Kaimu Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili Tanzania
Consolata Mushi akitoa taarifa kwa Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo
Dkt.Harrison Mwakyembe kuwa taasisi yake tayari imekwisha sajili jumla ya
wahitimu 1224 katika kanzidata ya wataalamu wa mafunzo ya lugha ya Kiswahili
kwa wageni,leo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa wahadhiri
wa Kiswahili katika chuo kikuu cha Dodoma.
Na.
Anitha Jonas – WHUSM, DODOMA
Baadhi ya watanzania
wamekuwa na hulka ya kutokuwa na matumizi sahihi ya baadhi ya maneno ya lugha
ya Kiswahili, hali ambayo imesababisha Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA)
ikiwa ni taasisi yenye dhamana kuanza
kutoa elimu sahihi yamatumizi ya maneno
ya lugha hiyo.
Kaimu Katibu Mtendaji
wa BAKITA Bibi. Consolata Mushi, hivi karibuni alipokuwa akizungumza kwa njia
ya simu na Afisa Habari wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Habari,
Bibi. Anitha Jonas alisema kuwa
baadhi ya watumiaji wa lugha ya Kiswahili wamekuwa wakifanya makosa ya matumizi
ya lugha ya Kiswahili.
Aidha, Bi.Consolata alisema kuwa baadhi ya maneno yamekuwa yakitumiwa
kimakosa na utumiaji huo umepelekea kuibua mgogoro wa kifikra miongoni mwa
watumiaji wa lugha husika hivyo kuepukana na madhara yanayoweza kuwa makubwa ni
bora kusahihisha matumizi hayo.
“Nitoe mfano ambao
ulisikika siku moja kupitia chombo fulani cha habari kuwa mtaalamu wa kilimo amewaasa
wakulima kutumia mbolea, utumiaji wa namna hii si tu kwamba unapotosha bali
unaharibu kabisa dhana nzima ya kile kinachosemwa,”alisema Bibi.Consolata
Akitolea mfano wa maneno ambayo yanapotoshwa
ni neno ‘asa’ kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili (2015) lina
maana ya “Kanya au kataza mtu kufanya jambo fulani”, na kusema kuwa matumizi hayo yanaweza kupotosha
na kuharibu maana ujumbe uliokusudiwa.
Vilevile, Bibi.Consolata
alifafanua matumizi sahihi ya neno ‘asa’
kuwa linaweza kutumika kwa kuonya mfano: “Walimu wamewaasa wanafunzi kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya” au
“Serikali yawaasa wazazi
wanaowaachisha watoto wao shule kwa ajili ya kuwaoza.
Kwa mujibu wa BAKITA
neno lingine ambalo limekuwa likipotoshwa
na watumiaji wa lugha ya Kiswahili ni mrabaha, chanzo cha upotoshaji wa neno hilo ni ubadilishaji wa
mpangilio wa vitamkwa vya mwisho vinavyounda neno hilo, badala ya kusema mrabaha watu husema mrahaba.
Mrabaha
maana yake ni, “Malipo yanayotolewa na mchapishaji kwa mtunzi wa kitabu kwa
kipindi fulani kama sehemu ya mauzo ya kitabu kinachohusika, au inaweza kuwa ni “Malipo yanayotolewa kama
sehemu ya faida inayotokana na biashara fulani.
Halikadhalika, neno mrahaba halina maana yoyote katika
lugha ya Kiswahili hivyo utumiaji wa neno hilo ni upotoshaji na watu wengi
wamekuwa wakifanya makosa katika matumizi yake.
No comments:
Post a Comment