa ufupi alieleza mchango na mafanikio ya Mzee Mkapa
akiwa Rais na baada ya kutoka madarakani na kusema kua Tanzania na Bara la
Afrika na dunia imepoteza mtu jasiri, mchapakazi, mcha Mungu, mfuatiliaji,
mwenye msimamo, mwanadiplomasia nguli na mpenda amani na mshikamano.
Aidha, alieleza kuwa
Mzee Mkapa ni Baba wa Demokrasia nchini, na kusema kuwa utoaji wa ruzuku wa
vyama vya siasa ulianza katika Awamu ya Mzee Mkapa ikiwa ni pamoja na kuahidi
kuwa Serikali yake inajengwa kwa misingi ya ukweli na uwazi ambapo baadae
aliunda Tume ya Warioba na hatimae kuunda TAKUKURU.
Alisema kuwa
Watanzania wengi wanamkumbuka Mzee Mkapa kwa mageuzi makubwa ya kiuchumi, jinsi
alivyoweka mipango na mikakati ya kupunguza umasikini nchini ukiwemo mpango wa
TASAF ambao mpaka awamu hii utakuwa umeshatumia TZS Trioni 4.19.
Alieleza jinsi
alivyofuta kodi ikiwemo kodi ya baskeli, mifugo na hatua ambayo inaonesha jinsi
alivyokuwa akiwapigania wanyonge na hatua za kuimarisha huduma za kijamii
nchini na kujenga sekta binafsi zikiwemo Benki kubwa nchini.
Rais Magufuli alisema
kuwa Hayati Mzee Mkapa alianzisha taasisi nyingi ili Tanzania ijitegemee
ikiwemo Bodi ya Mfuko wa Barabara, TANROAD hatua ambayo ilipelekea ujenzi wa
barabara za lami na madaraja kadhaa hapa nchini.
Aliongeza kuwa
Mafanikio mengi ya kiuchumi misingi yake mengi iliwekwa katika uongozi wa Rais
Mkapa ambapo pia, diara ya maendeleo ilianzishwa na Rais huyo ambapo chimbuko
lake ni CCM ambacho Rais Mkapa alikitumikia na kukipenda sana.
Alijitahidi katika
kuimarisha sekta ya elimu, maji,maslahi ya wahadhiri, kuimarisha sekta ya afya
pamoja na kusimamia amani na utulivu
huku akisimamia haki na usawa duniani hatua ambayo ilipelekea kuzifumbua macho
nchi zinazoendelea duniani.
Sambamba na hayo,
alisema kuwa Mzee Mkapa aliimarisha sekta ya michezo pamoja na kuwaimarisha
wasanii ikiwa ni pamoja na kuujenga uwanja wa Taifa wa Michezo na hapoa hapo
alitamka kuwa kuanzia leo uwanja huo uitwe Mkapa Stadium.
Alieleza kua katika
uongozi wa Mzee Mkapa pia, ndicho kipindi kilichoundwa Chama cha hati miliki
(COSOTA) ikiwa na lengo la kuwasaidia wasaniii, uwanzishwaji wa vitengo vya
habari na kutunga Sheria namba 30 ya kuanzisha Wakala ambapo kupitia sheria
hiyo taasisi nyingi zimeundwa na kuleta mafanikio makubwa.
Sambamba na hayo, Rais
Magufuli alieleza jinsi Mzee Mkapa alivyokuwa na uwezo wa kulea na kuibua
vipaji vya viongozi wa ngazi za juu hapa nchini akiwemo yeye mwenyewe, Rais
Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na Mgombea Urais kupitia CCM kwa upande
wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi.
“Kifo cha Mzee Mkapa
kimeacha alama duniani...serikali ninayoiongoza itadumisha mambo yote mazuri
yaliyoasisiwa na Mzee Mkapa.....Mzee Mkapa ni shujaa wangu na ni mtu muhimu
sana katika maisha yangu na hata nilipopatwa na shida ama kupambana na
changamoto mbali mbali mzee Mkapa hakuniacha alinilea kama mtoto wake”,alisema
Magufuli.
“leo hapa Mkapa hayupo
nimesikitika kuwaona wawili tu hiii inaumiza sana, mtakumbuka katika siku za
hivi karibuni viongozi hawa watatu walikuwa pamoja katika uzinduzi wa kitabu
cha Mkapa walikuwa pamoja....kwa hakika ilikuwa ikiependeza sana na kufurahisha
sana lakini sasa hatutawaona mkiwa watatu tena” aliongeza Magufuli huku
akibubujika na machozi.
Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaaliwa Majaaliwa alisema kuwa ni vyema
Watanzania wakamuezi kiongozi huyo pamoja na yale yote mazuri aliyoyafanya na
kuwafanyia Watanzania pamoja na nchi za jirani ya Tanzania.
Nae Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki na Amidi wa Sherehe alisoma wasifu wa Hayati Benjamin William Mkapa
na kuyaeleza maisha yake yote kuanzia familia, masomo, kazi zake, uongozi wa
serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Pia, alieleza
mafanikio ya Rais Mkapa katika uongozi wake ikiwa ni pamoja na kusimamia
ukombozi wa nchi za Bara la Afrika na
jinsi alivyoheshimika katika nchi za Kusini mwa Afrika na kupelekea kupewa
nishani ya Juu kutokana na juhudi zake hizo.
Aidha, alieleza jinsi
alivyochangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa Tanzania na mikakati
aliyoiweka ikiwa ni pamoja kuhakikisha uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa
kisiasa unakuwepo.
Profesa Kabudi
alieleza kuwa maradhi yaliyopelekea kifo cha Hayati Mzee Mkapa ni Moyo kusimama
hafla pamoja na Malaria.
Waziri Mkuu wa Burundi
Jenerali Alain Guillaume Bunyoni kwa upande wake akitoa salamu za pole kwa
niaba ya Rais wa Burundi na wananchi wa nchi hiyo wanaungana mkono na wanatoa
pole kwa msiba huo mkubwa uliowapata ndugu zao wa Tanzania.
Nae Balozi Ahmada
Elbadui Mohammed Faki, Balozi wa Comoro nchini Tanzania kwa niaba ya Mabalozi
wanaofanya kazi zao hapa nchini alitoa neno la pole kwa Rais Magufuli pamoja na wananchi wote wa Tanzania na kueleza
jinsi Hayati Mkapa alivyokuwa jasiri katika kupambana na uhuru wa nchi za Bara
la Afrika.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
No comments:
Post a Comment